Open main menu

Hamed bin Mohammed el Murjebi

(Elekezwa kutoka Tippu Tip)

Mfanyabiashara

Baba yake alikuwa mfanyabiashara Mwarabu Muhammed bin Juma, mama yake Bint Habib bin Bushir, alikuwa ni Mwarabu wa tabaka la watawala toka Muscat.

Hamed aliingia katika shughuli za biashara tangu umri wa miaka 12 akafaulu katika biashara ya misafara kati ya Zanzibar na Kongo.

Akiwa na umri mdogo, Hamad aliongoza kundi la wanaume 100 kwenda Afrika ya Kati kutafuta watumwa na pembe za ndovu.[1] Baada ya kuvamia maeneo mengi alirudi Zanzibar kuimarisha vyanzo vyake na kukusanya watu wa kumsaidia ili arudi bara.[2] Hapa alipokea jina la Tippu Tip. Kwa mujibu wake mwenyewe, jina hilo lilitokana na mlio wa bunduki yake wa 'tiptip. [3]

Alipanga misafara ya mahamali waelfu akipeleka bidhaa kutoka Bagamoyo kupitia Tabora hadi Ujiji kwa Ziwa Tanganyika na ndani ya Kongo. Bidhaa alizobeba alizitumia kujipatia pembe za ndovu na watumwa; watumwa walisaidia kubeba pembe za ndovu njia ya kurudi hadi pwani. Hamed alitajirika sana. Athira yake ilipanuka katika Kongo ya Mashariki hadi alitawala eneo kubwa sana.

Kukutana na wapelelezi Wazungu

Hamed akapata jina huko Ulaya kwa sababu alikutana na wasafiri na wapelelezi Wazungu kama David Livingstone, Veney Cameron, Henry Morton Stanley, Eduard Schnitzer (Emin Pascha), Hermann von Wissmann na Wilhelm Junker ambao mara nyingi walipata misaada muhimu kutoka kwake.[4] Kati ya mwaka 1884 na 1887 alikuwa mtu mwenye mamlaka katika sehemu kubwa za Mashariki ya Kongo.

Gavana wa Mfalme wa Ubelgiji

Wabelgiji walipoanza kujenga ukoloni wao Kongo walimkuta kama mtawala wa Kongo ya Mashariki wakapatana naye na kumpa cheo cha gavana ya Mkoa wa Chutes Stanley ("maporomoko ya Stanley", leo Kisangani) mwaka 1887 alichoshika kwa miaka michache.

Mwanzoni mwa 1887, Stanley aliwasili Zanzibar na kumtaka Hamad awe gavana wa Wilaya ya Stanley Falls kwenye Dola Huru la Kongo, iliyokuwa koloni binafsi la mfalme wa Ubelgiji. Mfalme Leopold II wa Ubelgiji na Sultani Barghash bin Said wa Zanzibar walikubaliana na tarehe 24 Februari 1887, Hamad alikubali. Wakati huohuo alikubali kuongoza safari za Stanley ili kwenda kumuokoa Mjerumani Emin Pasha (E. Schnitzer), gavana wa Kiosmani wa Equatoria (eneo la Misri ya Kiosmani, Sudan Kusini ya leo).

 
Nyumba ya Tippu Tip in Mji Mkongwe, Zanzibar.

Vita ya Kongo-Arabu

Wakati akiwa gavana, Vita vya Kongo-Arabu vilianza.

Mwaka 1886, wakati akiwa Zanzibar, mgogoro ulizuka kati ya ngome yake ya Maporomoka ya Stanley na jeshi dogo la "Dola Huru la Kongo" likiongozwa na Kapteni Walter Deane na Luteni Dubois. Wafuasi wa Hamad walidai kuwa Deane aliiba mtumwa wa kike toka kwa ofisa wa Kiarabu. Lakini Deane alidai kuwa mtumwa huyo alikimbia kutokana na kupigwa na mmiliki wake na alimchukua ili kumsaidia. Wafuasi wa Hamad walianzisha mashambulizi dhidi ya ngoma ya Deane. Baada ya siku nne, walinzi wa ngome hiyo waliishiwa na risasi na hivyo wakakimbia.

Kurudi Zanzibar

Mabadiliko ya ukoloni yaliharibu biashara yake akarudi Zanzibar 1890/1891 alipobaki bila misafara mipya hadi kifo chake mwaka 1905.

Hamed amejipatia nafasi katika historia ya Afrika ya Mashariki kwa kuandika tawasifu au kumbukumbu ya maisha yake yeye mwenyewe. Katika lugha ya Kiswahili ni mfano wa kwanza wa tawasifu. Pia ni mfano wa pekee wa kumbukumbu ya kimaandishi ya matokeo ya siku zile zisizoandikwa na Mzungu lakini na mwenyeji. Aliandika kwa lugha ya Kiswahili akitumia mwandiko wa Kiarabu. Mfasiri katika Ukonsuli wa Ujerumani kwenye kisiwa, Heinrich Brode alinakili muswada wake kwa herufi za Kilatini na kuongeza tafsiri ya Kijerumani iliyochapishwa mwana 1902 pale Berlin[5].

Brode alitumia kazi hii kwa kutunga kitabu chake juu ya Hamed kilichochapishwa 1905 na kutafsiriwa kwa Kiingereza kwenye mwaka 1907[6].

Kifo

Hamad alifariki 13 Juni 1905, kutokana na ugonjwa wa malaria nyumbani kwake Mji Mkongwe.

Jina lake linajulikana kama mfano wa mabaya ya biashara ya watumwa iliyoharibu maeneo makubwa huko Kongo kabla ya mwanzo wa ukoloni. Yeye mwenyewe aliona watumwa ni sehemu tu ya biashara yake akitajirika hasa na biashara ya pembe za ndovu.

Marejeo

 1. Hinde 1897, p. 8
 2. Hinde 1897, p. 9
 3. (1972) Tippu Tip and the East African slave trade. Hamilton, 42. Retrieved on 24 November 2017. “For two months Tippu Tip's caravan camped in Chungu's territory and punitive parties were sent out looking for Samu and his men. According to Tippu Tip this was the time he was given his nick-name because guns went 'tiptip, in a manner too terrible to listen to'.” 
 4. Stanley, H. M., 1899, Through the Dark Continent, London: G. Newnes, Vol. One (ISBN 0486256677), Vol. Two (ISBN 0486256685)
 5. Autobiographie des Arabers Schech Hamed bin Muhammed el Murjebi, genannt Tippu Tip. Transscribirt und übersetzt von Dr. II. Brode.Mittheilungen des Seminars für Orientalische Sprachen zu Berlin Dritte Abtheilung, 1902,uk 175 online hapa
 6. Tippoo Tib, The story of his career in Central Africa, narrated from his own accounts by Dr. Heinrich Brode, London, Edward Arnold 1907, online hapa

Vyanzo

 • Bennett, Norman Robert. Arab vs. European: Diplomacy and war in Nineteenth-Century East Central Africa. New York: Africana Publishing Company, 1986.
 • Brode, Heinrich. Tippoo Tib: The Story of His Career in Zanzibar & Central Africa. Translated by H. Havelock with preface by Sir Charles Elliot. London: Arnold, 1907 (Online version).
 • Edgerton, Robert B. (2002). The Troubled Heart of Africa: A History of the Congo. New York: St. Martin's Press. ISBN 0-312-30486-2.
 • Hinde, Sidney Langford (1897). The Fall of the Congo Arabs. 
 • Maisha ya Hamed bin Mohammed el Murjebi yaani Tippu Tip kwa maneno yake mwenyewe, kimefasiriwa na W.H. Whitely (toleo la Kiswahili - Kiingereza), East Africa Literature Bureau 1974
 • (2004) Africa since 1800. Cambridge University Press. ISBN 0-521-83615-8. 
 • Sheriff, Abdul. Slaves, Spices & Ivory in Zanzibar: Integration of an East African Commercial Empire into the World Economy, 1770-1873. London, Nairobi, Tanzania, Athens,OH: James Currey, Heinemann Kenya, Tanzania Publishing House, Ohio University Press, 1987.

Viungo vya nje