Historia ya Surinam
Historia ya Surinam inahusu eneo hilo la Amerika Kusini linalounda jamhuri ya Surinam.
Waindio, Wahispania na Waingereza
haririWakazi asilia wa Surinam walikuwa Waindio hasa Waarawak na Wakaribi waliokalia sehemu za pwani na savana.
Mwaka 1498 Kristoforo Kolumbus alipita mwambaoni akifuatwa mwaka 1499 na Amerigo Vespucci. Msafara wa upelelezi sehemu za bara ulifanywa na Wahispania mwaka 1500.
Mwaka 1651 Waingereza walijenga kituo cha kwanza cha kudumu kwenye mdomo wa mto Surinam (karibu na Nieuw Amsterdam wa leo) kilichotekwa na Waholanzi mwaka 1667. Kutokana na mkataba wa amani ya Breda wa mwaka uleule eneo hili lilibadilishwa na eneo la New York (Marekani) ya leo iliyowahi kukaliwa na Waholanzi.
Utawala wa Uholanzi
haririHivyo Surinam ya leo imekuwa koloni la Uholanzi tangu mwaka 1667 kwa jina la "Guyana ya Kiholanzi". Wakati ule ilikuwa pamoja na Guyana ya leo (1815-1966: Guyana ya Kiingereza).
Waholanzi waliendeleza biashara ya mashamba makubwa ya miwa, pamba, kokoa na kahawa wakitumia kazi ya watumwa Waafrika.
Kati ya miaka 1799 hadi 1815 Uholanzi ilivamiwa na Ufaransa na kutawaliwa kama sehemu ya himaya ya Napoleoni. Wakati ule Uingereza ilitwaa makoloni ya Uholanzi na kuyatawala.
Baada ya Mkutano wa Vienna (1815) Surinam ilirudishwa lakini Guyana ya leo ilibaki kama koloni la Guyana ya Kiingereza.
Utumwa na kutokea kwa Wabusinenge
haririKati ya Waafrika wengi waliolazimishwa kuwafanyia kazi mabwana wa mashamba makubwa wengine walifaulu kutoroka na kukimbia porini. Huko walianzisha makazi yao na kuishi maisha huru. Katika Guyana waliitwa Wabusinenge au "Bosneger" ("Weusi wa porini"). Walianzisha makabila mapya na kuchagua viongozi wao.
Historia yao ilianza baada ya Waingereza kuanzisha mashamba ya kwanza walipotumia kazi ya watumwa. Kuna taarifa ya mwaka 1690 ya kuwa kikosi cha Weusi wa porini walishambulia shamba la Imanuel Machato kwenye mto Cassewijne, kumwua na kuondoka na watumwa wake. Waholanzi na pia Waingereza walijaribu mbinu mbalimbali kuwashinda wale Weusi wa porini walioonekana kuwa tishio kwa utaratibu wa utumwa na uchumi wa kikoloni.
Lakini kuanzia mwaka 1749 Waholanzi walijaribu kupatana na Wabusinenge na mwaka 1760 kukawa na mkataba wa amani wa kwanza ambamo serikali ya kikoloni ilikubali uhuru wa kabila moja la Wabusinenge. Wale waliahidi kutopokea watumwa wapya wakimbizi bali kuwarudisha kwa Waholanzi.
Katika koloni jirani la Kiholanzi la Berbice (leo: Guyana) kulitokea uasi mkubwa wa watumwa dhidi ya mabwana wao kuanzia tarehe 23 Februari 1763. Wazungu wote waliacha mashamba yao na kukimbilia mjini walipoweza kujihami. Watumwa wengi waliondoka na kujificha porini baada ya kufika kwa wanajeshi Waholanzi waliokuja kukandamiza ghasia hiyo.
Mwisho wa utumwa na wafanyakazi kutoka Asia
haririTarehe 1 Julai 1863 Uholanzi ulifuta utumwa na watumwa 35,000 walipewa uhuru lakini walipaswa kuendelea kama wafanyakazi kwa muda wa miaka 10.
Baadaye wengi wao hawakutaka tena kufanya kazi mashambani. Hivyo wafanyakazi walitafutwa Uhindi, Uchina na katika koloni la Uhindi ya Mashariki ya Kiholanzi (leo: Indonesia). Ndiyo asili ya sehemu kubwa ya wakazi wa Surinam ya leo.
Uhuru
haririMwaka 1954 Surinam pamoja na Antili za Kiholanzi ilipewa madaraka ya kujitawala.
Tangu mwaka 1973 kulikuwa na majadiliano kuhusu uhuru kamili uliopatikana tarehe 25 Novemba 1975. Serikali za kwanza zilikuwa na matatizo ya kisiasa. Wakazi wengi sana -jumla 1/3 ya wananchi- walihamia Uholanzi kwa hofu ya kwamba mambo yatakuwa mabaya.
Udikteta na vita vya wenyewe kwa wenyewe
haririBaada ya miaka minne ya kwanza kulitokea mapinduzi ya kijeshi tarehe 25 Februari 1980. Serikali ya kijeshi iliongozwa na soli Desi Bouterse.
Awali wananchi wengi na pia serikali ya Uholanzi walikubali watawala wapya. Lakini tangu mwaka 1982 mbinu za mabavu na unyama zilionekana kwa kuuawa kwa wapinzani mbalimbali.
Mwaka 1985 kikundi cha Wabusinenge chini ya Ronnie Brunswijk waliojiita "Jungle Comando" kilianza vita vya msituni dhidi ya serikali. Vita vilipigwa kwa ukatili na unyama miaka miwili hadi shinikizo kutoka nchi za nje -hasa Uholanzi- lililazimisha serikali kukubali uchaguzi huru.
Uchaguzi wa Novemba 1987 ulileta ushindi wa vyama vya upinzani vilivyoanzisha serikali mpya chini ya Ramsewak Shankar. Lakini Bouterse alifanya mapinduzi tena na kumwondoa Shankar madarakani tarehe 24 Desemba 1990.
Hali ya wasiwasi iliendela hadi uchaguzi mpya wa 1991 ulioleta serikali ya Ronald Venetiaan.
Mnamo Agosti 1992 mkataba wa amani ulisainiwa na wapinzani wa "Jungle Comando" na kumaliza kipindi cha vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Historia ya Surinam kama enzi zake au matokeo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |