Hernando Cortes

(Elekezwa kutoka Hernán Cortés)

Hernándo (pia: Hernan) Cortés (1485 - 2 Desemba 1547) alikuwa conquistador Mhispania aliyevamia milki ya Azteki na kufanya Mexiko kuwa koloni la Hispania.

Hernando Cortes.

Kuzaliwa na kukulia Hispania

hariri

Cortés alizaliwa mjini Medellín katika mkoa wa Extremadura nchini Hispania kama mwana wa Martín Cortés na Catalina Pizarro Altamirano.

Alianza masomo ya sheria kwenye chuo kikuu cha Salamanca lakini hakumaliza.

Kuhamia Amerika

hariri

Mwaka 1504 alisafiri kwenda koloni jipya kwenye visiwa vya Karibi alipopewa kazi na gavana wa kisiwa cha Hispaniola.

Mwaka 1511 aliongozana na Diego Velázquez de Cuéllar gavana mpya wa Kuba akawa katibu wake akatajirika akisimamia migodi ya dhahabu na mashamba makubwa.

 
Njia ya msafara wa Cortez

Msafara wa kwenda Mexiko

hariri

Mwaka 1518/1519 gavana Velasquez aliandaa msafara wa upelelezi wa Mexiko bara. Hadi wakati ule Wahispania walitawala visiwa kadhaa vya Karibi lakini waliwahi kusikia kuhusu kuwepo kwa dhahabu nyingi barani. Velasquez aliandaa jeshi la Wahispania 670 na jahazi kadhaa akampa Cortez amri ya jeshi hilo. Dakika ya mwisho Velasquez alikuwa na mashaka juu ya Cortez akamtumia barua asiende, lakini Cortez aliamua kuupuza barua hiyo na kuendelea na mipango ya safari.

Cortes kujitegemea

hariri

Tarehe 18 Februari 1519 Cortez aliondoka Havanna kwa jahazi 11. Alikanyaga bara karibu na mdomo wa mto Tabasco na kushinda wenyeji. Wenyeji hao walimpa watumwa 20 na mmojawao alikuwa binti kwa jina la Malinche aliyejua lugha mbalimbali na baadaye alikuwa mfasiri wa Wahispania, pia mpenzi wake Cortez.

Cortes aliunda mji wa Veracruz na kupeleleza pwani ya Mexiko bara. Kwa tendo hilo alitimiza maagizo yake lakini hakutaka kurudi chini ya mamlaka wa gavana wa Kuba. Alijitangaza kuwa na cheo cha kapteni mkuu akakusanya dhahabu iliyopatikana na kuituma Hispania moja kwa moja kwa sababu alitaka kutambuliwa na mfalme wa Hispania kama mkuu wa koloni la pekee. Jahazi zote nyingine zilichomwa moto ili kuzuia watu wake wasiweze kurudi Kuba.

Kuelekea Milki ya Azteki

hariri

Mwezi Agosti 1519 alianza safari ya kwenda Tenochtitlan, mji mkuu wa milki ya Azteki uliokuwepo kwenda nyanda za juu za Mexiko. Njiani alifanya mikataba na makabila na milki ndogo zilizokuwa chini ya Azteki lakini zilikuwa tayari kuasi kwa msaada wa wageni. Hasa mji wa Tlaxcala uliendelea kuwa msaidizi mwaminifu wa Wahispania.

 
Mapigano kati ya Wahispania na Waazteki (mchoro wa Kiazteki)

Teknolojia bora yashinda pamoja na magonjwa

hariri

Mara kadhaa Cortes alipaswa kupigana na makabila na milki hizo lakini Wahispania walishinda kwa sababu silaha zao zilikuwa bora. Wahispania walikuwa na panga za feleji na mavazi ya chuma ya kukinga mwili. Walikuwa pia na aina ya bunduki; hata kama bunduki hizo zilifyatua risasi mojamoja tu, ziliua kwa umbali, tena kwa njia isiyoeleweka na wenyeji. Waindio walikuwa na silaha za ubao na mawe; hawakuanza bado kutumia metali kwa silaha. Kwa njia hiyo Wahispania 400 waliweza kushinda jeshi la watu 100,000. Hasa kikosi la wanajeshi waliopanda farasi kilitisha sana wenyeji kwa sababu Amerika haikujua wala farasi wala watu waliopanda wanyama.

Baadaye magonjwa yalisaidia Wahispania. Waliposhambulia Tenochtitlan mara ya mwisho Mhispania aliugua ndui ugonjwa usiojulikana Amerika hadi wakati ule. Wahispania walikuwa na kinga asilia, wachache tu waliambukizwa kati yao, lakini Waindio walikufa kwa maelfu.

 
Cortes pamoja na Malinche mbele ya wawakilishi wa mfalme Montezuma (Mchoro wa Kiindio)

Kuingia Tenochtitlan

hariri

Mwezi Oktoba 1519 walifika Cholula uliokuwa mji wa pili katika milki ya Azteki. Huko Cortez alichinja wenyeji elfu kadhaa alipohofia wangemshambulia.

Mwishowe mfalme Montezuma aliwakaribisha Wahispania waingie Tenochtitlan. Mji huu ulijengwa kwenye visiwa ndani ya ziwa la Aliwapa makazi mjini na zawadi nyingi za dhahabu akiwatazama kwa nia ya kuwajua vizuri zaidi. Cortez aliona ya kwamba hali ya jeshi lake dogo katika mji huu mkubwa ilikuwa ya hatari akamua kumkamata mfalme Montezuma kama mateka. Kwa jina Montezuma aliendelea kutawala kama mfalme mkuu lakini hali halisi alikuwa mfungwa wa Cortez. Wakubwa Waazteki walikaa kimya kwa sababu walisita kumhatarisha mfalme, ila tu jemadari wa pwani alishambulia Wahispania karibu na mji mpya wa Veracruz. Kwa amri wa Cortez mfalme alimwita huyu jemadari aje Tenochtitlan alipokamatwa na kuuawa na Wahispania.

Ushindi dhidi ya Wahispania kutoka Kuba

hariri

Katika hali hii gavana wa Kuba alituma jeshi la askari Wahispania 1200 kwa shabaha ya kumkamata Cortez. Huyu aliposikia habari hizi aliacha wanajeshi 150 mjini Tenochtitlan kwa maagizo ya kumwangalia mfalme na yeye mwenyewe alielekea pwani na askari 250. Katika shambulio la usiku alifaulu kumkamata mkuu wa jeshi hili akawa mfungwa wake. Wanajeshi wake wengi walijiunga na upande wa Cortez aliyewaahidi windo kubwa hasa dhahabu.

Vita ya Tenochtitlan

hariri

Wakati huohuo makamu wake huko Tenochtitlan alikuwa alishambulia sherehe ya Waazteki katika hekalu moja na kuua watu wengi. Wenyeji wa mji hawakunyamaza tena na kuanza vita dhidi ya Wahispania waliojifunga katika jumba la kifalme. Cortez pamoja na jeshi lake lililoongezeka alirudi kwa mbio lakini Waazteki hawakuwa tayari tena kumsikia Montezuma. Waliendelea kushambulia jumba la kifalme na tar. 1 Julai 1520 Montezuma aliuawa. Cortes aliamua kukimbilia Tlaxcala na katika usiku alifaulu kuondoka Tenochtitlan lakini mamia wa askari zale waliuawa. Njiani aliweza kushinda jeshi kubwa la Waazteki 200,000 na kufika Tlaxcala alipopata nafasi ya kupumzika.

Hapa aliweza kupata wanajeshi wapya kutoka pwani. Wahispania wa Kuba walisikia habari za dhahabu na mamia walifika kwa nia ya kujiunga na Cortez. Aliviringisha Tenochtitlan kwa jeshi lake na kwa msaada wa wasaidizi wake maindio kama Tlaxcala na kuzuia chakula kisifike mjini. Shambulio hili lilidumu siku 80. Watu wa mjini walianza kufa njaa na magonjwa. Wahispania walishambulia tena na tena kwa kutumia bunduki na mizinga. Mji ulichomeka moto polepole na kuharibiwa. Mwishowe mlipuko wa ugonjwa wa ndui uliua watu wengi na kuwadhoofisha zaidi watetezi wa mji. Tar. 13 Agosti 1521 Cuauhtémoc mfalme wa mwisho wa milki ya Azteki alikamatwa alipojaribu kukimbia mji mkuu na hii ilikuwa mwisho wa milki yake.

Imekadiriwa ya kwamba zaidi ya 200,000 Waazteki walikufa wakati wa mfungizo na uvamizi wa Tenochtitlan.

Mtawala wa Mexiko

hariri

Cortes alitambuliwa na Kaisari Carlos V akapewa cheo cha gavana wa "Hispania mpya" akatawala Mexiko akiendelea kupanusha himaya yake. Alijenga Tenochtitlan upya kama "Jiji ya Mexiko". Lakini alikuwa na maadui wengi hasa gavana wa Kuba Velasquez na marafiki zake katika serikali ya Hispania. Cortes alishtakiwa mara kwa mara serikalini na mitume mbalimbali litumwa kumchungulia.

1524 Cortes aliongoza msafara wa Kijeshi katika kusini ya Mexiko na wakati ule makamu wake mjini Mexiko alionyesha unyama dhidi ya wenyji. Hii ilitosha kumpumzisha Cortes. 1528 alisafiri kwenda Hispania kwa nia ya kujitetea mbele ya Carlos V. Aliweza kukanusha mashtaki akapewa cheo cha kiungwana akarudi kama kamanda mkuu wa kijeshi lakini bila madaraka ya kiserikali.

Alipofika 1530 alikuta koloni katika hali ya uasi na fujo akarudisha utaratibu. Akaendelea kufanya misafara ya upelelezi na 1536 alifika kwenye rasi ya Kalifornia.

Kurudi Hispania

hariri

Mwaka 1541 alisafiri tena Hispania akitafuta fidia za pesa alizowahi kutumia kwa misafara yake alizotekeleza kwa niaba ya serikali lakini alishindwa mahakamani.

Aliongozana na Kaisari Carlos V katika vita dhidi ya Waosmani huko Algiers.

Alibaki Hispania akiendelea kufuatalia madai yake dhidi ya serikali lakini majaribio yote yalishindikana. 1547 alipoamua kurudi Mexiko aligonjeka na kuaga dunia huko Hispania 2 Desemba 1547.

Viungo vya Nje

hariri
 
Wikimedia Commons ina media kuhusu: