Chuchunge

(Elekezwa kutoka Msusa)
Chuchunge
Chuchunge mabaka-meusi (Hemiramphus far)
Chuchunge mabaka-meusi (Hemiramphus far)
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Chordata (Wanyama wenye ugwe wa neva mgongoni)
Nusufaila: Vertebrata (Wanyama wenye uti wa mgongo)
Ngeli: Actinopterygii (Samaki walio na mapezi yenye tindi)
Oda: Beloniformes (Samaki kama ngarara)
Familia: Hemiramphidae (Samaki walio na mnasaba na chuchunge)
T.N. Gill, 1859
Ngazi za chini

Jenasi 8 na spishi 60, 18 katika Afrika:

Chuchunge, chuchungi, vidau, viroho, makule, mikeke au misusa ni samaki wa baharini wa familia Hemiramphidae katika oda Beloniformes ambao taya la chini ni refu zaidi sana kuliko taya la juu (isipokuwa katika spishi za jenasi Chriodorus na Oxyporhamphus).

Wanatokea katika maji vuguvugu ya dunia na huogelea karibu na uso wa maji. Huishi baharini hasa lakini spishi kadhaa hukaa katika mito na milango yao. Ingawa sio muhimu sana kwa biashara, samaki hawa wa malisho husaidia uvuvi wa mafundi na masoko ya kienyeji duniani kote. Pia huliwa na samaki wengine mbuai wenye thamani ya biashara, kama vile sulisuli, nguru na papa.

Mofolojia

hariri

Chuchunge ni samaki waliorefuka na kunyooshwa na waliotoholewa ili kuishi katika maji ya wazi. Wanaweza kukua hadi urefu sanifu (yaani bila pezimkia) wa zaidi ya sm 40 katika kisa cha chuchunge mwembamba. Magamba ni makubwa kiasi yenye umbo la duaradufu laini na hutolewa kwa urahisi. Hakuna miiba katika mapezi. Sifa ya kutofautisha ni kwamba jozi ya tatu ya mifupa ya juu ya koromeo imeungana katika kombe. Chuchunge ni moja ya familia kadhaa za samaki ambazo hukosa tumbo, na zote zina kifaa cha mataya ya koromeo (kinu cha koromeo). Takriban spishi zote zina taya la chini lililorefuka, angalau wakiwa wachanga, ingawa kipengele hiki kinaweza kupotea wakati samaki wanapokomaa, kwa mfano katika jenasi Chriodorus.

Kama ilivyo kawaida kwa samaki wa maji wazi wanaoishi karibu na uso wa maji, takriban spishi zote zina rangi ya fedha, nyeusi zaidi juu na nyeupe zaidi chini, mfano wa kivuli cha kinyume. Ncha ya taya la chini lina rangi inayong'aa ya nyekundu au machungwa katika spishi nyingi.

Chuchunge huwa na mabadiliko kadhaa ili kujilisha kwenye uso wa maji. Macho na pua ni juu ya kichwa na taya la juu ni sabili, lakini taya la chini siyo. Pamoja na umbo lao lililonyooshwa na mkusanyiko wa mapezi kuelekea nyuma, mabadiliko haya yanaruhusu chuchunge ili kujasisi, kukamata na kumeza chakula kwa ufanisi.

Msambao na makazi

hariri

Chuchunge huishi bahari vuguvugu, hasa karibu na uso, katika bahari za Atlantiki, Hindi na Pasifiki. Idadi ndogo hupatikana katika milango ya mito. Takriban spishi zote za chuchunge wa baharini zinajulikana kutoka kwenye pwani za bara, lakini baadhi huenea katika Pasifiki ya Magharibi na Katikati, na spishi moja ni ya kienyeji katika Nyuzilandi. Hemiramphus ni jenasi ya bahari za dunia yote.

Ekolojia na mwenendo

hariri

Kujilisha

hariri

Chuchunge wa baharini hula kitu chochote na kujilisha kwa miani, mimea ya baharini kama vile nyasi-bahari, planktoni, invertebrata, kama vile vipepeo-bahari na gegereka, na samaki wadogo. Angalau katika kisa cha spishi fulani za kinusutropiki wachanga ni wa mbuai zaidi kuliko wapevu. Baadhi ya spishi za kitropiki hujilisha kwa wanyama wakati wa mchana na kwa mimea wakati wa usiku, lakini spishi nyingine zinabadilishana kati ya ugwizi majira ya joto na ukulamimea majira ya baridi. Kwa zamu yao huliwa na samaki wengi muhimu kwa ekolojia na kwa biashara, kama vile sulisuli, nguru na papa, na hivyo ni kiungo kikuu kati ya viwango-trofia.

Mwenendo

hariri

Chuchunge wa baharini kwa kawaida ni samaki wa makundi wanaojilisha karibu na uso wa maji. Kwa mfano chuchunge wa bahari ya kusini Hyporhamphus melanochir hupatikana katika ghuba tulivu, bahari za kipwani na milango ya mito yaliyozunguka Australia ya kusini katika maji hadi kina cha m 20. Spishi hii huunda makundi karibu na uso wa maji usiku lakini kuogelea karibu zaidi na sakafu ya bahari wakati wa mchana, hasa kati ya nyanja za nyasi-bahari.

Chuchunge ni watungishaji kwa nje. Kwa kawaida hutaga mayai na mara nyingi wananazalisha idadi ndogo ya mayai makubwa kuliko samaki wengine wa ukubwa wao, kwa kawaida katika maji ya kipwani ya kina kidogo, kama vile nyanja za nyasi-bahari. Mayai mengi yana kipenyo cha mm 1.5-2.5 na yana nyuzi za kujiambata. Yanatoa lava wakati yalipokua hadi kipenyo cha mm 4.8-11.

Tunajua kidogo kiasi kuhusu ekolojia ya chuchunge wachanga wa baharini, ingawa makazi ya milango ya mito yanaonekana kuwa yanapendelewa na angalau spishi kadhaa. Wanakua kwa kasi katika miaka ya kwanza na baadaye ukuaji unapungua.

Chuchunge sio lengo kubwa la uvuvi wa kibiashara, ingawa uvuvi mdogo upo mahali kadhaa, kwa mfano kuambaza pwani ya Afrika ya Mashariki. Chuchunge hukamatwa kwa njia mbalimbali zinazojumuisha majuya, majarife ya karibu na uso, nyavu za mkononi chini ya taa usiku, na nyavu za kukokota. Hutumiwa wabichi, wakavu, waliokaushwa kwa moshi au waliotiliwa chumvi, na huchukuliwa kama chakula kizuri. Hata hivyo, hata mahali ambapo chuchunge wanalengwa na uvuvi, huwa na umuhimu wa sekondari wakilinganishwa na spishi nyingine za kulika za samaki.

Spishi za Afrika

hariri

Marejeo

hariri
  • Rashid Anam & Edoardo Mostarda (2012) Field identification guide for the living marine resources of Kenya. FAO, Rome.
  • Gabriella Bianchi (1985) Field guide to the commercial marine brackish-water species of Tanzania. FAO, Rome.

Viungo vya nje

hariri