Upendo kamili
Upendo kamili (1Yoh 4:18) ndio hasa ukamilifu wa Kikristo (Kol 3:14), ambao ni wajibu kwa Wakristo wote kuulenga kutokana na maana halisi na upana wa amri kuu ya upendo (Math 22:37)[1].
Ufafanuzi wa teolojia
haririBaadhi wanadhani si lazima kuwa na upendo mkubwa ili kutimiza kikamilifu amri kuu; kwao ukamilifu haulengi amri hiyo, bali utekelezaji wa mashauri kadhaa yaliyo juu zaidi. Thoma wa Akwino alijibu kwamba wote wanapaswa kulenga ukamilifu, kila mmoja kadiri ya hali yake (k.mf. ndoa au utawa), ingawa hawadaiwi kuwa wakamilifu tayari. Amri kuu inataka wote kwa jumla walenge ukamilifu wa upendo, walau kwa njia ya kawaida, wakati nadhiri za kitawa zinabana wale walioziweka waulenge kwa njia ya pekee ya wito wao. “Ukamilifu wa upendo, unaofanya maisha ya Kikristo yawe kamili, umo hasa katika kumpenda Mungu kwa moyo wote na jirani kama nafsi yetu. Kwa hiyo ukamilifu umo hasa katika kushika amri”, si katika kutimiza nadhiri[2].
Kimsingi ukamilifu umo katika upendo; tusidhani huo unaagizwa kwa kiwango fulani tu, halafu unakuwa shauri. Amri hiyo inadai wazi ukamilifu: “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote”. Mipaka iko wapi? Vilevile: “na jirani yako kama nafsi yako” (Lk 10:27). Kila mmoja anajipenda iwezekanavyo, tena anapaswa kujitakia uzima wa milele si kwa kiwango cha chini tu, bali pasipo mpaka, kwa sababu hajui Mungu anataka kumfikishia wapi. Ni hivyo kwa kuwa upendo ndio lengo la amri yoyote, na katika utashi lengo halipo kwa kiwango fulani tu, bali katika ukamilifu wake, tofauti na njia za kulifikia. Lengo tunalitaka au hatulitaki; hatuwezi kulitaka nusu. Daktari hawezi kutaka mgonjwa apone nusu; anapima dawa, lakini analenga afya kamili. “Kwa nini ukamilifu huo usiagizwe kwa binadamu, ingawa hakuna anayeweza kuwa nao katika maisha haya?” (Augustino). Yaani, amri ya kumpenda Mungu unadai hata ukamilifu wa mbinguni, si kama hali ya kutimizwa mara moja, bali kama lengo ambalo wote wajiwekee.
Lengo la amri nyingine, zilizo chini ya amri kuu, ni kuondoa vile ambavyo vinapinga upendo na vinataka kuuangamiza; kumbe lengo la mashauri ya Kiinjili ni kusukumia mbali vile vinavyoweza vikazuia utekelezaji kamili wa upendo, ingawa haviupingi, k.mf. ndoa, shughuli za kidunia n.k. “Amri… na mashauri… vinashikwa vizuri vinapotimizwa ili kumpenda Mungu na kumpenda jirani kwa ajili ya Mungu, katika ulimwengu huu na ule ujao” (Augustino). “Ndiyo sababu katika Mafundisho ya Wazee, abati Musa alisema: Mafungo, makesha, kutafakari Maandiko, kwenda uchi na kukosa vitu si ukamilifu, bali vifaa au njia za ukamilifu; huo haumo katika mambo hayo, ila kwa njia hizo unafikiwa kwa kasi na hakika zaidi” (Thoma wa Akwino). Ndiyo njia zinazoelekea ukamilifu; lakini wenyewe ni kumfuata Yesu kwa upendo: “Ukitaka kuwa mkamilifu, enenda ukauze ulivyo navyo, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni, kisha njoo unifuate” (Math 19:21). Tunaweza kuwa fukara kwa hiari kutokana na sababu isiyo ya kidini (k.mf. kwa kudharau utajiri kifalsafa) au kwa upendo wa Mungu; kwa vyovyote si sharti la ukamilifu. Huo umo hasa katika kutekeleza vizuri zaidi na zaidi amri kuu isiyo na mipaka. Wote wanapaswa walau kulenga ukamilifu huo: kwao si afadhali tu, bali ni wajibu sawa na ule wa kuelekea mbinguni, ambapo upendo wa Mungu utatawala kikamilifu, kisiwepo tena kitu kinachoweza kuupunguza.
Upendo wa Mungu haupatikani katikati
haririFundisho la kuwa amri kuu haina mipaka kwa jinsi ilivyotolewa linathibitika kwa kuzingatia kuwa lengo tunalolizungumzia si mojawapo la katikati (kama vile malimwengu), bali ni lile kuu, yaani Mungu mwenyewe, aliye wema usio na mipaka. Ikiwa mgonjwa anajitakia afya pasipo kiwango, zaidi sisi tunapaswa kutamani upendo wa Mungu pasipo kiwango, kwa kuwa hatujui ni kipi ambacho Mungu anataka kutufikishia na kweli atatufikishia tukiwa waaminifu. “Binadamu hawezi kamwe kumpenda Mungu anavyotakiwa kupendwa; kama vile hatutaweza kamwe kumuamini na kumtumainia inavyotupasa” (Thoma wa Akwino). Tofauti na maadili ya kiutu, lengo, sababu na kipimo halisi cha yale ya Kimungu ni Mungu mwenyewe, ukweli wake na wema wake usio na mipaka. Kwa hiyo hatuwezi kumuamini mno na kumtumainia mno; hatutaweza kamwe kumpenda anavyostahili. Hivyo tunazidi kuona amri kuu isivyo na mipaka: inadai wote hapa duniani waulenge upendo wa Mungu ulio safi na wenye nguvu zaidi na zaidi.
Tumaini linapatikana kati ya kukata tamaa ya wokovu na kuudai kipumbavu, lakini anayeutarajia kipumbavu si kwamba anamtumainia mno Mungu, bali anabadili sababu ya kutumainia, akitumaini kitu ambacho Mungu hawezi akaahidi, k.mf. msamaha pasipo majuto halisi. Vilevile kilema cha wepesi wa kuamini si katika kumuamini mno, bali katika kusadiki yamefunuliwa na Mungu mambo yaliyobuniwa na binadamu.
Kusahau kuwa katikati adilifu ni pia kilele, na kudhani maadili ya Kimungu yamo hasa katikati (kama maadili ya kiutu), ndiyo tabia ya mtu wa wastani anayejisingizia kuwa na kiasi. Mtu wa namna hiyo yupo kati ya uadilifu na uovu, tena anakaribia uovu kuliko uadilifu: “Mtu wa wastani kweli anapendezwa na kila kitu, lakini hapendezwi na chochote hata achangamke… Anachukia tamko lolote, kwa kuwa kila tamko linapinga tamko lingine tofauti. Kumbe ukijifanya kidogo rafiki na kidogo adui wa kila jambo, atakuona mwenye busara na kiasi. Mtu wa wastani anasema katika yote kuna mchanganyiko wa mema na mabaya, kwa hiyo tusiwe na msimamo mkali katika kupima mambo. Ukisisitiza ukweli kwa nguvu, mtu wa wastani atasema unajiamini mno. Mtu wa wastani anasikitika kuwa Ukristo una dogma; angependa ufundishe maadili tu; ukimuambia maadili ya Ukristo yanatokana na dogma zake kama matokeo na sababu yake, atakujibu umezidisha… Kama neno ‘kuzidisha’ lisingekuwepo, mtu wa wastani angelitunga… Kwa kawaida mtu wa wastani anaonekana mtaratibu; hawezi kuwa mnyenyekevu, la sivyo angeacha kuwa wa wastani. Mnyenyekevu anakataa uongo, hata ukitukuzwa na ulimwengu wote, naye anaupigia magoti ukweli… Mtu mwenye upendo hawezi kamwe kuwa wa wastani” (Ernest Hello).
Wajibu wa kusonga mbele kuelekea uzima wa milele
haririSababu ya mwisho ya amri ya upendo kutokuwa na mipaka ni kwamba tunaelekea uzima wa milele, nasi tunasafiri vizuri kadiri tunavyokua katika upendo ambao unatakiwa kustawi mfululizo mpaka mwisho wa safari. Hilo si shauri tu, yaani jambo bora la hiari, bali ni agizo, linatakiwa, hivi kwamba mtu ambaye hapa duniani hataki kukua katika upendo anamchukiza Mungu. Njia ya uzima wa milele haikusudiwi kwa kusimama wala kulala, bali kwa kutembea tu. Kwa msafiri ambaye hajafikia mwisho wa lazima wa safari yake, kusonga mbele si shauri, ni sharti. Basi, tunapomuelekea Mungu, tunasonga mbele Kiroho, kwa kukua katika upendo: ndicho tunachotakiwa kuomba.
Ikiwa hivyo, tusipotimiza bado kikamilifu amri hiyo, je, tunaivunja? Jibu la hakika ni hapana, kwa kuwa “ili tuepe uvunjaji huo inatosha tushike kwa namna fulani sheria ya upendo kama wanavyofanya wanaoanza” (Thoma wa Akwino). Ni kweli kwamba upendo wa Mungu unaingia wote kabisa katika lengo la amri hiyo; hata ukamilifu wa mbinguni hauwekwi kando, kwa kuwa ndio lengo ambalo tulikusudie, lakini hatuivunji amri tukitimiza upendo kwa kiasi. Kiwango cha chini cha kumpenda Mungu ni kutopenda chochote kuliko yeye, wala kinyume chake wala sawa naye; asiye na kiwango hicho hatimizi amri. Kinyume na hicho, kuna kiwango cha upendo kisichoweza kufikiwa hapa duniani, nacho ni kumpenda Mungu kwa kumlenga kweli mfululizo. Hatuvunji amri kama hatujafikia ukamilifu huo, wala viwango vya katikati, mradi tuwe na kiwango cha chini. Lakini tukisimama katika kiwango hicho hatutimizi kikamilifu amri kuu.
Ni kosa kudhani eti! Upendo usiokamilika tu ni wa lazima, na viwango vyake vya juu ni vya shauri. Hivyo vimeagizwa walau kama lengo, hata ikiwa si kwa sasa hivi. Ni sawa na mtoto ambaye asipokua anavyotakiwa, hatabaki mtoto, bali atakuwa mbilikimo. Upande wa roho pia sheria ya ukuaji ina masharti makali: ikiwa mbegu ya Kimungu tuliyotiwa kwa ubatizo haistawi, ina hatari kubwa ya kusongwa na magugu. Hakika katika njia ya wokovu, watu walio tofauti na jinsi wanavyotakiwa kuwa si waliozama katika mafumbo, bali wachelewaji na vuguvugu.
Yapo matatu yatokanayo:
- Katika njia ya Mungu, asiyesonga mbele, anarudi nyuma: kwa sababu kwetu ni sheria kusonga mbele mfululizo, na asiyefanya hivyo anakuwa mchelewaji, kama garimoshi linalosimama mno kwenye stesheni lisifuate ratiba.
- Ustawi wa upendo unatakiwa kuwa wa kasi zaidi na zaidi kadiri tunavyomkaribia Mungu na kuvutwa naye. Ndivyo jiwe linavyoanguka kasi kadiri linavyokaribia ardhi na kuvutwa nayo.
- Hatimaye, ikiwa ndio ukuu wa amri ya upendo, ni lazima tuamini kwamba tutazidi kupewa neema za msaada ili tulifikie lengo hilo, kwa sababu Mungu haagizi kamwe yasiyowezekana. Anatupenda mno, kuliko tunavyoweza kudhani. Ni juu yetu kuitikia. Baada ya kumpenda kwa moyo wote, kwa hisia ya mapenzi, tumpende kwa akili yote, kwa upendo mtendaji, kwa nguvu zote wakati wa majaribu, na hatimaye kwa roho yote, iliyoachana na vurugu za hisi, ili tumuabudu “katika roho na kweli” (Yoh 4:23,24).
Kwa jumla fundisho hilo linatuonya tusitenganishe utakatifu na wokovu wa milele, kama wanavyofanya wanaosema, eti! Mimi sitakuwa mtakatifu kamwe; inanitosha niokoke. Hilo ni kosa kubwa. Kugeuka watakatifu zaidi na zaidi ndiyo njia ya wokovu; mbinguni kutakuwa na watakatifu tu, kwa hiyo kila mmojawetu anapaswa kulenga utakatifu.
Tazama pia
haririTanbihi
hariri- ↑ Chapter V of the Dogmatic Constitution on the Church, Lumen gentium discusses the Universal Call to Holiness:
...all the faithful of Christ of whatever rank or status, are called to the fullness of the Christian life and to the perfection of charity; ...They must follow in His footsteps and conform themselves to His image seeking the will of the Father in all things. They must devote themselves with all their being to the glory of God and the service of their neighbor. Pope Paul VI, Lumen gentium, §40, November 21, 1964 Archived Septemba 6, 2014, at the Wayback Machine
- ↑ The Second Vatican Council, in the Dogmatic Constitution on the Church, speaks with clarity of the universal call to holiness, saying that no one is excluded: “The forms and tasks of life are many but holiness is one — that sanctity which is cultivated by all who act under God’s Spirit and… follow Christ, poor, humble and cross-bearing, that they may deserve to be partakers of his glory” (Lumen Gentium, n. 41)" [1]
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Upendo kamili kama historia yake, matokeo au athari zake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |