Delta
Delta (kutoka jina la herufi ya alfabeti ya Kigiriki) ni mdomo wa mto wenye umbo la kufanana na herufi ya Kigiriki Δ (=delta) sawa na pembetatu.
Kutokea kwa delta ya mto
haririUmbo hili hutokea kama maji ya mto yanabeba matope, mchanga na mashapo mengine hadi mdomo wake baharini au ziwani. Maji ya mto yakiingia baharini hupunguza mwendo wake na nguvu ya kubeba yaliyomo ndani yake. Mashapo yanashuka chini: kwanza sehemu zake nzitonzito kama changarawe, halafu mchanga, halafu udongo. Mashapo hayo yanalala ganda baada ya ganda na kuimarika hadi kuonekana juu ya uwiano wa maji. Sehemu hizo za mashapo yaliyoimarika zinakuwa kama kizuizi kinacholazimisha mto kugawa mwendo wake. Kwa njia hii mikono mbalimbali inatokea. Mimea inaanza kukua kwenye nchi mpya ikiwa mizizi yao inashika na kuimarisha nchi hii.
Mto unaendelea kupeleka mishapo yake mdomoni na kujenga delta yake ndani ya bahari jinsi inavyoonekana kwenye mto Nile ambako delta imetoka nje ya mstari wa pwani.
Ikiwa bahari ina tofauti kubwa kati ya maji kujaa na kupwa mdomoni mwa mto tena bahari haina kina kubwa hutokea mlango wa mto wenye umbo la V (kama faneli) kwa sababu mwendo wa maji kujaa na kupwa unazuia kutelemka na kuimarika kwa mashapo.
Mito mikubwa yenye mdomo wa delta
haririPamoja na mto Nile kuna mito mingi mikubwa yenye mdomo wa delta:
- Afrika kuna delta ya mto Niger katika Nigeria na ya mto Zambezi katika Msumbiji
- Amerika kuna delta za Amazonas (Brazil) na Mississippi (Marekani)
- Asia ina delta kubwa za Tigri-Eufrate (Irak), Indus (Pakistan), Ganga/Brahmaputra (India na Bangladesh), Krishna-Godavari na Kaveri (India), Ayeyarwady (Myanmar), Mekong (Vietnam) na Yangtse (Uchina).
- Ulaya kuna delta kubwa za Rhine (Uholanzi), Rhone (Ufaransa), Danubi (Romania), Ebro (Hispania), Volga na Lena (Urusi)
Delta ya barani
haririWakati mwingine delta inatokea barani pasipo bahari. Kuna hasa aina mbili: ama mto unakwisha barani (hasa kama ni jangwa) au mto unaendelea.
Huko Mali kuna delta ya barani ya mto Niger; mto unajigawa kwa mikono mbalimbali katika eneo kubwa la maziwa na maeneo ya matopematope.
Mto Okavango unakwisha kwenye delta yake katika jangwa la Kalahari (Botswana). Delta hii ni eneo lenye mimea na wanyama wengi katikati ya jangwa kubwa. Delta inavuta watalii wengi kila mwaka.
Makala hii kuhusu eneo fulani bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu eneo hilo kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Je, unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.
|