Maadili ya kiutu ni yale yanayotakiwa kupatikana katika binadamu yeyote ili aweze kutenda kwa uadilifu kadiri ya utu wake unaomtofautisha na wanyama, yaani hasa akili inayomwezesha kufikiria na kuelewa maana na matokeo ya matendo yake.

Maadili yakipambana na vilema, vioo vya rangi vya karne ya 14 katika Niederhaslach Church.
Maadili bawaba

Kadiri ya wanafalsafa wa Ugiriki wa kale Plato na Aristotle, maadili hayo ni mengi (si chini ya 40), lakini yanategemea manne (maadili bawaba): busara, haki, nguvu na kiasi.

Katika Biblia ya Kikristo

hariri

Katika Biblia, upendo unadai pamoja na imani na tumaini (maadili ya Kimungu), maadili ya kiutu, ambayo yote yanategemea manne ya msingi: busara, haki, nguvu na kiasi. “Huwafundisha watu kiasi, na ufahamu, na haki, na ushujaa; wala hakuna mambo ya kuwafaa zaidi kwa maisha” (Hek 8:7).

Maadili ya kiutu yanapatikana na kukua kwa juhudi za kutenda mema hadi kuzoea na kupata msimamo. Katika kufanya hivyo tunasaidiwa na neema ya Mungu. “Uweza wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa... mkijitahidi sana kwa upande wenu, katika imani yenu tieni na wema, na katika wema wenu maarifa, na katika maarifa yenu kiasi, na katika kiasi chenu saburi, na katika saburi yenu utauwa, na katika utauwa wenu upendano wa ndugu, na katika upendano wa ndugu, upendo. Maana mambo hayo yakiwa kwenu na kujaa tele, yawafanya ninyi kuwa si wavivu wala si watu wasio na matunda, kwa kumjua Bwana wetu Yesu Kristo” (2Pet 1:3,5-8).

Tunahitaji busara kwa sababu ndiyo adili linalotakiwa kuongoza utekelezaji wa mengine yote, kwa kuzingatia kila mara yaliyo mema kweli kwetu na kuchagua namna inayofaa kuyafikia. “Iweni na busara kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua” (Math 10:16). “Wale wenye busara walitwaa mafuta katika vyombo vyao pamoja na taa zao” (Math 25:4). “Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia? Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki, wakisema, ‘Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza’” (Lk 14:28-30).

Tunahitaji haki kwa sababu ndiyo msimamo wa kumpatia kila mmoja kile anachostahili. “Mwenye kanzu mbili na ampe asiye na kanzu; na mwenye vyakula afanye vivyo hivyo... Msidhulumu mtu, wala msishitaki kwa uongo; tena mtoshewe na mshahara wenu” (Lk 3:11,14). “Mpeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na yaliyo ya Mungu mpeni Mungu” (Mk 12:17).

Tunahitaji nguvu kwa sababu ndiyo msimamo wa kutorudi nyuma mbele ya ugumu wa kutenda mema yanayotupasa. “Mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka” (Math 24:13).

Tunahitaji kiasi kwa sababu ndio msimamo wa kutumia vitu kadiri inayotufaa tu. Hasa ni muhimu kuwa na kiasi katika masuala ya jinsia. “Usizini. Wala usiibe... Wala usimtamani mke wa jirani yako... wala kitu chochote alicho nacho jirani yako” (Kumb 5:18-19,21). “Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe” (1Kor 6:18).

Kati ya maadili mengine, Yesu alihimiza hasa upole na unyenyekevu, yanayotulinganisha naye kwa namna ya pekee. “Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu, kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu” (Math 11:29). “Mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu, na mtu anayetaka kuwa wa kwanza wenu, atakuwa mtumwa wa wote. Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi” (Mk 10:43-45).

Maadili ya kiutu yanavyoinuka katikati ya vilema viwili vinavyopingana

hariri

Maadili ya kiutu yanainuka katikati ya pande mbili tofauti, ambazo mmoja umezidisha na mmoja una upungufu. Kwa mfano, adili la nguvu linainuka katikati ya woga (unaokimbia hatari bila ya sababu yenye msingi) na ushupavu (unaotaka kuvunjika kichwa bila ya sababu ya kutosha).

Lakini, ebu! Hiyo katikati isieleweke vibaya. Wanaopenda anasa na watu vuguvugu wanataka kusimama katikati si kwa kupenda uadilifu, bali kusudi waepe matatizo ya vilema vinavyopingana pande hizo mbili. Hao wanachanganya hiyo katikati na ule wastani ambao haupatikani kama kilele katikati ya vilema viwili vinavyopingana bali katikati ya uovu na uadilifu.

Wastani huo unakimbia uadilifu wa juu ukijisingizia kuwa “pengine yaliyo bora yanazuia yaliyo mema”, ukiwa na maana ya kwamba, eti! “Mara nyingi au daima yaliyo bora yanazuia yaliyo mema”.

Kumbe hiyo katikati halisi ya uadilifu haisimami tu kati ya vilema viwili vinavyopingana, bali inainuka juu ya upotovu wa pande hizo mbili tofauti: busara halisi iko juu ya upumbavu na ya ujanja; ukarimu uko juu ya uroho na ya ubadhirifu; adili la ibada liko juu ya kudharau dini na ya ushirikina.

Tena hiyo katikati inaelekea kuinuka zaidi na zaidi, pasipo kupotoka upande mmoja wala upande mwingine, kadiri uadilifu unavyokua, kwa kuwa inafuata kanuni ya juu na lengo la juu.

Maadili ya kiutu katika teolojia ya Kikatoliki

hariri

Ili tuzielewe taratibu za muundo wa Kiroho, ni muhimu tujue vizuri maadili ya kiutu, yaliyo chini ya yale ya Kimungu. Jina linavyosema, ya kwanza, yanayopatikana kwa kurudiarudia vitendo vyake, yanajulikana na Wapagani pia kwa kuwa lengo lake linajulikana na akili. Baadhi ya vijana waliojitoa kwa Mungu hawayajali vya kutosha; kinyume chake wengine wenye umri mkubwa zaidi, kisha kutambua umuhimu wake hawajali tena vya kutosha maadili ya Kimungu, ambayo ni bora pasipo mfano, kwa kuwa ndiyo yanayotuunganisha na Mungu.

Basi tupande ngazi kwa ngazi hadi uadilifu unaopita maumbile. Tuone kwanza mtu mwenye dhambi ya mauti anavyoweza kuwa na maadili ya bandia, k.mf. kiasi cha mchoyo; yeye anakitekeleza si kwa kupenda uadilifu, bali kwa kupenda fedha. Vilevile akilipa madeni si kwa kutekeleza haki bali kwa kukwepa gharama za kesi.

Juu kuliko hayo maadili ya bandia, mtu mwenye dhambi ya mauti anaweza kuwa na maadili halisi ya kiutu aliyojipatia. Wako wengi wanaofuata kiasi ili kuishi akili inavyotaka, na kwa ajili hiyohiyo wanalipa madeni na kuwalea vizuri watoto wao. Lakini mtu akibaki katika dhambi ya mauti, ni dhaifu katika kutekeleza uadilifu, hata ule wa kiutu. Maadili yake hayana msimamo, kwa kuwa utashi wake haumuelekei Mungu: badala ya kumpenda kupita yote, anajipenda kuliko Mungu. Halafu, maadili mengine yanayotakiwa kuyasaidia hayo hayapo, hivyo yanakosa mshikamano. Anayeendesha gari la kukokotwa na farasi kadhaa, anahitaji kila mmojawao awe amezoea kazi hiyo: vilevile adili moja haliendi bila ya lingine; yote yanahusiana na kuongozwa na busara. Basi, ili maadili ya kiutu yawe imara ni lazima yashikamane, na hiyo inadai mtu asibaki katika dhambi ya mauti, bali utashi wake ulenge kuishi na Mungu; ni lazima ampende kuliko nafsi yake, jambo lisilowezekana pasipo neema ya utakaso. Akiipata tu, maadili yote yanaweza kushikamana na kuwa imara; nayo chini ya upendo yanakuwa chanzo cha matendo yanayostahili uzima wa milele.

Maadili ya Kimungu yanatuinua na kuturekebisha kuhusu lengo lipitalo maumbile na kuhusu njia zipitazo maumbile zinazoweza kulifikia. Bila ya hayo, maadili ya kiutu hayatoshi: kuna tofauti ya dhati kati ya kiasi walichokieleza Wapagani na kile cha Kikristo (k.mf. kati ya ufukara wa mwanafalsafa na ule wa Kiinjili), kwa sababu kanuni na lengo ni tofauti. Cha kwanza kinataka mtu ale tu kipimo cha wastani ili kufuata akili, kutodhuru afya au kufikiri vizuri. Kumbe kiasi cha Kikristo kinamtaka ajipatie chakula ili kuishi kama mtoto wa Mungu, akielekea uzima wa milele; hivyo kinadai maisha magumu zaidi: kinadai mtu autese mwili wake “na kuutumikisha” (1Kor 9:27), kusudi asiwe tu raia mwadilifu wa nchi yake, bali pia mwenyeji “pamoja na watakatifu” na mtu “wa nyumbani mwake Mungu” (Ef 2:19). Tofauti hiyohiyo ipo kati ya adili la ibada linalotakiwa kumpatia Muumba heshima anayostahili, na adili la ibada la Mkristo linalomtolea Mungu, asili ya neema, sadaka ya misa ipitayo maumbile. Kwa kuwa ni tofauti ya ngazi, aina ya kwanza inaweza kustawi mfululizo kwa kurudiarudia vitendo vyake, bila ya kufikia kiwango kidogo cha aina ya pili iliyoinuliwa na neema inayotia utakatifu.

Kinachoongoza maadili hayo mawili yenye jina lilelile ni tofauti: upande mmoja ni akili ya binadamu tu, upande wa pili ni imani iliyomiminwa na Mungu.

Ni malengo mawili tofauti na nia mbili tofauti, ambapo busara haijui nia zipitazo maumbile, ila ikiangaziwa na imani inakuja kuzijua kwa kujua ukuu usio na mipaka wa lengo letu, yaani kumuona Mungu; hapo inakuja kujua uovu wa dhambi ya mauti, thamani ya neema inayotia utakatifu na ya neema za msaada ambazo ziombwe kila siku, na hazina ya sakramenti zilizowekwa kwa faida yetu. Vilevile kuna tofauti kubwa kati ya utaratibu ulioelezwa na mwanafalsafa Aristotle na unyenyekevu wa Kikristo unaozitegemea kweli za imani. Kuna tofauti kubwa kati ya ubikira wa wanawake waliokabidhiwa kuchochea daima moto wa miungu, na ule wa Mkristo aliyejiweka wakfu mwili na moyo kwa Mungu ili kumfuata Yesu kikamilifu zaidi.

Upendo unapoturekebisha tulenge uzima wa milele, unarekebisha maadili pia kuhusu njia zipitazo maumbile za kufikia wokovu. Walioendelea Kiroho wanaongozwa zaidi na kwa namna wazi na hiyo nia ipitayo maumbile, kumbe nia ya kibinadamu ndiyo inayozidi kuwaongoza wengine. Katika dhambi ya mauti mtu anajipenda kuliko Mungu na kwa umimi anaelekea kutotimiza hata wajibu wa kiutu.

Maelekezo ya teolojia ya kiroho

hariri

Hatimaye, tuzingatie Injili na walimu wa Kiroho walivyosisitiza baadhi ya maadili ya kiutu ambayo yanahusiana zaidi na Mungu na kulingana zaidi na maadili ya Kimungu: ibada na toba (zinazompatia Mungu heshima na malipizi anavyostahili), upole (ukiambatana na subira), usafi kamili (au ubikira) na unyenyekevu ambao ukituinamisha mbele ya Mungu unatuinua juu ya ufinyu wa moyo na ya kiburi na kutuelekeza tuzame katika mambo ya Mungu na kuungana naye. “Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu, kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu” (Math 11:29). Yesu tu, kwa jinsi alivyojengeka katika ukweli, aliweza kusema juu ya unyenyekevu wake pasipo kuupoteza papo hapo.

Maadili ya kiutu na yale ya Kimungu (ambayo yayaongoze ya kwanza) ni utendaji wa aina mbalimbali wenye kulingana vizuri ajabu, dhambi nyepesi isipokuja kuvuruga. Sehemu zote za muundo huo wa Kiroho zinakua pamoja kama vidole vya mkono mmoja. Kutokana na mshikamano uliopo maadili yote yanakua pamoja na upendo, hasa maadili ya kumiminiwa, kwa kuwa yale ya kujipatia pengine yanastawi kidogo zaidi yasipofanyiwa mazoezi. Hatuwezi kuwa na upendo mkubwa pasipo unyenyekevu mkubwa; ni kama tawi la juu la mti linalozidi kuinuka kadiri mzizi unavyozidi kupenya ardhi. Tunapaswa kukesha kitu chochote kisije kikaharibu ulinganifu huo, kama inavyowatokea wale ambao wanadumu katika neema inayotia utakatifu lakini wanajali elimudunia na mafungamano na watu kuliko ustawi wa imani, tumaini na upendo wa Mungu.

Ushujaa wa maadili ya kiutu

hariri

Kwa kuwa hatuwezi kueleza ushujaa wa kila adili la kiutu, tutaongea kwanza juu ya ushujaa wa unyenyekevu na upole; maadili hayo yanaleta sura ya Kikristo na kufungua njia ya kusema juu ya ushujaa wa maadili ya nguvu, busara, haki na yale yanayohusu mashauri ya Kiinjili.

Unyenyekevu na upole wa kishujaa

hariri

Unyenyekevu ni wa kishujaa unapofikia ngazi za juu zilizofafanuliwa na Anselm wa Canterbury, yaani si tu kutambua tunastahili dharau pande fulanifulani, bali kutaka watu wasadiki hivyo, kuvumilia waseme hivyo, kupokea dharau zao na hatimaye kupenda tutendwe hivyo, ili tulingane na Bwana aliyechagua kupatwa na aibu kuu za mateso kwa wokovu wetu.

Unyenyekevu huo unadhihirishwa na utaratibu mkubwa wa kudumu: “Kila mtu atatambulikana kwa uso wake; mwenye ufahamu atajulikana kwa sura yake popote umkutapo, nazo nguo za mtu, na finyo la kutoa meno, na mwendo wake, huonyesha mara alivyo yeye mwenyewe” (YbS 19:29-30). Uso mtulivu, mnyenyekevu, usiocheka mno, pamoja na mwendo mzito, mnyofu, usio na unafiki, vinashuhudia kuwa mtu anajisikia daima mbele ya Mungu na kuongea naye kwa ndani. Hivyo aliye mnyenyekevu na mtaratibu kweli anasema juu ya Mungu hata kwa mwenendo wake na kwa kimya chake.

Unyenyekevu wa kishujaa unaendana na kiasi hichohicho cha upole. Kwa njia ya adili hilo mtu anafikia kujitawala kikamilifu, hata kushinda ubaya kwa wema badala ya kuupinga kwa hasira. Ngazi za juu za upole ni kutofadhaishwa na matusi, kufurahia kitakatifu matokeo bora yanayotokana nayo, na hatimaye kumhurumia mtukanaji kwa matokeo mabaya yanayoweza kumpata. Ndivyo Yesu alivyolia juu ya Yerusalemu kwa kuwa ulikosa shukrani; alisikitikia maangamizi ya mji huo kuliko kifo kikatili kitakachompata.

Nguvu ya kishujaa na moyo mkuu

hariri

Ndani ya mtu aliyekamilika unyenyekevu na upole vinaendana na maadili ya nguvu na moyo mkuu ambayo yanaonekana kuwa kinyume chake, kumbe yanakamilishana navyo.

Nguvu ni adili la kiutu linalotuimarisha katika kulenga mema magumu tusiogope mapingamizi makubwa. Inatawala hofu yetu mbele ya hatari, kazi za kuchosha, lawama na yale yote yanayoweza kupooza juhudi za kuelekea mema; halafu inatuzuia tusisalimu amri tunapopaswa kupambana. Nguvu inaratibu pia ushupavu na uchangamfu usiofaa ambavyo vinaelekeza kutenda bila kujali lolote. Matendo yake makuu ni mawili: kukabili hatari na kustahimili magumu. Tunapaswa kuyavumilia kwa upendo wa Mungu, na kwa hakika ni vigumu kustahimili muda mrefu kuliko kujitosa wakati wa kuchangamka.

Nguvu inaendana na subira katika kuvumilia huzuni za maishani bila kuhangaika wala kulalamika, halafu inaendana na ustahimilivu unaovumilia muda mrefu, na udumifu katika kutenda mema ambao ni kinyume cha ukaidi katika kutenda mabaya. Adili la nguvu linahusiana pia na moyo mkuu unaosukuma kutenda makuu katika maadili yote, ukikwepa ulegevu pasipo kuangukia makosa ya kujiamini, kujivuna au kutaka kuringa.

Kipaji cha nguvu kinaliongezea ukamilifu wa juu zaidi na kutuandaa tupokee uvuvio wa Roho Mtakatifu ukija kututegemeza mbele ya hatari, na kuondoa hangaiko la kujisikia hatuwezi kutimiza wajibu mkubwa wala kuvumilia majaribu yanayotukabili. Kipaji hicho kinadumisha “njaa na kiu ya haki” katika hali yoyote. Ushujaa wa adili la nguvu unadhihirishwa hasa na kifodini kinachovumiliwa ili kutetea ukweli wa imani au adili fulani. Nje ya kifodini, adili la nguvu na kipaji cha nguvu, pamoja na subira na moyo mkuu vinatumika kila palipo na haja ya kutenda kishujaa au kuvumilia makubwa. Nguvu hiyo ya Kikristo inatofautiana na uvumilivu wa mwenye kiburi, kwa sababu inaendana na unyenyekevu, upole na unyofu mkubwa. Huo wa mwisho ni wa kishujaa unapopenda ukweli hata kukwepa kila undumakuwili, uongo, ulaghai, utata, ingawa unajua kutunza siri usiseme yale yote yaliyomo moyoni.

Busara ya kishujaa

hariri

Hiyo inazungumziwa kidogo, lakini katika nafasi ngumu busara pia inakuwa ya kishujaa. Adili hilo linahusu utekelezaji wa ukweli, yaani ukweli katika matendo. Ndiyo sababu Bwana alisema, “Iweni na busara kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua” (Math 10:16). Si rahisi kulinganisha kila mara maadili hayo, lakini yote mawili ni ya lazima kwa Mkristo anayetakiwa si tu kuwa mwadilifu kamili, bali kutenda daima kama mwana wa Mungu, akimtegemea kikamilifu na kuzidi kujua anavyomtegemea. Busara ya Kikristo katika ngazi ya juu inajua wazi mema yanayompasa mtoto wa Mungu, na inaelekeza kwa imara maadili mengine yayatende kitakatifu. Wanaolenga ukamilifu wanatakiwa kulenga maadili yote kwa ngazi ya juu, jambo linalodai kiwango hichohicho cha busara walau kuhusu utakatifu wao wenyewe. Adili hilo ni la lazima zaidi kwa wale wanaopaswa kushauri na kuongoza wengine.

Tunapoiamini mno busara yetu, Mungu akitaka kututakasa anatuacha tuangukie makosa ya wazi, au tusahau au kutozingatia mambo, na matokeo yake yanatuaibisha. Baada ya takaso hilo busara inaweza ikawa ya kishujaa na kuongozana na kiwango cha juu cha kipaji cha shauri ambacho tunapokea uvuvio wa Kimungu wa kuhisi la kufanya katika nafasi ngumu.

Inatokea vile Bwana anapomfanya mtumishi wake atende namna ambazo wengi wanaona hazina busara, k.mf. Mt. Fransisko wa Asizi katika kupenda ufukara. Ndivyo walivyofanya wale wote ambao kwa uvuvio wa Mungu walikabili kazi ngumu zaidi, kama kuokoa makahaba au majambazi hata kuwafanya watawa; hapo walijikuta katika nafasi ambapo kutenda na kutotenda kulionekana vilevile kukosa busara, hata iliwapasa kumuomba Bwana uvuvio wa kipaji cha shauri, pamoja na kutulia mikononi mwake. Busara kamili haitenganiki na sala ya kudumu kwa kupata mwanga wa Mungu; vilevile inaelekeza kusikiliza mashauri mazuri ya wanaoweza kutuangazia na inadhihirisha ukomavu wa roho.

Kuhusu mambo ya pekee yapitayo maumbile, busara halisi inachukua tahadhari: haiyakanushi kimsingi, bali inayapima na kuyatolea tamko pale tu inapolazimika na baada ya kumuomba Mungu mwanga. Busara hiyo ya hali ya juu inadhihirika pia katika kupima miito ya pekee. Ushujaa wa adili hilo unadhihirika hasa katika matendo ambayo binadamu anayaona hayana busara, kumbe matokeo yake yanakuja kuonyesha yalivyokuwa na busara ya juu. Ndivyo Mwokozi alivyowatuma mitume wake kumi na wawili waongoe ulimwengu bila chombo chochote cha kibinadamu.

Haki ya kishujaa

hariri

Ili tupate picha ya haki kamili tukumbuke adili hilo halikatazi tu wizi na utapeli, bali pia uongo wowote, unafiki, ulaghai, kuvunja siri, kuwakosea watu heshima kwa masingizio, masengenyo na vitendo, kuwahukumu bila msingi na kuwacheka kwa dharau. Mara nyingi haki yetu ina dosari tunapoitekeleza walau kiasi kwa faida yetu, k.mf. tukilipa madeni ili kukwepa pia gharama ya kesi, au tukisema ukweli kwa kuzingatia usumbufu unaoweza ukatokana na uongo. Hapo inahitaji kutakaswa kama maadili mengine yote. Haki kamili inahitajiwa na wale wanaolenga muungano wa dhati na Mungu, kwa kuwa wanatakiwa wasiwe na kosa lolote dhidi ya wenzao bali watimize wajibu wowote wa haki na upendo kwao. “Uishindanie kweli hata kufa, naye Bwana atakupigania wewe. Usiwe mwepesi wa kunena, mlegevu wa kutenda, msahaulifu. Usiwe kama simba nyumbani mwako, mwenye kutuhumu watumishi wako. Mkono wako usinyoshwe kupokea, ukarudishwa wakati wa kulipa” (YbS 4:28-31).

Mtu aliyefikia hatua ya muungano anatakiwa kutimiza kishujaa aina zote za haki, zikiwa ni pamoja na usawa. Ashike kikamilifu sheria zote za Mungu na za kibinadamu, za Kanisa na za nchi. Akipaswa kugawa mema au mizigo, afanye hivyo kadiri ya stahili za kila mmoja, asijali undugu wala urafiki. Aepe dhara lolote kwa yeyote. Haki ya kishujaa inadhihirika hasa pale ambapo ni vigumu kuipatanisha na mapendo ya dhati: kwa mfano jaji anapotakiwa kumhukumu mwanae mwenye makosa; au mkubwa anapotakiwa kumtuma mwanae mpenzi wa Kiroho mahali pa mbali na pa hatari.

Ushujaa wa maadili ya kitawa

hariri

Adili la ibada linadhihirika kuwa la kishujaa mtu anapotimiza wajibu alionao upande huo bila kujali upinzani mkali wa ndugu wa ukoo na wengineo. Linadhihirika vilevile katika utekelezaji wa nadhiri ya kutenda yaliyo bora, na katika uanzilishi wa familia ya kitawa kati ya matatizo makubwa ambayo kwa kawaida yanaendana nao.

Ufukara wa kishujaa unajinyima vyote, ukiridhika na riziki za lazima tu, ili kufanana na Bwana ambaye hakuwa na mahali pa kupumzikia. Asiyetamani chochote hakosi kitu, ni tajiri Kiroho na mwenye heri. Usafi wa moyo wa kishujaa unadhihirika hasa katika ubikira wa kudumu, mtu anapoishi mwilini maisha ya Kiroho tu hata akasahau vurugu zote za hisi kwa kuzoea kuzishinda. Hatimaye utiifu wa kishujaa unadhihirika katika kujikatalia kikamilifu matakwa ya binafsi, mtu asipofanya chochote bila ruhusa ya wakubwa, akiwatii wote bila kujali walivyo, hata wasipomuonyesha wema. Pengine anadaiwa kutii maagizo magumu, kama vile Abrahamu alivyodaiwa sadaka ya mwanae pekee. Hapo anahitaji imani kubwa ambayo imuonyeshe Mungu ndani ya wakili wake. Ni nafasi ya giza ambayo ikivukwa vizuri inaleta mwanga mkubwa, kwa kuwa Bwana anamlipa kwa ukarimu yule anayetii hivyo.

Basi, ni wazi jinsi ushujaa wa maadili ya kiutu unavyoyafanya yatumikie upendo na kuandaa muungano wa dhati na Mungu.

Viungo vya nje

hariri