Sakramenti
Sakramenti katika mapokeo na imani ya Ukristo ni ishara na chombo cha neema ya Mungu.
Jina hilo linatokana na neno la Kilatini "sacramentum" linalofanana na lile la Kigiriki "mysterion" (siri au fumbo) .
Ni mafumbo kwa kuwa ishara ya nje (vitendo na vitu vinavyosindikizwa na maneno maalumu) zinamletea mtu neema zisizoonekana.
Wakatoliki wanasadiki zina uwezo huo bila kutegemea utakatifu au sifa nyingine ya mhudumu anayezitoa kwa mwamini. Zinatenda "ex opere operato" (kwa Kilatini "kwa tendo kutendeka").
Kwa ajili hiyo ni lazima sakramenti ziwe zimewekwa na Yesu Kristo ambaye alizikabidhi kwa Kanisa ili liendeleze kazi yake ya kutakasa binadamu wote mahali kote na nyakati zote.
Jina
haririNeno "sakramenti" liliingia katika Kiswahili kupitia lugha za Ulaya kama Kiingereza. Asili yake ni Kilatini sacramentum inayotokana na Kilat. sacro au sacer kwa maana ya "takatifu". Wakati wa Roma ya Kale ilimaanisha "kiapo kitakatifu" alichotoa mwanajeshi mbele ya mkuu wake.
Waandishi Wakristo Waroma walianza mapema kutumia neno hili kwa kutafsiri Kigiriki mysterion iliyotumika kutaja matendo na mafundisho yanayoweka mbele ya macho ya waumini ile "siri ya Ufalme wa Mungu" (Mk 4:10) iliyotajwa na Yesu. Tertuliani aliyeandika kwa Kilatini mnamo mwaka 200 alilinganisha "sacramentum" (yaani kiapo) ya askari ambayo kwake ni mwanzo wa maisha mapya kama mwanajeshi na matendo ya ubatizo na chakula cha Bwana yanayomwingiza Mkristo katika jumuiya mpya ya Kanisa[1].
Historia
haririKatika milenia ya kwanza, neno lilitumika kwa ibada yoyote. Kwa mfano, Agostino wa Hippo alisema Kanisa linaishi kwa sakramenti nyinginyingi, akiorodhesha maji ya baraka, ndoa, ekaristi, mazishi n.k.
Baadaye jina likaja kutumika kwa namna ya pekee kutajia zile ibada zilizowekwa na Yesu mwenyewe, ingawa pengine linaendelea kutumika kwa maana pana ya "ishara na chombo". Kwa mfano, "Kanisa ni sakramenti ya umoja".
Katika Kanisa Katoliki
haririSakramenti za Wakatoliki na Waorthodoksi |
---|
|
Kuanzia Thoma wa Akwino (karne ya 13) Kanisa Katoliki linaorodhesha sakramenti saba zilizowekwa na Yesu Kristo:
- Ubatizo: hupewa watu wazima, vijana na hata watoto wachanga kama ishara ya kwamba wamelakiwa katika uhai mpya,
- Kipaimara: hupewa mbatizwa ili awe thabiti katika imani,
- Ekaristi: ni sakramenti inayofanya Mkristo ashiriki Mwili na Damu ya Kristo,
- Kitubio: ni sakramenti anayopewa Mkristo anapokwenda kukiri kwa majuto dhambi zake,
- Mpako wa wagonjwa: ni sakramenti ya Mkristo anapokuwa mgonjwa sana,
- Daraja takatifu: ni sakramenti ya kumwezesha Mkristo kuwa kiongozi ndani ya Kanisa,
- Ndoa: ni sakramenti wanayopeana wanaarusi wakiamua mustakabali wao kuwa wa pamoja maisha yote.
Kwa njia yake Yesu anaingia katika maisha ya binadamu ili kuwaunganisha naye hasa katika fumbo la Pasaka (yaani kifo na ufufuko wake).
Idadi hiyo ilithibitishwa na Mtaguso wa Trento katika karne ya 16.
Sakramenti tatu za kwanza ni za kumuingiza mtu katika Ukristo.
Sakramenti mbili zinazofuata ni za uponyaji wa roho na mwili.
Sakramenti mbili za mwisho ni za kuhudumia ushirika katika Kanisa na katika familia iliyo kanisa dogo.
Katika karne ya 20, hasa katika Mtaguso wa pili wa Vatikano, Kanisa Katoliki limejipanga upya katika kuhakikisha sakramenti ziadhimishwe kwa imani. Kwa ajili hiyo linadai zitanguliwe na tangazo la Neno la Mungu ambalo zinakamilisha kazi yake zikiwa "chemchemi na kilele cha maisha yote ya Kikristo"[2].
Kwa Waorthodoksi
haririMakanisa ya Waorthodoksi yanakubali mafumbo hayo yote saba, ingawa hayaelekei kuyaorodhesha.
Kwa Waprotestanti
haririKuanzia Martin Luther, Waprotestanti walikataa kwa kiasi tofauti mtazamo huo wa mapokeo na kuadhimisha sakramenti zile tu zilizotajwa wazi katika Agano Jipya kuwa ziliagizwa na Yesu, hasa Ubatizo na Meza ya Bwana.
Tanbihi
hariri- ↑ Roo, William A. van (1992). The Christian Sacrament. Roma: Ed. Pontificia Univ. Gregoriana. p. 37. ISBN 978-8876526527., online hapa
- ↑ Taz. Misale ya Waamini, toleo la mwaka 2021, uk. 1237-1438
Viungo vya nje
hariri- Herbermann, Charles, ed. (1913). "Sacraments". Catholic Encyclopedia. Robert Appleton Company.
- The Council of Trent on the Sacraments (Catholic)
- The Sacraments in the Orthodox Church Ilihifadhiwa 7 Oktoba 2008 kwenye Wayback Machine.
- Exploring the Sacraments in Anglican Ministry
- Baptism, Eucharist, & Ministry Ilihifadhiwa 5 Desemba 2008 kwenye Wayback Machine. (an ecumenical statement by the World Council of Churches)
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Sakramenti kama historia yake, matokeo au athari zake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |