Samweli
Samweli (kwa Kiebrania: שְׁמוּאֵל Šəmuʼel, maana yake labda ni "Anayemsikiliza Mungu"; 1070 - 1000 KK hivi) ni mtu muhimu wa Historia ya wokovu ya Agano la Kale.
Katika Biblia anatajwa kama mwamuzi wa mwisho na mkuu kuliko wote, tena kama nabii tangu utotoni. Ndiye mwanzilishi wa ufalme wa Israeli kwa kuwa kwa agizo la Mungu alimpaka mafuta Sauli awe mfalme wa taifa lake, tena, baada ya huyo kukataliwa kwa ukaidi wake, alimpaka vilevile Daudi, ambaye kutoka uzao wake akaja kutokea Masiya[1].
Habari zake zinasimuliwa katika Vitabu vya Samweli.
Kanisa Katoliki na madhehebu mbalimbali za Ukristo vinamheshimu kama mtakatifu hasa tarehe 20 Agosti[2].
Vitabu vya Samweli
haririVitabu viwili vya Biblia ya Kikristo vinaitwa kwa jina la mtu huyo, ambaye kwa njia yake Israeli ilianza kuwa na umoja zaidi na hatimaye kuwa ufalme. Badala ya kila kabila kujitegemea, yote 12 yalikubaliana yawe na kiongozi mmoja wa kudumu ambaye cheo chake kirithiwe na mwanae. Kwa umoja huo waliweza kushinda maadui wao wengi.
Vitabu hivyo vimekusanya kumbukumbu zote kuhusu mwanzo wa ufalme (1070-972 hivi K.K.), yaani kuhusu Samweli mwenyewe na wanaume wawili aliowapaka mafuta watawale Israeli kwa niaba ya Mungu: kwanza Sauli, halafu Daudi. Kumbukumbu hizo zilikuwa nyingi na tofauti, hivyo tunakuta humo tata nyingi kuliko katika vitabu vingine vyote vya Biblia. Hasa mna hoja za kukubali mfumo wa ufalme na hoja za kuukataa.
Ukuu wa Samweli ulidokezwa kwanza na uzazi wake wa ajabu, kwa kuwa mama yake, Ana, alikuwa tasa akampata baada ya kusali na kuweka nadhiri (1Sam 1). Hivyo baada ya miaka michache alihamia Shilo kwenye sanduku la agano kama mtumishi wa kuhani Eli.
1Sam 3 inasimulia wito wake: akiwa amelala karibu na sanduku hilo akaamshwa na Mungu mara tatu mpaka akafundishwa na Eli kumtambua na kumuitikia Mungu. Hapo akamtabiria Eli adhabu kali, na hivyo Israeli ikajua kuwa amefanywa nabii wa Bwana.
Samweli aliwaamua Waisraeli kwa kuwakomboa mikononi mwa Wafilisti (1Sam 7), lakini ni muhimu hasa kwa kuwaanzishia ufalme kwa kuwaweka wakfu kwanza Sauli halafu Daudi. Kadiri ya 1Sam 8, yeye na Mungu hawakupendezwa na jinsi Waisraeli wengi walivyotaka kuiga mtindo wa mataifa yote: Samweli aliwaangalisha kuhusu matatizo na unyonyaji wa wafalme, naye Mungu aliona katika ombi hilo uasi ambao Waisraeli wanamkataa asiwatawale tena, lakini akamuagiza Samweli awakubalie.
Ukweli ni kwamba mfalme aliwekwa wakfu kwa Mungu kama mwakilishi wake akitakiwa kutimiza matakwa yake, hasa kwa kusikiliza anamuambia nini kwa kinywa cha manabii wake. Ndiyo sababu Samweli alizidi kumuelekeza Sauli, na hatimaye akamkataa kwa ukaidi wake. Mabishano kati ya Samweli na Sauli ni mwanzo wa mabishano yote kati ya manabii na wafalme ambao hawakutaka kumtii Mungu, na hatimaye wakadhulumu na kuua manabii wake.
Mamlaka ya neno la Mungu lililoletwa na nabii ilitakiwa kuwa juu ya mamlaka ya serikali na nguvu ya kijeshi alivyokuwa navyo mfalme. Lakini mara nyingi wafalme, kwa kujivunia cheo chao, walishindwa kumnyenyekea nabii wa Mungu, wakaona afadhali kufuata manabii wengine wengi waliosema uongo ama kwa kudanganywa na matarajio yao ama kwa kujipendekeza kwa mfalme na kwa taifa lote.
Sala yake (1Sam 3:10)
hariri"Nena, Bwana, kwa kuwa mtumishi wako anasikia".
Tazama pia
haririTanbihi
haririViungo vya nje
haririMakala hii kuhusu mtu wa Biblia bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Samweli kama habari za maisha au kazi yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |