Binadamu

(Elekezwa kutoka Wanadamu)
Binadamu

Uainishaji wa kisayansi
Domeni: Eukaryota
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Chordata (Wanyama wenye ugwe wa neva mgongoni)
Ngeli: Mamalia (Wanyama wenye viwele wanaonyonyesha wadogo wao)
Oda: Primates (Wanyama wanaofanana kiasi na binadamu)
Familia ya juu: Hominoidea (Wanyama kama binadamu)
Familia: Hominidae (Walio na mnasaba na binadamu)
Nusufamilia: Homininae (Wanaofanana sana na binadamu)
Jenasi: Homo
Linnaeus, 1758
Spishi: H. sapiens
Linnaeus, 1758
Nususpishi: H. s. sapiens

Binadamu (pia mwanadamu[2]) ni neno lenye asili ya Kiarabu linalomaanisha "Mwana wa Adamu", anayeaminiwa na dini za Uyahudi, Ukristo na Uislamu kuwa ndiye mtu wa kwanza.

Mchoro wa uenezi wa jenasi Homo katika miaka milioni mbili ya mwisho. Rangi ya samawati Inaonyesha uwepo wa spishi fulani wakati na mahali fulani.[1]
Ramani ya uenezi wa binadamu ([ka] inamaanisha miaka elfu).

Binadamu kadiri ya sayansi

hariri

Kisayansi jina hilo linaweza kutumika kwa maana ya Homo sapiens ili kumtofautisha na viumbehai wengine wa jenasi Homo ambao wote walitoweka walau miaka 12,000 hivi iliyopita.

Watu wote walioko leo hii ni spishi ileile na tofauti zinazoonekana kati ya maumbile yao katika sehemu mbalimbali za dunia ni ndogondogo tu.

Utafiti juu ya DNA umethibitisha kwamba binadamu wote wametokana na watu waliokuwepo Afrika walau miaka 300,000 hivi iliyopita.

Kwa namna ya pekee, upimaji wa DNA ya mviringo, ambayo kila mmoja anarithi kwa mama tu, umeonyesha kuwa binadamu wote waliopo duniani wanachanga mama mmoja aliyewahi kuishi miaka 160,000 hivi iliyopita[3].

Halafu upimaji wa kromosomu Y, ambayo kila mwanamume anarithi kwa baba tu, umeonyesha kuwa wanaume wote waliopo duniani wanachanga baba mmoja aliyewahi kuishi walau miaka 120,000 hivi iliyopita[4], kidogo tu kabla ya watu kuanza kuenea katika bara la Asia labda kufuatia pwani za Bahari ya Hindi.

Hata hivyo, miaka hii ya mwisho imegundulika katika baadhi ya wanaume wenye asili ya makabila ya Wabangwa na Wambo (Camerun, Afrika ya Kati) aina ya kromosomu Y tofauti sana na ile ya wanaume wengine wote waliowahi kupimwa, kiasi cha kukadiria zimetofautiana miaka 350,000 hivi iliyopita.

Vilevile, upimaji wa DNA ya mstari kwa jumla umeonyesha uwezekano wa kwamba baadhi ya binadamu wa leo, wale wasio wa Kusini kwa Sahara, wana asilimia 1-6 ya urithi wa kibiolojia kutoka kwa aina nyingine za Homo, hususan Homo neanderthalensis, ile ya pango la Denisova na ile iliyorithiwa na baadhi ya watu wa visiwa vya Andaman (India).

Kama hao waliweza kweli kuzaliana na Homo sapiens na kuacha uzao uliojiendeleza maana yake walikuwa spishi moja na yeye. Hapo asili ya binadamu inatakiwa kuhesabiwa ya zamani zaidi sana kuliko miaka 200,000 iliyofikiriwa kwanza[5].

Uenezi wa binadamu

hariri

Kutoka bara la Africa watu walienea kwanza Asia , Australia na Ulaya, halafu Amerika toka kaskazini hadi kusini.

Hatimaye, katika karne ya 20 watu walikwenda kukaa kwa muda katika bara la Antaktika kwa ajili ya utafiti.

Upekee wake

hariri

Ingawa binadamu ana undugu mkubwa wa kibiolojia na sokwe na viumbe vingine, ustawi wake hauna mfano, kiasi cha kufanya wengi waamini kwamba tofauti iliyopo inadai kuelezwa kwa uwemo wa roho ndani ya mwili wake; roho ambayo dini hizo zinasadiki imetiwa na Mungu moja kwa moja.

Binadamu kadiri ya Biblia

hariri

Kadiri ya Biblia, binadamu ameumbwa “kwa mfano wa Mungu” (Mwa 1:27), mwenye roho isiyokufa. Hivyo, Mungu amependa kuwasiliana na watu, akijitambulisha na kujitoa kwetu, tuweze kuishi katika urafiki naye na hatimaye tushiriki heri yake.

Ameshirikishwa naye ukuu juu ya viumbe vyote vinavyoonekana. “Nikiziangalia mbingu zako, kazi ya vidole vyako, mwezi na nyota ulizoziratibisha; mtu ni kitu gani hata umkumbuke, na binadamu hata umwangalie? Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu; umemvika taji ya utukufu na heshima” (Zab 8:3-5). “Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake; lakini ninyi nimewaita rafiki, kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu” (Yoh 15:15). Amefanya hivyo kwa maneno na matendo yanayoshikamana sana kwa kuwa maneno yanafafanua matendo, nayo matendo yanathibitisha maneno.

Mungu ametufunulia pia ukweli juu yetu wenyewe akijibu kabisa maswali yanayotusumbua kuhusu maana na lengo la maisha yetu. “Mungu hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli” (1Tim 2:4). “Mungu si mtu, aseme uongo” (Hes 23:19). Yeye hadanganyiki wala hadanganyi.

Kati ya viumbe vinavyoonekana, mtu tu ni nafsi, akiwa na uwezo wa kujifahamu, kujitawala, kujitolea na kupendana na wengine. Basi, anapaswa kulinda hadhi hiyo asitawaliwe na tamaa za kila aina. Akifanya hivyo anatimiza mpango wa Mungu juu yake na kupendana naye.

Malaika na watu ndio viumbe pekee vyenye hiari ya kuchagua wenyewe wachangie mpango wa Mungu au la. “Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi, chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako; kumpenda Bwana, Mungu wako, kuitii sauti yake, na kushikamana naye; kwani hiyo ndiyo uzima wako” (Kumb 30:19-20).

Malaika na watu wanaweza kuchagua hata wawe wema au wabaya milele. “Kulikuwa na vita mbinguni: Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, yule joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake; nao hawakushinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni” (Ufu 12:7-8).

Chaguo letu binadamu linafanyika siku kwa siku kwa kuchukua misimamo mizuri au mipotovu kuhusu dini na maadili. “Mwayachunguza Maandiko, kwa sababu mnadhani kwamba ninyi mna uzima wa milele ndani yake; na hayo ndiyo yanayonishuhudia. Wala hamtaki kuja kwangu mpate kuwa na uzima” (Yoh 5:39-40).

Binadamu ni umoja wa mambo mawili: roho iliyoumbwa na Mungu moja kwa moja, na mwili ulioumbwa naye kwa njia ya wazazi. Maumbile hayo yanatakiwa kukamilika kwa kupokea na kutimiza upendo wa Mungu aliyesema, “’Na tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi’. Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba” (Mwa 1:26-27).

Hivyo, mwili wetu ni muhimu, kwa sababu umeumbwa na Mungu, umetwaliwa na Mwanae ili atuokoe, umehuishwa na Roho Mtakatifu atakayeutukuza siku ya ufufuo kwa mfano wa Yesu. “Mwili si kwa zinaa, bali ni kwa Bwana, naye Bwana ni kwa mwili. Naye Mungu alimfufua Bwana, na tena atatufufua sisi kwa uweza wake. Je, hamjui ya kuwa miili yenu ni viungo vya Kristo? Basi nivitwae viungo vya Kristo na kuvifanya viungo vya kahaba? Hasha! Au hamjui ya kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye?… Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu?” (1Kor 6:13-16,19).

Utotoni anasukumwa tu na haja za umbile lake, ambazo ni muhimu kwake na anazilenga bila ya kuhitaji juhudi.

Lakini akikua anaanza kutambua tunu za maadili na dini, ambazo ni njema, ni muhimu kwa zenyewe na zinamdai azifuate kwa nia imara hadi afikie lengo.

Kwa bidii za kudumu za namna hiyo anamlenga hasa Mungu, wema mkuu.

Anapopitia misukosuko ya ujana asikubali kushindwa na vionjo wala asikate tamaa, kwa kuwa Mungu amemuumba atawale hata nafsi yake na mwili wake.

Mtu wa kwanza kuumbwa na Mungu kadiri ya Biblia alikuwa Adamu, akifuatwa na Eva mkewe. Hapo “Mungu aliona kila kitu alichokifanya, na tazama ni chema sana” (Mwa 1:31).

Hata hivyo, baada ya dhambi ya asili anadaiwa bidii katika kutekeleza tunu ili wema alionao uzae matunda.

Basi, apanie kukuza wema aliojaliwa ili kesho awe mtu bora kama mzazi, raia, kiongozi wa dini na jamii n.k.

Penye nia pana njia hata ya kuelekea utakatifu utakaokamilika katika uzima wa milele.

Binadamu amekabidhiwa na Mungu dunia, lakini hasa amekabidhiwa nafsi yake mwenyewe. Itamfaa nini kujua na kutawala ulimwengu, asipojijua na kujitawala kweli?

Binadamu na elimunafsia

hariri

Karne XX imeleta maendeleo makubwa katika elimunafsia (= saikolojia). Hivyo anaweza kutambua vizuri mema na mabaya yaliyomo ndani mwake.

Lakini akitaka kujifahamu haitoshi asikilize mafundisho hayo au kusoma vitabu vingi juu yake.

Anahitaji kuishi katika mazingira bora ambapo ajisikie nyumbani, huru na mtulivu kwa kupendana na wenzake, kusikiliza watu wanaomfahamu (hasa walezi wake) wanasema nini juu yake, kujipatia muda wa kutulia peke yake na kujifikiria kulingana na maneno yao, kujichunguza kwa makini kuanzia miaka ya utotoni.

Kwa kuwa utu unategemea urithi, mazingira na utashi wa kila mmoja, anapaswa kuchunguza hayo yote yaliyochangia kumjenga.

Mara kwa mara ajitenge na watu na shughuli ili kutathmini tena maisha yake, kupima maono yake na kuweka maazimio ya kufaa, bila ya kusahau kwamba uhai wake ni fumbo, kwa kuwa unamtegemea Mungu.

Tazama pia

hariri

Tanbihi

hariri
  1. Stringer, C. (2012). "What makes a modern human". Nature. 485 (7396): 33–35. doi:10.1038/485033a. PMID 22552077.
  2. Maneno "Binadamu" na "Mwanadamu" ni maneno mawili yaliyo tofauti kimatamshi lakini yenye maana moja kidhana. Neno "Binadamu" kietimolojia huundwa na maneno mawili tofauti ambayo hutokana na lugha ya Kisemiti katika lahaja za Kiarabu na Kiebrania ambapo neno "Bin" etimolojia yake ni lugha ya Kiarabu ambapo neno hilo Bin humaanisha "Mtoto wa jinsia ya kiume". Halikadhalika neno "Adamu" etimolojia yake ni kutoka katika lugha ya Kiebrania ambapo neno hilo Adamu hutokana na neno "Adamah" lenye maana ya "Ardhi". Kwa upande mwingine neno "Mwanadamu" huundwa kutokana na etimolojia mbili tofauti kutoka katika lugha za Kiswahili na Kiebrania ambapo katika etimolojia ya lugha ya Kiswahili hutoka neno "Mwana" ambalo humaanisha "Mtoto" na ambapo pia etimolojia yake hutoka katika neno la Kibantu "Omona/Umwana" lenye maana ya "Mtoto wa jinsia ya kiume au kike". Hivyo basi, kietimolojia inaposemwa "Bin-Adamu" humaanishwa "Mtoto wa jinsia ya kiume wa kiumbe hai yeyote mwenye asili ya ardhi" yaani "Adamah", na halikadhalika inaposemwa "Mwana-Adamu" humaanishwa "Mtoto wa jinsia ya kiume au kike aliyetokana na kiumbe hai yeyote mwenye asili ya udongo".
  3. Although the original research did have analytical limitations, the estimate on the age of the mt-MRCA has proven robust. More recent age estimates have remained consistent with the 140–200 kya estimate published in 1987: A 2013 estimate dated Mitochondrial Eve to about 160 kya (within the reserved estimate of the original research) and Out of Africa II to about 95 kya.
  4. Another 2013 study (based on genome sequencing of 69 people from 9 different populations) reported the age of Mitochondrial Eve between 99 to 148 kya and that of the Y-MRCA between 120 and 156 kya.
  5. Omo Kibish Formation and its neighboring sites in Ethiopia have produced some of the earliest examples of fossilised human and australopithecine remains and stone tools. Richard Leakey's work there in 1967 found some of the oldest remains of primitive Homo sapiens. Earlier believed to be around 125,000 years old, more recent research indicates they may in fact date to c.195,000 years ago. "The Oldest Homo Sapiens: Fossils Push Human Emergence Back To 195,000 Years Ago", ScienceDaily. (en) 

Viungo vya nje

hariri