Ukuta wa Berlin (kwa Kijerumani Berliner Mauer) ulitenganisha sehemu mbili za jiji la Berlin (Ujerumani) kuanzia 13 Agosti 1961 hadi 9 Novemba 1989. Ukuta huo ulikuwa na urefu wa kilomita 45.3 ukiwa sehemu ya mpaka kati ya madola mawili ya Ujerumani yaliyokuwepo kuanzia 1949 hadi 1990. Ukuta wa Berlin ulikuwa mfano uliojulikana zaidi wa "pazia la chuma" katika Ulaya lililotenganisha nchi za kikomunisti za Ulaya mashariki na nchi za Ulaya magharibi. Takriban watu 200 waliuawa walipojaribu kuvuka ukuta kutoka mashariki kwenda magharibi.

Ukuta wa Berlin mnamo mwaka 1980
upande wa kushoto: Berlin Mashariki (angalia kanda la mauti mbele ya ukuta wamapopita askari; hapo walinzi walipaswa kumfyatulia risasi kila mtu aliyeingia);
upande wa kulia: Berlin Magharibi ambako ukuta ulichorwa picha na vijana
Eneo la Berlin Magharibi lilikuwa kama kisiwa ndani ya Ujerumani Mashariki

Utangulizi: Ugawanywaji wa jiji la Berlin

hariri

Chanzo cha ukuta kilikuwa ugawanywaji wa jiji la Berlin baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia tangu 1945. Nchi washindi ziliamua kuigawa Ujerumani yote. Wakaanzisha kanda nne zilizotawaliwa na Umoja wa Kisovyeti, Marekani, Uingereza na Ufaransa. Jiji la Berlin lilikuwa ndani ya kanda ya Kisovyeti lakini likiwa mji mkuu wa Ujerumani, lilitangazwa kuwa mkoa wa pekee likigawanywa pia katika kanda nne za washindi. Mashariki ya Berlin ilikuwa sehemu ya nchi ya kikomunisti Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ujerumani na magharibi ya jiji ilikuwa chini ya mamlaka ya Marekani, Uingereza na Ufaransa.

Tangu mwaka 1946 washindi walianza kutoelewana, na kipindi cha vita baridi kilianza ambako nchi za magharibi (Marekani, Uingereza, Ufaransa) zilisimama dhidi ya nchi za mashariki zilizoongozwa na Umoja wa Kisovyeti.

Migongano ya kimasilahi ya pande hizi mbili ilisababisha kutokea kwa madola mawili ndani ya Ujerumani, moja chini ya uangalizi wa nchi za magharibi (Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani) na nyingine chini ya usimamizi wa Kisovyeti (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kijerumani). Berlin ya Mashariki iliunganishwa na Ujerumani ya Mashariki ikawa mji mkuu wake. Berlin ya Magharibi iliendelea kama mkoa wa pekee chini ya usimamizi wa nchi washindi wa vita ikawa kama kisiwa ndani ya Ujerumani ya Mashariki.

Mwaka 1948/49 Wasovyeti walijaribu kuondoa nchi za magharibi katika Berlin kwa kuzuia umeme, maji na usafirishaji wa vyakula na bidhaa kwa jumla kuingia Berlin Magharibi. Nchi za magharibi walilisha wakazi wa mji kwa njia ya ndege ("daraja la angani") hadi Wasovyeti walipoondoa vizuizi.

Wakimbizi kwenda magharibi

hariri

Kwenye sehemu ya mashariki Wasovyeti waliweka serikali ya kikomunisti iliyoanzisha mfumo wa kiimla chini ya uongozi wa chama cha kikomunisti. Katika miaka ya 1950 hali ya uchumi na maisha ya wananchi ilianza kusogea mbele baada ya uharibifu wa vita lakini upande wa magharibi uchumi uliendelea haraka kuliko upande wa mashariki.

Mfumo wa siasa ya imla, ukandamizaji wa makanisa, utaifishaji wa makampuni ya binafsi na kubaki nyuma kiuchumi vilisababisha kuondoka kwa watu wengi waliohamia magharibi walipopokewa kama raia kamili. Serikali ya Ujerumani ya Mashariki ilianza kujenga uzio mpakani na magharibi ikaweka walinzi wenye silaha walioambiwa kufyatulia risasi kama watu watajaribu kuvuka uzio wa mpakani.

Lakini Berlin bado ilikuwa mji mmoja. Mpaka kati ya kanda za mbili kisiasa haukuwa na vizuizi na mara nyingi ulikuwepo katikati ya barabara fulani, hivyo haikuwezekana kuzuia watu kupita jinsi walivyozoea.

Harakati ya kuondoka kwa watu wengi ilileta matatizo makali kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kijerumani iliyokosa wafanyakazi kwa uchumi wake. Hadi 1960 zaidi ya watu milioni 2 katika jumla ya milioni 19 waliondoka mashariki kuhamia magharibi. Baada ya kujengwa kwa uzio ya mpakani wakimbizi wengi walipitia Berlin penye nafasi rahisi ya kuhamia magharibi. Hapa walipokewa katika makambi na kuhamishwa Ujerumani ya Magharibi kwa njia ya ndege maana barabara zote zilipita katika eneo la Ujerumani ya Mashariki.

Ujenzi wa ukuta wa Berlin

hariri

Mwaka 1961 serikali ya Mashariki iliona ni lazima kuzuia wakimbizi wengi kwenda Berlin Magharibi. Hapo walikata shauri la kutenganisha sehemu mbili za jiji kwa njia ya ukuta na fensi. Walipata kibali cha uongozi wa Umoja wa Kisovyeti wakaandaa akiba za matofali, saruji na waya ya miiba.

Usiku wa tarehe 12 kwenda 13 Agosti 1961 wanajeshi na polisi elfu kadhaa walitumwa kusimama mpakani mjini Berlin walipoangalia wafanyakazi walioanza kujenga ukuta na kufunga mpaka ndani ya jiji. Madirisha na milango ya nyumba zilizokaa mpakani moja kwa moja yalifungwa pia na wakazi walipaswa kutumia milango ya nyuma. Usafiri kwa mabasi na treni kati ya pande mbili za jiji ukasimamishwa vilevile.

Ukuta uliendelea kujengwa hata sehemu za nje ya Berlin ya Magharibi ambako jiji linakutana na mashamba ama kwa kujenga uzio mkubwa au ukuta pia.

Muundo wa ukuta

hariri
 
Onyo la mpakani

Tangu kuanzishwa mwaka 1961 hadi mwisho wake mwaka 1989 ukuta uliendelea kuboreshwa na kupanuliwa. Nyumba zilizosimama zikabomolewa polepole na wakazi wakahamishwa.

Penye nafasi uzio au ukuta wa pili iliongezeka kwa kusudi la kuzuia watu wasikaribie mno. Lakini upande wa magharibi watu walikuwa huru kufika ukutani na baada ya miaka kadhaa vijana na wasanii wa magharibi walitumia ukuta kwa kuchora picha kwa hiari yao.

Sehemu za ukuta wa Berlin
kufuatana na wizara ya usalama wa dola wa JKU mwaka 1989[1][2]
Urefu (km) Aina ya kizuizi
156,4 Vizuizi vya kuzunguku Berlin Magharibi vyenye kimo kati ya mita 3.40 und 4.20 m
111,9 Kuta za saruji au jiwe
44,5 Uzio wa
43,7 Vizuizi vya mpakani ndani ya jiji kati ya Berlin Mashariki na Magharibi)
0,5 Mabaki ya kuta za nyumba
124,3 Barabara ya kijeshi kando la ukuta
Idadi majengo
186 Minara ya walinzi (jumla 302 zilizozunguka Berlin Magharibi)
259 vituo vya mbwa walioshikwa na waya
20 vituo vya walinzi chini ya ardhi

Mpaka uliozunguka Berlin Magharibi ulikuwa na urefu wa 17 km jumla; 45 km kati ya hizi zilikuwa ndani ya jiji lenyewe za kutenganisha pande mbili za jiji.

Jeshi la ulinzi wa mpaka lilikuwa na askari 11,500 kwa ajili ya mpaka wa Berlin pekee; kila wakati askari 2,500 walikuwa na zamu ya kulinda mpaka wa Berlin pekee.

Wanajeshi walikuwa na amri kumzuia yeyote aliyejaribu kukaribia na kupanda ukuta au fensi ya mpakani. Waliambiwa kutumia silaha kama kizuizi cha mwisho.

Picha za ukuta

hariri

Tanbihi

hariri

Viungo vya nje

hariri
 
WikiMedia Commons
Wikimedia Commons ina media kuhusu: