Historia ya Ureno
Historia ya Ureno inahusu eneo ambalo siku hizi linaunda Jamhuri ya Ureno.
Historia ya awali
haririKatika karne za KK Ureno ilikaliwa na makabila yaleyale ya Wakelti kama Hispania.
Waroma walitaja eneo lote la Ureno na Hispania ya leo kwa jina la "Iberia".
Tangu mwaka 450 KK sehemu za nchi zilitawaliwa na Wafinisia wa Karthago, na baada ya mwaka 200 KK yote ikawa sehemu ya Dola la Roma.
Baada ya kuporomoka ya Dola hilo mnamo 470 BK makabila ya wahamiaji wa Kigermanik walikuwa mabwana wa eneo lote.
Tangu mwaka 711 Waarabu walivamia nchi na kuitawala.
Vita vya kuwaondoa tena viliendelea kwa karne kadhaa.
Uhuru
haririTangu mwaka 1143 mtawala wa eneo la mji wa Kale katika kaskazini alikuwa na uwezo wa kutosha kujitetea dhidi ya Waarabu na pia dhidi ya majirani wa eneo la Kihispania.
Baada ya ushindi katika vita dhidi ya Wahispania mwaka 1128 Afonso I alijitangaza kuwa mtawala wa kujitegemea na baadaye alichukua cheo cha mfalme. Alitumia jina la mji Kale iliyojulikana kama "Porto Kale" (bandari ya mji wa Kale) iliyokuwa "Portokale" na baadaye "Portogale".
Nchi hii ndogo ilifaulu kutunza uhuru wake hata baada ya maeneo yote mengine ya jirani kuunganishwa katika ufalme mpya wa Hispania.
Nchi hii ndogo ilikuwa kati ya nchi muhimu zaidi duniani kwa karne mbili za 15 na 16. Wafalme wake walilenga jitihada na nguvu za nchi kwa teknolojia za usafiri baharini.
Wareno waliweza kuboresha jahazi zao hadi kupita nchi zote za dunia na kwa muda wakafaulu kwenda mbali.
Wareno waligundua njia ya kuvuka rasi ya Afrika Kusini na kufika kwenye bandari za Afrika ya Mashariki hata Bara Hindi.
Ureno ilitajirika kutokana na biashara kati ya India, Asia na Ulaya. Wareno walijenga vituo kama vile maboma ya Msumbiji na Mombasa (Kenya) wakiwa mabwana wa pwani ya Afrika ya Mashariki.
Lakini nguvu za nchi ndogo hazikuweza kutetea haya yote. Baada ya kujitokeza kwa mataifa mengine kama vile Uturuki, Uholanzi, Uingereza na Ufaransa, Wareno walipaswa kuwaachia maeneo mengi.
Kati ya makoloni ya Ureno yalibaki hasa Msumbiji, Angola, Guinea Bisau, Cabo Verde, São Tomé na Príncipe katika Afrika, Brazil katika Amerika ya Kusini (hadi 1822) pamoja na maeneo madogomadogo kama Goa kwenye Bara Hindi, Timor ya Mashariki katika funguvisiwa ya Indonesia, mji wa Makao katika Uchina.
Jamhuri
haririMwaka 1910 Ureno iliona mapinduzi ikawa jamhuri.
Tangu 1926 hadi 1974 ilikuwa na serikali za kidikteta.
Baada ya mapinduzi ya 1974 Ureno iliacha makoloni yake yaliyobaki isipokuwa Makao kwa sababu Uchina haukuwa tayari kuipokea hadi 1999.
Ureno ikajiunga na Umoja wa Ulaya mwaka 1986 ikaona tena maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Historia ya Ureno kama enzi zake au matokeo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |