Tetemeko la ardhi
Tetemeko la ardhi (pia: zilizala) ni mishtuko ya ghafla ya ardhi. Inatokea mara kwa mara, lakini mara nyingi ni hafifu mno: haisikiki na wanadamu ila tu inapimwa na mitambo ya wataalamu.
Hatari za matetemeko ya ardhi
Tetemeko kubwa laweza kusababisha uharibifu mkubwa na vifo, hasa kutokana na majengo yanayoanguka.
Baharini tetemeko laweza kusababisha tsunami, yaani wimbi kubwa lenye hatari pale linapofika pwani.
Tetemeko la ardhi lenyewe kwa kawaida haliui au kujeruhi watu bali matokeo yake ndiyo. Katika mazingira ya kienyeji hata zilizala kali inaweza kupita bila hasara kubwa; nyumba za kienyeji zilijengwa kwa kutumia vifaa asilia vyepesi. Mfano wa kisasa ni tetemeko la ardhi la Kagera 2016 ambalo kitovu chake na mishtuko mikali ililotokea sehemu ya vijijini, upande wa kaskazini wa kata ya Nsunga, Wilaya ya Missenyi, lakini waathiriwa wengi waliripotiwa kwa umbali wa kilomita 60-70 mjini Bukoba penye majengo makubwa.
Kuharibika kwa majengo
Tatizo ni nyumba zilizojengwa kwa mata nzito kama matofali, simenti, kuta nene (hata za udongo) na ghorofa bila kufikia kiwango cha juu cha usalama. Kuanguka kwa majengo ya aina hii kunasababisha wajeruhiwa wengi na watu wanaokufa.
Pamoja na kuanguka kwa majengo miji ya kisasa ina pia nyaya za umeme na mabomba ya gesi zinazopita mle. Nyaya za umeme zikikatika zinasababisha mara nyingi kuwaka kwa moto, pamoja na hatari ya pigo la umeme. Mabomba ya gesi zinaweza kuvunjika na gesi inayotoka ina hatari ya mlipuko na moto.
Banguko mlimani
Hatari za tetemeko la ardhi linaongezeka mlimani maana mishtuko inaweza kusababisha banguko, yaani kuteleza chini kwa upande wa mlima unaofunika kila kitu kilichopo njiani mwake. Banguko kubwa inaweza kufunga njia ya mto na kuunda lambo linalofanya mto kupanuka na kutokea kwa ziwa. Kamba lambo la banguko si imara kuna hatari ya mafuriko baada ya muda.
Mfano ni eneo chini ya Ziwa Sarez nchini Tajikistan ambako banguko kubwa baada ya tetemeko la ardhi mwaka 1911 liliziba mto Murghab na ziwa kubwa lilitokea. Ilhali bado kuna matetemeko ya ardhi katika eneo hili kuna hatari ya kamba lambo la 1911 litavunjika tena na maji ya ziwa kuhatarisha maisha ya watu malakhi.[1]
Tsunami
Hatari kuu ni mitetemeko inayotokea chini ya bahari kwa sababu ya mawimbi ya tsunami yanayoharibu kila kitu kwenye kanda la pwani linaloathiriwa.
Tsunami ya Krismasi 2004 kwenye Bahari Hindi ilisababishwa na mwendo wa mabamba mawili ya ganda la dunia uliosababisha kipande kikubwa kusogezwa juu kiasi cha mita 30 katika muda wa dakika chache.
Mwendo huu wa tako la bahari ulisababisha wimbi lililosambaa kote katika Bahari Hindi na kupaa juu pale lilipofika mwambaoni hadi kimo cha mita 30 likaua takriban watu 275,000 kwenye pwani za Indonesia, Sri Lanka, Thailand, India hadi Somalia, Kenya, Tanzania na Afrika Kusini.
Sababu
Kwa ufupi
Mara nyingi sababu ya tetemeko ni miendo ya vipande vinavyofanya sehemu ya nje ya dunia. Umbo la dunia unafanana kiasi na chungwa: nje kuna ganda imara (linaitwa ganda la dunia) na ndani yake sehemu kubwa ni giligili ya moto. Lile ganda la nje si kipande kimoja, ila vipande mbalimbali vinavyoelea juu ya giligili moto ndani ya dunia. Vipande hivi kwa lugha ya kitaalamu huweza kuitwa mabamba ya ganda la dunia. Pale ambako vipande hivi vinagusana na kusukumana kunatokea msuguano na kushikana au kuachana kwa mabamba hayo kunasababisha mishtuko ya tetemeko la ardhi.
Maelezo ya ndani zaidi
Ili kufahamu sababu hiyo ya matetemeko ya ardhi, inabidi kufahamu mambo yanayoendelea chini ya ardhi. Kwanza ni lazima kufikiria muundo wa Dunia. Dunia ina umbo la tufe kubwa. Umbali uliopo baina ya pande mbili za dunia ni kilomita elfu kumi na tatu hivi. Katika sehemu ya nje ya Dunia, ardhi ni thabiti (ngumu). Kwa nje Dunia ina gamba la mwamba mgumu. Gamba hilo lina unene unaofikia baina ya kilomita kumi na kilomita hamsini.
Kama ungeweza kusafiri chini ya ardhi, yaani kuvuka gamba hilo, ungeona kwamba mazingira ni tofauti sana. Chini ya gamba la nje unafika katika "koti la dunia", na huko yote ni mwamba na chuma katika hali ya joto kali. Hivyo mwamba na chuma ndani ya Dunia si imara bali umeyeyuka, kama matope joto (inayoitwa zaha) yanayotoka nje ya volkeno wakati wa mlipuko.
Hali ya mwamba huo ulioyeyuka wenye joto mno ndani ya dunia unafanana na hali ya sufuria ya maji ya kuchemka. Katika sufuria tunaona mwendo fulani, na tukiweka jani kwenye maji tunaona jinsi linavyozunguka pamoja na maji ambayo yanachemka. Maana ndani ya kiowevu kinachochemka kuna mwendo. Mwendo kama huo unapatikana pia kwenye mwamba ulioyeyuka ndani ya Dunia. Hivyo gamba la nje linaathiriwa na mikondo ndani ya mwamba ulioyeyuka, na mikondo yake. Kwa sababu ya kusukumwa, gamba huvunjika. Kwa hiyo badala ya pande moja zima la gamba, kuna baadhi ya mapande makubwa ya gamba yanayosogezwa yakiwa na kani kubwa.
Katika baadhi ya sehemu za Dunia, mapande hayo yanakutana yakisukumana. Wakati huo, nguvu kubwa mno inasukuma mwamba thabiti wa gamba kuelekea juu na chini. Ndivyo hivyo baada ya miaka mingi sana, safu za milima zinavyojengwa. Pia pande moja linaposukumwa chini ya pande jingine, bonde kubwa sana linajengwa. Kwa mfano, kuna ufa mkubwa sana uliopo chini ya bahari, katika pwani ya Kalifornia magharibi mwa Marekani. Karibu na pwani ya nchi zilizopo katika pwani ya magharibi ya bara la Amerika, kuna milima mingi kutokana na pande hilo kusukumwa juu. Pia, karibu na pwani, kuna mifereji ambapo chini ya bahari imekwenda chini sana, kwa ajili ya pande jingine lililosukumwa chini.
Katika maeneo ambayo mapande yanatenganishwa, gamba ni jembamba, na mwamba ulioyeyuka unaondoka. Ukiona ramani ya dunia, sehemu ya mashariki ya bara la Amerika na sehemu ya magharibi ya mabara ya Afrika na Ulaya, utaona kwamba inawezekana zamani sana mabara hayo yalikuwa bara moja tu. Pia, katika chini ya bahari kati ya Afrika na Marekani, wachunguzi wameona kwamba katika mstari wa katikati baina ya mabara hayo, kuna idadi kubwa ya miamba ilioyeyuka iliyotoka ardhini.
Baadhi ya wakati mapande hayo yanateleza pole pole. Lakini mara kwa mara yanasimama badala ya kuendelea kuteleza. Hivyo nishati inajengeka. Nishati inapoachiwa - kwa kawaida kwenye mipaka baina ya mapande tofauti - mapande yanasogea kwa ghafula na kwa haraka. Hivyo, ardhi inatetemeka. Ndivyo matetemeko ya ardhi yanavyotokea. Wachunguzi wameona kwamba matetemeko ya ardhi mara nyingi yanatokea katika maeneo hayo ambayo yana milima mingi na nyufa. Kwa mfano, kuna hatari ya matetemeko Kalifornia nchini Marekani. Mitetemeko mingi yaani zaidi ya asilimia 80 hutokea katika beseni ya Pasifiki.
Katika mazingira ya volkeno tetemeko lasababishwa na miendo ya magma chini ya volkeno hasa wakati wa mlipuko.
Vipimo
Wataalamu hupima tetemeko kwa njia mbalimbali. Kuna skeli mbili zilizotumiwa mara nyingi ni zile za Richter na Mercalli. Katika miaka ya nyuma skeli mpya imeanza kutumiwa kimataifa ni "moment magnitude scale" (kifupi MMS, skeli ya kiasi cha nguvu) inayofanana zaidi na skeli ya Richter lakini iko makini zaidi kwa kutofautisha matetemeko makubwa.
Skeli ya matetemeko ya ardhi kufuatana na Richter na Mercalli | |||||
---|---|---|---|---|---|
Skeli ya Richter |
Skeli ya Mercalli |
Athira |
Idadi ya mitetemeko ya ardhi | ||
Tani TNT |
|||||
0 hadi 1.9 |
I |
hupimika kwa mitambo tu, haisikiki na wanadamu |
0.001–0.7 |
(4..4000)·106 |
nyingi sana zaidi ya 700,000 |
2 hadi 2.9 |
II |
inasikiwa na watu wachache wakilala pinduli huwa na mwendo kidogo |
1–22 |
(4..90)·109 |
300,000 |
3 hadi 3.9 |
III |
husikiwa na watu wachache mishtuko hulingana na lori linalopita bilauri zinazokaa pamoja kabatini zinatoa sauti hafifu |
30–700 |
(0,1..3)·1012 |
49,000 |
4 hadi 4.9 |
IV hadi V |
husikiwa na watu wengi. Mwendo wa penduli unaonekana kabisa Bilauri na sahani zatitima, magari huanza kubembea Vitu vinaweza kuanguka |
(1–22)·10 |
(4..90)·1012 |
6,200 |
5 hadi 5.9 |
VI |
watu hustuka na kukimbia kutoka nyumba zao viti, kabati na vitanda husukumwa kuta za nyumba zapata ufa |
(30–700)·10 |
(0,1..3)·1015 |
800 |
6 hadi 6.9 |
VII hadi IX |
husikiwa na watu wote wa eneo kwa hofu hata wakiwa kwenye gari nyumba zaanza kubomolewa Miti inabembea kama wakati wa upepo mkubwa Watu hujeruhiwa; penye majengo hafifu watu wanakufa lakini majengo yaliyo imara hayaharibiki Kwenye pwani kuna uwezekano wa mawimbi makubwa (chanzo cha tsunami) |
(1–22)·106 |
(4..90)·1015 |
120 |
7 hadi 7.9 |
X hadi XI |
watu honesha hofu kubwa wakijaribu kutoka nje ya nyumba kwa namna yoyote; nyumba nyingi zaharibiwa ; ufa zatokea katika ardhi; mabomba ya maji na gesi yavunjika watu hujeruhiwa na kuuawa kwenye pwani tsunami inaweza kutokea |
(30–700)·106 |
(0,1..3)·1018 |
18 |
8 hadi 8.9 |
XII |
uharibifu mkubwa; majengo yote yanaanguka au hayafai tena; maeneo makubwa yaharibiwa Kwenye pwani tsunami hadi kina cha mita 40 |
(1–22)·109 |
(4..90)·1018 |
kila baada ya miaka 5 |
9.0 na zaidi |
— |
Maafa makubwa; uharibifu kama juu; maisha yote yaweza kuzimwa kimahali Inawezekana pia: vipande vya uso wa ardhi huhamishwa; visiwa kupotea au kutokea; mabamba ya ganda la dunia yaonekana yamesukumwa; |
— |
— |
hakuna takwimu; tetemeko la aina hii labda kila baada ya miaka 10 hadi 100 |
Tanbihi
- ↑ The terrain below the Sarez Lake in Tajikistan is in danger of catastrophic flood if the landslide dam formed by the earthquake, known as the Usoi Dam, were to fail during a future earthquake. Impact projections suggest the flood could affect roughly 5 million people. Fresh alert over Tajik flood threat, BBC 2003
Viungo vya nje
- http://earthquake.usgs.gov/activity/past.html Ilihifadhiwa 6 Januari 2006 kwenye Wayback Machine.
- http://www.emsc-csem.org/#2 European-Mediterranean Seismological Centre
Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Tetemeko la ardhi kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |