Tawa ni kata ya Wilaya ya Morogoro Vijijini katika Mkoa wa Morogoro, Tanzania, yenye Postikodi namba 67214.

Kata ya Tawa
Nchi Tanzania
Mkoa Morogoro
Wilaya Morogoro Vijijini
Idadi ya wakazi
 - Wakazi kwa ujumla 12,166

Katika sensa ya mwaka 2022 wakazi walihesabiwa 12,166 [1]. Kwa mujibu wa sensa iliyofanyika mwaka wa 2012, kata ilikuwa na wakazi wapatao 11,019 waishio humo.[2]

Wenyeji wa kata hiyo ni Waluguru. Kuna wakazi Wakristo na Waislamu wanaoishi kwa umoja na undugu.

Historia ya jina Tawa

hariri

Tawa ni neno la Kiluguru lenye maana ya: kusuka, kufuma, kazi ya kufuma, ususi ama kazi ya ususi. Jina Tawa (linalobeba Kata ya Tawa) inasemekana limetokana na umaarufu wa wazee wa miaka ya 1800 katika ufumaji wa vifaa mbalimbali (vya utamaduni) vilivyokuwa vinatumika kwa matumizi mbalimbali vya nyumbani. Vifaa hivyo ni pamoja na nyungo, vitanga, majamvi, mikeka, vikapu, matenga pamoja na viezekeo vya nyumba (majengo) aina ya makuti.

Vijiji na taasisi

hariri

Kata ya Tawa inundwa na vijiji vinane ambavyo ni: Tawa, Kitungwa, Logo, Uponda, Milawilila, Kifindike, Kisarawe pamoja na Kilemela.

Katika Kata ya Tawa kuna shule za msingi nane ambazo ni: Shule ya Msingi Tawa, Shule ya Msingi Bandasi, Shule ya Msingi Kitungwa, Shule ya Msingi Kifindike, Shule ya Msingi Uponda, Shule ya Msingi Milawilila, Shule ya Msingi Logo, na Shule ya Msingi Kilemela. Kata hii ina shule ya sekondari moja (shule ya kata) ambayo inaitwa Shule ya Sekondari ya Tawa.

Pia kuna hospitali moja ya serikali ambayo ina hadhi ya Kituo cha Afya na inaitwa Kituo cha Afya Cha Tawa. Kituo hiki kina hadhi ya Hospitali ya wilaya.

Kata hii pia ina taasisi mbalimbali nyingine za serikali, na za kidini. Lipo Kanisa Katoliki la Mt. Yakobo Tawa pamoja na misikiti kadhaa.

Uchumi

hariri

Shughuli kuu za kiuchumi katika kata hii ni kilimo na biashara.

Kilimo

hariri

Wakazi wa kata ya Tawa kwa asili ni wakulima wa mazao ya nafaka na mikunde kama vile mahindi, mtama pamoja na mpunga, maharagwe, mbaazi, kunde. Pia wanalima kwa wingi mazao ya matunda kama vile machungwa, mananasi, maembe, machenza pamoja na maparachichi. Mazao mengine ya biashara yanayolimwa kwa wingi ni pilipili mtama, tangawizi, bizari, karafuu, ndizi, mihogo, magimbi pamoja na viazi vikuu.

Soko kuu la mazao yanayolimwa kata ya Tawa ni mji wa Morogoro, Jiji la Dar es Salaam pamoja na Jiji la Dodoma.

Biashara

hariri

Shughuli kuu za biashara zinazofanyika katika kata hii ni pamoja na biashara ya kusafirisha mazao ya matunda kama vile machungwa, mananasi, maembe, machenza pamoja na maparachichi.

Utamaduni

hariri

Utamaduni wa watu wa kata ya Tawa (Waluguru) ni aina iliyo tofauti kabisa na makabila mengine. Mkuu wa Kata hiyo kihistoria (kama ilivyokuwa kwa kata za Kibogwa, Kibungo Juu, Tegetero, Kisemu, Konde, Kasanga na maeneo yote ya Mgeta) alijulikana kwa jina maarufu la Kingalu.

Wenyeji wa Morogoro huwarithisha vizazi vyao maadili, mila, tamaduni na desturi vizazi vyao kwa unyago na ngoma mbalimbali.

Ni utamaduni wa wenyeji wa kata hiyo, pale ambapo binti amevunja ungo anawekwa ndani kwa muda usiopungua mwezi mmoja ambako anakula na kulala tu bila kufanya kazi yoyote wala kuonana na mtu yeyote yule isipokuwa yule aliyeteuliwa na ukoo kuonana naye. Akiwa ndani binti hupewa mafundisho ya aina mbalimbali na kungwi Archived 13 Agosti 2019 at the Wayback Machine. aliyeteuliwa kufanya kazi hiyo. Hufundishwa juu ya kuanzisha na kukuza familia, mahusiano kati ya mume na mke, maadili, nidhamu, mila, desturi na utamaduni katika jamii. Aidha, siku ya mwisho ya binti kutoka kukaa ndani, kabla ya kutoka nje inaandaliwa sherehe kubwa ambapo vyakula na vinywaji mbalimbali huandaliwa, ngoma mbalimbali huchezwa kwa siku mbili (inategemea matakwa ya familia).

Kwa vijana wa kiume historia inaonesha kuwa walikuwa wakipewa mafundisho (yanayoshabihiana na mafundisho ya mabinti) wakati wa kuingizwa jando (kipindi cha kutahiriwa).

Utamaduni wa ngoma za wenyeji wa kata ya Tawa historia yake haijapatikana. Hata hivyo utamaduni wa ngoma katika kata hiyo umechanganyika na wa ngoma za asili ya makabila za Wazaramo, Wapogoro na Wamakonde. Ngoma maarufu kwa wenyeji wa kata ya Tawa ni: Mdundiko Kibende, Mbeta, Gombesugu, Mkwajungoma n.k.)

Utalii

hariri

Aidha, miongoni mwa maeneo maarufu ya utalii katika kata ya Tawa ni pamoja na Maporomoko ya Mto Mmanga (eneo walikotega mitambo ya mabomba ya maji yanayotumika kwa matumizi ya nyumbani kwa kijiji cha Tawa na vijiji vyingine vya jirani); pia safu ya Milima ya Uluguru iliyoko maeneo ya Luhanga (kuelekea Kata ya Kibogwa)

Tanbihi

hariri
  Kata za Wilaya ya Morogoro Vijijini - Mkoa wa Morogoro - Tanzania  

Bungu | Bwakira Chini | Bwakira Juu | Gwata | Kasanga | Kibogwa | Kibuko | Kibungo | Kidugalo | Kinole | Kiroka | Kisaki | Kisemu | Kolero | Konde | Lundi | Matuli | Mikese | Mkambalani | Mkulazi | Mkuyuni | Mngazi | Mtombozi | Mvuha | Ngerengere | Selembala | Singisa | Tawa | Tegetero | Tomondo | Tununguo


  Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Morogoro bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Tawa kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
Tafadhali usiingize majina ya maafisa na viongozi wa sasa maana wanabadilika haraka mno.