Yohane Baptista de La Salle

Yohane Baptista de la Salle (kwa Kifaransa Jean-Baptiste de La Salle) alizaliwa Reims, Ufaransa, tarehe 30 Aprili 1651 akafariki Saint-Yon, Rouen, Ufaransa, tarehe 7 Aprili 1719.
Alikuwa padri wa Kanisa Katoliki na mlezi wa vijana wengi, ambaye kwa ajili yao alianzisha shirika la Mabradha wa Shule za Kikristo. Anahesabiwa mwanzilishi wa shule Katoliki duniani. De La Salle anahesabiwa pia kuwa wa kwanza kuendesha chuo cha ualimu (1685).
Anaheshimiwa kama mtakatifu na msimamizi wa walimu. Sikukuu inaadhimishwa kila tarehe 7 Aprili au 15 Mei.
MaishaEdit
Akifuata njia ya upadri tangu utotoni, alimaliza masomo na kupata upadirisho tarehe 9 Aprili 1678.
Miaka miwili baadaye alipata udaktari wa teolojia.
De La Salle aliingia kazi ya malezi taratibu, bila ya kukusudia, kadiri ya matukio na watu aliokutana nao.
Juhudi zake za kuanzisha shirika la mabradha tu kwa ajili ya kuendesha shule zilipata upinzani kwa sababu ulikuwa mpango mpya.
Pia mbinu zake zilikuwa hazijazoeleka, kama vile kutumia lugha ya kawaida na kutodai ada yoyote.
Hata hivyo alifaulu kuanzisha mtandao wa shule nchini Ufaransa.
Heshima baada ya kifoEdit
Alitangazwa na Papa Leo XIII kuwa mwenye heri tarehe 19 Februari 1888 na mtakatifu tarehe 24 Mei 1900.
Papa Pius XII alimtangaza msimamizi wa walimu wote tarehe 15 Mei 1950.
Athari yakeEdit
Kazi yake ilienea haraka. Leo duniani shirika lake lina mabradha 6,000 (mbali ya walei na watawa 75,000 wanaoshiriki kazi yao) wanaolea vijana kama 900,000 katika vituo vya malezi 1,000 vya nchi 84.
Tazama piaEdit
TanbihiEdit
Viungo vya njeEdit
- Complete works of St John Baptist de La Salle PDF format
- De La Salle Christian Brothers worldwide official website
- The Vocation of the Brothers United States & Canada
- Compendium of Lasallian Resources
- Founder Statue in St Peter's Basilica