Anselm wa Canterbury
Anselm wa Canterbury (Aosta, leo nchini Italia, 1033 au 1034 – Canterbury, Uingereza, 21 Aprili 1109) alikuwa kati ya wanafalsafa na wanateolojia muhimu zaidi wa zama za kati huko Ulaya.
Baada ya kujiunga na monasteri wa Wabenedikto wa Bec huko Ufaransa, alipopata sifa kama kiongozi wa kiroho na mlezi, kama mhubiri wa mrekebishaji wa umonaki, alichaguliwa (1093) kuwa askofu mkuu wa Canterbury (Uingereza).
Sala, masomo na utawala ndiyo mambo yaliyojitokeza zaidi katika maisha yake aliyoyatumia katika nchi tatu tofauti. Maisha ya Kiroho ya dhati aliyokuwanayo yalimwezesha kuwa mlezi bora wa vijana, mwanateolojia wa pekee, kiongozi mwenye busara na mtetezi wa uhuru wa Kanisa mbele ya serikali.
Mwaka 1163 alitangazwa kuwa mtakatifu.
Mwaka 1720 alitangazwa na Papa Klementi XI kuwa mwalimu wa Kanisa kutokana na ubora wa maandishi yake yaliyoandaa nyakati zijazo na kumfanya ajulikane kama mwanzilishi wa teolojia ya shule.
Maisha
haririUtoto na ujana
haririAnselm alizaliwa mwaka 1033 au 1034 mjini Aosta[2] au karibu nao [3] Aosta katika ufalme wa Burgundy (leo katika mkoa wa Valle d'Aosta, inapotumika lugha ya Kifaransa nchini Italia).[2] Familia yake ilikuwa tajiri na ya kisharifu na upande wa mama ilihusiana na watawala wa Savoy[4].
Baba yake, Gundulf, mwenye asili ya Kilombardi, alikuwa mkali na kutapanya mali kwa anasa, tofauti na mama, Ermenberga aliyekuwa na maadili mema ya dini. Ndiye aliyeshughulikia malezi ya kwanza ya Anselm, kifungua mimba, halafu akamkabidhi kwa Wabenedikto wa Aosta.
Kufuatana na ndoto aliyoipata, Anselm alijisikia kuitwa na Mungu kwa kazi muhimu na alipofikia umri wa miaka 15, alitamani kuingia monasteri, lakini hakuruhusiwa kabisa na baba yake.[2] Jambo hilo lilimfanya augue; lakini alipokuwa mahututi na kuomba kuvikwa kanzu ya Kibenedikto kama faraja ya mwisho, baba alimkatalia tena. Kisha kupona na kufiwa mama yake aliacha masomo na kuishi kistarehe tu.
Alipofikia miaka 23, Anselm aliondoka nyumbani, akavuka milima ya Alps na kutangatanga katika Burgundy na Ufaransa akijitafutia mang’amuzi mapya. Baada ya miaka mitatu,[3] akivutiwa na sifa ya Lanfranko wa Pavia (priori wa Abasia ya Bec), alikwenda Normandia mwaka 1059.
Chini ya huyo, Anselm alianza upya kusoma kwa bidii akawa mwanafunzi mpendwa na mshauri wake.
Mwaka uliofuata, kisha kuishi kidogo huko Avranches na kutathmini wito wake, aliingia rasmi malezi ya kitawa kama mnovisi akiwa na miaka 27 akapata upadrisho.
Kuanzia hapo kanuni ya Benedikto wa Nursia iliathiri kabisa mawazo na maisha yake.[5]
Juhudi za kiroho pamoja na masomo vilimfanya arudie katika ngazi ya juu urafiki na Mungu aliokuwanao utotoni.
Miaka huko Bec hadi Canterbury
haririMwaka 1063, Lanfranko aliteuliwa abati wa Caen na Anselm akapewa nafasi yake kama priori wa Bec na mwalimu wa shule ya monasteri, ingawa alikuwa ameishi kama mmonaki miaka mitatu tu. [6]
Anselm alishika nafasi hiyo kwa miaka 15 akidhihirisha vipaji vyake kama mlezi mahiri, asiyebana vijana, bali akiwaachia nafasi ya kukua kwa uhuru wa kufaa. Ingawa alikuwa mkali kwake na kwa wengine kuhusu nidhamu ya kimonaki, alipenda zaidi kuhimiza kuliko kulazimisha.
Halafu akachaguliwa kwa kauli moja awe abati kutokana na kifo cha Herluin wa Bec, mwanzilishi wa abasia hiyo, kilichotokea mwaka 1078. Aliwekwa wakfu na askofu wa Evreux tarehe 22 Februari 1079.[7]
Chini ya Anselm, Bec ikawa kituo bora cha elimu Ulaya, ikivuta wanafunzi kutoka nchi mbalimbali,[8] ingawa masomo hayakuwa na nafasi ya kwanza katika umonaki.[9]
Akiwa Bec aliandika vitabu vya kwanza vya falsafa, Monologion (1076) na Proslogion (1077–1078).
Humo aliandika, “Nakuomba, ee Mungu, nikufahamu, nikupende, nikufurahie. Nisipoweza kufikia furaha kamili katika maisha haya, niweze walau kusonga mbele siku kwa siku, mpaka furaha hiyo itakapokamilika”.
Vitabu hivyo vilifuatwa na Majadiliano kuhusu Ukweli, Hiari na Anguko la Ibilisi.
Wakati huo alijitahidi pia kulinda uhuru wa abasia dhidi ya mamlaka za nje.[10]
Hapo katikati wamonaki wengi walikaribishwa Uingereza ili kuwaletea wenzao wa ng’ambo urekebisho uliozidi kuenea barani Ulaya. Mchango wao ulikubaliwa kiasi kwamba Lanfranko akawa askofu mkuu wa Canterbury.
Mara kadhaa Anselm alitembelea Uingereza kwa ombi la Lanfranko, ili kufundisha wamonaki na kumsaidia kusimamia mali ya abasia katika magumu yaliyofuatana na uvamizi wa William I wa Uingereza na Wanormani wenzake.
Kazi yake ilipendeza wenyeji wa huko kiasi kwamba Lanfranko alipofariki mwaka 1089,[11] mwenyewe alichaguliwa kushika nafasi yake kama Askofu mkuu wa Canterbury.
Askofu mkuu wa Canterbury
haririKuanzia Desemba 1093 alipopata daraja takatifu hiyo, alishindana mara kadhaa na wafalme wa Uingereza Williamu II na Henri I ili kutetea uhuru wa Kanisa lisiingiliwe na serikali; kwa sababu hiyo mara mbili ilimpasa kwenda uhamishoni (1103-1106). Katika msimamo wake aliungana na Papa.
Hatimaye upatanisho kati ya mfalme na Papa ulimwezesha kurudi Canterbury, alipoakiwa na wakleri na walei kwa shangwe.
Anselm, kabla hajafariki huko tarehe 21 Aprili 1109 alitumia miaka yake ya mwisho kulea wakleri katika maadili na kufanya utafiti katika masuala mbalimbali ya teolojia.
Kitabu maarufu zaidi alichokiandika miaka hiyo ya mwisho kati ya Uingereza na Italia, kinaitwa Cur Deus homo? (Kwa nini Mungu kawa mtu?) na kimeathiri kwa miaka elfu mtazamo wa Kanisa la Magharibi kuhusu fumbo la wokovu.
Anselm aliacha pia mkusanyo mkubwa wa Sala na wa Tafakuri, mbali na Barua nyingi, ambazo zinawezesha kuona mafungamano ya kirafiki aliyokuwa nayo kwa wanafunzi wake.
Anselm anakumbukwa si tu kama mwanateolojia, bali pia kama mwanafalsafa, hasa kwa utafiti wake kuhusu unum argumentum, yaani hoja kuu inayojitegemea na kujitosheleza katika kuthibitisha uwepo wa Mungu na sifa zake.
Imani na akili
haririMtu mwenye uwezo mkubwa wa kuchimba nadharia, Anselm alitafuta, kwa kufuata nyayo za Plato na Agostino wa Hippo, namna ya kukutanisha imani na akili.
Aliona akili ya binadamu ni chombo muhimu cha utafiti wa teolojia. Bila shaka, alidai kwanza imani, akisema, "Nasadiki ili nielewe, na nisiposadiki kwanza sitaweza kuelewa.
Hivyo, Anselm alirithi kutoka kwa Agostino kauli credo ut intelligam, intelligo ut credam (yaani "nasadiki ili nielewe, naelewa ili nisadiki").
Utafiti wa ukweli unategemea imani, lakini hiyo peke yake haitoshi, inadai pia aina mbalimbali za uthibitisho wa akili. Katika hilo akili, sawa na imani yenyewe, ana mwongozo wa hakika katika mwanga wa Mungu ambao usipokuwepo akili haiwezi kabisa kupenya fumbo la Mungu.
Kwa maneno mengine, akili haitoi matamko, bali inasaidia kuelewa imani.
Anselm ni kati ya wataalamu wa kwanza waliounganisha falsafa na teolojia, kadiri ya neno fides quaerens intellectum (yaani "imani inadai akili"), litakalokuwa msingi wa teolojia ya shule.
Pamoja na kuchochea hamu kubwa ya kuelewa mafumbo ya Mungu kwa kutumia mantiki, yeye alilenga daima “kuinua akili izame ndani ya Mungu”, akiendelea kukiri kwamba kazi ya kumtafuta Mungu haina mwisho, walau duniani.
Aliweka bayana kwamba yeyote yule anayetaka kusoma teolojia hawezi kutegemea akili yake tu, bali anatakiwa kustawisha maisha ya imani ya dhati. Hivyo kazi ya mwanateolojia apitie hatua tatu: 1) imani, zawadi ambayo Mungu anatutolea bure nasi tuipokee kwa unyenyekevu; 2) mang’amuzi, yanayopatikana kwa kutekeleza Neno la Mungu katika maisha ya kila siku; 3) ujuzi halisi, unaotegemea si mpangilio wa fikra tu, bali sala hasa.
Ndiyo maana aliandika, “Ee Bwana, sijaribu kupenya ukuu wako, kwa sababu sithubutu kabisa kulinganisha uelewa wangu na ukuu huo; ila natamani kuelewa kwa kiasi fulani ukweli wako, ambao moyo wangu unausadiki na kuupenda. Kwa kuwa mimi sijitahidi kuelewa ili nisadiki, bali nasadili ili nielewe. Kwa sababu nasadiki hii pia: kwamba nisiposadiki, sitaweza kuelewa”.
Anselm alimheshimu Bikira Maria pia kwa moyo wa kitoto: “Maria, ndiwe yule ambaye moyo wangu unajitahidi kumpenda, ndiwe yule ambaye ulimi wangu unatamani motomoto kumsifu”.
Sala zake
haririBwana, wewe ni Mungu wangu, wewe ni Bwana wangu lakini mimi sijakuona.
Wewe umeniumba na kuniumba upya, umenijalia mema yangu yote, lakini mimi sijakufahamu.
Nimeumbwa ili nikuone lakini sijafanya hilo ambalo kwa ajili yake nimeumbwa…
Unifundishe kukutafuta na ujionyeshe ninapokutafuta: siwezi kukutafuta usiponifundisha, wala kukuona usipojionyesha.
Nikutafute kwa kukutamani na nikutamani kwa kukutafuta, nikuone kwa kukupenda na nikupende kwa kukuona.
Nakuomba, Bwana,
unijalie nionje kwa upendo yale ninayoyaonja kwa ujuzi;
unijalie nijue kwa upendo ninayoyajua kwa akili.
Nakuwia kuliko uhai wangu wote, lakini sina zaidi, tena peke yangu siwezi kukurudishia uhai huo kikamilifu.
Univute kwako, Bwana, katika utimilifu wa upendo.
Mimi mzima ni wako kwa uumbaji; unifanye wako kwa upendo pia. Bwana, moyo wangu uko mbele yako.
Najaribu, lakini peke yangu siwezi kitu; fanya nisichoweza.
Unikaribishe katika chumba cha ndani cha upendo wako.
Naomba, natafuta, napiga hodi.
Wewe uliyenijalia kuomba, unijalie nipate; uliyenijalia kutafuta, unijalie nione; uliyenifundisha kupiga hodi, unifungulie.
Tazama pia
haririTanbihi
hariri- ↑ Martyrologium Romanum
- ↑ 2.0 2.1 2.2 Walsh, Michael, ed. Butler's Lives of the Saints. (HarperCollins Publishers: New York, 1991), pp. 117
- ↑ 3.0 3.1 Charlesworth, M. J., trans. and ed. St. Anselm's Proslogion. (University of Notre Dame Press: Notre Dame, 2003), pp. 9.
- ↑ R. Southern. St. Anselm: Portrait in a Landscape. (Cambridge University Press: 1992), pp. 8. http://books.google.com/books?hl=en&lr=&id=lxf-LvQvvwIC&oi=fnd&pg=PR15&dq=anselm+of+canterbury+r-southern&ots=e6-_fZ6v0B&sig=3rOwM0tvC4VVInlSWl099J0dyjE#PPA8,M1
- ↑ R. Southern. St. Anselm: Portrait in a Landscape. (Cambridge University Press: 1992), pp. 32. http://books.google.com/books?hl=en&lr=&id=lxf-LvQvvwIC&oi=fnd&pg=PR15&dq=anselm+of+canterbury+r-southern&ots=e6-_fZ6v0B&sig=3rOwM0tvC4VVInlSWl099J0dyjE#PPA8,M1
- ↑ Charlesworth, M. J., trans. and ed. St. Anselm's Proslogion. (University of Notre Dame Press: Notre Dame, 2003), pp. 10.
- ↑ Vaughn, Sally. "St Anselm of Canterbury: the philosopher-saint as politician." Journal of Medieval History. 1 (1975), 279–306: 282.
- ↑ Charlesworth, M. J., trans. and ed. St. Anselm's Proslogion. (University of Notre Dame Press: Notre Dame, 2003), pp. 15.
- ↑ Charlesworth, M. J., trans. and ed. St. Anselm's Proslogion. (University of Notre Dame Press: Notre Dame, 2003), pp. 13.
- ↑ Vaughn, Sally. "St Anselm of Canterbury: the philosopher-saint as politician." Journal of Medieval History. 1 (1975), 279–306: 281.
- ↑ Charlesworth, M. J., trans. and ed. St. Anselm's Proslogion. (University of Notre Dame Press: Notre Dame, 2003), pp. 16.
Marejeo
hariri- Charlesworth, M. J., trans. and ed. St. Anselm's Proslogion. (University of Notre Dame Press: Notre Dame, 2003)
- Foley, George C. Anselm's Theory of the Atonement." 1909. Online access Oct. 23, 2009
- Janaro, John. "Saint Anselm and the Development of the Doctrine of the Immaculate Conception: Historical and Theological Perspectives." The Saint Anselm Journal. 3.2 (Spring 2006) 48–56 Archived 28 Mei 2010 at the Wayback Machine.
- Southern, R. St. Anselm: Portrait in a Landscape. (Cambridge University Press: 1992)
- Vaugh, Sally. "St. Anselm: Reluctant Archbishop?" Albion: A Quarterly Journal Concerned with British Studies. 6:3 (Autumn, 1974), 240–250
- Vaughn, Sally. "St Anselm of Canterbury: the philosopher-saint as politician." Journal of Medieval History. 1 (1975), 279–306
- Vaugh, Sally. "Robert of Meulan and Raison d'État in the Anglo-Norman State, 1093–1118" Albion: A Quarterly Journal Concerned with British Studies. 10:4 (Winter, 1978), 352–373
- Vaughn, Sally. "Anselm: Saint and Statesman." Albion: A Quarterly Journal Concerned with British Studies. 20:2 (Summer, 1988), 205–220
- Vaughn, Sally. "St. Anselm and the English Investiture Controversy Reconsidered". Journal of Medieval History 6 (1980): 61–86
- Walsh, Michael, ed. Butler's Lives of the Saints. (HarperCollins Publishers: New York, 1991)
Viungo vya nje
hariri- "St. Anselm of Canterbury (1033—1109)" article by Greg Sadler in the Internet Encyclopedia of Philosophy
- Professor Jasper Hopkins: Anselm of Canterbury containing English translations of nearly every major work by St. Anselm
- "Introducing...Anselm of Canterbury" Archived 15 Desemba 2011 at the Wayback Machine.. Three lectures giving an overview of Anselm's works (with particular reference to faith and reason) by Dr. Michael Reeves on www.theologynetwork.org Archived 15 Desemba 2011 at the Wayback Machine.