Ufalme wa Wavandali
Ufalme wa Wavandali ulienea kwa karne moja (429-534) katika maeneo ya Algeria na Tunisia ya leo, pamoja na kutawala visiwa vya Mediteraneo magharibi.
Hao walikuwa kabila kubwa la Kigermanik la mashariki ambao katika karne tano za kwanza BK walihama kutoka sehemu za Poland ya leo hadi Afrika ya Kaskazini wakiunda ufalme wao.
Historia
haririInaonekana ya kwamba walianza kuondoka kwao Ulaya ya mashariki kutokana na uvamizi wa Wahunni.
Mwaka 406 BK walivuka mto wa Rhine wakaingia Gallia (leo Ufaransa), mwaka 409 wakavamia Hispania.
Kutoka Hispania ya Kusini walivuka bahari ya Mediteraneo mwaka 429 na kuingia Afrika ya Kaskazini iliyokuwa jimbo la Dola la Roma.
Kuna taarifa ya jemadari Mroma wa wakati ule ya kwamba walikuwa jumla ya wanaume wenye silaha kati ya 15,000 hadi 20,000, kwa hiyo pamoja na familia zao takriban watu 80,000.
Wavandali waliteka Afrika ya Kaskazini yote iliyokuwa jimbo tajiri sana katika Dola la Roma likilimwa sehemu kubwa ya ngano kwa ajili ya mahitaji ya Italia.
Mwaka 430 waliteka mji wa Hippo, maarufu kutokana na askofu wake Agostino, ambao ukawa makao makuu ya mfalme wao Genseriki.
Mwaka 439 waliteka pia mji wa Karthago na mfalme akaufanya mji wake mkuu. Uvamizi wa Karthago uliwapatia Wavandali pia jahazi nyingi za kijeshi za Waroma. Hali hiyo iliwawezesha kushambulia hata mji wenyewe wa Roma mwaka 455, lakini hawakukaa, ila baada ya kuuvamia na kuuharibu walirudi Afrika.
Ufalme wa Wavandali ulidumu karibu karne moja na kuchangia kudhoofisha Kanisa la huko kwa dhuluma zao dhidi ya Wakristo wenyeji waliokataa Uario wa Wavandali.
Katika karne ya 6 Kaisari Justiniani I wa Bizanti (Roma ya Mashariki) alimaliza utawala wao akivamia Afrika ya Kaskazini na kuirudisha katika Dola la Roma tangu mwaka 534.
Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Ufalme wa Wavandali kama enzi zake au matokeo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |