Maadili ya Kimungu
Katika Ukristo maadili ya Kimungu ni yale yanayotokana na Mungu na kumwezesha binadamu kuhusiana naye inavyotakiwa, yaani kwa:
Maadili ya Kimungu |
---|
|
Kwa maadili hayo, yale ya kiutu yanakuwa hai na bora, kwa mfano wa Yesu Kristo. Kadiri ya Kanisa Katoliki, tofauti na yale ya kiutu, maadili ya Kimungu hayawezi kupatikana kwa juhudi anazofanya mtu, bali kwa neema tu: yanamiminiwa rohoni, yaani katika akili na katika utashi.
Katika teolojia ya Kanisa Katoliki
haririMaadili ya Kimungu ni maadili ya kumiminiwa yanayomhusu Mungu mwenyewe aliye lengo letu kuu. Tofauti na hayo, maadili ya kiutu yanahusu njia za kufikia lengo hilo.
Imani
haririKati ya maadili ya Kimungu, imani inatuwezesha kusadiki yale yote ambayo Mungu ametufunulia, kwa kuwa ndiye ukweli wenyewe. Ni kama hisi ya Kiroho inayotuwezesha kusikia muziki safi wa Kimungu usiojulikana kwa njia nyingine yoyote. Kuna tofauti kubwa kati ya kusoma Injili kihistoria au kitaalamu na kuiamini kama Neno la Mungu, kwa kuwa kusadiki ni tendo linalopita umbile letu na la malaika, likituingiza katika ulimwengu wa juu. “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu” (Ef 2:8). Ndiyo msingi wa kufanywa waadilifu, kwa kuwa inatujulisha lengo lipitalo maumbile tunalopaswa kulikusudia. “Ibrahimu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa haki” (Mwa 15:6; Rom 4:3,9). “Walakini haikuandikwa kwa ajili yake tu kwamba ilihesabiwa kwake; bali na kwa ajili yetu sisi tutakaohesabiwa vivyo hivyo, sisi tunaomwamini yeye aliyemfufua Yesu Bwana wetu katika wafu” (Rom 4:23-24). Sisi tutaokoka tu kwa imani hiyo ambayo ni zawadi ya Mungu. Kanisa lilitamka rasmi dhidi ya Wapelajiupande kwamba hata mwanzo wa imani ni neema. Imani hiyo inapita kabisa maumbile, si kama muujiza unaoonekana au kama utabiri wa tukio la kawaida tu (k.mf. mwisho wa vita); kwa sababu imani inamhusu Mungu mwenyewe katika maisha yake ya ndani, ambayo hayawezi kujulikana kimaumbile, tena kwa sababu tunasadiki kwa kutegemea mamlaka ya Mungu aliyejifunua, ambayo pia haiwezi kujulikana na maumbile. Imani inatufanya tushike kwa namna ipitayo maumbile na isiyoweza kukosa, yale ambayo Mungu ametufunulia kadiri tunavyofundishwa na Kanisa lililokabidhiwa ufunuo huo.
“Tazama, msomi fulani anachimba mafundisho ya Kikatoliki bila ya kuyakataa kwa ukaidi, bali anakariri, ‘Heri nyinyi mlio na imani; mimi pia ninapenda kuwa nayo lakini siwezi’. Anasema ukweli: anataka asiweze (bado); kwa sababu kusoma na kuwa na nia njema hakufikii daima kujua ukweli, ili ionekane wazi kuwa hakika ya akili si hakika kuu inayotegemeza mafundisho ya Kikatoliki… Kinachotokea ndani mwetu tunapoamini ni tukio la mwanga wa ndani unaopita umbile letu... Mwongofu atawaambia, ‘Nilisoma, nilitafakari, nilitaka nisifike; lakini siku fulani, siwezi kusema vipi, kwenye pembe ya njia, au nyumbani karibu na moto, sijui, sikuendelea kuwa yuleyule, nimesadiki... Kilichotokea ndani mwangu katika nukta ya kupata hakika kuu ni jambo tofauti kabisa na yale yote yaliyotangulia’. Mwakumbuke wanafunzi wale wawili waliokwenda Emau” (Henri Lacordaire).
Imani tunayomiminiwa ni kama uwezo wa kusikia ambao unapita maumbile na kutufanya tusikilize sauti ya Mungu kupitia manabii na Mwanae mwenyewe, kabla hatujakaribishwa kumuona uso kwa uso. Mtu anayesoma Injili bila ya imani, na mwingine mwenye imani, ni tofauti kama watu wawili wanaosikiliza wimbo fulani, lakini mmojawao ana karama ya muziki, mwingine hana. Wote wanasikia noti zote, lakini yule wa kwanza tu anaelewa undani na ujumbe wa wimbo ule. Vivyo hivyo mwamini tu, hata kama hajui kusoma, anashika Injili namna ipitayo maumbile kama Neno la Mungu, wakati msomi pamoja na elimu yake yote hawezi kuishika hivyo pasipo imani ya kumiminiwa. “Yeye amwaminiye Mwana wa Mungu anao huo ushuhuda ndani yake.
Asiyemwamini Mungu amemfanya kuwa mwongo, kwa kuwa hakuuamini huo ushuhuda ambao Mungu amemshuhudia Mwanawe” (1Yoh 5:10). Miaka mia iliyopita mtu angeshangaa kuambiwa siku moja ataweza kusikia kwa redio muziki unaochezwa wakati huohuo katika nchi nyingine. Kwa imani ya kumiminiwa tunasikia muziki wa mbinguni, ambao baadhi ya nyimbo zake ni ma[[fumbo ya Utatu, umwilisho, ukombozi, ekaristi na uzima wa milele. Kwa kusikiliza hayo tunaongozwa zaidi na zaidi kule unakotokea muziki huo bora.
Tumaini na upendo
haririIli tuelekee kweli lengo hilo na kulifikia, tumepewa mabawa mawili, tumaini na upendo. Pasipo hayo tunaweza kuelekea tu tunapoelekezwa na akili yetu; kumbe tukiwa nayo tunarukia tunapoelekezwa na imani. Kama vile akili yetu pasipo mwanga wa imani haiwezi kujua lengo letu lipitalo maumbile, utashi wetu pia hauwezi kuelekea lengo hilo nguvu zake zisipozidishwa na kuinuliwa kwenye ngazi ya juu. Kwa tumaini tunatamani kumpata Mungu, na kusudi tumfikie tunategemea si nguvu za umbile letu, bali msaada aliotuahidia, yaani yeye aliye tayari daima kusaidia. Upendo unatufanya tumpende Mungu namna bora zaidi, isiyojitafutia faida; si tu ili tumpate hapo baadaye, bali kwa ajili yake na kuliko tunavyojipenda, kutokana na wema wake usio na mipaka, unaopendeza kuliko fadhili zake zote. Unatufanya tumpende hasa kama rafiki aliyetangulia kutupenda. Unamuelekezea vitendo vya maadili mengine yote ukiyahuisha na kuyafanya yaweze kustahili. Ndiyo nguvu yetu kuu ipitayo maumbile, nguvu ya upendo ambayo wakati wa dhuluma imeshinda vipingamizi vyote, hata katika viumbe dhaifu kama watakatifu Anyesi na Lusia. Hivyo mwenye mwanga wa imani anamuelekea Mungu kwa mabawa ya tumaini na upendo. Akitenda dhambi ya mauti, mara anapoteza neema inayotia utakatifu na upendo, kwa kuwa anajitenga na Mungu akiacha kumpenda kuliko nafsi yake. Hata hivyo huruma ya Mungu inamuachia imani na tumaini (mpaka atakapotenda dhambi dhidi ya maadili hayo) awe bado na mwanga wa kumuelekeza njia, na aweze bado kutegemea huruma isiyo na mipaka ili kuomba neema ya uongofu.
Kati ya maadili hayo ya Kimungu, upendo ndio la juu zaidi, nao utadumu milele pamoja na neema inayotia utakatifu, ambapo badala ya imani na tumaini mtu atakuwa na Mungu akimjua waziwazi, bila ya hofu ya kupotewa naye. “Upendo haupungui neno wakati wowote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika… Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo (1Kor 13:8,13). Ndio utendaji wa juu wa muundo wa Kiroho: maadili matatu ya Kimungu ambayo yanastawi pamoja, halafu maadili ya kiutu yanayoendana nayo.
Marejeo
hariri- Paradise Restored - The Social Ethics of Francis of Assisi, A Commentary on Francis's 'Salutation of the Virtues', by Jan Hoebrichts, Franciscan Institute Publications, 2004. ISBN 978-0-8199-1008-0
Viungo vya nje
hariri- Theological Virtues Ilihifadhiwa 7 Mei 2012 kwenye Wayback Machine. from Catholic Definitions
- The Virtues - Catechism of the Catholic Church
- Contrary, Heavenly, and Cardinal Virtues Ilihifadhiwa 15 Machi 2015 kwenye Wayback Machine.
- The Three Theological Virtues Ilihifadhiwa 17 Machi 2012 kwenye Wayback Machine. at About.com