Isidori wa Sevilia
Isidori (Cartagena, leo nchini Hispania, 560 - Sevilia, Hispania, 4 Aprili 636) alikuwa askofu mkuu wa Sevilia, maarufu kwa elimu yake kubwa aliyowarithisha hasa watu wa Ulaya Magharibi wa Karne za Kati.
Tangu zamani anaheshimiwa kama mtakatifu na babu wa Kanisa.
Mwaka 1722 Papa Inosenti XIII alimuongezea sifa ya mwalimu wa Kanisa.
Maisha
haririAlizaliwa na Severianus na Turtura huko Cartagena, Hispania, mwaka 560, akiwa wa nne kati ya watoto watano, ambao wanne kati yao wanaheshimiwa na Kanisa Katoliki kama watakatifu: Leandri wa Sevilia, Fuljensi wa Ecija, Florentina wa Cartagena naye mwenyewe. Kati yao, watatu walikuwa maaskofu, na wa kike alikuwa mtawa.
Kaka yake, Leandro, msomi aliyeshika maisha magumu, ndiye aliyemlea kwa nidhamu kubwa baada ya kifo cha baba yao, akimtengenezea mazingira ya kimonaki ambamo awajibike katika masomo akitumia maktaba yao kubwa ili kujiandaa akabili matatizo ya wakati ule.
Kutokana na matatizo hayo, akiwa bado mtoto ilimbidi aonje uchungu wa kupelekwa uhamishoni. Hata hivyo alichangamkia utume wake wa kurudisha nchi yao katika Kanisa Katoliki na ustaarabu wa Kirumi.
Kisha kuwa mkleri huko Sevilia, mwaka 599 Isidori alimrithi kaka yake Leandro kama askofu wa jimbo kuu hilo, akaliongoza kwa miaka 37, akijitahidi pande zote: katika teolojia, liturujia, sheria za Kanisa n.k.
Kama rafiki yake Gregori Mkuu, ilimbidi Isidori pia asifuate elekeo lake la kujisomea bali ajitose kwa upendo kushughulikia wokovu wa watu wake. Ndivyo alivyoandika: “Mtu wa Kanisa upande mmoja anatakiwa kuwa amesulubiwa kwa ulimwengu kwa kufisha mwili wake, upande mwingine anatakiwa kukubali uamuzi wa Kikanisa - unapotokana na mapenzi ya Mungu - wa kuwa awajibike kwa unyenyekevu kutawala, hata asipotaka… Kwa kuwa watakatifu hawatamani kushughulikia mambo ya dunia na wanaugua kwa ndani pale ambapo kwa mpango wa fumbo wa Mungu wanabebeshwa majukumu kadhaa… Wanafanya wanachoweza ili kuyakataa lakini wanakubali kile walichotaka kutupa na wanafanya walichopendelea kukwepa. Kwa sababu wanaingia katika dhati ya moyo na humo wanatafuta kujua utashi wa fumbo wa Mungu unawaomba nini. Hapo wakitambua kwamba imewapasa kunyenyekea mipango ya Mungu, wanainamisha mioyo yao kwa nira ya matakwa yake”.
Kwa msingi huo, alipojadili suala la ubora wa maisha ya sala, aliandika: “Yesu mwokozi ametuachia mfano wa maisha ya utendaji pale ambapo wakati wa mchana aliwajibika kufanya ishara na miujiza mjini, lakini alionyesha maisha ya sala hasa alipojitenga mlimani na kutumia usiku kusali… Hivyo mtumishi wa Mungu, akimuiga Kristo, awajibike katika sala hasa bila kujikatalia maisha ya utendaji. Isingekuwa vizuri kufanya tofauti. Kwa sababu, kama vile tunavyopaswa kumpenda Mungu kwa kuzamia sala, tunapaswa pia kumpenda jirani yetu kwa matendo”.
Alishika nafasi ya maana katika matukio ya nchi yake wakati huo ilipotawaliwa na kabila la Kijerumani la Wavisigoti, ambao aliwavuta kutoka uzushi wa Ario kwenye imani ya Mtaguso wa kwanza wa Nisea na ya Mtaguso wa kwanza wa Konstantinopoli. Katika hilo alifurahia sana wongofu wa Hermenegild, mrithi wa ufalme wa Wavisigoti.
Alishiriki Mtaguso IV wa Toledo (633) uliolenga kuunganisha liturujia maalumu ya Kihispania. Ndiye mwakilishi bora wa liturujia hiyo, aliyoirekebisha na kuistawisha.
Alipokaribia kufa, aliamua kupokea kitubio cha hadharani kadiri ya ibada aliyoitunga mwenyewe.
Kutokana na malezi aliyoyapata, alistawisha elimu yoyote, ya Kikristo na ya kidunia, na fasihi kuliko watu wote wa wakati wake.
Maandishi
haririAliandika sana juu ya mambo mbalimbali: sayansi, historia, teolojia, maadili, sheria za Kanisa na ufafanuzi wa Biblia akitumia madondoo ya asili na aina tofauti sana, pengine bila kuyasanisi kwa mpango wa kuridhisha. Juhudi yake ilikuwa kutopoteza chochote cha zamani kilichoweza kusaidia siku za mbele.
Vitabu muhimu zaidi ni vile 20 vya Etymologiae, ambavyo aliviandika hasa kwa ajili ya malezi ya wakleri na vilikusanya ujuzi wote wa wakati ule, vikatumika sana katika Karne za Kati.
Hivyo alipata kuwa kiungo kati ya mababu wa Kanisa, ambaye ni wa mwisho wao upande wa magharibi, na hatua iliyofuata.
Tafsiri
haririTafsiri yake ya kwanza kwa Kiingereza ni: Barney, Stephen A., Lewis, W. J., Beach, J. A. and Berghof, Oliver (translators). The Etymologies of Isidore of Seville. Cambridge: Cambridge University Press, 2006. ISBN 0521837499, ISBN 9780521837491.
Tazama pia
haririTanbihi
haririVyanzo
hariri- Henderson, John. The Medieval World of Isidore of Seville: Truth from Words. Cambridge: Cambridge University Press, 2007. ISBN 0-521-86740-1.
- Herren, Michael. "On the Earliest Irish Acquaintance with Isidore of Seville." Visigothic Spain: New Approaches. James, Edward (ed). Oxford: Oxford University Press, 1980. ISBN 0-19-822543-1.
- Englisch, Brigitte. "Die Artes liberales im frühen Mittelalter." Stuttgart, 1994.
- Jones, Peter. "Patron saint of the internet" Archived 1 Mei 2008 at the Wayback Machine., telegraph.co.uk., 27 Agosti 2006 (Review of The Etymologies of Isidore of Seville, Cambridge University Press, 2006 (ISBN 0-521-83749-9)
- Shachtman, Noah. "Searchin' for the Surfer's Saint", wired.com., 25 Januari 2002
Viungo vya nje
hariri- Baadhi ya maandishi yake kutoka The Latin Library
- Chronicon (katika tafsiri ya Kiingereza) Archived 15 Februari 2009 at the Wayback Machine.
- The Etymologiae (complete Latin text)
- Henry Wace, Dictionary of Christian Biography, ccel.org
- Encyclopædia Britannica, 1911 edition: Isidore of Seville, 1911encyclopedia.org
- Order of St. Isidore of Seville, st-isidore.org