Silika kadiri ya Wagiriki
Silika kadiri ya Wagiriki wa kale zinategemea mambo manne yaliyomo mwilini mwa binadamu na yalidhaniwa kuutawala, yaani nyongo, neva, damu au limfu.
Kwa maneno mengine, zamani walidhani silika nne za msingi walizoziainisha zinategemea kile kinachotawala mwili wa mtu. Labda asili ya upambanuzi huu ni mganga Hipokrate (aliyekufa mwaka 377 K. K.).
Dhana hiyo haikubaliki tena, lakini wengiwengi wanafuata bado upambanuzi huo kadiri ya jambo linalojitokeza zaidi katika silika ya mtu, yaani hasira, huzuni, uchangamfu au upole.
Msingi wake ni jinsi yanavyochanganyikana kwa namna tofauti mambo mawili: wepesi wa kuhemka na elekeo la kutenda.
Aliye na yote mawili kuliko kawaida ni mtu wa hasira. Aliye na lile la kwanza kuliko kawaida lakini la pili kidogo kuliko kawaida ni mtu wa huzuni. Aliye na lile la kwanza kidogo kuliko kawaida lakini la pile kuliko kawaida ni mtu wa uchangamfu. Hatimaye aliye na yote mawili kidogo kuliko kawaida ni mtu wa upole.
Kwa kujibu maswali kadhaa tunaweza kujua tunayo kwa asilimia ngapi, na hivyo tunalingana na taswira mojawapo kwa kiasi gani.
Kila silika inapakana na nyingine mbili ambazo zinafanana nayo upande wa wepesi wa kuhemka au upande wa elekeo la kutenda, kumbe ni kinyume cha ya nne ambayo hailingani nayo wala upande wa wepesi wa kuhemka wala upande wa elekeo la kutenda.
Silika ya hasira
haririMwenye tabia hiyo anaitikia mambo kwa kusisimka mara kwa nguvu, halafu athari yake inadumu muda mrefu nafsini mwake.
Sifa njema ya silika hiyo tajiri sana ni akili kali, uwezo wa kukusanya mawazo, utashi imara, udumifu, utendaji mwingi, moyo mkuu, ufadhili. Anachukia pumziko na upotevu wa muda. Ana nia na mambo; kila mara anavutiwa na mipango mikubwa na kuanza mara kuishughulikia, asirudi nyuma mbele ya matatizo. Mara nyingi anakuwa kiongozi, mtawala, mtume mkubwa.
Kasoro zake: msimamo wake unamuelekeza kuwa mgumu, kutojali, kutakabari, kuwa kaidi, kukasirika. Mara nyingi ana uchu wa madaraka na ukuu. Katika mafungamano hana ulaini wala haelewi sana uchungu wa wengine.
Msisimko wake katika utendaji na hamu kubwa ya kufanikisha mipango yake vinamfanya akanyage vipingamizi vyovyote na kuonekana hana moyo. Akipingwa anaweza akawa katili; akishindwa anaweza akatunza chuki hadi saa ya kulipa kisasi. Miguso yake inazama katika ukali wa hisia zake.
Asitende harakaharaka, asiamini misukumo ya kwanza kutoka moyoni. Atekeleze unyenyekevu halisi, ahurumie walio dhaifu, asimdhalilishe yeyote, asitawale kwa mabavu. Akifaulu kuratibu milipuko ya hasira yake na kuelekeza vizuri nguvu zake anajipatia upole bora na kuwa wa thamani sana. Kazi ngumu zinafanikiwa mikononi mwake kutokana na utashi na udumifu alionao. Kwa urahisi fulani anaweza akafikia utakatifu mkuu. Kati ya Watakatifu Wakristo walikuwa na silika hiyo Mtume Paulo, Jeromu, Ignasi wa Loyola, Fransisko wa Sales na wengine wengi.
Silika ya huzuni
haririMwenye tabia hiyo anaitikia mambo kwa msisimko ambao mwanzoni ni dhaifu na wa shida, lakini unakuwa wa nguvu na wa dhati akiendelea kuathiriwa; tena kwa kawaida ni wa muda mrefu: hasahau kwa urahisi.
Sifa njema: miguso yake ni ya ndani, lakini haijitokezi sawasawa. Kwa kawaida ana akili kali na ya kina, akiivisha mawazo kwa kutafakari kwa utulivu. Anaelekea kukaa pweke na kufuata ibada na maisha ya kiroho. Hivyo anaweza akawa msomi mkavu anayejifungia kutafuta elimu au mwanasala anayezama katika mambo ya Mungu. Anavutiwa na sanaa na kufaa upande wa sayansi. Akipenda si rahisi kukata upendo. Ni mwepesi kuhurumia na kufadhili (hasa wagonjwa), akijitolea hadi ushujaa. Anapatwa na uchungu akiona watu baridi na wasio na shukrani. Utashi wake unategemea hali ya mwili: ni dhaifu sana akiishiwa nguvu, kumbe una juhudi akiwa na afya na kupata furaha kidogo. Ni mtu wa kiasi, havurugwi na maono.
Kasoro: hasa ni elekeo kubwa mno kwa huzuni. Anaweza akatarajia daima mabaya, akaona magumu tu, akazidisha ukubwa wa matatizo. Kwa hiyo anakwepa watu, hajitokezi, ana aibu, hajiamini, ana wasiwasi juu ya maadili yake, anashindwa kuamua, anakata tamaa. Anasitasita kwa kuogopa atashindwa, hivyo anapoteza fursa nyingi. Anateseka na bila ya kukusudia anasababisha wengine pia wateseke. Anaweza akapatwa na donda baya nafsini mwake, anapoonja peke yake uchungu wote, kwa kukosa ari ya kuutokeza. Hali hiyo ikizidi na kumfanya adaidai mambo ya pekee au kutokeza uchovu wa neva, hafai kuishi kijumuia. Mwenye silika hiyo anapenda kujieleza vizuri katika uongozi wa kiroho, lakini hawezi kwa sababu ya kujikusanya mno kwa ndani. Kiongozi amuelewe hivyo na kutumia busara na adabu sana. Amsaidie kumtegemea Mungu, kukabili maisha kwa amani na kutarajia mema. Pia aamini zaidi kuwa anafaa kwa makuu. Kwa kutumia elekeo lake kwa fikara aelewe hana sababu ya kuguswa mno, kuogopa na kujitenga. Pengine apumzike na kula vizuri. Hasa aachane na wasiwasi na woga kwa kuweka maazimio imara na kulenga makuu kwa moyo na tumaini. Kati ya Watakatifu Wakristo walikuwa na silika hiyo Mtume Yohane, Bernardo wa Klervoo, Alois Gonzaga, Teresa wa Mtoto Yesu na wengineo.
Silika ya uchangamfu
haririMwenye tabia hiyo anasisimka kwa urahisi na nguvu mbele ya chochote, lakini itikio hilo ni la muda mfupi. Kumbukumbu ya mambo yaliyopita haisababishi msisimko mpya. Silika hiyo ni kinyume cha ile ya huzuni: haina wepesi wa kuhemka, bali inaelekea utendaji.
Sifa njema: ni msemaji, mfurahivu, mwenye heshima kwa wote, msikivu na mtiifu kwa wakubwa, mnyofu na wazi (pengine kupita kiasi). Anaelekea kusifu mno kuliko kulaumu. Anashangaa kuona watu wakichukia utani wake usiofaa, kwa kuwa anaudhani mzuri kabisa. Hajui ukaidi. Anaguswa na kutiwa huruma na matatizo ya watu, halafu anajitolea kweli. Wema wake unapendeza, ari yake inaambukiza na kuvutia wengi. Kwa kuwa anafurika mapendo, ni mwepesi kufanya urafiki na kuufuata kwa bidii. Akichukizwa anaitikia pengine kwa ukali na matusi, lakini anasahau yote mara, hatunzi kinyongo. Anajua kushughulika kwa kuwa anakabili maisha kwa utulivu, akitarajia daima mazuri, asirudi nyuma mbele ya matatizo. Ana kumbukumbu na ubunifu mkubwa, hivyo anafaulu katika sanaa na mahubiri, lakini hawi mwenye hekima zaidi, kwa kuwa akili yake ni nyepesi, inadaka kwa urahisi, ila haina kina.
Kasoro zake ni kubwa kama sifa njema: hasa ni ujuujuu, ugeugeu na tamaa za mwili. Ujuujuu unatokana na uerevu na urahisi wa fikra unaomfanya adhani ameelewa mara suala lolote, kumbe amelihisihisi tu. Ndiyo sababu tathmini zake ni za harakaharaka, mara nyingi si sahihi, pengine hazina ukweli wowote. Katika masomo ni mvivu: anapenda upana wa ujuzi, anaoweza kuuonyesha ili kujipatia sifa, kuliko kina chake. Ugeugeu unatokana na ufupi wa muda wa maitikio yake: mara anacheka, mara analia; ghafla anaacha uchangamfu mkubwa na kupatwa na huzuni kubwa vilevile. Anatubu makosa mapema na kwa moyo, lakini anayarudia katika nafasi ya kwanza, kwa kuwa anasisimka mno, hana nguvu na moyo ashinde tamaa za mwili zinazostawi kutokana na umotomoto wa silika hiyo. Kwake ni vigumu kutawala macho, masikio na ulimi wake. Katika sala anatawanya mawazo kwa urahisi. Hapendi sadaka, kujikana, kujitahidi kwa kudumu. Vipindi vya bidii kubwa vinafuatwa na vingine vya kuvunjika moyo.
Aelekeze umotomoto wa mapendo yake kwenye lengo bora: akichanganyikiwa na Mungu atakuwa mtakatifu mkubwa, kama Mtume Petro, Agostino wa Hippo, Teresa wa Yesu, Fransisko Saveri na wengineo. Lakini ni lazima ashinde kabisa kasoro zake. Dhidi ya ujuujuu azoee kutafakari na kupima mambo yote, aelewe masuala pande zote, kwa kutabiri matatizo yanayoweza kutokea, asitarajie mema tu. Dhidi ya ugeugeu asitegemee maazimio tu, hata akiyaweka kwa moyo, kwa kuwa atayavunja mara. Amtii kabisa kiongozi wa kiroho, ashike ratiba ambayo iwe imekubaliwa naye na kupanga yote bila ya kuacha nafasi kwa utashi wake dhaifu. Ajitafiti kwa bidii na kujiadhibu vikali kwa makosa. Katika sala asitafute faraja za kihisi, bali adumu katika ukavu pia. Dhidi ya tamaa mbaya awe mwangalifu daima, akikwepa nafasi yoyote ya hatari, akikusanya mawazo na kutawala hisi za ndani na za nje, akizuia hasa macho kwa kukumbuka mang’amuzi ya kusikitisha. Amuombe Mungu kwa unyenyekevu na udumifu neema ya usafi ambayo inatoka mbinguni tu.
Silika ya upole
haririMwenye tabia hiyo anasisimka kidogo tu. Itikio lake kwa lolote ni dhaifu au halipo kabisa. Haatiriki nafsini mwake kwa kuwa alama yoyote inafutika mara.
Sifa njema: anatenda polepole lakini kwa mfululizo, mradi asidaiwe juhudi kubwa mno. Hatawaliwi na maono. Hachukizwi sana na matusi, maradhi wala kutofanikiwa. Anadumu kuwa mtulivu, mwenye kiasi na busara. Anajua kukabili maisha, kwa sababu anafikiri sana na kutenda kwa hakika, akifikia malengo yake pasipo kutumia nguvu zaidi, kwa kuwa anaondoa vipingamizi badala ya kuvivunja. Anazungumza kwa haki na namna ambayo inaeleweka na kuvutia. Ana moyo mwema, ingawa unaonekana baridi. Ikiwa lazima atajitolea hata kishujaa, lakini si kwa ari na kwa kusukumwa na umbile lake la uvivu. Hajitokezi. Kimwili ana sura ya kupendeza, tipwatipwa, mwendo wa taratibu. Pengine akili yake ni kubwa sana. Anafaa kwa utafiti wa sayansi unaodai subira ya muda mrefu, si kwa ubunifu wa mambo mapya. Mwanateolojia Thoma wa Akwino kwa kufaidika na sifa bora za silika hiyo alifanya kazi kubwa kwa utulivu na utaratibu.
Kasoro: anapoteza fursa nyingi kwa kuchelewa kuzitumia. Hata katika shida za haraka ni kama amesinzia. Hajali sana yanayotokea nje yake. Anaishi kama kwa ubinafsi. Hafai kuagiza wala kutawala. Hapendi matendo ya toba na malipizi: hakuna hatari kuwa atajidhuru kwa hayo! Anahitaji kuwa na msimamo (wa imani) na kujilazimisha afanye juhudi za mpango na za kudumu. Polepole atafika mbali, mradi aache kusinziasinzia na kupiga uvivu. Badala yake alenge makuu. Ajirekebishe si kwa kujizuia (inavyompasa mwenye silika ya hasira iliyo kinyume chake), bali kwa kujichochea na kuamsha nguvu zilizosinzia.
Tanbihi
haririMarejeo
hariri- Arikha, Noga (2007). Passions and Tempers: A History of the Humours Ilihifadhiwa 24 Machi 2017 kwenye Wayback Machine.
- Helminen, Päivi (1999). Discovering Our Potential: An Introduction to Character Types Ilihifadhiwa 10 Mei 2012 kwenye Wayback Machine.
- Rudolf Steiner (1909). The Four Temperaments
Viungo vya nje
hariri- Four Temperaments Test Ilihifadhiwa 3 Septemba 2014 kwenye Wayback Machine., personality test.
- In Our Time (BBC Radio 4) episode on the four humours in MP3 format, 45 minutes
- John T. Cocoris, Psy.D. Description of the 4 Primary Temperaments at fourtemperament.com Ilihifadhiwa 2 Oktoba 2014 kwenye Wayback Machine.
- Descriptions of The Temperament Blends Ilihifadhiwa 9 Oktoba 2014 kwenye Wayback Machine.