Nabii Isaya

Nabii Isaya (kwa Kiyahudi יְשַׁעְיָהוּ, yaani "YHWH anaokoa"), kuhani wa Yerusalemu mwenye elimu nzuri, alizaliwa katika Ufalme wa Yuda mwaka 765 KK hivi, akatabiri kwa muda usiopungua miaka 40 akiingilia kati matukio yote ya siasa, ambayo yalikuwa ya kutisha kutokana na nguvu za Waashuru ambao waliangamiza Israeli na kukaribia kufuta hata ufalme wa Kusini.

Nabii Isaya alivyochorwa mwaka 1904 hivi.

Maandishi yake yanapendeza kuliko yote ya Agano la Kale, hasa upande wa ushairi. Lakini ukuu wa Isaya uko hasa upande wa imani.

Tangu kale huheshimiwa kama mtakatifu.

Sikukuu yake huadhimishwa tarehe 9 Mei[1][2].

Unabii wakeEdit

Kuanzia wito wake alioupata hekaluni, alipong’amua kwamba Mungu ni mtakatifu kabisa, yaani tofauti mno na yeyote na chochote (6), alitawaliwa na wazo la utukufu wa Mungu na la unyonge wa binadamu anayehitaji kutakaswa naye. Kwa msingi huo alidai wafalme na wananchi wote wa Yuda wamtegemee Mungu tu, si mataifa yenye nguvu, hata upande wa siasa na mbele ya hatari kubwa namna gani.

Lakini toka mwanzo aliambiwa hatasikilizwa, hivyo ikambidi atabiri adhabu. Kweli hali haikuwa shwari, ndiyo sababu wengi walishindwa kuamini na kutulia, wakaendelea kujifanyia mipango na kutafuta msaada kutoka kwa binadamu, hasa Farao wa Misri. Hapo Mungu alimuagiza Isaya atembee uchi mwaka mmoja unusu ili kudokeza kuwa Wamisri watafanywa watumwa wa Waashuru wasiweze kusaidia kitu (20:1-6).

Katika kutuliza watu alimtabiria mfalme Ahazi kwamba mwanamwali atamzaa mtoto wa kiume atakayethibitisha uwepo wa Mungu pamoja na watu wake, jina lake Emanueli linavyomaanisha. (7:1-17) Kweli mke wa Ahazi alimzaa Hezekia atakayeendeleza ufalme wa ukoo wa Daudi, lakini utabiri huo ulimlenga zaidi Yesu, mwana wa Bikira (walivyoelewa watafsiri wa kwanza wa Biblia katika Kigiriki) ambaye kweli ni Mungu pamoja nasi, na ni mwana wa Daudi ambaye atatawala milele kwa amani na haki (11:1-9).

Hivyo, pamoja na adhabu kwa utovu wao wa imani (22:1-14), Isaya aliwatabiria watu wa Yuda kuwa Mungu hataangamiza kabisa taifa lake, bali ataacha mabaki yake ambayo yataleta wokovu (10:20-23): katika mabaki hayo Bikira atamzaa Masiya ambaye ni Mungu pamoja nasi, mwana wa Daudi ambaye ataleta amani na haki duniani.

Nafasi ya mwisho kwa Isaya kutuliza watu ilikuwa mwaka 701 K.K. ambapo jeshi kubwa la Waashuru lilizingira Yerusalemu na kutamka maneno ya kumkufuru Mungu. Isaya aliwarudishia jibu la dharau, nao kweli wakakimbia haraka baada ya kupatwa na tauni.

Isaya ni maarufu pia kwa ubora wa mashairi yake yaliyofanya ujumbe wake upendeze na uguse zaidi. Kwa sababu hiyo wengi walipenda kuyakariri na kuyasoma na hata kuiga mtindo wake: ndiyo maana kitabu chake kiliongezewa maandishi mengine mengi mpaka miaka mingi baada ya mwenyewe kuuawa kwa kukatwa kwa msumeno.

Tazama piaEdit

TanbihiEdit

  1. Martyrologium Romanum: ex Decreto Sacrosancti oecumenici Concilii Vaticani II instauratum auctoritate Ioannis Pauli P.P. II promulgatum, Romae 2001, ISBN 8820972107
  2. https://catholicsaints.info/isaiah-the-prophet/

MarejeoEdit

Viungo vya njeEdit

Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Wikiquote ina mkusanyiko wa dondoo kuhusu:
  Makala hii kuhusu mtu wa Biblia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Nabii Isaya kama habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.