Willibrod Peter Slaa (alizaliwa Kwermusi, wilaya ya Mbulu, 29 Oktoba 1948) ni mwanasiasa wa Tanzania.

Alikuwa katibu mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), chama kinachoongoza mpaka sasa kambi ya upinzani katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hadi alipojiuzulu nafasi ya ukatibu mkuu na uanachama wa Chadema mwaka 2015 baada ya ujio wa waziri mkuu mstaafu Edward Lowassa ambaye alipewa nafasi ya kugombea urais mwaka huo.

Alikuwa mgombea wa urais wa chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 na kushika nafasi ya pili kwa asilimia 27.05 ya kura zote, akiachwa na Jakaya Kikwete wa CCM aliyeongoza kwa kupata asilimia 62.83, kadiri ya matokeo rasmi ambayo hayajasadikiwa na wananchi wote.

Kabla ya kugombea urais mwaka 2010 alikuwa mbunge wa Karatu miaka 1995-2010; baada ya kugombea urais akawa si mbunge tena.

Elimu

Willibrod Slaa alisoma shule ya msingi Kwermusi iliyoko wilayani Mbulu miaka 1958-1961 na baadaye shule ya kati (middle school) ya Karatu miaka 1962-1965.

Baada ya darasa la nne Slaa alijiunga na seminari ya Dung'unyi mkoani Singida miaka 1966-1969 na kusoma sekondari. Kisha akaendelea na masomo ya juu ya sekondari katika seminari ya Itaga mkoani Tabora miaka 1970-1971 alikohitimu kidato cha sita.

Alipomaliza kidato cha sita katika seminari ya Itaga alikuwa ameshafanya maamuzi ya kuwa mtumishi wa Kanisa Katoliki. Alijiunga na seminari kuu ya Kibosho miaka 1972-1973 na kupata stashahada ya falsafa iliyompa sifa ya kuhadiliwa na seminari kuu ya Kipalapala iliyopo Tabora kati ya mwaka 1974 na 1977 na alipata fursa ya kubobea zaidi masomo ya falsafa na teolojia huku pia akisoma stashahada ya teolojia katika chuo kikuu cha Makerere nchini Uganda.

Baada ya safari ndefu ya kuusaka utumishi Slaa alipadrishwa (alipewa upadri rasmi) mwaka 1977 na baada ya utumishi wa miaka michache alijiunga na chuo kikuu cha Kipapa cha Urbaniana nchini Italia akisomea udaktari wa sheria za Kanisa ulio maarufu kama J.C.D. (Juris Canonic Doctor) kati ya mwaka 1979 na 1981. Katika mfumo wa Kanisa Katoliki J.C.D ndiyo shahada ya juu katika masomo ya sheria za Kanisa.

Uongozi Kanisani

Slaa alianza kuwa kiongozi tangu alipokuwa mwanafunzi pale Kipalapala ambapo alichaguliwa kuwa rais wa wanafunzi; mapadri wanasema alikuwa mmoja wa viongozi wazuri sana kupata kuongoza Kipalapala.

Pia Slaa amewahi kua msaidizi wa askofu na mkurugenzi wa maendeleo katika Jimbo Katoliki la Mbulu.

Amewahi kua Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kwa muda wa miaka tisa (mihula yote mitatu). TEC ndiyo chombo cha juu cha kusimamia ushirikiano ndani ya Kanisa Katoliki Tanzania.

Slaa anaelezwa kama katibu mkuu mwenye ufanisi mkubwa tangu TEC ianzishwe. Miundombinu mingi ya Kanisa Katoliki ilianzishwa na kukamilishwa kipindi ambacho Slaa alikuwa katibu wa TEC.

Katika siasa

Slaa alijitoa kwenye upadri mwaka 1991. Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa maaskofu kadhaa, Slaa alifanya hivo kwa kufuata taratibu za Kanisa Katoliki na aliacha mwenyewe bila kufukuzwa, kushinikizwa ama kupewa onyo.

Aliingia kwenye kinyang'anyiro cha ubunge mwaka 1995 akiomba ridhaa ya kuwatumikia wananchi kupitia tiketi ya CCM na alishinda katika kura za maoni za chama hicho. Vikao vya CCM vilipokutana Dodoma vikamuengua na kumweka tena mbunge anayemaliza muda wake, Patrick Qorro. Wananchi wa Karatu wakamuomba agombee ubunge kupitia chama kingine na ndipo Slaa alipambana na wagombea wa vyama vingine kama CCM, CUF, NCCR MAGEUZI, UDP na aliwashinda wote kwa kupata asilimia 52, akifuatiwa na mgombea wa CCM aliyepata asilimia 44.

Uchaguzi uliofuata, mwaka 2000, Slaa alishiriki na kupata ushindi mkubwa zaidi. Tena kwenye uchaguzi wa mwaka 2005 Slaa aligombea kwa awamu ya tatu na kupata ushindi wa asilimia 50 dhidi ya asilimia 49 za Patrick Tsere wa CCM.

Katika CHADEMA amewahi kuwa makamu mwenyekiti kabla hajachaguliwa kuwa katibu mkuu mwaka 2004, mwaka ambao Freeman Mbowe alichaguliwa kuwa mwenyekiti. Mwaka 2015 Willbroad Peter Slaa aliwashangaza wengi, wanachama wa Chadema na Watanzania kwa ujumla, pale alipotangaza kujiuzulu nafasi ya ukatibu mkuu wa Chadema, kujitoa uanachama wa Chadema na kuachana na siasa, kwa ujumla kwa madai ya kupinga ujio wa waziri mkuu mstaafu Edward Lowassa ambaye ndiye aliyepewa nafasi ya kugombea Urais kupitia Chama hiko katika uchaguzi mkuu mwaka 2015.

Tazama pia

Marejeo