Somo la Kimungu
Somo la Kimungu (kwa Kilatini: Lectio Divina), hasa somo la Biblia, ni kati ya njia kuu za utakatifu zilizotolewa kwa Wakristo wote[1]. Mara nyingi udanganyifu, uzushi na uhuni vinaambukiza kupitia vitabu vibaya, kumbe “kusoma vitabu vitakatifu ni uzima wa roho” (Ambrosi).
Biblia
haririJeromu alisimulia jinsi alivyovutiwa kusoma kwa juhudi Maandiko matakatifu. Alipoanza kutawa, akipenda bado vitabu vya fasihi, aliota yuko mbele ya Mungu na kuulizwa kwa ukali ni nani. Alipojieleza kuwa Mkristo, Hakimu mkuu akamjibu, “Mwongo wewe, u mfuasi wa Sisero; kwa sababu hazina yako ilipo, ndipo ulipo moyo wako pia”. Mara akaagiza apigwe mijeledi. “Nilipoamka nilitambua haikuwa ndoto tu, bali kweli, kwa sababu mabegani nilikuwa na alama za mapigo niliyoyapata. Kuanzia hapo nimesoma Maandiko matakatifu kwa bidii nyingi kuliko nilivyokuwa nikisoma vitabu visivyo vya dini kwanza”. Basi, aliandika, “Usingizi ukukute tu ukisoma, tena angalia sana usipatwe na usingizi juu ya kitabu tofauti na Maandiko matakatifu”.
Kwa Wakristo hakuna kitabu wanamoweza kuchota uzima kuliko katika kile alichokiandika Mungu. Hasa Injili, maneno ya Mwokozi na matukio ya maisha yake yawe fundisho hai la kulizingatia daima. Yesu alijua kufanya mambo makuu yaeleweke kwa wote kutokana na usahili alioutumia. Tena neno lake halibaki nadharia tu, bali linaongoza mara kwenye unyenyekevu halisi, upendo wa Mungu na wa jirani. Katika kila neno alitafuta tu utukufu wa Baba aliyemtuma na wokovu wa watu. Turudie daima maneno ya hotuba ya mlimani (taz. Math 5-7) na yale yaliyofuata karamu ya mwisho (taz. Yoh 13-17). Tutakuta ndani yake neema inayotuongoza kuiga kila siku vizuri zaidi maadili ya Mwokozi na upendo wake wa kishujaa kwa msalaba. Pamoja na ekaristi, ndiyo lishe halisi ya watakatifu: Neno la Mungu tuliloletewa na Mwanae pekee, Neno aliyefanyika mwili. Chini ya herufi zake limefichika wazo hai la Mungu, ambalo vipaji vya akili na hekima vinatuwezesha kulichimba na kulionja zaidi na zaidi.
Baada ya Injili hakuna kinachotulisha kuliko Matendo ya Mitume na Nyaraka zao. Ndiyo mafundisho ya Mwokozi ambayo wafuasi wake wa kwanza, walioagizwa kutulea katika shule yake, waliyatekeleza na kuyafafanua jinsi waamini walivyohitaji. Maisha ya kishujaa ya Kanisa la mwanzoni, uenezi wake kati ya matatizo makubwa, yale yote yanayoelezwa na Matendo ya Mitume ni fundisho la kumtumainia Mungu na kujiachilia kwake. Hakuna kurasa za dhati na hai kuliko zile za Nyaraka kuhusu Nafsi na kazi za Kristo (taz. Kol 1), uangavu wa maisha ya Kanisa na ukuu wa upendo wa Mwokozi kwake (taz. Ef 1-3), kufanywa waadilifu kwa kumuamini Kristo (taz. Rom 1-11), ukuhani wa milele wa Yesu (taz. Eb 1-9). Halafu tukizingatia maadili ya Nyaraka, hakuna mahimizo ya nguvu zaidi kwa ajili ya upendo, uwajibikaji, udumifu, subira, utakatifu, pamoja na kanuni za hakika kuhusu namna ya kuwatendea wakubwa, watu wa hali moja nasi, wadogo, tena watu dhaifu, wakosefu, walimu wa uongo. Hakuna maelezo hai zaidi kuhusu wajibu wa Wakristo wote kwa Kanisa.
Katika Agano la Kale kila Mkristo anapaswa kuzijua hasa Zaburi, zinazodumu kuwa sala ya Kanisa.
Tukirudia kusoma mfululizo, kwa heshima na upendo, Maandiko matakatifu, tutakuta ndani yake mwanga na nguvu mpya daima. Mungu amelitia neno lake uweza usioisha, nasi kisha kusoma vitabu vingi na kuvikinai karibu vyote, hatimaye tutairudia Injili kama utangulizi wa mwanga wa milele.
Maandishi ya watakatifu
haririBaada ya Biblia, vitabu vya watakatifu ndivyo vinavyotuangaza na kutuwasha zaidi. Vimeandikwa kwa mwanga na mpako wa Roho Mtakatifu, ingawa si kwa uvuvio ule usioweza kukosea.
Kanisa Katoliki linashauri tujue vitabu bora vya Bazili Mkuu, Yohane Krisostomo, Jeromu, Augustino, Yohane Kasiano, Leo Mkuu, Denis, Benedikto, Gregori Mkuu na Maksimo Muungamadini.
Tujue pia yanayohusu maisha ya Kiroho katika maandishi ya Anselmi, Bernardo, Richard wa Mt. Viktori, Alberto Mkuu, Thoma wa Akwino, Bonaventura, Anjela wa Foligno, Yohane Tauler, Henri Suso, Katerina wa Siena, Yohane Ruysbroeck na Thomas wa Kempis, mtunzi wa Kumfuasa Yesu Kristo.
Kwa karne zilizofuata, tusome vitabu vya Inyasi wa Loyola, Alois wa Blois, Teresa wa Yesu, Yohane wa Msalaba, Alois wa Granada, Fransisko wa Sales, Alois Lallemant, Vinsenti wa Paulo, Yakobo B. Bossuet, Alois Maria wa Montfort na Alfonso Maria wa Liguori.
Kuhusu waandishi wa karne za mwishomwisho, walio muhimu zaidi kati yao wanajulikana na wote, hasa Teresa wa Mtoto Yesu.
Maisha ya watakatifu
haririTuongeze kusoma maisha ya watakatifu, ambayo daima yanavutia na mara nyingi yanaweza kuigwa. Vitabu hivyo vinatueleza walivyotenda, katika nafasi pengine ngumu, wenzetu wa kiume na wa kike, ambao mwanzoni walikuwa na kasoro na udhaifu sawa nasi, lakini polepole neema ikaja kushinda umbile lao kwa kuliponya, kuliinua na kulitia uzima mpya. Ndani mwao tunaona maana halisi na uzito wote wa neno la Thoma wa Akwino: “Neema haiangamizi umbile, bali inalikamilisha”. Katika watakatifu, hasa kwenye hatua ya muungano, mema ya umbile yanalingana kweli na neema.
Katika maisha yao tuzingatie zaidi yanayoweza kuigwa; mambo ya pekee tuyaone tu kama ishara ya Kimungu tuliyopewa ili tutoke usingizini na kutambua yaliyo ya ndani na ya juu zaidi katika maisha ya Kikristo ya kawaida. Kwa mfano, maumivu ya waliotiwa madonda ya Yesu yatukumbushe Mateso ya Mwokozi yanapaswa kuwa nini kwetu na jinsi tunavyotakiwa kuimba vizuri zaidi kwenye Njia ya Msalaba, “Mama mtakatifu, fanya hivi, / choma kabisa moyoni mwangu / madonda ya Msulubiwa”. Neema ya watakatifu kadhaa kunywea donda la Moyo wa Yesu itukumbushe kila Komunyo inavyopaswa kuwa motomoto na bora kuliko ile iliyotangulia. Mifano ya watakatifu kuhusu unyenyekevu, subira, tumaini, upendo usiokoma, inatuvuta kuliko mafundisho ya kinadharia tutekeleze maadili: “Mawazo pekee hayasukumi”.
Inafaa zaidi kusoma maisha ya watakatifu yaliyoandikwa na watakatifu, kama vile yale ya Fransisko wa Asizi yaliyoandikwa na Bonaventura; yale ya Katerina wa Siena yaliyoandikwa na Raimundi wa Capua, kiongozi wake; na yale ya akina Teresa waliyoyaandika wenyewe.
Misimamo inayohitajika ili kufaidika na masomo hayo
haririSala iliyofanywa vizuri mwanzoni inatupatia neema ya msaada ya kusoma kwa imani, ili kumtafuta Mungu katika maandishi ya Kiroho, tukiepa udadisi usio na maana, majivuno ya akili na elekeo la kuhukumu tunayoyasoma badala ya kufaidika nayo. Tusiridhike na ujuzi tu, bali tuone namna ya kutekeleza wenyewe, tukiwa na hamu hai tena nyofu ya ukamilifu. Hapo tutapata faida kubwa, hata tukisoma kuhusu “maadili madogomadogo” (Fransisko wa Sales), kwa kuwa yote yanafungamana na adili kuu la upendo.
Waliosonga mbele katika njia ya ukamilifu, pengine ni vizuri warudie kusoma yale yanayowafaa wanaoanza: wataona yote kwa mwanga wa juu zaidi na kushangaa yaliyofichika ndani yake; k.mf. katika mistari ya katekisimu ndogo inayohusu lengo la kuwepo duniani: “kumjua, kumpenda na kumtumikia Mungu ili kupata uzima wa milele”. Vilevile inafaa wanaoanza wachungulie ukuu wa ukamilifu wa Kikristo, mradi wasidai kuruka juu kabla hawajapewa neema hiyo. Kwa kuwa lengo la kulifikia ni la mwisho katika utekelezaji, lakini ni la kwanza katika nia: toka mwanzo ni lazima tukusudie kufikia utakatifu ule utakaotuwezesha kuingia mbinguni mara baada ya kufa.
Ikiwa wanaoanza na wanaoendelea wana hamu kubwa ya utakatifu, watakuta katika Maandiko matakatifu na katika vitabu vya watakatifu yale yanayowafaa na watafundishwa na mlezi wa ndani. Lakini ni lazima tusome polepole: si kumeza vitabu, bali kupenyezwa na yale tunayoyasoma. Hapo masomo ya Kiroho yatageuka kuwa sala. Kwa Benedikto kusoma ni kidato cha kwanza katika ngazi ifuatayo ya kupanda juu: “Lectio (kusoma), cogitatio (kufikiri), studium (kuzingatia), meditatio (kutafakari), contemplatio (kutazama)”.
Inafaa pia turudie kusoma baada ya miaka vitabu bora vilivyokwishatusaidia. Maisha ni mafupi: turidhike kusoma na kurudia kusoma vile ambavyo kweli vina mhuri wa Mungu, bila kupoteza muda kwa vile visivyo na uhai wala thamani. Ni afadhali kuchimba kitabu kimoja bora kuliko kusoma kijuujuu vile vyote vya waandishi wa Kiroho.
Halafu tusome kwa roho ya ibada, “kwa kutafuta si ujuzi tu, bali hasa ladha” ya mambo ya Mungu (Bernardo). “Asomaye na afahamu” (Math 24:15), akimuomba mwanga wa kuelewa vema. Wanafunzi wa Emau hawakuelewa utabiri wa manabii mpaka Bwana alipofungua akili zao. Ndiyo sababu Bernardo alisema, “Sala ikatishe somo”: hapo tu litalisha roho na kuelekeza kusali[3].
Hatimaye ni lazima tuanze mara kutekeleza tuliyoyasoma: “Kila asikiaye maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba… Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga” (Math 7:24,26). “Kwa sababu sio wale waisikiao sheria walio wenye haki mbele za Mungu, bali ni wale waitendao sheria watakaohesabiwa haki” (Rom 2:13). “Iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu” (Yak 1:22).
Hapo somo litazaa matunda mema: “Nyingine zilianguka penye udongo mzuri; zikamea, zikazaa moja kwa mia… ndio wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao hulisikia neno, na kulishika; kisha huzaa matunda kwa kuvumilia” (Lk 8:8,15). Ndivyo lilivyokuwa somo alilolifanya Augustino aliposikia: “Chukua na kusoma”; alifungua Nyaraka zilizokuwa mezani, akasoma, “Kama ilivyohusika na mchana na tuenende kwa adabu; si kwa ulafi na ulevi, si kwa ufisadi na uasherati, si kwa ugomvi na wivu. Bali mvaeni Bwana Yesu Kristo” (Rom 13:13-14). Mara akaongoka, akajitenga kwa muda, akajiandikisha kwa ubatizo: matunda yakawa kweli mara mia kwa faida ya wengi hadi leo.
Tanbihi
hariri- ↑ Opening to God: Lectio Divina and Life as Prayer by David G. Benner 2010 ISBN|0-8308-3542-3 pages 47–53
- ↑ The Way of Perfection by Teresa of Avila 2007 ISBN|1-4209-2847-3 page 145
- ↑ Vatican website: Angelus Nov 6 2005
Marejeo
hariri- Basil Pennington (1998), Lectio Divina: Renewing the Ancient Practice of Praying the Scriptures (ISBN|0-8245-1736-9).
- Geoff New, Imaginative Preaching: Praying the Scriptures so God Can Speak through You, Langham Global Library, (ISBN|9781783688999).
- Sr Pascale-Dominique Nau, When God Speaks: Lectio Divina in Saint John of the Cross, the Ladder of Monks and the Rule of Carmel (Rome, 2012). (ISBN|978-1291037029) [1]
- Guigo II the Carthusian, The Ladder of Monks translated by Sr Pascale-Dominique Nau, OP, Rome, 2013 [2].
- Jean Khoury, Lectio Divina at the School of Mary (2018), (ISBN|978-1976811722) [3].
Viungo vya nje
hariri- Benedictine resources for Lectio Divina (Original missing. Archived copy: [4])
- Lectio Divina at the Carmelite Website
- Jean Khoury resources for Lectio Divina
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Somo la Kimungu kama historia yake, matokeo au athari zake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |