YHWH (yaani, “Mimi Ndimi”) ni herufi nne ambazo kwa Kiebrania zinaandikwa יהוה. Ni konsonanti zinazounda jina la Mungu lililo muhimu kuliko yote linalopatikana mara 6,828 hivi katika Biblia ya Kiebrania kuanzia Mwa 2:4.

Jina YHWH kwa alfabeti ya Kiebrania cha zamani (karne ya 10 KK hadi 135 BK), ya Kiaramu cha zamani (karne ya 10 KK hadi karne ya 4 BK) na ya mraba (karne ya 3 hadi sasa).

Jina hilo halipatikani kabisa katika vitabu vya Wimbo Ulio Bora, Kitabu cha Mhubiri na Kitabu cha Esta.

Matumizi katika Uyahudi hariri

Wayahudi walizidi kuliheshimu jina hilo hata wakaacha kulitamka wakati wa kulikuta katika Maandiko Matakatifu; badala yake walitumia neno mbadala, mara nyingi אֲדֹנָי, Adonai, yaani Bwana.

Kwa sababu hiyo watafsiri wa kwanza wa Biblia kwenda lugha ya Kigiriki (LXX) walilitafsiri jina "יהוה" kwa neno Κύριος, kirios, yaani Bwana.

Kwa kuzoea hivyo, katika kutoa madondoo ya Agano la Kale, Wakristo wa kwanza walitumia tafsiri hiyohiyo.

Katika Agano Jipya hariri

Ndiyo sababu, katika Agano Jipya jina hilo halipatikani, isipokuwa kifupi kama Yah, hasa katika shangilio la Kiebrania Aleluya, yaani Msifuni Bwana. Pia Yesu alifunua Umungu wake kwa kujisemea, “Mimi Ndimi” na kwa kukubali kuitwa, “Bwana”.

Pamoja na hayo, alisali na kufundisha kusali kwa kumuelekea “Aba” yaani, “Baba”. Ndilo jina ambalo linampendeza zaidi na kutuingiza katika fumbo lake kama wana ndani ya Mwana pekee ambaye “Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba” (Fil 2:9-11). “Msalipo, semeni, ‘Baba, jina lako litakaswe’” (Lk 11:2). “Mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, ‘Aba!’ yaani, ‘Baba!’” (Rom 8:15).

Pamoja na hayo tena, Yesu aliposulubiwa, Ponsio Pilato, liwali wa Palestina, aliamua apewe adhabu ya kifo kulingana na shtaka la viongozi wa Wayahudi waliodai mtuhumiwa huyo alijitangaza kuwa mfalme na kupinga mamlaka ya Kaisari wa Dola la Roma, kwa wakati huo Tiberius, ingawa Pilato alikuwa ametambua shtaka halikuwa la kweli, bali lilitokana na husuda.

Kadiri ya Injili ya Yohane (19:19-22), Pilato mwenyewe alisisitiza kwamba, katika maandishi yaliyotakiwa kuwajulisha watu sababu ya adhabu hiyo, iwekwe wazi kwamba Yesu aliuawa kama mfalme wa Wayahudi, ingawa neno hilo lilichukiza viongozi wa taifa.

Maneno ya ilani hiyo yaliandikwa katika lugha tatu:

  • Kilatini (Iesus Nazarenus Rex Iudaeorum),
  • Kigiriki (Ἰησοῦς ὁ Ναζωραῖος ὁ Bασιλεὺς τῶν Ἰουδαίω). Kutokana na herufi hizo, Wagiriki wanaandikwa INBI.
  • Kiebrania (ישוע הנוצרי ומלך היהודים). Kumbe, herufi za kwanza za maneno hayo kwa Kiebrania ni יהוה, YHWH, na ni kama kwamba zinamtangaza Yesu kuwa Mungu.

Herufi zenyewe hariri

 
Ukuta wa mbele wa Basilika la Mt. Louis, lililojengwa mwaka 1834 huko St. Louis, Missouri, una jina hilo upande wa juu.

Herufi hizo nne, zikisomwa kutoka kulia kwenda kushoto ni:

Kiebrania Jina la herufi Matamshi
י Yodh "Y"
ה He "H"
ו Waw "W", "O" au "U")
ה He "H" (au kimya mwishoni mwa neno)

Matamshi hariri

Kwa kuwa jina liliachwa kutajwa, na maandishi asili hayakuwa na vokali, matamshi yake sahihi hayajulikani kwa hakika.

Hata hivyo, leo wataalamu wengi wanakubaliana kulitamka Yahweh.

Jehovah hariri

Watafsiri kadhaa wa Biblia wanaandika jina la YHWH kuwa "Jehovah" au "Yehovah". Asili yake ni kosa la kusoma Biblia ya Kiebrania. Kiasili waandishi wa Kiebrania hawakutumia alama za vokali na miswada ya kale haionyeshi vokali. Mnamo karne ya 2 BK, wakati Wayahudi wengi hawakutumia tena Kiebrania kama lugha mama, nakala za Biblia zilianza kupewa alama za vokali katika matini. Pale ambapo jina YHWH יהוה ilitokea, waandishi waliongeza vokali za neno mbadala kwa kukumbusha msomaji asisome hilo; maneno mbadala yalikuwa mara nyingi אדני (pamoja na vokali zake אֲדֹנָי adonay - Bwana) au pia שםא (pamoja na vokali zake שְׁמָא shemah - Jina).

Hii ilileta jina YHWH kuandikwa kwa vokali za אֲדֹנָי 'adonay, tokeo lake lilikuwa Yahowah.

Wakati wasomi Wakristo katika karne za kati walianza kufanya utafiti katika lugha asilia za Biblia, wengine walichukua umbo la YaHoWaH kama jina halisi wakafundisha hivyo. Kwa njia hii "Jehovah" au "Yehovah" imepata mahali pake katika tafsiri kadhaa, hasa toleo la Kiingereza la King James Bible lililoendelea kuwa msingi wa tafsiri kwa lugha mbalimbali.

Dhehebu dogo la Mashahidi wa Yehova linafundisha "Jehovah / Yehova" kuwa jina sahihi la Mungu katika Biblia na kwao ni lazima kulitumia.[1]

Marejeo hariri

  1. https://www.jw.org/en/jehovahs-witnesses/faq/name-jehovahs-witnesses/#?insight[search_id]=82505676-b6d5-4297-a84f-34dd3d486b77&insight[search_result_index]=0 Kwa Nini Mnaitwa Mashahidi wa Yehova?, tovuti ya wenyewe, iliangaliwa Desemba 2019

Viungo vya nje hariri

  Makala hii kuhusu mambo ya Biblia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu YHWH kama historia yake au athari wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.