Bruno Mkartusi

(Elekezwa kutoka Bruno wa Cologne)

Bruno Mkartusi (Cologne, Ujerumani, 1030 hivi - Serra San Bruno, Italia, 6 Oktoba 1101) alikuwa padri na mmonaki wa Kanisa Katoliki aliyeanzisha shirika la kitawa ambalo linadumu mpaka leo (Wakartusi).

Mtakatifu Bruno.
Bruno, mwanzilishi wa Wakartusi.

Kisha kufundisha teolojia nchini Ufaransa, akitamani maisha ya upwekeni, alianzisha na wanafunzi wake wachache katika bonde la Chartreux shirika ambapo upweke uendane na kiwango kidogo sana cha maisha ya kijumuia.

Ingawa aliitwa Roma na Papa Urbano II, ili kumsaidia kukabili mahitaji ya Kanisa, alifaulu kutumia miaka yake ya mwisho upwekeni karibu na monasteri ya La Torre huko Calabria[1].

Tangu kale anaheshimiwa kama mtakatifu. Papa Leo X aliidhinisha kwa sauti tu heshima hiyo kwa Wakartusi tarehe 19 Julai 1514, halafu tarehe 17 Februari 1623 Papa Gregori XV alieneza heshima hiyo kwa Kanisa Katoliki lote.

Sikukuu yake inaadhimishwa katika tarehe ya kifo chake[2].

Maisha

hariri

Bado kijana alikwenda Reims (Ufaransa), ambapo mwaka 1057 askofu Gervas alimkabidhi uongozi wa shule iliyomlea.

Mwaka 1076 aliacha shughuli zake shuleni na jimboni (kama katibu mkuu) akamkimbilia mtawala mdogo Ebal wa Roucy, kutokana na askofu Manase wa Gournay kumchukia kwa sababu ya kumlaumu kwa kosa la usimoni. Aliweza kurudi Ufaransa mwaka 1080 tu, baada ya Manase kuondolewa na mtaguso maalumu.

Wito wa kimonaki

hariri

Katika miaka hiyo migumu, ndipo wito wake wa kimonaki ulipojitokeza. Katika barua yake mojawapo Bruno alisimulia jinsi alivyoweka nadhiri ya kujitoa wakfu kwa Mungu pamoja na marafiki wawili.

Kisha kurudi Ufaransa, alikwenda kwenye makao ya upwekeni ya Molesme, chini ya uongozi wa Roberto wa Molesme, mwanzilishi wa urekebisho wa Citeaux wa shirika la mtakatifu Benedikto. Halafu, pamoja na wenzi sita (mapadri 4 na mabruda 2), alitafuta mahali pa faragha kabisa ili kuanzisha monasteri, akapewa na askofu wa Grenoble, Ugo wa Grenoble, ambaye alisukumwa na njozi. Eneo hilo la kufaa lilikuwa bonde katika milima iliyoitwa «Cartusia» (kwa Kifaransa «Chartreuse»).

Kartusi

hariri

Monasteri ilianza kujengwa katikati ya mwaka 1084, kwenye mita 1175 juu ya usawa wa bahari. Kanisa tu lilijengwa kwa mawe, ili liweze kuwekwa wakfu, kama ilivyofanyika mwaka 1085.

Miaka sita baadaye Papa Urban II, aliyekuwa mwanafunzi wake huko Reims, alimuita Roma, atumikie Ukulu mtakatifu. Bruno hakuweza kukataa, hivyo aliacha upweke kwa wenzake.

Huko Italia

hariri
 
Mt. Bruno alivyochongwa na Manuel Pereira (1652, R.A.B.A.S.F., Madrid, Hispania).
 
Bruno akikataa uaskofu alivyochorwa na Vicente Carducho, Museo del Prado (Hispania).

Bruno alipotii wito wa Papa, alihisi kuwa jumuia yake kwa kukosa uongozi wake itaingia jaribuni; na kweli ilisambaratika. Lakini alifaulu kuwarudisha Kartusi waendelee chini ya Landuino.

Pamoja na hayo, Bruno hakuweza kuzoea mazingira na majukumu ya Roma, akitamani kurudi upwekeni.

Urbano II alipokimbia Roma, kutokana na kaisari Henri IV kuvamia Dola la Papa na kumteua antipapa Klementi III, Bruno alimfuata Papa Italia Kusini.

Kwa pendekezo la Papa, alichaguliwa askofu mkuu wa Reggio Calabria, lakini alikataa.

Hatimaye alikubaliwa kwenda upwekeni Italia kusini.

Katika mkoa wa Calabria

hariri

Mwaka 1090 mtawala Roger I wa Sicilia alimtolea eneo kwenye mita 790 juu ya usawa wa bahari, mahali palipoitwa Torre, leo Serra San Bruno, katika mkoa wa Calabria.

Huko Bruno alianzisha makao ya upwekeni ya Mtakatifu Maria, na karibu kilometa 2 bondeni - ambapo leo ipo Certosa di Serra San Bruno - alianzisha kwa ajili ya mabruda monasteri ya Mtakatifu Stefano.

Halafu, mwaka 1094 hivi, Roger alipompatia msaada wa familia ya Mulè, Bruno aliipangia mahali pa mbali kidogo, ambapo sasa ipo Serra San Bruno.

Bruno, akirudia maisha aliyoyacha Ufaransa, alimalizia maisha yake kwa miaka 10 upwekeni. Wakati huo alitembelewa na Landuino, mwandamizi wake huko Kartusi.

Mnamo Juni 1101 Roger alifariki dunia, akiwa na Bruno karibu naye. Tarehe 6 Oktoba Bruno pia akafariki, akizungukwa na wafuasi wake.

Tazama pia

hariri

Tanbihi

hariri

Viungo vya nje

hariri
  Makala hii bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.