Alfonso Maria wa Liguori

Alfonso Maria wa Liguori (Marianella, leo katika jiji la Napoli, nchini Italia, 27 Septemba 1696 - Nocera de' Pagani, katika wilaya ya Salerno, 1 Agosti 1787), pamoja na kuwa mtawa na padri mwanzilishi wa shirika la Mkombozi Mtakatifu sana, halafu askofu wa Kanisa Katoliki, anajulikana kama mwanateolojia wa maadili, mwalimu wa maisha ya Kiroho kwa wote, hasa watu wa chini, mwandishi wa vitabu vingi sana, mwanashairi, mchoraji na mwanamuziki.

Alfonso Maria wa Liguori, anayejulikana kama "Doctor Zelantissimus" ("Mwalimu mwenye bidii sana").

Alikuwa kielelezo cha mchungaji mwenye ari na wema katika kutangaza Neno la Mungu na kuadhimisha sakramenti ili kuokoa watu, akitia maanani hisia na miguso, si hoja za akili tu, ili kuwaelekeza wawapende Mungu na majirani[1].

Alitangazwa mapema na Papa Pius VII kuwa mwenye heri tarehe 15 Septemba 1816, halafu Papa Gregori XVI alimtangaza mtakatifu tarehe 26 Mei 1839, na Papa Pius IX kuwa mwalimu wa Kanisa mwaka 1871. Yeye tu alipewa cheo hicho kabla ya miaka mia tangu afe.

Sifa hiyo ilimfaa kwa sababu nyingi, hasa utajiri wa mafundisho yake kuhusu maadilidini yaliyotoa sawasawa msimamo wa Kikatoliki, hivi kwamba Papa Pius XII alimtangaza pia msimamizi wa waungamishi na wa wanateolojia ya maadili.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 1 Agosti[2].

Utoto na ujana

hariri

Alfonso alizaliwa Marianella, Napoli, Italia, tarehe 27 Septemba 1696, akiwa mtoto wa kwanza kati ya wanane wa sharifu tajiri Giuseppe de' Liguori na Anna Maria Caterina Cavalieri.

Baba yake alimpatia mapema walimu bora, hivi kwamba alipofikia umri wa miaka 12 aliweza kujiandikisha kwenye chuo kikuu cha Napoli ambapo miaka 4 baadaye akapata udaktari wa sheria za nchi na za Kanisa (1713).

Kwa ruhusa ya pekee aliweza kuanza kazi kama wakili akiwa na miaka 16 tu. Akiwa na sifa kubwa kuliko mawakili wengine wote wa mahakama ya Napoli, kwa miaka 8 mfululizo alishinda kesi zote.

Mwaka 1718 alifanywa hakimu wa "Regio Portulano" ya Napoli, na miaka michache baadaye akawa balozi wa kardinali Altan, naibu wa mfalme.

Pamoja na hayo alimtamani Mungu na ukamilifu hata akaja kuacha kazi yake, ikiwa ni pamoja na umaarufu na utajiri.

Wito na upadri

hariri

Kushindwa kesi muhimu, kuchukia uovu uliozidi kuenea mahakamani, kuhudhuria Chama cha Madaktari kwenye Oratorio wa Wafiliponeri pamoja na kutembelea na kuhudumia wagonjwa wa hospitali kuu ya Napoli, iliyoitwa 'degli Incurabili' (yaani 'ya Wasioponyeka'), ndiyo chanzo cha wito wa upadri, aliouitikia kwa kujiunga na seminari mwaka 1723, bila kujali upinzani wa baba aliyemtaka aoe.

Huko pia alipata walimu bora waliomuingiza katika ujuzi wa Biblia, historia ya Kanisa na maisha ya Kiroho, akajipatia elimu pana ya teolojia aliyoitumia baadaye katika uandishi.

Alipewa upadrisho tarehe 17 Desemba 1726, akiwa na umri wa miaka 30, akaendelea kuishi nyumbani kwa mzazi, lakini kwa kutekeleza huduma zake mpya alijiunga na chama cha kijimbo cha Misheni za Kitume.

Mbali ya mahubiri makanisani, alianzisha mikutano ya jioni kwa ajili ya watu duni zaidi ili kuwaeleza Injili kwa unyofu mkubwa. Wengi wao walikuwa wametekwa na vilema mbalimbali, kama vile ujambazi, lakini yeye kwa wema wa ajabu aliwafundisha kusali na kuongoka akipata mafanikio makubwa. Katika mitaa mibovu zaidi ya Napoli yalizidi kuongezeka makundi ya watu waliokutana jioni katika nyumba za binafsi na maduka ili kusali na kutafakari Neno la Mungu chini ya makatekista wengi aliowaandaa pamoja na mapadri wengine ili wayatembelee mara kwa mara asiache kuwasimamia na kuwasaidia kiroho mwenyewe.

Baada ya kushinda upinzani wa wengi, mikutano hiyo iliidhinishwa na kardinali Fransisko Pignatelli ikaanza kufanyika katika vikanisa vingi vya mji huo. Ilikuwa nafasi ya kufaa kwa malezi ya kimaadili, kwa maendeleo ya kijamii na kwa mshikamano kati ya mafukara: wizi, mapigano na ukahaba karibu vilitoweka.

Mwaka 1730, ili apone vizuri baada ya kuugua ugonjwa wa mapafu, alifuata agizo la waganga la kwenda kwenye vilima vya Scala na Ravello, alipoanza kuwahubiria wakulima na wachungaji fukara. Akiguswa na ujinga wao upande wa dini, pamoja na ugumu wa maisha yao kwa jumla, aliamua kuacha mji mkuu na kujitosa kwa ajili ya watu hao, ingawa awali alikuwa amefikiria kwenda kuinjilisha mataifa ya Kipagani.

Kutokana na tetemeko la ardhi ambalo mwaka 1731 liliupata mji wa Foggia na kutaka kusababisha waamini waasi, alikwenda huko. Umati uliokusanyika mbele ya kanisa kuu ulishuhudia kwamba alionekana kuelea hewani (tarehe 30 Novemba 1735).

Shirika la Mkombozi Mtakatifu Sana

hariri

Mwaka 1732, akiwa na miaka 36, alihama Napoli akaanzisha shirika la Mkombozi (Waredentori) huko Villa degli Schiavi (leo Villa dei Liberi katika wilaya ya Caserta) akiliweka chini ya usimamizi wa askofu Tomaso Falcoia. Shirika hilo, ambalo baadaye akawa mkuu wake, lilikuwa na lengo la kuinjilisha maskini walioishi mashambani, na likaja kukubaliwa na Papa Benedikto XIV mwaka 1749.

Chini yake, watawa hao waliinjilisha huko na huko, wakifikia hata vijiji vya porini, wakihimiza watu kuongoka na kuishi Kikristo hasa kwa njia ya sala.

Maisha ya shirika yalikabiliwa na majaribu na upinzani mkali, lakini mwanzilishi aliweza kulidumisha kwa uvumilivu usiokata tamaa na kwa kutumia ujuzi wake wa sheria. Hivyo Waredentori walieneza Neno la Mungu kwa unyofu hadi Poland.

Miaka iliyofuata Alfonso aliandika vitabu vingi vya maisha ya kiroho, teolojia ya dogma, maadili na utetezi wa imani. Lakini pia alitunga nyimbo nyingi kwa lugha rasmi ya Kiitalia na kwa Kinapoli, kama ule maarufu zaidi, "Tu scendi dalle stelle" kwa ajili ya Noeli.

Askofu

hariri

Mwaka 1762 Papa Klement XIII, akizingatia wema na ari yake katika uchungaji, alimfanya akubali kuwa askofu wa jimbo la Sant'Agata de' Goti.

Wakati wa njaa ya kutisha iliyoupata Ufalme wa Napoli mwezi Januari 1764, Alfonso aliweza kuzuia mateso ya watu wake kwa kiasi kikubwa, akihimiza mikopo na kupambana na ulanguzi pamoja na kuchochea uchumi uliokwama tangu miaka 2.

Mwaka 1774 alionekana mahali pawili kwa wakati mmoja, yaani huko Roma katika kumhudumia na kumzika Papa Klemens XIV na huko Sant'Agata de' Goti akiwa ameganda siku mbili kwenye kochi.

Mwaka 1775, baada ya kufanya kazi kubwa (alikuwa ameweka nadhiri ya kutopoteza muda kamwe) na kupata lawama nyingi, pamoja na kudhoofika kiafya, aliacha uongozi wa jimbo kwa sababu za afya akahamia kwenye nyumba ya shirika huko Nocera de' Pagani (leo sehemu hiyo ni katika kijiji cha Pagani, wilaya ya Salerno), alipobaki akiendelea kuandika hadi kufariki kwake tarehe 1 Agosti 1787.

Tukisoma kijuujuu kuhusu mwisho wa maisha yake, tutadhani alikuwa akipitia usiku wa hisi, ambao mara nyingi unaendana na vishawishi vikali dhidi ya usafi wa moyo na ya subira. Kwa mzee huyo aliyekwishatimiza miaka 80 vilikuwa vikali hivi hata mtumishi wake akajiuliza kama atarukwa na akili. Lakini tukizingatia kazi yote iliyokwishatendwa na neema rohoni mwa mtakatifu mkubwa kama huyo, tutatambua majaribu hayo yalimpata hasa kwa ajili ya wengine, na ya shirika alilolianzisha kwa mateso mengi.

Sala yake

hariri

Yesu wangu, nasadiki kuwa umo katika sakramenti takatifu.

Nakupenda kuliko vyote na kukutamani rohoni mwangu.

Kwa kuwa sasa siwezi kukupokea katika sakramenti, njoo moyoni mwangu walau kiroho.

Kama umeshafika nakukumbatia na kujiunga nawe kabisa.

Usiruhusu nitengane nawe kamwe.

Maandishi na ujumbe wake

hariri

Alfonso alitunga vitabu 111, vikiwemo vile kwa ajili ya umati na vile kwa ajili ya wataalamu wa teolojia (hasa ya maadilidini) na wa utetezi wa imani.

Baadhi ya vile maarufu zaidi ni hivi vifuatavyo:

  • Massime eterne, 1728
  • Pratica di amar Gesù Cristo, 1768
  • Storia delle Eresie, 1768
  • Canzoncine spirituali, 1732
  • Visite al Ss. Sacramento, 1745
  • Theologia moralis (I edizione), 1748
  • Glorie di Maria, 1750
  • Apparecchio alla morte, 1758
  • Del Gran mezzo della preghiera, 1759
  • Vera sposa di Gesù Cristo, 1760
  • Considerazioni sopra la passione di Gesù Cristo, 1760
  • Dell'uso moderato della opinione probabile, 1765

Inakadiriwa kuwa vitabu vyake vimetafsiriwa katika lugha 72, na kuwa vimetolewa mara 21,500, kuliko vile vya Wakatoliki wengine wote.

Kati yake, maarufu zaidi ni “Utekelezaji wa Kumpenda Yesu Kristo”, “Kauli za Milele”, “Njia Kuu ya Sala” na “Utukufu wa Maria”. Mtindo wake sahili na wa kupendeza, uliolenga hasa watu wa kawaida kabisa, ulichangia kumfanya aathiri maisha ya Kikristo ya umati katika karne zilizofuata.

Hasa katika kitabu chake muhimu zaidi, “Teolojia ya Maadili”, Alfonso alipendekeza uwiano mzuri kati ya madai ya sheria ya Mungu - ambayo imeandikwa mioyoni mwetu, imefunuliwa kikamilifu na Kristo na kufafanuliwa rasmi na Kanisa - na nafasi ya dhamiri na hiari ya binadamu - ambaye anakomaa kwa kuambatana na ukweli na wema.

Dhidi ya ukali wa misimamo ya matapo ya wakati ule ndani ya Kanisa, hasa Ujanseni, uliokatisha tamaa tu, kwa kumchora Mungu wa kutisha, tofauti sana na habari njema aliyotangaza Yesu, alihimiza wote kutegemea bila kipimo huruma ya Mungu inayotuokoa.

Kwa msingi huo aliwaelekeza kwenye utakatifu kama lengo la maisha haya: “Mungu anataka wote wawe watakatifu, kila mmoja katika hali yake: mtawa kama mtawa, mlei kama mlei, padri kama padri, mtu wa ndoa kama mtu wa ndoa, mfanyabiashara kama mfanyabiashara, askari kama askari, na vilevile kwa hali yoyote ya maisha”.

Pia alihimiza wachungaji na waungamishi kufuata kiaminifu mafundisho ya Kanisa kuhusu maadili pamoja na kuwa na upendo mpole ili waelewe watu na kuwafanya wajisikie wanasindikizwa, wanategemezwa na kutiwa moyo katika safari ya Kiroho.

Hakuchoka kukariri kwamba mapadri ni ishara wazi ya huruma isiyo na mipaka ya Mungu, ambaye anasamehe na kuangaza akili na mioyo ya wakosefu ili waongoke.

Alisisitiza nguvu ya sala kwa binadamu: ndiyo chombo kikuu cha wokovu, kwa sababu inatuweka wazi kwa Mungu na kwa neema yake ili tutimize kila siku matakwa yake na kufikia utakatifu. Kwa ajili hiyo aliandika: “Mungu hamnyimi mtu yeyote neema ya kusali, ambayo inamsaidia kushinda aina zote za tamaa na vishawishi. Nami nasema, tena nitaendelea kusema maisha yangu yote, kwamba wokovu wetu unategemea tu sala”. Kifupi alitamka: “Anayesali ataokoka, asiyesali atapotea”.

Alfonso alifundisha sana maadili na matendo ya ibada, akihimiza hasa kutembelea na kuabudu Ekaristi: “Hakika, kati ya ibada zote, baada tu ya ile ya kupokea sakramenti, kumuabudu Yesu katika Sakramenti Kuu ndiyo ile inayoshika nafasi ya kwanza, inayompendeza Mungu na kutufaa sisi zaidi… Lo, jinsi inavyopendeza kuwa na imani mbele ya altare… ili kumtolea mahitaji yetu kama anavyofanya rafiki kwa rafiki yake anayemtegemea kabisa”.

Maisha ya Kiroho aliyoyafundisha, kiini chake ni Kristo na Injili yake. Mara nyingi tafakuri juu ya mafumbo ya Umwilisho na Mateso ya Mwana wa Mungu zilikuwa mada za mahubiri yake, kwa sababu katika matukio hayo binadamu wote wanapewa ukombozi kwa wingi.

Kwa kuwa ibada yake ilimuelekea kwanza Kristo, ilienea pia katika kumheshimu Bikira Maria, aliye tunda bora la ukombozi na mshiriki wa kazi ya Mwanae. Alieleza kwamba heshima kwa Mama Maria ni faraja kubwa wakati wa kufa.

Kuhusu nafasi hiyo ya mwisho ya maisha duniani, alisisitiza kutafakari uzima wa milele tulioitiwa ili kushiriki moja kwa moja heri ya Mungu, na vilevile uwezekano wa kutisha wa kupotea milele: kwa kufikiria hayo tunaweza kuishi kwa utulivu na uwajibikaji mkubwa zaidi na hatimaye kukabili kifo kwa kutegemea wema wa Mungu.

  • MT. ALFONSI MARIA WA LIGUORI, Kutimiza Mapenzi ya Mungu – tafsiri ya J. A. Sipendi – ed. Tanganyika Mission Press – Tabora

Tazama pia

hariri

Tanbihi

hariri

Viungo vya nje

hariri