Vita vya kwanza vya Italia na Ethiopia

Vita vya kwanza vya Italia na Ethiopia vilitokea kati ya Italia na Ethiopia miaka 1895-1896. Waethiopia walishinda na kuhakikisha uhuru wa nchi yao hivyo kufanya Ethiopia nchi ya pekee ya Afrika iliyofaulu kuzuia ukoloni[1].

Picha ya Kiethiopia inayoonyesha mapigano ya Adowa
Negus Menelik II kwenye mapigano ya Adowa - mchoro katika gazeti la Kifaransa Le Petit Journal.
Gazeti la Kifaransa "La Vie Illustree" linaloonyesha sherehe ya mwaka 1904 ya wanajeshi Waethiopia kwenye maandamano kukumbuka ushindi wa Adowa.

Mwaka 1889 mtemi wa Shewa Menelik II alijitangaza Negus wa Ethiopia baada ya kushinda mapigano kati ya watemi wa Ethiopia yaliyofuata kifo cha Negus aliyemtangulia Yohane IV. Katika hilo Menelik alisaidiwa na Waitalia ambao walikuwa wameshika Eritrea tayari.

Mnamo Mei 1889 Menelik alifanya mkataba wa Wuchale alimokubali utawala wa Italia juu ya kanda ya pwani pamoja na maeneo kadhaa ya nyanda za juu za Tigray yakiwemo mazingira ya Asmara ya leo.

Italia ilidai, kutokana na nakala ya Kiitalia ya mkataba huo, haki ya ulinzi juu ya Ethiopia[2]. Nakala ya Kiethiopia haikuonyesha vipengele kuhusu ulinzi wa Italia juu ya ufalme wa Ethiopia[3]. Menelik aliimarisha utawala wake na mwaka 1893 alikana mkataba.

Italia ilijibu kwa kuvamia Ethiopia kwa jeshi kubwa mnamo Oktoba 1895. Menelik aliweza kukusanya takriban wanajeshi 100,000 na kuwaongoza hadi Tigray (jimbo jirani na Eritrea)[4].

Mapigano ya kwanza ndani ya Tigray ya Amba Alagi (7 Desemba) na ya Mekelle hayakuenda vizuri kwa Waitalia. Waethiopia walishindwa kuteka boma la Mekelle, lakini Waitalia walifungwa ndani kwa wiki tatu. Mwishowe waliondoka baada ya mapatano na Negus Menelik II na kurudi Eritrea[5].

Sehemu kubwa ya jeshi la Italia haikuingia bado katika mapigano. Gavana jenerali Oreste Baratieri alikataa kuwashambulia Waethiopia baada ya kujua idadi yao kubwa. Lakini alijua ya kwamba Menelik hataweza kulisha askari wengi hivi kwa muda mrefu katika milima ya Tigray, akataka kusibiri hadi jeshi la Negus litakapoanza kusikia njaa na kupungua.

Lakini serikali ya Roma ya waziri mkuu Francesco Crispi, baada ya kupokea habari za mapigano ya kwanza, iliona aibu ya kushindwa na Waafrika ikamwamuru gavana ashambulie mara moja.

Mapigano ya Adowa hariri

Baratieri aliongoza jeshi lake la vikosi vinne katika milima ya Tigray.

Jeshi lake lilikuwa na vikosi vitatu vya Waitalia na kikosi kimoja cha askari kutoka Eritrea. Jumla ya wanajeshi ilikuwa 17,700 na mizinga 65. Hii ilikuwa nusu ya Waitalia wote waliopatikana katika Eritrea.

Baratieri alijua ya kwamba kulikuwako kambi kubwa ya Waethiopia karibu na mji wa Adowa, alitaka kuwashambulia asubuhi wakati wa kucha kabla hawajaamka. Lakini vikosi vyake vilipotea njia gizani: waliposogea mbele usiku hawakufika kwa utaratibu mzuri mahali walipokutana na jeshi la Negus.

Jeshi la Menelik lilikuwa la wanajeshi 80,000 hadi 100,000. Wengi wao walikuwa na bunduki zilizonunuliwa katika miaka iliyotangulia na Menelik kutoka kwa wafanyabiashara Waitalia.

Wakati wa asubuhi wa tarehe 1 Machi 1886 kikosi cha kwanza cha askari Waeritrea chini ya maafisa Waitalia kiligonga moja kwa moja kambi la Ras Alula aliyekuwa tayari. Makelele yaliamsha Waethiopia wote waliochukua haraka nafasi zao juu ya milima wakiwashambulia Waitalia waliosogea mbele bondeni.

Baada ya masaa sita mapigano yalikwisha. Waitalia walishindwa, wengi kuuawa na wengine walikimbia wakirudi Eritrea. Wanajeshi wao 7,000 waliuawa na 1,500 kujeruhiwa, 3,000 wakawa wafungwa, kati yao jenerali mmoja. Waethiopa walipoteza watu 4,000 - 5,000 na 8,000 kujeruhiwa. Waitalia walipaswa kuacha nyuma mizinga yote, bunduki 11,000 na vifaa vingi.

Menelik hakuwafuata Waitalia ndani ya Eritrea. Sababu hazieleweki waziwazi lakini wataalamu hutaja sababu mbalimbali:

  • Menelik alijua hata kama angewafukuzwa Waitalia wote katika Eritrea angejiweka katika hatari ya kuletwa kwa jeshi lote la Italia dhidi yake, kwa sababu Italia ingejaribu kuondoa aibu. Alijua ya kwamba asingeweza kushinda vita kamili dhidi ya nchi iliyoendelea.
  • Menelik alikuwa ameandaa kuvunja jeshi kabla ya mapigano juu ya upungufu wa vyakula Tigray na kutokana na idadi kubwa ya wanajeshi wake kuwa wenyeji wa sehemu zingine. Pia Menelik aliona vigumu kulisha jeshi kubwa kiasi hicho.
  • Menelik alikumbuka mkataba wake wa kwanza alimokubali utawala wa Italia katika Eritrea.

Baada ya mapigano hariri

Waethiopia waliwatendea wafungwa Wazungu vizuri lakini walikata askari wafungwa Waeritrea 800 mkono na mguu wa kuume.

Baada ya habari hizi kufika Italia serikali ya Crispi ilipinduliwa. Serikali mpya ilipaswa kukubali uhuru wa Ethiopia katika mkataba wa amani tarehe 26 Oktoba 1896. Ethiopia ilikubali mamlaka ya Italia juu ya koloni lake katika kaskazini. Wafungwa walirudishwa.

Ushindi wa Menelik ulihakikisha uhuru wa Ethiopia kama nchi pekee pamoja na Liberia isiyowekwa chini ya ukoloni wa Ulaya katika bara la Afrika.

Marejeo hariri

  1. "5 Fascinating Battles of the African Colonial Era". Encyclopaedia Britannica. https://www.britannica.com/list/5-fascinating-battles-of-the-african-colonial-era. Retrieved 14 June 2020.
  2.  Gardner, Hall (2015). The Failure to Prevent World War I: The Unexpected Armageddon. Ashgate. ISBN 978-1-4724-3058-8, uk.107
  3. Gardner 2015, p. 107
  4.  Marcus, Harold G. (1995). The Life and Times of Menelik II: Ethiopia 1844–1913. Red Sea Press. ISBN 978-1-56902-010-4, uk 160}}
  5.  Prouty, Chris (1986). Empress Taytu and Menilek II: Ethiopia 1883–1910. Red Sea Press, uk. 144–151