Historia ya Malawi
Historia ya Malawi inahusu eneo la Afrika Mashariki ambalo wakazi wake leo wanaunda Jamhuri ya Malawi.
Wakazi wa kwanza wa Malawi walikuwa wawindaji-wakusanyaji Wasan.
Katika karne ya 10 BK walifika Wabantu wenye ujuzi wa kilimo na uhunzi. Wengi walizidi kuelekea kusini, lakini wengine walihamia nchini.
Hakuna habari za kimaandishi kabla ya kufika kwa Wazungu. Tangu karne ya 16 ufalme wa Wamaravi ulikuwepo upande wa kusini wa ziwa.
Wamaravi walipanua utawala wao. Lakini katika karne ya 19 walishambuliwa sana na Wayao walioendesha biashara ya watumwa wakiwakamata katika eneo la ziwa na kuwapeleka hadi pwani ya Bahari Hindi kama vile Kilwa.
Mwaka 1859 Mwingereza David Livingstone alifika ziwani.
Wamisionari walimfuata, hasa Wapresbiteri kutoka Uskoti, waliotafuta wafuasi wa Ukristo na kumpambana na wafanyabiashara ya utumwa.
Mwaka 1891 serikali ya Uingereza iliweka nchi upande wa magharibi na kusini kwa ziwa chini ya ulinzi wake ikawa „Nyassaland Protectorate“, halafu tangu 1907 koloni la Unyasa.
Wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia Waingereza waliogopa kushambuliwa kutoka Afrika ya Mashariki ya Kijerumani wakachukua hatua za kudai huduma za nyongeza kutoka kwa wananchi. Hii ilisababisha ghasia ya John Chilembwe dhidi ya wakoloni.
Baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia Waingereza waliunganisha Unyasa na Rhodesia (leo Zambia na Zimbabwe) kuwa Shirikisho la Afrika ya Kati mwaka 1953. Shirikisho hilo halikudumu hadi mwisho wa ukoloni kutokana mielekeo tofautitofauti katika sehemu tatu za shirikisho.
Katika Unyasa daktari Hastings Kamuzu Banda alijitokeza kuwa mwanasiasa aliyependelewa na wananchi wengi, akawa waziri mkuu wakati wa Unyasa kupata madaraka ya kujitawala katika mambo ya ndani na baadaye rais wa kwanza wa taifa.
Mwaka 1964 Unyasa (Nyassaland) ilikuwa nchi huru kabisa lakini bado sehemu ya Jumuiya ya Madola chini ya malkia wa Uingereza kwa miaka miwili ya kwanza.
Mwaka 1966 Banda alitangaza kura ya katiba mpya iliyopokewa na wananchi. Nchi ilipata jina la Malawi na chama cha Malawi Congress Party kikawa chama pekee.
Banda aliendelea kutawala, akatangazwa kuwa rais kwa muda wote wa maisha yake mwaka 1971.
Mabadiliko ya kimataifa baada ya kuporomoka kwa Ukomunisti na ukuta wa Berlin miaka 1989/1990 yalileta shinikizo kote Afrika dhidi ya serikali zilizofuata mtindo wa chama kimoja. Shinikizo hilo lilimkuta Banda mzee na mgonjwa ilhali watu wa familia yake wakitawala kupitia yeye. Hali ya uchumi ilikuwa duni, rushwa na magendo juu.
Mwaka 1993 serikali yake ililazimishwa kukubali kura ya wananchi wote walioamua kumaliza mfumo wa chama kimoja na kuanzisha kipindi kipya.
Uchaguzi huru wa mwaka 1994 ulimaliza utawala wa MCP ukamfanya Bakili Muluzi wa United Democratic Front (UDF) ndiye rais aliyechaguliwa mara ya pili 1999.
Katika uchaguzi wa mwaka 2004 alishinda tena mgombea wa UDF, ndiye Bingu Mutharika aliyeapishwa kuwa rais wa Malawi tarehe 24 Mei 2004 huko Blantyre.
Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Historia ya Malawi kama enzi zake au matokeo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |