Bwana Heri
Bwana Heri bin Juma (pia: bana Heri) alikuwa sultani wa Saadani iliyokuwa bandari ya biashara kwenye mwambao wa Bahari Hindi (katika Tanzania kaskazini-mashariki ya leo) tangu miaka ya 1870.
Bwana Heri | |
Bwana Heri na wanawe mnamo 1890] | |
Nchi | Tanzania |
---|---|
Kazi yake | sultani |
Mtawala wa Saadani
haririKatika sehemu ya pili ya karne ya 19 Saadani iliona kuongezeka kwa biashara yake kwa sababu, pamoja na Pangani na Bagamoyo, ilikuwa moja ya bandari ya Mrima zilizokuwa karibu na Zanzibar. Saadani kama miji mingine ya pwani ilifaidika na biashara ya misafara iliyoleta bidhaa kutoka nchi za mbali na kulipa ushuru.
Bwana Heri alipaswa kumtambua Sultani wa Zanzibar kama mkubwa lakini akafaulu kutetea nafasi yake kama mtawala aliyejitegemea. Mwaka 1882 aliweza kushinda jeshi la Sultani Sayyid Bargash aliyetaka kutawala Saadani moja kwa moja.
Kati ya wageni wengi waliopita Saadani alikuwepo pia mpelelezi kijana kutoka Ujerumani, kwa jina Hermann von Wissmann, aliyefika mwaka 1881 akisafiri pamoja na Tippu Tip na kurudi miaka kadhaa baadaye akiwa na cheo tofauti.
Kuja kwa Wajerumani
haririMwaka 1888 Sultani Sayyid Khalifa wa Zanzibar alikodisha eneo lake katika bara kwa Kampuni ya Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki. Kampuni hiyo ilipewa kazi ya kukusanya kodi zote na maafisa wake walianza kazi yao kwa ukali. Bwana Heri, pamoja na viongozi wengine, aliona amesalitiwa na Sultani hakuwa tayari kukubali utawala wa Wajerumani.
Vita ya Abushiri
haririUpinzani dhidi ya Wajerumani na pia Sultani wa Zanzibar ilianzia Pangani ukiongozwa na Abushiri. Bwana Heri aliunga mkono upinzani wa Abushiri dhidi ya Wajerumani akipata usaidizi wa makabila ya eneo lake, hasa Wazigua.
Wajerumani walituma kikosi cha kijeshi chini ya mpelelezi wa awali Hermann von Wissmann aliyekuwa na silaha za kisasa. Wissmann alishambulia Saadani tarehe 6 Juni 1889 na Bwana Heri alipaswa kukimbia. Aliendela na vita ya msituni.
Baada ya kushambuliwa tena na jeshi la Wajerumani katika Januari na Machi 1890 uwezo wake ulikwisha. Sayyid Khalifa aliwasiliana naye na Wissmann akatayarisha kujisalimisha kwake tarehe 6 Aprili 1890. Wissmann alimkumbuka Bwana Heri tangu ziara yake ya mwaka 1881 akamheshimu kama mtawala. Hivyo hakumwua kama Abushiri kwa sababu alimwona kama mtawala halali aliyeshindwa katika vita akamwambia kujenga Saadani upya.
Upinzani wa wenyeji ulishindwa lakini ulisababisha mwisho wa utawala wa kampuni ambayo ilionekana haina uwezo kukandamiza uasi wa Waafrika. Serikali ya Ujerumani iliamua kuchukua utawala wa Afrika ya Mashariki ya Kijerumani mikononi mwake kama koloni la serikali ya Ujerumani.
Mwisho wake
haririMwaka 1894 Bwana Heri alijaribu tena kupambana na Wajerumani lakini alishindwa kwa mara ya pili. Akaondoka bara kwenda Dodoma alipokufa baadaye.
Viungo vya nje
hariri- Maisha ya Bwana Heri (Kiingereza) Archived 27 Septemba 2007 at the Wayback Machine.
Makala hii kuhusu mtu huyo bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Bwana Heri kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |