Kwa matumizi tofauti ya jina hili angalia hapa Manda


Mji Mdogo na Kata ya Manda
Nchi Tanzania
Mkoa Njombe
Wilaya Ludewa
Idadi ya wakazi
 - Wakazi kwa ujumla 4,564 (2,022)
Mbuyu mkubwa karibu na bandari ya Manda.

Manda ni mji mdogo wa Wilaya ya Ludewa katika Mkoa wa Njombe, Tanzania. Msimbo wa posta ni 59423.

Mazingira

hariri

Mji mdogo wa Manda upo kwenye mwambao wa Ziwa Nyasa karibu na mdomo wa mto Ruhuhu mpaka Lupingu. Manda ina vivutio vingi sana, ikiwemo ufukwe maridhawa wa Ziwa Nyasa, aina mbalimbali za samaki kama Mbasa, Ngumbu, Mbelele, Mawoma na milima ya Livingstone. Ukiwa juu ya milima ya Livingstone utaona vizuri sana Ziwa Nyasa na nchi ya Malawi ambayo zamani ilikuwa inaitwa Nyasaland.

Mto Ruhuhu ndio mto mkubwa unaoingiza maji mengi zaidi katika Ziwa Nyasa, tena si kwa upande wa Tanzania tu. Upande mmoja wa Mto Ruhuhu kuna kijiji cha Kipingo na upande mwingine kijiji cha Lituhi.

Historia fupi

hariri

Manda zama za Afrika ya Mashariki ya Kijerumani ilijulikana kwa jina la Wiedhafen [1] ikawa kitovu cha biashara kwenye sehemu ya Kijerumani ya ufuko wa Ziwa Nyasa kabla ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia.

Manda ilianzishwa kwenye mwezi Mei mwaka 1897 na kuwa ofisi ndogo ya Mkoa wa Langenburg (DOA). Baadaye ofisi ndogo ya serikali ilifungwa, Wiedhafen na eneo lake vilihamishwa kwenda Mkoa wa Songea. Wajerumani walichagua mahali pa Wiedhafen-Manda kwa sababu ilifikiwa na njia ya misafara kati ya Kilwa na Ziwa Nyasa na kuwa na bandari asilia. Kulikuwa na kituo cha posta ya Kijerumani. [2]

Wakazi

hariri

Katika sensa ya mwaka 2022 wakazi wa kata walihesabiwa kuwa 4,564 [3]. Wakati wa sensa iliyofanyika mwaka wa 2012, kata ilikuwa na wakazi wapatao 4,304 [4] walioishi humo.

Wenyeji wa Manda ni kabila la Wamanda na lugha yao ya asili ni Kimanda. Lugha hiyo hufanana sana na lugha ya Kingoni na ina maneno mengi ya Kiingereza. Wamanda wanapatikana katika wilaya za Ludewa, Mbinga na Nyasa kuanzia Lituhi, Ndongosi na kata za jirani upande wa wilaya ya Nyasa.

Vijiji maarufu vya Wamanda ni pamoja na Igalu, Ilela (Ilela ilihama kutoka ziwani; zamani hiyo sehemu ilikuwa ndiyo Ngelenge), Luilo, Mbongo, Masasi, Ngelenge (Ngelenge zamani ilikuwa inatiwa Kulondoni; kwa sasa Ngelenge inaunganisha vijiji vya zamani vya Kuliwolelo, Kuntudu, Kupanda, Kutakanini na Kulondoni), Kumasasi, Nsungu, Kipingo, Lihanguli.

Wamanda wa Ndongosi wengi wao walihamia Ndongosi wakitokea Lituhi na vijiji vya karibu kama Kunkaya, Kumangori n.k. kutokana na kiongozi mmoja wa serikali kuundanganya uongozi wa juu wa serikali kwa manufaa yake kwa kudai ati, Lituhi yote ipo majini.

Manda kuna Kanisa kubwa la Anglikana la Mt. Thomaso na bandari ya kale ya Manda-Wiedhafen. Hapo kwenye mbuyu mkubwa kuna kibao cha heshima ya Mdachi aliyejitolea kupigana vita upande wa Wajerumani, lakini alifia Ruanda, wilaya ya Mbinga. Kuna kanisa kubwa la Kikatoliki pale Lituhi ambalo lilijengwa mwaka 1942. Makanisa mengine ya Kikatoliki yapo Ngelenge, Nsungu na Igalu. Kwa ujumla vijiji vyote vya Manda vina makanisa ya Anglikana na Katoliki.

Mila moja kubwa sana ya Wamanda ni kuzuru kila mwaka makaburi ya waliotutangulia kwa Mwenyezi Mungu. Hii ndiyo sababu kubwa sana ya Wamanda kupenda kurudi kwao wakati wa likizo zao.

Vyakula vya asili vya wakazi wa Manda ni ugali wa muhogo na samaki.

Ngoma za asili za wakazi wa Manda ni Mganda, Kihoda na Ligambusi. Wamanda wamepata elimu sana kutokana na misingi ya misheni za Anglikana na Katoliki, maana shule zote zilikuwa za misheni. Kwa hiyo Wamanda wengi ni Wakristo wa Anglikana na Katoliki. Kati ya Wamanda kuna maprofesa na madaktari na wanasiasa maarufu kama hayati Horace Kolimba mwanasheria kitaaluma (kati ya wanafunzi wa kwanza walianza kusoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pale Mnazi Mmoja - leo Chuo wa Watu Wazima (Institute of Adult Education) - aliyekuwa katibu mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambaye aliweka misingi imara ya chama, Profesa Crispini Haule ambaye alikuwa Waziri Mdogo wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dr Aleck Chaponda na chama chake cha siasa, Dr Christopher D. Mlosy Ndomba, mchumi ambaye anafanya kazi katika shirika la utafiti wa sayansi na viwanda la Afrika Kusini (Council for Scientific and Industrial Research of South Africa, CSIR), na kabla ya kujiunga na CSIR alikuwa mtaalamu katika Shiririka la Kazi la Umoja wa Mataifa - International Labour Organization (ILO), mwimbaji maarufu Capitani John Komba.

Marejeo

hariri
  1. ling. Makala Wiedhafen Archived 5 Julai 2007 at the Wayback Machine. katika Koloniallexikon ya 1920; "Wiedhafen" ilikuwa kiasili jina la bandari ndogo nchini Ujerumani pale ambako mto Wied unaingia katika mto Rhein.
  2. Linganisha Rudolf Pfitzner, Deutsches Kolonial-Handbuch, Band I, Berlin 1901, uk. 339 (online hapa kwenye archive.org)
  3. https://www.nbs.go.tz, uk 210
  4. "Sensa ya 2012, Njombe - Ludewa DC" (PDF). Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2004-01-02. Iliwekwa mnamo 2017-03-16.
  Kata za Wilaya ya Ludewa - Mkoa wa Njombe - Tanzania  

Ibumi | Iwela | Kilondo | Lifuma | Luana | Lubonde | Ludende | Ludewa | Lugarawa | Luilo | Lumbila | Lupanga | Lupingu | Madilu | Madope | Makonde | Manda | Masasi | Mavanga | Mawengi | Milo | Mkongobaki | Mlangali | Mundindi | Nkomang'ombe | Ruhuhu


  Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Njombe bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Manda (Ludewa) kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
Tafadhali usiingize majina ya maafisa au viongozi wa sasa maana wanabadilika mno.