Ono ni hali inayompata binadamu au mnyama kwa ndani, lakini inajitokeza kwa nje (inaonekana). Ni tofauti na hali ya makusudi, kwa kuwa linasababishwa na jambo fulani. Ndiyo maana katika Kiingereza linaitwa passion, neno la mkopo kutoka lile la Kilatini passio linalotokana na kitenzi patior (kupatwa). Si lazima ono liwe hai, kali na tawala.

Ono.

Maono ni mbalimbali, lakini yale ya msingi ni:

  • upande mmoja pendo (kwa jambo fulani), linalosababisha hamu (ya jambo hilo) na hatimaye furaha (jambo likipatikana); upande huo pengine kuna tumaini na ujasiri;
  • upande mwingine chuki (kwa jambo fulani), linalosababisha hofu (ya jambo hilo), hasira (dhidi ya hilo) na hatimaye huzuni (jambo likipatikana); upande huo pengine kuna hali ya kukata tamaa.

Kwa msingi huo, Thoma wa Akwino alifafanua ono kama “badiliko la hisi linalotokana na kukabili jema au baya la kihisi na linaloendana na tukio la kimwili katika muundo wake, k.mf. pigo la moyo”. Mabadiliko ya utashi ni ya roho tu, kumbe ono linaendana daima na tukio la kimwili kwa sababu hisi zinaendana na viungo.

Mtazamo wa maadili

hariri

Wanaotetea anasa wanasema maono yote ni maadilifu kama ustawi wa umbile letu; kinyume chake wengine wanayalaumu kwa kuwa yanapingana na akili na kuvuruga roho. Kumbe yenyewe si maadilifu wala maovu, ila yanakuwa maadilifu kadiri yanavyochochewa au kuratibiwa na akili na utashi yaelekee lengo adilifu. La sivyo yanakuwa maovu kwa kutolingana na akili nyofu na kulenga yasiyokubalika. Yesu alikusudia kuonyesha hasira takatifu alipofukuza wafanyabiashara hekaluni na kupindua meza zao. Vivyo hivyo bustanini alikusudia kuwa na “huzuni nyingi kiasi cha kufa” (Mk 14:34) ili tuelewe inavyotupasa kuhuzunikia dhambi zetu.

Tendo linalotumia maono kulifikia lengo adilifu linastahili zaidi, kwa kuwa Mungu ametujalia hisi vile alivyotujalia kumbukumbu, ubunifu na mikono tuvitumie kutendea mema. Kwa hiyo, “haiwezekani kutenda chema kikubwa pasipo maono” (Blaise Pascal), yaani pasipo hisi kuwaka ari ya upendo. Kinyume chake, maono yasiyoratibiwa yanakuwa vilema: pendo la kihisi linakuwa ulafi na uzinifu, chuki ya kihisi inakuwa wivu na kijicho, hofu inakuwa woga na uzembe. Hapo yanakuwa nguvu ya kutenda maovu badala ya kuwa nguvu ya kutenda mema.

Mtazamo wa maisha ya Kikristo

hariri

Basi, maono hayatakiwi kung’olewa ila kuratibiwa kusudi tusiwe baridi kama watu walioganda, wala wakali kama mito iliyofurika. Hapo hisi zetu hazitafanana na zile za wanyama, bali zitalingana na hadhi yetu kama viumbe vyenye akili na watoto wa Mungu. Tufikirie hisi za Yesu zilivyokuwa kutokana na usafi wa moyo, subira na udumifu hata msalabani. Hapo tutaona jinsi hisi zetu zinavyotakiwa kuwa zaidi na zaidi chini ya akili iliyoangazwa na imani, chini ya utashi uliohuishwa na upendo; tena jinsi mwanga na moto hai ya Roho inavyotakiwa kuenea katika maono yetu ili kuyatakasa na kuyatumia kwa kumtumikia Mungu na jirani. “Furahini pamoja nao wafurahio; lieni pamoja nao waliao” (Rom 12:15). Watakatifu wana uwezo mkubwa ajabu wa kushiriki maono ya wenzao. Pengine wao tu wana neno la kuwatia moyo wenye huzuni.

Kwa hiyo tunapaswa kuratibu maono kulingana na lengo na hali. Katika nafasi ngumu tunaweza kuonja huzuni, hofu au hasira kubwa bila kutenda dhambi. Musa alipoona Waisraeli wanaabudu ndama wa dhahabu alikasirika na kuwaadhibu vikali (taz. Kut 32:19-20); kinyume chake kuhani Eli alihukumiwa kwa kutowakasirikia wanae (taz. 1Sam 3:11-14). Mpanda farasi anahitaji mara hatamu mara kiboko; vilevile ni lazima pengine kuyazuia maono, pengine kuyachochea ili kujiamsha dhidi ya uzembe, aibu na woga. Ni kazi ngumu kumtawala farasi mwenye nguvu, na vilevile kuratibu silika zenye uwezo wa kutenda makuu. Lakini jinsi inavyopendeza, baada ya miaka 10 au 15 ya mapambano na nafsi yetu, kuona tabia imebadilika na kutiwa chapa ya Kikristo!

Hasa mwanzoni mwa maisha ya Kiroho tusitende bila kufikiria vya kutosha, wanavyofanya wengi. Hiyo ni dhambi dhidi ya busara na ya kipaji cha shauri, na inatufikishia kuhukumu bila msingi: ni kama mtu anayeshuka ngazi haraka mno hata akaanguka, jambo ambalo lisingetokea kama angeteremka taratibu. Tuzingatie kwanza lengo la kulifikia hadi kazi ya kufanya, pasipo kupuuzia yaliyopo katikati, yaani kumbukumbu ya yaliyopita, uzingatifu wa hali ya sasa, utabiri wa vizuio vinavyoweza vikatokea, usikivu wa mashauri muhimu. Ni lazima tuchukue muda ili kuamua polepole kabla hatujatenda, halafu itatupasa pengine kutenda mara moja. Lakini tukitenda kwa msukumo wa utashi au maono pasipo kuyapitia hayo tutayumba na kuanguka.

Haraka hiyo inatokana na kwamba utendaji wa kibinadamu unashika nafasi ya utendaji wa Kimungu; tunatenda kwa kuhemka, pasipo kufikiria, wala kuomba mwanga, wala kushauriwa na kiongozi wa Kiroho. Haraka hiyo inasababisha matendo ambayo yanakosa busara na hivyo yana matokeo ya kusikitisha. Mara nyingi inatokana na kuzingatia tu lengo la mara moja bila kuona linavyohusiana na lengo kuu linalotupasa: hapo kwa kuona tu lengo la kibinadamu tunalikusudia kwa utendaji wa kimaumbile, tusiombe vya kutosha msaada wa Mungu.

Haraka hiyo inaweza ikafanya vijana wenye juhudi watake kufikia ukamilifu mapema kuliko neema inavyowajalia, wakiruka vituo, wasizingatie hatua za katikati wala haja ya kuratibu maono. Inawatokea kama wanafunzi ambao mwanzoni mwa masomo wanajitahidi kutokana na upya wa mambo; lakini udadisi ukiisha, au juhudi zikihitajika zaidi, unafuata uzembe. Wanaingia hatari ya kudanganyika, halafu udanganyifu ukiisha, wanatumbukia uzembe na kuacha nia ya kuwajibika. Hatuwezi kufikia mara uwiano mzuri wa uadilifu. Tunapaswa kutembea kasi, lakini bila kupiga “hatua kubwa nje ya njia” (Augustino). Matokeo ya haraka hiyo ni kupoteza utulivu wa ndani na kupatwa na mafadhaiko na mahangaiko ambayo hayazai kitu ila yanafanana kijuujuu na utendaji wa kufaa. Dawa ni kujiweka chini ya Mungu na kulinganisha matakwa yetu na ya kwake. Hatutaridhika zaidi na nafsi zetu, ila tutaonja amani kubwa, na mara kwa mara furaha halisi ndani ya Mungu.

Ili turatibu maono tunapaswa kuepa na kupinga: upande mmoja umotomoto wa tabia unaoendana na kujiamini mno, upande mwingine uzembe na uvivu ambavyo vinaleta madhara makubwa zaidi. Tujitafiti kila siku kuhusu kazi hiyo ya polepole lakini ya daima, tukiona umuhimu wa kuratibu mwenendo wetu au, kwa usahihi zaidi, wa kudumu waaminifu kwa neema ambayo tusipokuwa nayo hatuwezi kufanya kitu kwa wokovu. Hapo ujasiri utasaidia adili la nguvu kutawala hofu ya kihisi. Vilevile upole utairatibu hasira itokane tu na ari ambayo ina subira bila kupotewa na umotomoto wake: hiyo ni dalili ya utakatifu.

Marejeo

hariri
  • René Descartes, Passions of the Soul in J. Cottingham et al. eds., The Philosophical Writings of Descartes Vol I (Cambridge 1985)