Gregori Mtendamiujiza
Gregori Mtendamiujiza (au Gregori wa Kaisarea Mpya; 213 hivi – 270 hivi) alikuwa askofu wa karne ya 3 maarufu kwa miujiza mingi aliyoipata kutoka kwa Mungu.
Kati ya waamini waliochangia ustawi wa Kanisa, maaskofu wa Asia Ndogo wanashika nafasi muhimu, na kati yao Gregori ana mahali pa pekee, ingawa tunajua kidogo tu kuhusu uchungaji wake, na maandishi yake kuhusu teolojia yamepotea kwa kiasi kikubwa.[1]
Tangu kale anaheshimiwa na Wakatoliki na Waorthodoksi kama mtakatifu.
Sikukuu yake huadhimishwa tarehe 17 Novemba[2].
Maisha
haririGregori alizaliwa Kaisarea Mpya (makao makuu ya mkoa wa Ponto, leo nchini Uturuki) mwaka 213 hivi.
Hapo awali aliitwa Theodoro ("zawadi ya Mungu"), jina lisilo la Kikristo tu. Familia ilikuwa haijaingia dini hiyo, ambayo yeye alikuja kuifahamu akiwa na umri wa miaka 14, baada ya kufiwa baba yake.
Pamoja na mdogo wake Atenodori alikuwa ametumwa Beirut (leo nchini Lebanon) kwa ajili ya masomo ya sheria; kutoka huko walisafiri hadi Kaisarea ya Palestina. Huko walisikia habari za msomi maarufu Origen, mkuu wa Chuo cha Katekesi cha Aleksandria, aliyekuwa anaishi huko. Udadisi uliwafanya wakamsikilize na kuongea naye; ndipo walipovutiwa sana[1] kiasi cha kusahau kabisa Beirut na sheria.
Gregori alieleza mbinu za mwalimu huyo katika kuongoa watu: unyofu, ari na hoja pamoja.
Gregori alianza masomo ya falsafa aliyoendelea kupendelea hata baada ya kuongeza teolojia, ndiyo sababu alijitahidi kuthibitisha kuwa Ukristo ndio falsafa pekee ya kweli.
Alibaki mwanafunzi wa Origen miaka saba, halafu akarudi Ponto ili kufanya kazi kama mwanasheria, kumbe Fedimo, askofu wa Amasea na askofu mkuu wa Ponto, alimfanya askofu wa Kaisarea, iliyokuwa na waamini 17 tu.
Wakati huo Gregori alikuwa na miaka 40, akaongoza jimbo lake miaka 13, aking'aa kwa ubora wa mafundisho, uadilifu na ari ya kitume.
Inasemekana kwamba alipofariki walikuwa wamebaki watu 17 tu wasio Wakristo. Inawezekana miujiza yake ilichangia mafanikio yake makubwa katika umisionari[3].
Tazama pia
haririTanbihi
hariri- ↑ 1.0 1.1 Leclercq, Henri. "St. Gregory of Neocaesarea." The Catholic Encyclopedia. Vol. 7. New York: Robert Appleton Company, 1910. 26 Jan. 2013
- ↑ Martyrologium Romanum: ex Decreto Sacrosancti oecumenici Concilii Vaticani II instauratum auctoritate Ioannis Pauli P.P. II promulgatum, Romae 2001, ISBN 8820972107
- ↑ https://www.santiebeati.it/dettaglio/78050
Maandishi
hariri- Opera Omnia by Migne, Patrologia Graeca pamoja na faharasa
Marejeo
haririMakala hii bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake? Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari. |