Wilaya ya Makete

(Elekezwa kutoka Makete)

Wilaya ya Makete ni wilaya mojawapo kati ya 6 za Mkoa wa Njombe.

Mahali pa Makete (kijani) katika mkoa wa Iringa katika ya umegaji.

Makao makuu ni Makete mjini (Iwawa).

Katika sensa ya mwaka 2022 wakazi walihesabiwa 109,160 [1]. Katika sensa ya mwaka 2002, idadi ya wakazi wa wilaya hiyo ilihesabiwa kuwa 106,061 [2].

Ongezeko hilo dogo kabisa hutokana na idadi kubwa ya watu wake kukimbilia mijini: hiyo ni kwa sababu ya uchache wa huduma za jamii, kama vile shule, hospitali, mawasiliano, pamoja na mfumuko wa bei n.k.

Sababu nyingine ni uenezi wa UKIMWI katika wilaya hiyo ambayo inashika nafasi ya kwanza kwa maambukizi nchini Tanzania.

Wenyeji wa Makete ni Wakinga wanaotumia lugha iitwayo Kikinga.

Aidha yapo makabila mengine kama Wawanji wanaoishi maeneo ya bonde la Matamba ambapo tarafa za Matamba na Ikuwo hasa ndiko kabila la Wawanji wanakoishi.

Tokea miaka ya 2000 kabila la Wakinga lilianza kufahamika sana nchini Tanzania kutokana na watu wake kuenea maeneo mengi wakijishughulisha na biashara mbalimbali, hususani biashara ya maduka ambayo imepelekea kuwapatia umaarufu mkubwa katika fani hiyo.

Maeneo ambayo watu hao wameenea kwa wingi ni kama vile Mbeya, hususani wilaya ya Tunduma, Dar es Salaam (Kariakoo) na Songea.

Hali ya hewa Makete ni baridi kiasi kwa maeneo ya kata kama za Kitulo, Mang`oto, Iwawa, Ipelele, Iniho, lakini maeneo mengine huwa na joto kiasi.

Chakula maarufu katika wilaya hii ni viazi ambavyo pia hutengenezwa ugali uitwao usuge ambao ni mchanganyiko wa viazi na unga au maharage.

Kilimo cha biashara ni pareto na miti ya mbao na matunda.

Wilaya hii pia inasifika kwa kilimo cha ngano na mahindi.

Wilaya ya Makete inategemea barabara mbili kuu ya kutoka Njombe na nyingine kutoka Mbeya, kipindi hiki moja ya kutoka Njombe inapitika, lakini barabara pacha zinazoingia mkoani Mbeya zimeharibika na haipitiki.

Ubovu wa barabara hizo umechangia kwa kiasi kikubwa kukwamisha usafirishaji wa pembejeo na hivyo hazifiki kwa wakati. Lakini pia umechangia kushindwa usafirishaji mazao kama matunda, viazi, pareto, mazao ya mbao, ngano, mahindi na mengine kwenda sokoni.

Barabara wilayani humo kama katika wilaya nyingine kama zinapitika, zinachangia kukuza uchumi wa wilaya hiyo, lakini zinazopokuwa mbovu zinachangia kupunguza kasi ya kukua kwa uchumi, pato la wananchi na maendeleo wilaya hiyo.

Ubovu wa barabara wilayani humo umepandisha bei ya bidhaa za madukani ambazo zinaingizwa wilayani humo kupitia Mbeya na Njombe. Bei ya bidhaa nyingi ni za kuruka, hasa katika maeneo ambayo barabara zimeharibika.

Kutokana na ubovu wa barabara hizo, wananchi wa maeneo ya Bulongwa wanabeba matunda, ngano na bidhaa nyingine kwa kichwa umbali mrefu kwenda kuuza mkoani Mbeya ambako soko linapatikana.

Adha za ubovu wa barabara zimewakumba pia wakazi wa Ipepele, Iniho na Matamba wilayani humo, ambao wamekuwa wakibeba viazi, mbao na mahindi vichwani umbali mrefu kwenda kufikisha kwenye maeneo ambako barabara zinafikika.[3]

Kutokana na ubovu wa barabara, mazao mengi ya wilaya ya Makete, yakiwamo ya mbao. yamekuwa yakikwama kusafirishwa na hivyo kukwamisha ukuaji wa uchumi wilayani na hivyo kuwakosesha wananchi kipato, ajira na mahitaji ya kila siku.

Pareto imekuwa ikisuasua kusafirishwa, hata kama hivi karibuni imefufuliwa baada ya miaka takribani kumi kufifia na wakulima kukata tamaa kutokana na soko la dunia la bidhaa hiyo kuanguka mwanguko wa mende.

Kufufuliwa kwa soko la zao hilo na kuanzishwa kwa malipo ya papo kwa hapo, kumechangia kuamsha ari ya wananchi kulima kwa wingi zao hilo, hata kama ubovu wa barabara unalazimisha baadhi ya mazao kuozea nyumbani.

Mahindi, ngano, shayiri na matunda ambayo yanalimwa kwa wingi Bulongwa na Matamba, yanaozea mitini. Watu wachache wenye uwezo wanabeba kichwani umbali mrefu kwenda kuuza. Wenyeji pia wana zao la miti ya ulanzi.[4]

Barabara ni chanzo cha maendeleo: zikijengwa kwa lami, zitasaidia kuongeza haraka pato la wananchi, kukuza uchumi wa nchi na kuondoa umaskini.

Katika siasa wilaya hii imeongozwa na wabunge watatu toka ianzishwe nao ni Tutemeke Sanga, ambaye ni marehemu kwa sasa, Hansi Kitine na Binirithi Mahenge ambaye yupo mpaka sasa anaongoza.

Utamaduni wa wilaya hii ni ngoma ya asili iitwayo Kivilela ambayo huchezwa na wanaume wakiwa na njuga na wanawake pia.

Tanbihi

hariri
  1. https://www.nbs.go.tz
  2. [1] Archived 10 Februari 2010 at the Wayback Machine.
  3. "Nakala iliyohifadhiwa". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2018-07-09. Iliwekwa mnamo 2017-06-25.
  4. "Nakala iliyohifadhiwa". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2008-06-24. Iliwekwa mnamo 2017-06-25.
  Kata za Wilaya ya Makete - Tanzania  

Bulongwa | Ikuwo | Iniho | Ipelele | Ipepo | Isapulano | Itundu | Iwawa | Kigala | Kigulu | Kinyika | Kipagalo | Kitulo | Lupalilo | Lupila | Luwumbu | Mang'oto | Matamba | Mbalatse | Mfumbi | Mlondwe | Tandala | Ukwama


  Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Njombe bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Wilaya ya Makete kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
Tafadhali usiingize majina ya maafisa au viongozi wa sasa maana wanabadilika mno.