Historia ya Saudia

Historia ya Saudia inahusu eneo ambalo leo linaunda ufalme wa Saudia.

Jina la nchi limetokana na lile la familia ya watawala, yaani la mtu aliyeianzisha, Chifu Ibn Saud wa Riyad. Yeye, baada ya kuondoka kwa jeshi la Waturuki Waosmani waliotawala Arabia kwa karne kadha, alishinda vita baina ya makabila ya Uarabuni mwa kati akaweza kuvamia na kutawala maeneo ya Najd na Hejaz na mwaka 1932 alitangaza Ufalme wa Uarabuni wa Saudia.

Watangulizi wa Ufalme wa Saudia

hariri

Kwa maelezo zaidi, Najd ilikuwa ndiyo chanzo cha harakati ya Wahabiya tangu karne ya 18 walioshikamana na nasaba ya Saud[1].

Mwaka 1744 kiongozi wa kikabila Muhammad bin Saud aliungana na kiongozi wa kidini Muhammad ibn Abd al-Wahhab na umoja huo wa familia ya Saud na kundi la kidini la Wahabiya uliweka msingi wa emirati ya Wasaudi Uarabuni.

Emirati ya Diriyah

hariri

Muhammad bin Saud alitawala kutoka mji wa Diriyah, ambao leo ni sehemu ya jiji la Riyad. Hadi kifo chake kwenye mwaka 1765 aliweza kupanua utawala wake juu ya Najd na pwani ya mashariki ya Uarabuni.

Mwanawe Abdul-Aziz bin Muhammad alimfuata hadi mwaka 1803. Itikadi kali ya Wahabiya ilimshawishi kuangalia Waislamu Washia kama wazushi na maadui na mwaka 1801 jeshi lake liliingia Iraki (jimbo la Waosmani) waliopoangamiza mji wa Karbala wenye kaburi la Ali ibn Abu Talib na watakatifu wengine wa Washia. Walibomoa makaburi na kuua wakazi 5,000.

Mwandamizi wake Saud bin Abdul-Aziz bin Muhammad bin Saud aliendelea kupanua mamlaka yake na mwaka 1805 alivamia pia miji mitakatifu ya Makka na Madina. Wasaudia waliongeza ada ya Waislamu waliofika kuhiji wakakataza desturi nyingi zilizokuwa kawaida kama matumizi ya ala za muziki, ukahaba na kunywa divai. Walijaribu pia kuboma kuba juu ya kaburi la Mtume Muhamad lakini walishindwa, wakaendelea kubomoa makaburi yaliyopambwa ya wenzake Muhamad.

Idadi ya Wahiji ilipungua sana. Sultani wa Waosmani Mahmud II, aliyekuwa pia na cheo cha khalifa wa Waislamu na mlinzi wa miji mitakatifu, alimtuma alitazamiwa kama mzushi na Wahabiya, aliona aibu kubwa. Hivyo alimtuma gavana wa Misri Muhamad Ali Pasha aliyerudisha Makka chini ya utawala wa Kiosmani, alimshinda Abdullah bin Saud, mwana wa Saud bin Abdul Aziz, na hatimaye kuteka mji mkuu wa Wasaudia, na hivyo kumaliza emirati yao ya kwanza mwaka 1818. Abdullah alitumwa Istanbul alipopewa adhabu ya kifo.

Emirati ya pili

hariri

Baada ya kundoka kwa jeshi la Wamisri katika Najd mwana wake Abdullah alirudi akaweza kuteka mji wa Riyad na kuanzisha tena emirati ndogo lakini mamlaka yake haikuenea mbali, alisimamia sehemu ya Najd pekee. Hapo watawala wa Saudi walipata mashindano na machifu wa Waarabu wa jirani, na mwaka 1891 walipaswa kuondoka Najd na kukimbilia Kuwait.

Emirati ya tatu

hariri

Lakini mwaka 1902 Abdul Aziz Ibn Saud alifaulu kuvamia tena Riyad na kuimarisha utawala wake huko. Wakati wa Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia hakushiriki katika vita ya Waarabu dhidi ya Waosmani, badala yake alishindana na makabila ya Najd ambayo hawakumtambua kama mkuu.

Mwaka 1921 aliweza kujitangaza Emir wa Najd. Hapo alivamia ufalme wa Hijaz akaushinda na mwaka 1926 Ibn Saud alijitangaza kuwa mfalme wa Hijaz. Mwaka uliofuata alianza kutumia cheo cha mfalme pia kwa Najd. Baada ya kutawala sehemu hizo mbili kwa namna ya pekee alitangaza maungano ya falme zote mbili kwenye mwaka 1932 akaanzisha Ufalme wa Uarabuni wa Saudia[2].

Tanbihi

hariri
  1. History of Arabia, tovuti ya Encyclopedia Britannica
  2. The Saud Family and Wahhabi Islam, Helen Chapin Metz, ed. Saudi Arabia: A Country Study. Washington: GPO for the Library of Congress, 1992
  Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Historia ya Saudia kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.