Mitholojia ya Kirumi

(Elekezwa kutoka Miungu ya Kiroma)

Mitholojia ya Kirumi ni jumla ya imani kuhusu miungu ya Roma ya Kale jinsi ilivyosimuliwa katika visasili na hadithi za kidini za utamaduni huo.

Dini bila vitabu vitakatifu hariri

Dini ya Roma ya Kale haikuwa na msahafu au vitabu vitakatifu kama Biblia, Qurani au Veda. Hadithi zilizoonyesha imani kuhusu miungu zilisimuliwa katika familia, kuimbwa na washairi na baadaye tu kuandikwa na waandishi bila kuunda andiko maalumu la kidini.

Dini ya wakulima hariri

Kiasili Waroma wa kale walikuwa wakulima na hiyvo dini yao iliangalia miungu iliyowakilisha nguvu asilia na matukio muhimu katika mazingira yao kama Tellus (ardhi), Ops (mavuno), Ceres (mazao ya shambani). Waroma waliwaza nguvu hizi kama kimungu wakitafuta kuziathiri kwa kuzipa uso wa mungu fulani aliyeweza kuabudiwa.

Kupokea miungu ya majirani na mataifa yaliyoshindwa hariri

Lakini Waroma wa Kale waliathiriwa wenyewe sana na majirani wao walioitwa Waetruski waliowaletea habari nyingi za miungu ya Kigiriki na hivyo mawazo mengi yenye asili ya Kigiriki yaliingia katika dini ya Kiroma. Mara nyingi walijaribu kulinganisha miungu ya Kigiriki na miungu yao wenyewe kwa kusema kwa mfano mungu Ares wa Wagiriki ni yeye yule kama Mars wa Kiroma, ni tofauti ya lugha tu.

Baada ya kupanua milki yao kuwa Dola la Roma lililojumlisha mataifa kwenye mabara matatu ya Ulaya, Afrika na Asia waliimarisha mtindo huo uliowasaidia kuwatawala wale watu wengi wenye tamaduni tofautitofauti. Walikubali miungu ya kila taifa kwa kuwaingiza katika dini yao ama kama jina tofauti ya mungu aliyekuwepo tayari kwao au kama nyongeza. Hii haikuwa vigumu mno katika imani yao iliyojua miungu mingi.

Miungu mikubwa na miungu ya nyumba hariri

Waroma waliabudu hasa miungu mikubwa 12 iliyosimamia mwendo wa dunia kwa jumla. Lakini katika maisha ya kila siku miungu inayoweza kuitwa midogo au miungu ya binafsi ilikuwa muhimu pia. Iliitwa Lares au Penati na kutazamwa kama mizimu ya marehemu iliyokaa karibu na au ndani ya nyumba ilhali haionekani. Kila asubuhi na wakati wa sikukuu fulani baba wa nyumba aliwatolea sadaka ndogo na sanamu zao zilikuwa na nafasi ya heshima katika nyumba.

Miungu mikubwa hariri

Jina la Kigiriki Jina la Kirumi Maelezo
Aφροδίτη (Afrodítē) Venus Mungu wa kike wa upendo na uzuri.
Aπόλλων (Apóllōn) Apollo Mungu wa nuru na ushairi.
Άρης (Ares) Mars Mungu wa vita.
Άρτεμις (Artemis) Diana Mungu wa kike wa uwindo.
Αθηνά (Athēná) Minerva Mungu wa kike wa elimu na hekima.
Δημήτηρ (Dēmḗtēr)

Δήμητρα (Dḗmētra)

Ceres Mungu wa kike wa mimea na kilimo.
Διόνυσος (Diónysos) Bacchus Mungu wa divai.
Έρως (Érōs) Amor Mungu wa mapenzi.
ᾍδης (Ádēs) Pluto Mungu wa kuzimu na bwana wa waliokufa.
Ήφαιστος (Ḗfaistos) Vulcanus Mungu wa volkeno na uhunzi.
Ήρα (Ḗra) Juno Mungu wa kike wa ndoa na malkia ya miungu.
Ερμής (Ermḗs) Mercurius Mjumbe wa miungu.
Ἑστία (Estía) Vesta Mungu wa kike wa moto.
Κρόνος (Kronos) Saturnus Mungu wa kilimo na mavuno.
Ποσειδῶν (Poseidṓn)

Ποσειδώνας (Poseidṓnas)

Neptunus Mungu wa bahari.
Ζεύς (Zeús)

Δίας (Días)

Jupiter

Iovis

Mungu wa radi na mfalme wa miungu.
  Makala hii kuhusu mambo ya dini bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu mada hii kama historia yake au uenezi wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.