Ezra (kwa Kiebrania: עזרא, ‘Ezrā; kwa Kiarabu: عُزَيْرٌ, Uzair) alikuwa kuhani na mwandishi aliyefanya kazi kubwa kwa taifa la Israeli katika miaka 480-440 KK [1].

Koreshi Mkuu akiruhusu Wayahudi kurudi Yerusalemu kutoka Babuloni (mchoro mdogo wa Jean Fouquet, 1470-1475 hivi).

Ezra alikuwa ametumwa na Mwenyezi Mungu. Alijua sana sheria ya Mungu (Ezra 7:6, 12): hakuisoma tu, bali pia aliitekeleza na kueleza maana yake kwa Wayahudi aliowakusanya ili kitabu cha Torati kiwafundishe watu jinsi ya kuishi kila siku (Ezra 7:10; Neh 8:8). Hapa tunaweza kuona asili ya mipango ya dini ya Kiyahudi iliyoendelezwa na waandishi wa baadaye. Lakini mifano ya dini hiyo ya wakati wa Yesu ilitofautiana sana na aina ya maisha iliyofundishwa na Ezra.

Ezra anaheshimiwa na Wayahudi, Wakristo na Waislamu vilevile kama mtakatifu.

Kwa Wakatoliki sikukuu yake huadhimishwa tarehe 13 Julai[2].

Kitabu chake

hariri

Kitabu chenye jina lake kinapatikana katika Biblia ya Kikristo katika Agano la Kale.

Kiasili kiliandikwa kwa lugha ya Kiebrania lakini kuna pia sehemu fupi za Kiaramu.

Andiko la Ezra lilitunzwa katika Biblia ya Kiebrania pamoja na Kitabu cha Nehemia kama kitabu kimoja lakini kimegawiwa baadaye kuwa vitabu viwili ambavyo Vulgata inavitaja kama "Esdras I" na "Esdras II". Vitabu hivyo viliandikwa kama mfululizo wa habari za vitabu vya Mambo ya Nyakati. Ndiyo sababu habari za Ezra zinaanzia wakati uleule ambapo habari za Mambo ya Nyakati zinamalizika.

Kitabu kinasimulia habari za Wayahudi chini ya utawala wa Waajemi.

Ni kwamba mwaka 587 KK mfalme wa Babeli alikuwa amevamia mji wa Yerusalemu, kubomoa hekalu la Sulemani na kumaliza ufalme wa Yuda. Wakazi walipelekwa Mesopotamia kwa uhamisho wa Babeli.

Kumbe mwaka 539 KK Waajemi chini ya mfalme Koreshi Mkuu walivamia Babeli ambayo ikawa jimbo la milki ya Uajemi. Koreshi aliwaruhusu Wayahudi waliopenda warudi Yerusalemu na kujenga upya hekalu.

Muda mfupi baada ya kufika Yerusalemu, Wayahudi walianza ujenzi huo. Madhabahu iliwekwa mahali pake tena, na katika mwaka wa pili misingi ya hekalu ikawekwa (Ezra 3:1-3, 8-10). Lakini wakati huo maadui walianza kuwapinga wajenzi wakasababisha kazi yote iahirishwe kwanza (Ezra 4:1-5, 24).

Kwa muda wa miaka 16 hivi haikufanyika kazi yoyote katika ujenzi wa hekalu jipya (Ezra 4:24). Kisha, mwaka 520 KK, Mungu aliwaita watu wawili miongoni mwa Wayahudi walioishi Yerusalemu ili wawaamshe na kuwahamasisha waendelee na kazi hiyo, wala wasilegee tena mpaka waimalize. Watu hao wawili walikuwa manabii Hagai na Zekaria (Ezra 5:1-2; Hag 1:1; Zek 1:1).

Mara watu walipoanza tena kazi ya ujenzi, upinzani mpya ulitokea (Ezra 5:3). Jambo hilo likawekwa mbele ya mfalme mpya wa Uajemi aliyeitwa Dario I (Koreshi alikuwa amefariki tangu miaka michache). Baada ya kuchunguza jambo hilo vizuri, Dario aligundua kwamba Koreshi alikuwa ametoa ruhusa ya kujenga hekalu. Kwa hiyo Dario akaandika amri mpya iliyothibitisha ile ya kwanza ya Koreshi ili kazi iendelee (Ezra 6:6-12).

Mahubiri ya Hagai ya kuamsha watu yalileta matokeo ya haraka, na baada ya wiki tatu Wayahudi walikuwa tena katika kazi yao ya kujenga hekalu.

Nabii Zekaria akamwunga mkono Hagai, akitoa mafundisho marefu zaidi yaliyokusudiwa kuleta mabadiliko ya kiroho katika maisha na matumaini ya watu.

Miaka minne baada ya kuanza tena kazi hiyo, hekalu lilimalizika (mwaka 516 KK; taz. Ezra 6:14-15; 4:24).

Katika mwaka 465 KK Artashasta (kwa Kiingereza: Artaxerxes) alikuwa mfalme wa Uajemi badala ya Xerxes I (Ahasuero). Katika mwaka wa saba wa utawala wake (yaani 458 KK), aliandika amri iliyompa Ezra mamlaka na fedha arudi Yerusalemu na kutekeleza matengenezo ya huko (Ezra 7:1, 7, 13).

Kutokana na uchunguzi wa tarehe zinazohusika, inaonekana kwamba matukio yaliyoandikwa katika mafungu ya kwanza ya kitabu cha Ezra (k.mf. yaliyohusika na Zerubabeli, Yoshua na kujengwa upya kwa hekalu), kwa kweli yalikuwa kabla ya kuzaliwa kwake Ezra. Bila shaka mwandishi wa kitabu cha Ezra alichunguza barua, hati na ripoti za historia nyingi ili kuandaa kitabu chake.

Inatupasa kusoma zaidi ya nusu ya kitabu mpaka tunapopata habari za wakati wa Ezra mwenyewe. Kurudi kwa Ezra kulikuwa kama miaka 80 baada ya Zerubabeli. Watu wa Yerusalemu walikuwa kizazi kingine kuliko wale waliorudi pamoja na Zerubabeli.

Katika mwaka wa 20 wa utawala wake, Artashasta alitoa amri ya pili iliyowaruhusu Wayahudi wengine warudi Yerusalemu kwa msaada wa fedha nyingi za serikali, wakati huo wakiongozwa na Nehemia (445 KK). Hekalu la Yerusalemu lilikuwa limemalizika zaidi ya miaka 70 iliyopita, lakini mji wenyewe ulikuwa bado na hali ya kusikitisha, na kuta za kuuzunguka zilikuwa hazijajengwa upya. Ilikuwa kwa kusudi la kujenga kuta hizo kwamba Nehemia alipata amri na msaada kutoka kwa Artashasta (Neh 2:1-8).

Labda Ezra alikuwa amerudi Yerusalemu miaka 13 kabla ya Nehemia. Marekebisho yake yalikuwa na matokeo madogo tu, wala haikuwa mpaka baada ya Nehemia kufika na kuwa liwali mkuu wa Yerusalemu, kwamba marekebisho yale yalileta matunda kwa wenyeji kwa jumla. Watu hao wawili walifanya kazi moja, wakiwaongoza watu wamrudie Mungu (Neh 8:9). Nehemia aliishi Yerusalemu kwa muda wa miaka 12 kabla ya kurudi tena Uajemi (Neh 2:1; 13:6). Baada ya muda akarudi tena Yerusalemu (Neh 13:6-7). Kitabu cha Nehemia kinaeleza matendo yake makuu mjini Yerusalemu.

Tazama pia

hariri

Tanbihi

hariri

Viungo vya nje

hariri
 
Wikiquote ina mkusanyiko wa dondoo kuhusu:
 
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Ufafanuzi
  Makala hii kuhusu mtu wa Biblia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Ezra kama habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.