Desmond Tutu

Mchungaji wa Afrika Kusini, mwanasiasa, askofu mkuu, mshindi wa Tuzo ya Nobel (1931-2021)

Desmond Mpilo Tutu (7 Oktoba 1931 - 26 Desemba 2021) alikuwa mwanatheolojia na askofu wa Kanisa Anglikana nchini Afrika Kusini. Anafahamika kwa kazi yake ya kutetea haki za binadamu na kupinga ubaguzi wa rangi nchini. Miaka 1985 hadi 1986 alikuwa askofu wa Johannesburg kisha askofu mkuu wa Cape Town hadi 1996. Katika nafasi zote mbili alikuwa Mwafrika wa kwanza kuchaguliwa.

Desmond Tutu, Askofu mkuu Emeritus wa Cape Town

Ulipofika mwaka wa 1984 alipokea Tuzo ya Nobel ya amani kwa kupigania bila silaha haki za Waafrika wote.

Familia na elimu

Desmond Mpilo Tutu alizaliwa katika familia ya mchanganyiko wa Waxhosa na Watwana. Baba yake Zachariah Tutu alikuwa Mxhosa na mwalimu mkuu wa shule ya msingi na mama yake Aletha Matlhare alikuwa mfanyakazi ya nyumbani.[1] Desmond alikumbuka familia ilikuwa maskini. Alisoma ualimu akamwoa Leah Nomalizo Shenxane akazaa naye watatoto wanne Trevor Thamsanqa, Theresa Thandeka, Naomi Nontombi (* 1960) na Mpho Andrea (*1963 mjiini London).

Ilhali sheria mpya ya apartheid iliagiza kwamba watoto Waafrika wapate elimu duni tu, Tutu aliachana na ualimu. Mwaka 1958 alianzisha kazi ya kiroho katika Kanisa Anglikana ya Afrika Kusini (iliyopinga siasa ya apartheid) akaanza kusoma uchungaji kwenye chuo cha theolojia cha St. Peter huko Johannesburg, aliposoma kwa mwalimu wake Trevor Huddleston aliyekuwa mkuu wa chuo. Mnamo mwaka 1960 alihitimu masomo akabarikiwa kama shemasi wa Kanisa Anglikana, na mwaka 1961 alibarikiwa kuwa kasisi[2]

Mwaka 1962 alihamia Uingereza kusoma theolojia. Tasnia yake ya uzamili ilikuwa kuhusu Uislamu katika Afrika ya Magharibi.[3] Alisema baadaye kuwa alitambua kuna ubaguzi wa rangi huko, lakini yeye na familia yake hawakuukata. Alivutwa na uhuru wa kutamka maono jinsi alivyoishuhudia kwenye "speakers' corner" kwenye Hyde Park London. Kipindi chake cha London kilimsaidia kuachana na uchungu wote dhidi ya watu weupe na kujisikia mdogo mbele yao.

Mwaka 1966, Tutu pamoja na familia walihamia Yerusalemu Mashariki aliposoma Kiarabu na Kigiriki kwa miezi miwili.[4] Aliporudi Afrika Kusini mnamo 1966 alifundisha kwenye chuo cha theolojia kisha Chuo Kikuu cha Botswana na Uswazi[5].

Kazi ya Baraza la Makanisa Duniani

Mnamo 1972 alirudi Uingereza alipokuwa naibu mkurukugenzi wa Mfuko wa Elimu ya Theolojia wa Baraza la Makanisa Duniani. Kikazi alihusika na kukubali maombi ya misaada ya gharama ya masomo kwa wanafunzi na vyuo.[6] Hivyo alitakiwa kutembelea nchi mbalimbali za Afrika akatunga taarifa juu ya safari zake.[7] Huko Zaire alikutana na ulaghai na rushwa pamoja na umaskini vilivyoenea chini ya utawala wa Mobutu Sese Seko. Katika ziara ya Nigeria aliandika kuhusu masikitiko ya Waigbo baada ya ugandamizaji wa uhuru wa Biafra. Alipenda serikali ya Jomo Kenyatta huko Kenya akasikitikia kufukuzwa kwa Wahindi katika Uganda chini ya Idi Amin.

Wakati ule alikutana na mafundisho ya theolojia ya ukombozi na majadiliano ya Black Theology kutoka Marekani.

Kasisi, Katibu Mkuu na Askofu

Mwaka 1975 alirudi tena Afrika Kusini alipokuwa padre kiongozi kwenye kanisa kuu la Mariamu mjini Johannesburg, akiwa Mwafrika wa kwanza katika nafasi hiyo. Hakuishi katika makazi rasmi ya padre kiongozi yaliyokuwapo kwenye "eneo jeupe" bali katika mtaa wa watu weusi. Usharika wake ulikuwa na washarika wengi weupe ilhali idadi ya Waafrika weusi ilikuwa ndogo zaidi na kwa jumla maarifa hayo yalimpa tumaini kwamba ushirikiano wa mbari tofauti utakuwa na nafasi nzuri nchini[8].

Mwaka uliofuata alichaguliwa kuwa askofu wa Lesotho. Baada ya kushika nafasi hiyo akachaguliwa mwaka 1978 kuwa katibu mkuu wa Baraza la Makanisa ya Afrika Kusini. Aliendelea katika ofisi hiyo hadi mwaka 1985. Wakati ule alifahamika zaidi kimataifa akisafiri na kukutana na viongozi wa serikali za nchi nyingi akitatafuta usaidizi wako kushawishi serikali ya Afrika Kusini kumaliza ubaguzi wa rangi. Kutokana na jitihada hizo aliteuliwa kupokea Tuzo ya Nobel ya Amani kwa mapambano yake dhidi ya ubaguzi wa rangi ya apartheid nchini Afrika Kusini bila kutumia mabavu.

Mwaka 1985 alichaguliwa na sinodi kuwa askofu wa Johannesburg, akiwa Mwafrika mweusi wa kwanza. Wakristo wake walikuwa 80% Weusi. Baada ya kuchaguliwa alitangaza mara moja kwamba ataomba jamii ya kimataifa kuanzisha vikwazo wa kiuchumi dhidi ya nchi yake kama sheria za ubaguzi hazifutwi. Askofu mpya alijitahidi sana kutembelea parokia za Wakristo weupe (kisheria watu walipaswa kuishi katika maeneo "meupe" au "meusi", hivyo hata parokia nyingi zilitengwa vile) na kujenga maelewano nao.

Wakati uleule kulikuwa na mapigano kati ya vijana Waafrika walioandamana dhidi ya serikali na polisi. Vifo viliongezeka kwa sababu polisi ilitumia silaha za moto kukandamiza maandamano, na Waafrika wenye hasira walishambulia watu walioaminiwa kupeleka habari kwa polisi. Tutu alijitahidi kuingilia kati akakataa kuuawa kwa hao walioshtakiwa kuwa wasaliti. Akafika pia mara kadhaa kwenye maandamano akiomba polisi kupunguza ukali. Hakukubali matumizi ya silaha pande zote lakini alikataa kulaani madai ya ANC. Tutu alisafiri Marekani na nchi nyingine, akihutubia wabunge na viongozi wengine na kudai nchi hizo zitumie vikwazo wa kiuchumi kubadilisha siasa ya Afrika Kusini. Mara kadhaa pasipoti yake ilikamatwa na polisi wakati wa kurudi akazuiliwa kusafiri tena kwa muda fulani.

Mwaka 1986 Tutu alichaguliwa kuwa Askofu Mkuu wa Cape Town na hivi kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikana katika Afrika Kusini. Alihamia nyumba rasmi ya askofu akipuuza sheria ya ubaguzi kwa sababu nyumba hiyo ilikuwa katika "eneo jeupe" na yeye angetakiwa kuomba kibali cha pekee kuishi huko ambacho hakufanya.

Mwaka 1988 alikutana na rais P.W. Botha kuombea uhai wa "Sharpeville Six", waandamanaji sita waliohukumiwa kifo baada ya maandamano ambako meya wa Sharpeville aliuawa. Tutu alitumia nafasi yake kuwasiliana na serikali za Marekani, Uingereza na Ujerumani kuwaombea hao sita. Hatimaye Botha alibadilisha hukumu ya kifo.

Wakati Nelson Mandela alipoachiliwa gerezani mwaka 1990, alilala usiku wa kwanza wa uhuru kwenye nyumba ya askofu. Mwaka uleule 1990 yalianza mapigano makali kati ya wafuasi wa ANC na harakati ya Inkatha katika KwaZulu-Natal na Tutu alitembelea viongozi wa pande zote mbili na pia familia zilizoathiriwa na mauaji yaliyotokea katika mapigano hayo. Tutu alialika viongozi wa vyama vya siasa kama ANC, PAC na AZAPO akiwabembeleza kukubali kampeni huru na kuachana na vitisho na mabavu dhidi ya wapinzani.

Tume ya Ukweli na Upatanisho

Mwaka 1996 Tutu alistaafu kama askofu mkuu. Rais Mandela alimteua kuwa mwenyekiti wa Tume ya Ukweli na Upatanisho iliyoundwa kuchungulia jinai zilizotekelezwa wakati wa mapigano dhidi ya apartheid. Wahanga wa jinai dhidi ya haki za binadamu walialikwa kutoa taarifa na watendaji wa jinai waliweza kufika mbele ya tume, kukiri matendo yao na kuomba msamaha.

Tutu alipendekeza mchakato wa hatua tatu: kwanza watendaji kukiri matendo yao bila kuficha chochote, pili msamaha kwa njia ya kisheria, tatu mtendaji anapaswa kusaidia wahanga kutengeneza maisha yake upya. Mwaka 1998 Tutu aliweza kumkabidhi rais Mandela taarifa ya tume.

Mteteaji wa Haki za Binadamu na Washoga

Tutu aliendelea kupigania haki za binadamu. Alipokuwa askofu, alianza kubariki wanawake kuwa makasisi akatetea nafasi kamili ya wanawake kanisani[9].

Alifahamika hasa kwa kutetea haki za mashoga. Tutu aliona ubaguzi dhidi ya mashoga kuwa sawa na ubaguzi dhidi ya watu weusi au dhidi ya wanawake. Alisema "Kama ingekuwa kweli kwamba Mungu anachukia mashoga, nisingemwabudu. Lakini si kweli."[10] Mwaka 2011 aliomba kanisa la Afrika Kusini kukubali ndoa za jinsia moja.

Alishiriki katika majadiliano kuhusu masuala ya Israeli na Palestina akitetea haki ya Israeli kuendelea kuwepo katika mipaka ya mwaka 1967 lakini alikemea serikali yake kwa kuenea katika ardhi ya Wapalestina na kutoheshimu haki za Wapalestina[11].

Mwaka 2006 Tutu alianzisha kampeni ya kimataifa ya kupambana na biashara ya watoto akisisitiza ni muhimu watoto wote waandikishwe serikalini baada ya kuzaliwa[12].

Katika hotuba za hadharani alikosoa marais Thabo Mbeki na Jacob Zuma; aliona Mbeki alitaka wanaANC wanyamaze mbele ya uongozi na kuitikia kila jambo linalotangazwa kutoka juu, pia alimkosoa Mbeki kwa kutopigana na mlipuko wa Ukimwi nchini. Alimwona Zuma kuwa mtu mwenye kasoro nzito za kimaadili baada ya mashtaka ya ubakaji na ulaji rushwa dhidi yake[13]. Alikemea pia siasa ya Afrika Kusini kuhusu Zimbabwe alipoona udikteta wa Robert Mugabe kuwa mbaya zaidi mwaka baada ya mwaka.

Maandishi yake

  • Crying in the Wilderness, 1982
  • Hope and Suffering: Sermons and Speeches, 1983
  • The Words of Desmond Tutu, 1989
  • The Rainbow People of God: The Making of a Peaceful Revolution, 1994
  • Worshipping Church in Africa, 1995
  • The Essential Desmond Tutu, 1997
  • No Future without Forgiveness, 1999
  • An African Prayerbook, 2000
  • God Has a Dream: A Vision of Hope for Our Time, 2004

Marejeo

  1. South African History Online: Archbishop Emeritus Desmond Mpilo Tutu. kwenye www.sahistory.org.za
  2. Eintrag: Desmond Tutu auf aaregistry.org
  3. Gish 2004, p. 35; Allen 2006, pp. 92, 95.
  4. Gish 2004, p. 39; Allen 2006, pp. 98–99.
  5. Archbishop Emeritus Mpilo Desmond Tutu
  6. Gish 2004, p. 53; Allen 2006, p. 123.
  7. Gish 2004, p. 53; Allen 2006, p. 124.
  8. Allen, John (2006). Rabble-Rouser for Peace: The Authorised Biography of Desmond Tutu. London: Rider. ISBN 978-1-84-604064-1. uk. 147 ff, [https://books.google.co.tz/books?id=IIxMu_US0ssC&printsec=frontcover&dq=desmond+tutu&hl=sw&sa=X&redir_esc=y#v=onepage&q=desmond%20tutu&f=false online hapa]
  9. Allen, John (2006), uk. 280
  10. http://news.bbc.co.uk/1/hi/world/africa/7100295.stm Tutu chides Church for gay stance, BBC 18.11.2007
  11. Allen (2006), uk. 388
  12. https://web.archive.org/web/20131008064019/http://news.bbc.co.uk/2/hi/africa/4289393.stm "Tutu calls for child registration". BBC News. 22 February 2005.
  13. https://web.archive.org/web/20080307052155/http://news.bbc.co.uk/2/hi/africa/5384310.stm "S Africa is losing its way - Tutu". BBC News. 27 September 2006.
  Makala hii bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.