Waanglikana
Waanglikana ni Wakristo wa madhehebu yenye asili ya Uingereza.
Katika karne ya 16 mfalme Henry VIII alitenga Kanisa la nchi hiyo na Kanisa Katoliki.
Baada ya farakano hilo, yalifanyika mabadiliko mbalimbali upande wa imani, ibada na sheria kuelekea Uprotestanti. Hata hivyo mwelekeo wa Kikatoliki uliendelea kuwepo, na bado una nguvu, hasa katika baadhi ya dayosisi. Hasa miaka hii ya mwisho mvutano kati ya pande hizo mbili umeongezeka hata kusababisha umoja kulegea.
Katika karne zilizofuata, kutokana na uenezi wa himaya ya Uingereza duniani, Anglikana ilienea sehemu nchi, na leo ina wafuasi wengi hasa Afrika (Nigeria, Uganda n.k.). Kwa jumla wanazidi milioni 85 katika nchi 165.
Majimbo yake 38 yanajitegemea, lakini yanaunda ushirika mmoja. Maaskofu wake wote wanakutana Lambeth kila baada ya miaka 10 chini ya Askofu mkuu wa Canterbury.
Historia
haririMfalme Henri VIII alitawala Uingereza miaka 1509-1547, wakati wa Martin Luther.
Alikuwa Mkatoliki aliyependa Kanisa lake. Lakini alikuwa na matatizo mawili juu ya Papa wa Roma.
Kwanza kabisa Uingereza ulikuwa na wajibu wa kumlipa Papa kila mwaka kodi ya pekee, tofauti na mataifa mengine ya Ulaya.
Pili, huyo mfalme alikuwa na tatizo la binafsi: alishindwa kuzaliana na mke wake mtoto wa kiume atakayerithi ufalme. Basi, akamwomba Papa apate kumwoa mwingine, lakini Papa alikataa kutokana na sheria za Kanisa.
Henri, aliyekuwa mtu wa hasira, aliitisha Bunge la Uingereza akawalazimisha wabunge kutangaza kwamba mfalme ndiye mkuu wa kanisa nchini. Halafu bunge lilikubali talaka yake.
Azimio lingine lilikuwa kutolipia tena kodi kule Roma, hivyo ikaingia katika mfuko wa Mfalme mwenyewe. Lakini Henri hakupenda mabadiliko katika mafundisho ya imani na desturi za ibada.
Baada ya kifo chake viongozi wa taifa waliamua kutengeneza kanisa kwa jumla. Hasa nyumba za watawa zilifungwa na mali zao zikachukuliwa na mfalme.
Askofu Mkuu Cranmer akachukua mafundisho mengi ya Luther na Calvin, lakini katika desturi za nje alibadilisha taratibu chache tu.
Hivyo Kanisa la Uingereza likajitokeza kuwa na hali mbili. Wale wanaokaza sana urithi wa kale pamoja na liturujia (mavazi ya wachungaji, kupiga magoti, kufanya alama ya msalaba kwa mkono wakati wa sala, kutunza kumbukumbu ya watakatifu) wanaitwa "High Church (Kanisa la juu)". Waanglikana wengine, waliovutwa zaidi na matengenezo ya Kiprotestanti na kutojali sana urithi wa kale wanaitwa "Low Church (Kanisa la chini)".
Kwa mambo ya nje wale wa "juu" wanafanana na Wakatoliki, na wale wa "chini" wanafanana zaidi na Wareformati. Lakini Waanglikana hujisikia kuwa na umoja; kwa kweli walifaulu kuliko madhehebu mengine kuunganisha pande zote mbili na kuepuka hatari ya kufarakana kama ilivyotokea mahali pengine.
Waanglikana wako katika nchi zote zilizokuwa chini ya ukoloni wa Kiingereza, kwani huko wamisionari wao waliweza kufanya kazi kwa urahisi.
"Majimbo" ya Waanglikana (Jimbo la Tanzania, Jimbo la Kenya, Jimbo la Uganda n.k., kila jimbo likiwa na madayosisi mbalimbali) hujitegemea, pamoja na kumkubali Askofu wa Canterbury (Uingereza) kuwa kiongozi wa kiroho kama mwenyekiti wa maaskofu wa Kianglikana lakini hana utawala.
Siku hizi Waanglikana wa Marekani wamekuwa wa kwanza kumbariki askofu wa kike (ni Mnegro) na askofu shoga, lakini katika suala la kupokea wanawake katika ukasisi na uaskofu na vilevile katika suala la ushoga majimbo yao yametofautiana kiasi cha kuelekea farakano.
Kwa sababu hizo, mnamo Januari 2016, Jimbo la Marekani lilisimamishwa kwa miaka 3.
Barani Afrika tunasikia hasa jina la Desmond Tutu, Askofu Mwanglikana aliyetetea haki za Waafrika dhidi ya ubaguzi wa rangi Afrika Kusini.
Viungo vya nje
hariri- Church of England, official site Ilihifadhiwa 31 Desemba 2007 kwenye Wayback Machine.
- All Souls' Church, London, Evangelical Ilihifadhiwa 25 Februari 2007 kwenye Wayback Machine..
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Waanglikana kama historia yake, matokeo au athari zake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |