Julius von Soden
Julius von Soden (5 Februari 1846 - 2 Februari 1921) alikuwa mwanasiasa wa Ujerumani aliyetawala makoloni mawili ya nchi hiyo barani Afrika: Kamerun na Afrika ya Mashariki ya Kijerumani. Baadaye alikuwa waziri kwenye serikali ya Ufalme wa Württemberg katika Ujerumani kusini-magharibi.
Maisha
haririJulius alizaliwa katika kambi la jeshi huko Ludwigsburg kusini-magharibi mwa Ujerumani. Baba yake alikuwa luteni kanali kwenye jeshi la Ufalme wa Württemberg. Familia walikuwa Wakristo wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri.
Mnamo mwaka wa 1849 familia ilihamia Stuttgart. Wazazi wake walifariki mapema. Mama yake Marie von Neurath aliaga dunia tarehe 28 Machi 1849, na baba yake Julius tarehe 13 Aprili 1854. Soden na dada zake watatu wakubwa walilelewa na bibi Charlotte von Neurath, mjane wa Waziri wa Sheria wa Württemberg.
Soden alianza shule Korntal, kisha akaenda sekondari huko Stuttgart. Mwalimu wake wa kwanza Julius Klaiber na walimu kwenye shule ya sekondari walimlea kwa upendo kwa elimu ya tamaduni za Ugiriki na Roma ya Kale. Katika maisha yake yote, Soden alipenda kusoma vitabu vya waandishi wa kale, hasa Homer na Dante. Mtazamo wake wa ulimwengu ulikuwa ukiathiriwa na mtheolojia David Strauss na mwanafalsafa Emmanuel Kant.
Baada ya kuhitimu shule mwaka wa 1864, Soden alianza kujifunza sheria katika Chuo Kikuu cha Tübingen, lakini baadaye alihamia Göttingen.
Wakati wa Vita ya Austria na Prussia ya 1866 alijikuta kwenye matata maana Julius alipenda siasa ya waziri mkuu wa Prussia, Otto von Bismarck, wakati familia yake ilipenda Austria. Alibaki Göttingen kwa maelezo kwamba haikuwa rahisi kusafiri wakati wa vita, akarudi Tübingen kwa ajili ya mitihani yake mwaka 1869.
Baada ya mtihani wa chuo alianza kazi ya sheria huko Heilbronn. Ilipofika Vita ya Ufaransa dhidi ya Ujerumani ya 1870 Soden alijitolea akihudumu katika wapandafarasi wa Württemberg. Wakati wa amani alirudi kwenye kazi yake ya sheria hadi kumaliza mtihani wa pili katika mfumo wa Ujerumani mwishoni mwa 1871.
Huduma ya kibalozi
haririTokeo la ushindi juu ya Ufaransa lilikuwa umoja wa Ujerumani na kuundwa kwa Dola la Ujerumani. Dola jipya lilianza kutuma mabalozi kwenye nchi za kigeni. Soden alitumia nafasi hiyo akapata ajira kama mwanadiplomasia Bukarest mnamo 1871. Baada ya nusu mwaka alihamishwa Algiers aliposimamia ubalozi mdogo ulioanzishwa huko (1872).
1876 alihamishwa tena kwenda Kanton (leo:Guangzhou) na Hong Kong, 1879 alikwenda Havana. Uhamisho kwenda Lima (Peru) ulifuata 1881/82 kama makamu wa balozi na mwanzo wa 1884 alitumwa Sankt Petersburg. [1]
Katika kazi yake alijifunza kwamba uendelezaji wa mawasiliano ya biashara ulipaswa kufanywa na wafanyabiashara, sio na wanadiplomasia.
Gavana wa koloni
haririAfrika ya Magharibi
haririMwaka 1884 Ujerumani ilianzisha koloni yake ya kwanza huko Afrika ya Magharibi. Mnamo Julai 1884 Soden aliteuliwa kuwa kamishna mkuu wa koloni ya Kijerumani ya Togo . Mwaka uliofuata alipewa pia kazi ya kuwa gavana wa kwanza wa Kamerun. Kabla ya kusafiri kwa meli, von Soden alishauriwa na mmisionari Friedrich Fabri na makampuni yaliyofanya biashara Afrika Magharibi.
Afrika ya Mashariki
haririBaada ya kuondoka kwa chansela Bismarck Soden alipenda kustaafu lakini chansela mpya Leo von Caprivi alimteua kutembelea Afrika ya Mashariki ya Kijerumani na kumpa taarifa kuhusu hali ya eneo hili; koloni iliwahi kuanzishwa na kampuni ya kibinafsi, Kampuni ya Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki iliyoongozwa na Karl Peters tangu mwaka 1885. Lakini ukali wa kampuni dhidi ya wenyeji wa pwani ulisababisha uasi mkubwa uliongozwa na Abushiri na Bwana Heri; utawala wa kampuni iliporomoka kabisa na serikali ya Ujerumani ililazimishwa kutuma kikosi cha wanajeshi chini ya Wissmann kilichozimia upinzani. Ilhali ilikuwa dhahiri kampuni ya Peters haikuwa na uwezo wa kutawala tena, serikali iliamua kuchukua koloni mkononi mwake na hapo taarifa ya von Soden ilikuwa muhimu.
Tarehe 1 Januari 1891 von Soden alipewa kazi ya kuwa gavana ya kwanza ya Afrika ya Mashariki ya Kijerumani alichukua madaraka ambayo hadi wakati ule yalitekelezwa na kamanda Wissmann ilhali Wissmann alirudishwa nyumbani kwa sababu aliwahi kuendesha vita mbalimbali na makabila ya ndani na hivyo kuvuka mno mipaka ya makisio yake.
Kati ya shughuli za kwanza Soden alizopaswa kutekeleza ulikuwa uhamisho wa mji mkuu kutoka Bagamoyo kuja Dar es Salaam na kazi ya kupanga mji mpya.
Hata hivyo, maagizo kwa von Soden yalisema asitumie pesa nyingi mno ajitosheleze na makisio yake; aimarishe utawala juu ya maeneo ya pwani na kukuza biashara. Kuhusu makabila ya ndani alenge kujenga uhusiano nao bila kuingia katika mapigano. Lakini katika nafasi yake hakuwa na mamlaka juu ya jeshi; Soden alikuwa gavana wa kiraia na jeshi la koloni lilikuwa chini ya kamandi ya wanamaji kule Ujerumani.[2]
1891 kamanda mpya wa jeshi la Schutztruppe von Zelewski[3] alipanga vita dhidi ya Wahehe chini ya chifu Mkwawa; Soden hakuona ulazima wa hatua hiyo lakini alinyamaza kwa sababu makao makuu ilikubali na yeye hakuona hatari. Zelewski alifika Uhehe kwenye Agosti 1891 akaanza kushambulia na kuchoma vijiji. Tarehe 16 Agosti 1891 alipofika Lugalo aliongoza kikosi chake cha askari na wapagazi 500 katika tego lilioandaliwa na Mkwawa; karibu jeshi lote liliangamizwa, wachache tu walirudi kwenye pwani.
Soden alipokea watumwa wa Mkwawa kujadiliana kuhusu amani lakini alimtuma tena luteni von Prince kulinda mpaka wa Uhehe. Von Prince aliendelea kuingia ndani ya Uhehe alipoanzisha kituo kipya, bila amri ya von Soden. Mkwawa alijibu kwa kushambulia kituo cha Kondoa mnamo tarehe 6 Oktoba 1892 na kushinda kikosi cha askari 35 chini ya luteni Mjerumani[4]. Wakati wa mapigano ya Lugalo kulikuwa pia na ugomvi baina jeshi la Schutztruppe na sehemu ya Wachagga kwenye mlima Kilimanjaro; askari mmoja aliwahi kuiba akauawa na luteni kiongozi wa kituo cha Wajerumani huko Marangu alikataa upatanisho; baada ya kuuawa kwa akida wa chifu Meli wa Moshi amani ilivunjwa kabisa. Kikosi kidogo cha askari kilichoelekea Moshi ilishambuliwa na Meli kwenye 10 Juni 1892, maafisa 2 Wajerumani kuuawa na wengine walikimbia[5]; wajerumani walikosa uwezo wa kufanya chochote dhidi ya Meli hadi mwisho wa 1892.
Katika hali hiyo von Soden aliomba kustaafu akaondoka mwanzo wa 1893.
Kurudi Ujerumani
haririVon Soden aliishi sasa Ujerumani; alipewa zawadi la shamba kubwa kama shukrani ya serikali hujo Vorra, Bavaria. Hapa alijjenga jumba kubwa na kuwa na nafasi ya mkabaila wa eneo.
Mnamo 1899, von Soden aliitwa kurudi Württtemberg ambako alipewa kazi ya katibu mkuu kwenye ofisi ya mfalme.
Mwaka uliofuata alioa mara ya kwanza akifunga ndoa na Helene von Sick (* 5. Februari 1856). Wakati ule alikuwa na umri wa miaka 54. Umri mkubwa wa wenzi wa ndoa labda ilikuwa sababu ya kukosa watoto katika ndoa yao.
Kuanzia mwaka 1900 hadi 1906 alikuwa waziri katika serikali ya ufalme wa Württemberg; alisifiwa hasa kwa jitihada za kuongeza njia za reli nchini. 1906 alirudi tena katika kazi ya katibu mkuu wa mfalme aliyotekeleza hadi 1916 alipostaafu baada ya kufikia umri wa miaka 70.
Wakati wa mwisho wa Vita Kuu ya kwanza ya Dunia aliona mapinduzi ya Novemba 1918 iliyokomesha ufalme na vyeo vya kikabaila. Mwaka 1920 akiwa na umri wa miaka 74, von Soden alitimiza hamu yake ya kusoma tena. Akajiandikisha kwenye Chuo Kikuu cha Tübingen akaingia katika kozi za falsafa, isimu na sanaa. Miezi michache tu baada ya muhula kuanza, alipata shida ya mwili mnamo Januari 1921, ikifuatiwa na ugonjwa wa siku 14. Julius von Soden alifariki dunia mnamo 2 Februari 1921, siku mbili kabla ya sikukuu ya kuzaliwa kwake kwa miaka 75. [6]
Marejeo
hariri- ↑ Soden, Julius Freiherr v. Ilihifadhiwa 19 Mei 2016 kwenye Wayback Machine. In: Deutsches Koloniallexikon, 1920, Bd. III, S. 369.
- ↑ John Iliffe (1979), A Modern History of Tanganyika, uk. 108
- ↑ Alikuwa Emil von Zelewski yeye yule aliyewahi kuwa makala ya Kampuni ya Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki huko Pangani kwenye mwaka 1888 na kwa ukali wake kuhamasisha wenyeji wa mji huo kupinga utawala wa kampuni.
- ↑ Tom von Prince (1914), Gegen Araber und Wahehe, uk. 182
- ↑ Volkens, Georg (1897): Der Kilimandscharo, uk. 36
- ↑ Nachruf auf Julius von Soden, in: Zeitung des Vereins Deutscher Eisenbahnverwaltung 61 (1921), S. 112.
Makala hii kuhusu mwanasiasa fulani bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Julius von Soden kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |