Historia ya Kuba inahusu eneo ambalo leo linaunda jamhuri ya Kuba.

Koloni la Hispania hariri

Kuba ilikuwa koloni la Hispania kuanzia kufika kwa Kristoforo Kolumbus mwaka 1492 hadi mwaka 1898. Wenyeji asilia walikuwa Waindio lakini wengi wao walikufa haraka kutokana na magonjwa kutoka Ulaya na ukali wa ukoloni wa Wahispania.

Baadaye uchumi wa mashamba makubwa ya sukari ulijengwa kwa nguvu ya watumwa kutoka Afrika.

Kuanzia miaka ya 1860 watu wa Kuba walianza kupinga utawala wa Hispania na pia kudai mwisho wa utumwa. Mnamo 1898 manowari ya Kimarekani SS Maine ililipuka katika bandari ya Havana na tukio hili lilikuwa msingi kwa Marekani kutangaza hali ya vita dhidi ya Hispania. Marekani ilishinda katika Vita vya Marekani dhidi ya Hispania na kutawala kisiwa katika miaka iliyofuata.

Uhuru chini ya usimamizi wa Marekani hariri

Baada ya majadiliano marefu Kuba ilipata uhuru wake kuanzia mwaka 1902 lakini ilipaswa kukubali mkataba uliotunza haki ya Marekani kungilia kati mambo ya ndani na kuipa Marekani eneo kwa kituo cha kijeshi.

Hadi mwaka 1934 Marekani iliingilia mara mbili na kupindua marais wawili wa Kuba, ama kwa kutuma jeshi lake au kwa kutumia wanajeshi wa Kuba. Eneo la Guantanamo Bay kusini mwa Kuba limebaki hadi leo kama kituo cha kijeshi cha Marekani.

Mkataba mpya kati ya Marekani na Kuba wa mwaka 1934 uliongeza haki za Kuba. Wakati huohuo uasi wa kijeshi ulimwingiza sajenti Fulgencio Batista kwenye uwanja wa siasa. Batista alijipandisha cheo hadi kanali akashika mamlaka yote ya kijeshi na kuteua marais waliotekeleza matakwa yake.

Mwaka 1940 alichaguliwa mwenyewe kuwa rais, akarudi 1952 kwa kugombea tena urais lakini, baada ya kuona angeshindwa, alipindua serikali kwa njia ya uasi wa kijeshi akasimamisha katiba na kuwa dikteta wa Kuba hadi mwaka 1959. Chini ya serikali ya Batista ulaji rushwa na athira ya kiuchumi ya makampuni ya Kimarekani viliongezwa. Ukali wa utawala na mauaji ya wapinzani wengi vilisababisha kutokea kwa vikundi vilivyokuwa tayari kupinga serikali ya dikteta kwa silaha.

Mapinduzi ya 1959 hariri

 
Fidel Castro, kiongozi wa mapinduzi na wa nchi kwa miaka 49.

Tangu mwaka 1953 mwanasheria Fidel Castro alijaribu kukusanya wafuasi kwa mapinduzi akishambulia kituo cha kijeshi cha Moncada akakamatwa na kutupwa jela.

Mwaka 1955 wafungwa walisamehewa na Batista. Castro alianza tena kukusanya wafuasi waliobaki katika "Harakati ya 26 Julai" (MR-26-7). Maandamano ya upinzani yalifuatwa na polisi kukamata wanaharakati. Fidel Castor pamoja na nduguye Raul walikimbia Meksiko. Hapo alikutana na tabibu Mwargentina Che Guevara.

Mwaka 1956 Castro pamoja na Guevara na wafuasi 80 walivuka bahari kwa jahazi "Granma" wakajificha katika milima ya Sierra Madre. Kutoka huko walianza kushambulia vikosi vya jeshi la Batista.

Polepole idadi ya wapiganaji waliojiunga nao iliongezeka na wanajeshi wa serikali mara nyingi walihamia upande wa Castro. Tarehe 1 Januari 1959 dikteta Batista alikimbia na kuondoka Kuba, vikosi wa wanamapinduzi waliingia Havana.

Baada ya mapinduzi hariri

Mwanzoni Castro alionekana kama msemaji mkuu wa mapinduzi akimtangaza mwanasheria Manuel Urrutia kama rais mpya. Fidel alichukua cheo cha waziri mkuu katika Februari 1959.

Hapo mwanzoni serikali mpya ilikuwa muungano wa wapinzani wa udikteta na wanamgambo kutoka milimani. Uchaguzi wa vyama vingi ulitangazwa kama shabaha mojawapo ya kurudisha demokrasia. Katika miezi iliyofuata wanasiasa wenye mwelekeo wa kati waliondolewa polepole na Castro aliongeza idadi ya Wamarxisti katika vyeo vya juu.

Kuanzia 1960 na baada ya jaribio la Marekani kumpindua Castro huyu aliongeza mwelekeo wake wa kisoshalisti. Baada ya kupingwa na Marekani, Castro alitafuta ushirikiano na usaidizi kutoka Urusi wa kikomunisti.

Castro alitangaza siasa ya kikomunisti akaendelea kutawala bila uchaguzi huru hadi alipojiuzulu mnamo Februari 2008 kwa sababu za afya. Baada yake aliongoza mdogo wake, Raul Castro, hadi mwaka 2018 Miguel Díaz-Canel alipochaguliwa kuwa rais wa nchi.

Tanbihi hariri

  Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Historia ya Kuba kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.