Abu Nuwas

(Elekezwa kutoka Abunuwasi)

Abu Nuwas (kwa Kiarabu أبو نواس) alikuwa mshairi Mwarabu aliyeishi 760-815. Katika utamaduni wa Kiswahili ni jina la mhusika katika hadithi za “Hekaya za Abunuwasi”.[1]

Abu Nuwas

Maisha

hariri

Mshairi Abu Nuwas alizaliwa Ahwaz (Irak). Mama yake alikuwa Mwajemi na baba alikuwa mwanajeshi Mwarabu ambaye hakupata kumjua. Jina lake halisi lilikuwa Hasan ibn Hani al-Hakami; 'Abu Nuwas' ni jina la kutania kutokana na nywele zake ndefu.

Akiwa kijana alipelekwa Basra (Iraq) akisaidia katika duka la moja al-Yashira. Huko Basra alihamia nyumba ya mshairi Walibah ibn al-Hubab aliyemfundisha elimu ya sarufi na pia elimu ya dini. Abu Nuwas aliendelea kujifunza mengi hata alikaa mwaka mmoja kati ya Waarabu Bedu jangwani ili aboreshe ujuzi wake wa lugha ya Kiarabu sanifu.

Baghdad

hariri

Akahamia Baghdad, mji mkuu wa Dola la Kiislamu lililotawala wakati ule maeneo makubwa kuanzia Afrika ya Mashariki hadi Afghanistan na Asia ya Kati. Alipendwa sana na watu wa mjini kwa sababu alianzisha aina mpya ya ushairi akiimba juu ya furaha za divai na mapenzi hasa na wavulana kuliko wasichana au wanawake.

Abu Nuwas akawa mshairi maarufu wa Kiarabu wa siku zile hadi ameitwa kutoa mashairi yake mbele ya Khalifa Harun ar-Rashid. Hata kama mashairi yake yalisababisha hasira ya wahubiri wa Kiislamu, Abu Nuwasi alilindwa na familia ya Barmaki waliokuwa mawaziri wa Khalifa. Wakati Abu Nuwas alipotupwa jela mara kadhaa waliweza kumwondoa gerezani tena.

Mwaka 798 Khalifa Harun ar-Rashid aliwaondoa Barmaki madarakani na kuwafunga jela; Abu Nuwasi alikimbilia Misri. Baada ya kifo cha Harun mwaka 809 alirudi Baghdad akikuta kuwa Khalifa mpya ni Muhammad ibn Harun al-Amin aliyewahi kuwa mwanafunzi wake. Miaka michache ya utawala wa al-Amin ilikuwa miaka ambako Abu Nuwasi alitunga mashairi mengi.

Baada ya al-Amin kupinduliwa na kaka yake al-Ma’amun aliyekuwa Mwislamu mkali, Abu Nuwas alianza kutunga mashairi yaliyolingana na mafundisho ya kidini. Lakini alishindwa kumbembeleza khalifa mpya.

Mnamo mwaka 815 alikufa ama kwa sababu aliuawa au wakati alipofungwa gerezani.

Nafasi kati ya Washairi Wakuu

hariri

Abu Nuwas anahesabiwa kati ya washairi wakuu wa lugha ya Kiarabu. Alikuwa na athira kubwa kwa washairi wa baadaye kama Omar Khayyám na Hafiz.

Pia jina lake limetajwa mara kadhaa katika hadithi za Alfu Lela U Lela.

Hadi leo wengine wanampenda sana lakini wengine wanamchukia kama mshairi bila maadili.

Abu Nuwas mshairi na Abunuwasi wa Afrika ya Mashariki

hariri

Waswahili wamejua zaidi umbo la jina kuwa "Abunuwasi" na wamecheka wakisoma "Riwaya za Abunuwasi". Lakini huyu Abunuwasi wa riwaya hana uhusiano na Abu Nuwas mshairi wa kihistoria zaidi ya kumpatia jina lake.

Hadithi zote za "Riwaya" zinasimuliwa katika nchi nyingine kwa majina tofauti. Waturuki humwita "Nasreddin Hodja", Wauzbeki "Hodja" pekee, watu wa Algeria "Ben Sikran", Waarabu wengine "Juba (Guba)", Waitalia wa Kusini "Giufa".

Huko Iraq kumbukumbu ya Abu Nuwas mshairi imechanganywa na hadithi za huyu mjinga mcheshi mwenye hekima anayejulikana katika nchi zote za Mediteraneo na Mashariki ya Kati. Hadithi katika "Riwaya za Abunuwasi“ zinatumia mapokeo ya urithi huo.

Lakini kuna angalau hadithi moja ya Abu Nuwas mwenyewe inayolingana na Abunuwasi wa “Riwaya” – inasaidia kuelewa jinsi gani jina lake limeunganishwa na urithi wa Guba – Nasreddin:

Hadithi ya Abu Nuwas na Harun ar-Rashid

hariri

“Abu Nuwas alipenda divai mno. Siku moja alipatikana hali amelewa sana wakati Khalifa Harun ar-Rashid alipita barabarani pamoja na askari zake. Khalifa Harun alimpenda Abu Nuwas mshairi hata aliwahi kukaa naye na kunywa naye lakini aliona hawezi kumruhusu kulewa barabarani mbele ya watu wote asionekane mwenyewe Khalifa anayedharau sharia ya Allah.

Hivyo ar-Rashid akamwendea Abu Nuwas alijeficha chupa nyuma yake akikishika kwa mkono wa kuume. “Unionyeshe mkono wako!” Khalifa alisema.

Abu Nuwas alishika chupa kwa mkono wa kulia nyuma yake akionyesha mkono wa kiume. “Unionyeshe mkono mwingine!” alidai ar-Rashid.

Tena mshairi alishika chupa kwa mkono wa kushoto akimwonyesha Khalifa mkono wa kulia. Akasema ar-Rashid: “Sasa unionyeshe mikono yote miwili!”

Abu Nuwas akakanyaga hatua moja nyuma hadi ukuta wa nyumba akashika chupa kwa matako yake ukutani akimwonyesha Khalifa mikono yote mawili. Huyu alidai akanyage hatua moja mbele.

“Ee amirulmuumina”, akajibu Abu Nuwas, “Wewe unajua ya kwamba chupa kitanguka chini nikitembea kitavunjika !”

Khalifa na askari wote walicheka sana. Abu Nuwas alitegemea kupokea viboko 80 lakini Khalifa alitangaza: “Mwenye akili kama huyu hawezi kuwa mlevi wala siwezi kumwadhibu kwa tendo la kushika chupa tu. Basi aende!"

Marejeo

hariri

Tanbihi

hariri
  1. Esat Ayyıldız. "Ebû Nuvâs’ın Şarap (Hamriyyât) Şiirleri". Bozok Üniversitesi İlahiyat Fakültesi Dergisi 18 / 18 (2020): 147-173.