Kumfuasa Yesu Kristo

Kumfuasa Yesu Kristo ni kitabu maarufu katika Ukristo kilichoandikwa na Thomas wa Kempis miaka 1418-1427 hivi[1] kwa kufuata mfumo wa kiroho wa Devotio Moderna[2].

Maandishi asili: De Imitatione Christi. Koninklijke Bibliotheek, Brussel, Ubelgiji.

Labda ndicho kitabu kinachosomwa zaidi na Wakristo tangu kilichotungwa, baada ya Biblia tu[3][4][5]. Kufikia mwaka 1650 kilikuwa kimechapwa tayari mara 745 katika tafsiri mbalimbali[6][7].

Kutoka lugha asili ya Kilatini (De Imitatione Christi) kiliwahi kutafsiriwa na Waanglikana kwa Kiswahili na hadi leo kinasomwa na waumini wengi wa madhehebu mbalimbali.

Hicho si kitabu cha teolojia, bali maisha halisi ambayo mtu aliyevutiwa na ukamilifu aliyaandika siku kwa siku kutokana na sala yake, pengine ya shida, pengine ya mwanga na utamu wa kimbingu. “Kina uzuri na nguvu ambavyo vinagusa na kutikisa na kuvutia sana mioyo dhaifu, isiyojali na hata isiyo na imani. Lakini walengwa asili si wakosefu, wala wanaoanza; kinadai wasomaji wawe wameendelea kiasi fulani katika uadilifu. Kinachotaka si kidogo, bali ni kutuinua tuzame katika mafumbo na kupata faraja za ndani za maisha ya muungano. Kwa kweli kuzama katika sala na kuungana kwa ndani na Mungu ndiko shabaha, lengo na haja ya dhati ya roho yetu, inayoweza kuona amani na pumziko ndani ya Mungu tu. Ndiyo sababu kila anayekisoma, hata akikosa kabisa ukamilifu na kukielewa kidogo tu, anaonja utamu wenye faraja asioweza kujielezea: kwa kuwa kinadokeza hiyo amani na hilo pumziko na kuelekeza roho iungane na wema mkuu” (pd. Dumas).

Kumfuasa Yesu Kristo kinalenga mafumbo

hariri

Ujuzi wa kifumbo wa Mungu ni ule unaopatikana kwa kuzingatia mambo si kwa akili, wala kwa imani tupu, bali kwa uvuvio maalumu wa Roho Mtakatifu katika sala ya kumiminiwa. “Ni ujuzi wa Mungu ambao unakaribia kuwa mang’amuzi” (Thoma wa Akwino) “Unatokana na athari ya Mungu ambayo inaifundisha roho kwa siri na kwa ukamilifu wa upendo, yenyewe isielewe hata ni kitu gani” (Yohane wa Msalaba).

“Kumfuasa Yesu Kristo” hakikomi kuhimiza unyenyekevu, kujikana na usikivu, ambavyo vinaandaa kumiminiwa sala hiyo na kuungana na Mungu: “Nimechoka kusoma na kusikia mengi mara kwa mara. Kwako napata yote ambayo nayatamani na kuyapenda. Wataalamu wote wanyamaze; viumbe vyote vikae kimya mbele yako. Wewe peke yako unifundishe! Kama mtu amezoea kujikusanya kwa ndani na kuwa mnyofu, ataelewa mambo mengi makuu pasipo shida; kwa sababu akili yake inaangazwa na mwanga wa juu” (I,3:1-3).

“Mtu gani ni huru kuliko asiye na tamaa duniani? Kwa hiyo ni lazima nipae juu ya viumbe vyote, na kujiachilia kabisa, niangalie mambo ya Mungu na kufahamu kwamba wewe Muumba hufanani na kiumbe chochote… Elimu ya mtu aliyejifunza kwa kazi yake ni tofauti sana na hekima ambayo mtu amepewa na Mungu katika sala. Hekima hiyo imetoka juu; ndiyo kazi ya mwangazo wa Mungu; ni bora sana kuliko elimu iliyopatikana kwa mtu kujisumbua akili yake. Wapo wengi wanaotamani miangazo ya roho, lakini hawapendi kujitendea yaliyopaswa kwa hali hiyo. Watu hao huzuiwa sana, kwa sababu hupenda mambo ya ajabu na kusikia utamu, bila kujitesa na kujikana barabara” (III,31:1-3).

Mbele Bwana anasema, “Ndimi ninayemuelimisha mnyenyekevu kwa dakika moja tu ajue ukweli wa milele vema sana, kuliko kwa kufundishwa na mwalimu mwingine miaka kumi. Mimi nafundisha bila mshindo wa maneno, bila kubishana kwa fujo, bila kutafuta sifa, bila kushindana. Ndimi nifundishaye kudharau malimwengu na kutupa furaha za sasa, kutaka mambo ya milele na kuyapenda, kuepa sifa za watu, kuvumilia dharau, kunitumikia mimi, kunipenda mimi peke yangu kwa moyo wote na kutotaka kitu ila mimi tu” (III,43:2). Sala ya kumiminiwa inayozungumziwa na kitabu hicho ni neema ya juu, lakini imo katika njia ya kawaida ya utakatifu; inatangazwa kuwa ya kutamaniwa kuliko yote: “Ndiyo niombayo, ndiyo nipendayo: tuungane kabisa sisi… nijifunze kuonja mambo ya mbinguni na ya milele… Ee Bwana Mungu, siku gani nitaungana nawe kabisa kama kuzama ndani mwako hata kujisahau? Wewe ndani mwangu, mimi ndani mwako; nipe tukae hivi sikuzote” (IV,13:1).

Masharti, yaani juhudi zinazodaiwa

hariri

Kwa ajili hiyo, kitabu hicho kinadai hasa kujikana na unyenyekevu: “Ujifunze kuzivunja nia zako, ukakubali kutumikia kwa kila namna. Piga vita motomoto upate kujishinda, wala usikubali jipu la majivuno kuvimba rohoni mwako. Ujifanye mdogo na mnyenyekevu mpaka watu wote waweze kutembea juu yako wakukanyage kama takataka ya njiani” (III,13:2-3). Kujikana hivyo ni kufisha umimi ili kuwa mali ya Mungu, ni kutojifanya tena lengo la yote ili kumlenga yeye mfululizo. “Mwanangu, ukitaka kupewa yote, ni sharti utoe yote bila kubakiza chochote kiwe mali yako” (III,27:1): hapo utapata amani ya ndani.

Usafi wa moyo na nia nyofu inayomlenga Mungu tu vinamuandaa mtu kumiminiwa sala inayomfanya ajiaminishe kwake na kuungana naye: “Naomba huruma yako hata unijalie neema moja iliyo bora, yaani moyo wangu mgumu ulainike kabisa mbele yako, nijae upendo wako nisijitafutie tena kitulizo chochote kwingine” (IV,4:2). Hapo tunaelewa matokeo mazuri ajabu ya upendo wa Mungu ambao “huchukua mzigo pasipo kuona uzito, hugeuza machungu yote kuwa matamu na mazuri… huelekeza kutenda makubwa, na kutamani makubwa zaidi… Hakuna kitamu kushinda upendo, wala chenye nguvu, wala cha ubora, wala kikubwa, wala kipendevu, wala kamili, wala kitimilifu duniani na mbinguni ila upendo tu. Upendo unatoka kwa Mungu, hauwezi kutulia isipokuwa kwa Mungu peke yake” (III,5:3). Kwa mtu aliyebandukana na yote na asiyejifanya tena lengo la chochote, muungano ndio tunda la kuzama katika wema mkuu.

Hivyo “Kumfuasa Yesu Kristo” kinaelekeza si kufanya juhudi tu, bali pia kuzama katika mafumbo, yaani kutimiza maadili ili kujaliwa muungano na Bwana. Maneno yake juu ya kuzama katika wema wa Mungu yanawafaa wote, mradi wakubali kufuata njia ya unyenyekevu, ya kujikana, ya kusali mfululizo na ya kuwa wasikivu kwa Roho Mtakatifu.


Tanbihi

hariri
  1. An introductory dictionary of theology and religious studies by Orlando O. Espín, James B. Nickoloff 2007 ISBN 0-8146-5856-3 page 609
  2. John H. Van Engen (1988). Devotio Moderna. Paulist Press. ku. 7–12. ISBN 978-0-8091-2962-1.
  3. Miola 2007, p. 285
  4. Catholic encyclopedia: Imitation of Christ
  5. Keen 2004, p. 175
  6. von Habsburg, Maximilian (2011). Catholic and Protestant Translations of the Imitatio Christi, 1425-1650: from Late Medieval Classic to Early Modern Bestseller. Ashgate. ISBN 9780754667650.
  7. A Journey Through Christian Theology by William P Anderson and Richard L. Diesslin 2000 ISBN 0-8006-3220-6 page 98

Marejeo

hariri

Viungo vya nje

hariri
 
Wikiquote ina mkusanyiko wa dondoo kuhusu:
  Makala hii kuhusu kitabu fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Kumfuasa Yesu Kristo kama Mwandishi wake, hadithi au matoleo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.