Hati hiyo, ndefu kuliko zote za Mtaguso wa pili wa Vatikano, inaitwa ya kichungaji kwa sababu inataka kutazama mambo kwa lengo la kuongoza maisha ya watu.

Ilitolewa siku ya mwisho ya mtaguso huo (8 Desemba 1965) kwa kura 2307 dhidi ya 75 za maaskofu na makasisi waliokuwepo.

Kama kawaida ya hati za Kanisa Katoliki, jina lake rasmi Gaudium et Spes linatokana na maneno ya kwanza katika lugha asili (Kilatini); tafsiri yake ni "Furaha na Matumaini".

Sehemu yake ya kwanza inaweka misingi ya imani, na sehemu ya pili inaonyesha msimamo wa Kanisa Katoliki kuhusu ulimwengu wa leo.

Kichwa kinasema wazi kuwa hati hiyo inahusu “Kanisa katika ulimwengu wa kisasa”, kwa kuwa Wakristo wanapaswa daima kuishi na kutenda “leo”, huku wakijua vizuri mambo yalivyo, wakitambua ishara za nyakati zijazo ili waone njia za kufaa kwa wokovu wa ulimwengu.

Bila ya shaka imepita miaka mingi tangu hati iandikwe, hivyo yameshatokea mabadiliko mengi, yaliyochunguzwa kwa makini na mapapa na sinodi mbalimbali waliojitahidi kutekeleza mafundisho ya mtaguso.

Ingawa baadhi ya mambo leo yanaonekana tofauti kidogo, hati hiyo inabaki muhimu: kwanza kwa mtazamo wake wa jumla, pili kwa mtindo wa kuwaelekeza watu katika mambo ya kawaida yanayowahusu maishani, tatu kwa mafundisho ya msingi yasiyoweza kubadilika, nne kwa kuwa misimamo mbalimbali inafaa mpaka leo.

Jambo kuu ni kwamba Kanisa halijioni tena mbali na ulimwengu, wala dhidi ya ulimwengu, bali ndani ya ulimwengu.

Wakristo wanasafiri duniani pamoja na binadamu wenzao, wakishirikiana nao katika yale yote yasiyopingana na imani na maadili ya Kikristo.

Hasa walei, ambao idadi yao ni karibu sawa na idadi ya wanakanisa wote, wanapaswa kuishi ulimwenguni kama chachu mpaka donge lote liumuke.

Basi, Kanisa linajisikia kuhusika kabisa na maisha ya watu wote, hasa mafukara.

Ndiyo maana maneno ya kwanza ya hati hiyo yanasema kuwa “furaha na matumaini, huzuni na mafadhaiko ya watu ni pia ya wanafunzi ya Kristo”.

Hati hiyo ni ujumbe wa Kanisa kwa watu wote unaotaka kuwasaidia waelewe mambo yanayotukia siku hizi, kwa kuwa katika hayo binadamu anaweza kujipatia maisha bora kweli na halafu uzima wa milele, au kinyume chake anaweza kudanganyika na kupotoka.

Siku hizi ugumu wa pekee kwa binadamu ni kwamba mabadiliko ya kila aina yanatokea haraka ajabu, tofauti na zamani: mtu wa kawaida hapati nafasi ya kuyafikiria kwa dhati na kuyachambua.

Hivyo hatari yake ni kufuata mkondo au kuongozwa na matukio badala ya kujifanyia mpango wa kumfaa, hata anaweza akafikia hatua ya kushindwa kujielewa ni nani, pamoja na kukosa msimamo maishani na raha moyoni mwake.

Basi, anahitaji kuchungwa na kuelekezwa kwa imani na upendo: ndiyo kazi ya Kanisa ambalo lina nafasi nzuri ya kuwatangazia watu majibu ya Injili kwa maswali yanayowakera.

Kwa ajili hiyo hati inamuongoza msomaji hatua kwa hatua kufikiria utatanishi wa kisasa katika nadharia, jamii, uchumi na siasa unaomfanya afadhaike, hasa akiona maendeleo hayafaidishi wote na pengine yanatumika dhidi ya binadamu.

Hivyo anaweza kutambua kuwa shida zinaanza moyoni mwake, ambamo mna mashindano makali na maswali ya msingi kama vile, “Mtu ni nani? Mateso na kifo vinavyodumu hata wakati huu wa maendeleo makubwa maana yake nini? Mtu ailetee nini jamii na atarajie kupata nini toka kwake? Baada ya maisha haya kutakuwa na nini?”.

Mtaguso ulisema jibu ni Yesu Kristo, mwokozi pekee, kiini na lengo la historia yote, msingi hasa usiobadilika; katika mwanga wake ukachunguza fumbo la binadamu na wito wake.

Sehemu ya kwanza

hariri

Sura ya kwanza

hariri

Sura hii inaeleza hadhi ya binadamu yeyote: ingawa karibu wote wanakubali kuwa mtu ni kiumbe bora duniani, Kanisa linasisitiza ukweli huo kwa kumuona na kumuita “sura ya Mungu” hata baada ya kuathiriwa na dhambi.

Ndio msingi wa heshima anayostahili katika mwili na zaidi katika roho ambayo kwa akili inaweza kujipatia ukweli na hekima, kwa [[dhamiri] inasikia wito wa Mungu, na kwa hiari inaweza kuuitikia.

Lakini Kanisa, pamoja na kusisitiza hiari kama wanavyofanya wengi siku hizi, linahimiza pia kuitumia vizuri, kwa kuwa mwishoni kila mtu atahukumiwa juu ya matumizi ya vipawa vyake.

Baada ya kukabili suala la kifo kwa kutangaza habari njema ya ufufuko, hati inakabili janga mojawapo la siku hizi, yaani kwamba wengi wanakanusha uwepo wa Mungu au wanaishi bila ya kumjali.

Mtaguso ulifikiria hasa ukomunisti na misimamo mingine ya kupinga na kuzuia dini zote, lakini badala ya kuilaani tu, umehimiza Wakristo wajadiliane na kushirikiana nayo, pamoja na kutoa ushuhuda wa maisha bora, ukikiri kuwa pengine mifano yao mibaya ndiyo iliyosababisha wengi wakose imani.

Mwisho inachorwa taswira ya Yesu Kristo, mtu mpya, ambaye pekee yake anaangaza fumbo la binadamu pamoja na uchungu na kifo.

Sura ya pili

hariri

Sura hii inatoa mafundisho kuhusu jamii yanayozingatia mpango wa Mungu wa kuwa watu waishi kwa ushirikiano: kuukamilisha kwa msingi wa haki ni muhimu kuliko maendeleo ya ufundi tu.

Kwa ajili hiyo kila mtu awajibike kuhusu wenzake wote bila ya kumsahau hata mmoja, akijifanya jirani wa wenye shida na kujitahidi kustawisha usawa kwa kutumia nafasi yoyote aliyonayo katika jamii.

Maadili ya kibinafsi hayakubaliki, bali wajibu mkuu mmojawapo ni kujihusisha na ustawi wa jamii na mshikamano ili wote kwa neema ya Kristo waishi kijamaa.

Sura ya tatu

hariri

Sura hii inatoa msimamo kuhusu utendaji wa binadamu ulimwenguni.

Hasa leo ambapo maendeleo ni ya haraka watu wanajiuliza kuhusu maana ya juhudi zao na namna ya kuziendeleza.

Ni hakika kuwa Mungu amewaagiza wafanye kazi na kutawala ulimwengu ili wote wapate hali ya maisha wanayostahili walio sura yake.

Wakristo wanapaswa kuwa mstari wa mbele bila ya kudhani eti, Mungu anauonea kijicho ushindi wowote wa binadamu juu ya maadui wake (ujinga, maradhi na ufukara).

Kinyume chake ushindi huo unatangaza ukuu wa Mungu aliyemuumba mtu akiwa na akili nyingi.

Lakini binadamu asisahau kuwa ubora wake hautokani na wingi wa vitu anavyojipatia, bali unategemea tunu za kiadili anazostawisha kwa kazi yake, hasa haki na udugu.

Shida ni kwamba mara nyingi akishindwa na dhambi anafuata ubinafsi au utaifa na kuanzisha miundo ya dhuluma na vita hata kutengeneza silaha za kutosha kuangamizia uhai wowote duniani.

Mbele ya hali hiyo Wakristo wanapaswa kutofuata mitindo ya ulimwengu bali njia ya upendo nyuma ya Kristo, wakiwa tayari kubeba msalaba wanaotwishwa wale wanaotafuta haki na amani.

Tumaini la uzima wa milele lisipunguze bidii za kuboresha maisha ya binadamu wa leo, kwa kuwa huyo anaandaliwa hapa duniani kuingia katika ufalme wa mbinguni.

Katika utendaji wake mtu ana haki ya kufuata taratibu za elimudunia, siasa n.k.

Imani haiogopi kumuachia nafasi hiyo, kwa kuwa Mungu yuleyule aliyejifunua kwetu kwa imani ameumba pia vitu vyote na kutujalia akili na uvumbuzi.

Mtaguso umelaumu mawazo finyu yanayogonganisha imani na sayansi.

Sura ya nne

hariri

Sura hii inaeleza yatokanayo na zile zilizotangulia, yaani uhusiano wa Kanisa na ulimwengu.

Kanisa likiwa na lengo la milele, linaishi duniani na wanae ni pia raia wa nchi zao.

Hivyo linachangia ustawi wa binadamu pamoja na kupokea kwa shukrani misaada mbalimbali ya walimwengu.

Lina ujumbe kwa watu wote kuhusu wokovu, lakini pia kuhusu maisha haya, hasa hadhi na haki za kila mtu.

Kwa hiyo, ingawa utume wa Kanisa ni wa kidini hasa, linashughulikia pia ustawi wa jamii na umoja wa mataifa.

Wakristo wasisahau tena majukumu yao ya kidunia, wala wasiyaone hayahusiki na imani.

Mojawapo kati ya makwazo makubwa zaidi ya nyakati zetu ni utengano huo kati ya imani na maisha ya Wakristo wengi.

Kwa namna ya pekee, walei wanapaswa kushughulikia malimwengu yote kwa mfano wa Yesu huko Nazareti.

Wasisubiri kuagizwa na wachungaji wao, kwa kuwa kuratibu hayo ni kazi ya walei hasa.

Mtaguso umekiri tena ukosefu wa wanakanisa na kuwahimiza kujirekebisha wasije wakazuia uenezaji wa Injili.

Vilevile umeshukuru kwa juhudi za watu wowote kwa ajili ya ustawi wa familia, utamaduni, uchumi, jamii, amani na mshikamano wa kimataifa, hata ukakiri Kanisa limefaidika sana na upinzani na dhuluma za maadui wake.

Sehemu ya pili

hariri

Baada ya kumaliza kueleza kwa jumla jinsi Kanisa linavyohusika na wito wa binadamu, hati hii katika sehemu ya pili inakabili masuala kadhaa yaliyo muhimu zaidi kwa watu wa leo.

Sura ya kwanza

hariri

Kati ya hayo sura ya kwanza inafafanua kwanza hadhi ya ndoa na familia na namna ya kuzipa nafasi za kufaa, kwa sababu mengine mengi yanategemea hali ya familia.

Baada ya kueleza utakatifu wa ndoa, kwa kuifananisha na hali ya kuwekwa wakfu kwa njia ya sakramenti za kudumu, mtaguso umeonyesha ubora wa upendo kati ya mume na mke na namna ya kuutekeleza, ukisisitiza unavyoelekea uzazi.

Hivyo watu wa ndoa wanapaswa kupanga kwa pamoja mbele ya Mungu na kwa kuzingatia mafundisho ya Kanisa ili wazae kwa busara na ukarimu.

Kwa namna ya pekee inasisitizwa kuwa ni lazima uhai wa binadamu kisha kuanza ulindwe kwa bidii zote: kuua mimba au mtoto ni maovu ya kutisha.

Katika magumu yanayohusu uzazi wa mpango, wanandoa wajitahidi kuwa na kiasi na kufuata usafi wa moyo jinsi inavyowafaa.

Hata jamii nzima inatakiwa kuchangia ustawi wa familia: viongozi watunge sheria na kufanya mipango kwa ajili hiyo; wanasayansi waendelee kutafuta njia halali za kupanga uzazi; mapadri wafanye juu chini familia ziishe kwa utulivu.

Sura ya pili

hariri

Sura hii inafikiria namna za kustawisha utamaduni, yaani zile namna maalumu ambazo binadamu anakabili maisha katika mazingira na nyakati mbalimbali kulingana na orodha ya tunu anazothamini.

Tofauti na wanyama, yeye hawezi kufikia hali ya maisha ya kumfaa kweli asipoyafanyia kazi mema yaliyoumbwa na Mungu ndani mwake na kandokando yake.

Kila kabila na kundi la watu lina utajiri wake ambamo binadamu achote ili kujiendeleza na kuwaendeleza wenzake.

Lakini huu wa leo ni wakati mpya wa historia kwa sababu ya mabadiliko ya haraka mno.

Upande mmoja zimefunguliwa njia mpya za kukuza na kueneza elimu na za kuunganisha aina tofauti za utamaduni.

Upande mwingine kuna hatari za kufuta hekima na sura maalumu za kila jamii, kuvuruga mafungamano kati ya vizazi, kuacha elimu ya juu mikononi mwa wataalamu tu n.k.

Kufuatana na amri ya upendo Wakristo wanatakiwa kuchangia na wenzao ujenzi wa ulimwengu ili wote waone vizuri kazi ya Mungu na namna ya kuiendeleza.

Kama vile yeye alivyotumia utamaduni wa watu ajifunue kwao, ndivyo Kanisa pia lilivyofanya na linavyopaswa kufanya katika kueneza habari njema.

Lenyewe limetumwa kwa mataifa yote, hivyo halibanwi na utamaduni wowote, bali linautumia na kuuchangia, linausafisha na kuuinua lisiishie ndani yake.

Ni wajibu wa wote kujitahidi kufuta ujinga kwa kueneza elimu hasa ya msingi ili kila mtu aweze kuchangia zaidi ustawi wa jamii.

Vilevile kila mtu aelewe wajibu wa kujiendeleza kiutu na Kiroho bila ya kutawaliwa na kazi za mikono tu, akitumia vitabu na vyombo vingine vya upashanaji habari, muda huru ulio nje ya kazi n.k.

Sura ya tatu

hariri

Sura hii inafundisha kuhusu maisha ya kiuchumi na ya kijamii ya mtu wa nyakati zetu.

Ni lazima huyo awekwe juu kabisa kuliko maendeleo ya vitu, kwa kuwa ndiye mtendaji, kiini na lengo la uchumi na la jamii.

Kumbe wengi wanazingatia sheria za uchumi tu ili kutajirika iwezekanavyo.

Matokeo ni kwamba mtengo kati ya mataifa, na kati ya matabaka ndani ya nchi, unazidi kuwa mkubwa.

Anasa za wachache zinaleta ufukara wa kutisha wa umati hata kuhatarisha amani duniani.

Binadamu wa leo anaweza kurekebisha hali hiyo, lakini yanahitajika mageuzi mengi katika mitazamo, mazoea na miundo pia.

Hapo tu ongezeko la uzalishaji litasaidia kweli, yaani litamsaidia mtu yeyote katika mahitaji yake yote (ya mwili, ya nafsi na ya roho).

Kwa ajili hiyo ni lazima uchumi usiachwe uende zake wala usitawaliwe na wachache, bali wote waweze kuuchangia ustawi na uongozi wake bila ya ubaguzi, wakisaidiwa kushika nafasi yao hasa kwa njia ya ustadi.

Kazi ya binadamu iheshimiwe kuliko mengine yanayohusu uchumi (k.mf. mtaji au malighafi).

Wote wana wajibu na haki ya kufanya kazi na kujipatia hivyo riziki za kutosha.

Vilevile wana haki ya kupata muda kwa maisha ya kifamilia, hasa akina mama.

Wafanyakazi ni haki yao kuchangia uongozi wa kampuni, na vilevile kuunda vyama vya kutetea haki zao hata kwa migomo.

Mojawapo kati ya mambo yaliyozingatiwa zaidi na mtaguso ni njaa ya umati; kwa ajili hiyo umekumbusha kuwa Mungu ameumba vyote kwa ajili ya wote, basi ni lazima mali zigawiwe kwa haki na upendo.

Ingawa mtu yeyote ana haki ya kumiliki vitu kadhaa, ni lazima kila mmoja awe na mali za kutosha, wasiwepo wenye kujipatia mali nyingi kiasi cha kuacha wengine wakose hata mahitaji.

Matajiri wawajibike haraka kuwashirikisha wengine, la sivyo watakuwa wauaji wa wenye njaa.

Hao wa mwisho ni haki yao kujipatia riziki kutoka utajiri wa wenzao.

Kadiri ya mazingira tunaweza kuwa na njia mbalimbali za kuhakikisha wote wapate riziki zao (desturi za ukarimu, pensheni n.k.).

Mashamba yagawiwe kwa wakulima wasiyonayo.

Pesa zitumike ili kuandaa nafasi za kazi kwa watu wa leo na wa kesho wa nchi zote (vitegauchumi).

Wakristo watafute ufalme wa Mungu hata katika uchumi na shughuli nyingine za kijamii.

Sura ya nne

hariri

Sura hii inafikiria siasa ambayo pia siku hizi inapitia mageuzi makubwa.

Mchango wa Kanisa ni kutetea heshima ya kila mtu kwa kusisitiza kwamba lengo la siasa ni ustawi wa jamii nzima kuanzia watu na familia.

Uongozi unahitajika ili kulinganisha kwa haki madai ya watu mbalimbali.

Wananchi wote waelimishwe kuhusu siasa ili watoe mchango wao kwa kutumia nafasi wanazopewa (kura n.k.) na kwa kutetea haki zao bila ya kuwadai mno viongozi.

Jamii na Kanisa vinawahudumia watu walewale lakini kwa namna tofauti, hivyo havichanganyikani bali ni vema vishirikiane.

Hata hivyo Kanisa halifungamani na siasa yoyote, liweze kutangaza kwa uhuru maadili yanayotakiwa hata katika siasa, likipima mambo yote na kuhimiza yaliyo mema.

Sura ya tano

hariri

Sura ya mwisho inaongelea ujenzi wa amani na umoja kati ya mataifa.

Wakati ilipoandikwa ulikuwa wa mafadhaiko makubwa kuhusu dunia nzima kuja kuangamizwa na wingi na ukali wa silaha zilizotengenezwa.

Kwa msingi huo suala la vita linatakiwa lifikiriwe upya kabisa, wote wasiridhike na misimamo ya zamani kuhusu masharti ya uhalali wake.

Vilevile Wakristo wa madhehebu yoyote waungane kati yao, tena na wote wenye mapenzi mema, katika kujenga amani na haki.

Kwa kuwa amani ya kweli sio tu kusimama kwa vita, labda kwa hofu tu ya silaha zilizolundikana; amani ni tunda la haki ambayo itafutwe mfululizo kwa bidii, tena ni tunda la upendo ule wenye msingi ndani ya Mungu.

Kuhusu vita vinavyoendelea huku na huku, kwanza ukatili wake upunguzwe (kumbe siku hizi umezidi kwa sababu ya silaha mpya, mashambulizi ya raia, uangamizaji wa kabila zima n.k.).

Utiifu kwa maagizo hauwezi kuwa kisingizio cha kutenda maovu, bali ni wajibu kuyakataa.

Mapatano ya kimataifa kuhusu vita yaheshimiwe na wote.

Ni wajibu wa viongozi wa nchi kuzilinda hata kijeshi, lakini wasitumie jeshi ili kugandamiza wengine.

Pia waheshimu dhamiri ya wasiojisikia kutumia silaha.

Vitendo vinavyowezekana leo vya kuangamiza miji mizima au maeneo mapana pamoja na wote waliopo ni makosa ya jinai yasiyovumilika.

Wanaotengeneza au kununua silaha ili kujikinga na maadui wasije wakashambuliwa, wafikirie hatari ya silaha hizo kuja kutumika kweli, tena hasara ya maskini wanaokosa misaada wanayostahili kwa sababu tu pesa nyingi sana zinatumika kwa silaha.

Yatafutwe mapema njia za upatanisho na muundo wa kimataifa wenye uwezo wa kudumisha amani na haki kwa wote.

Hapo katikati akiba za silaha zipunguzwe kwa mpango wa pamoja.

Viongozi na watu wao waache utaifa na misimamo yo yote inayotenganisha watu.

Hasa malezi ya vijana na upashanaji habari vieneze mawazo ya amani na mitazamo mipana yenye faida kwa binadamu wote.

La sivyo watu watafikia tu ile amani ya kutisha itakayopatikana kwa kufa wote.

Kanisa likisema hivi haliachi kutumaini na kuhimiza wongofu wa mioyo.

Kuhusu kujenga umoja kati ya mataifa, mara nyingi misingi ya kutoelewana ni hali tofauti mno za uchumi, nia ya kutawala, dharau ya wengine na vilema mbalimbali.

Basi, ushirikiano mkubwa unaowezekana leo uwe njia ya kutatua matatizo hayo na kukidhi mahitaji ya watu, hasa maskini.

Miundo ya kimataifa iliyopo iwajibike kuzingatia zaidi nchi zinazoendelea, wakimbizi na wengine wenye shida maalumu.

Ingawa miaka ileile ya mtaguso nchi nyingi zilipata uhuru wa kisiasa, hali ya uchumi inazirudisha chini ya ukoloni mamboleo; basi, mshikamano uendeleze kweli nchi hizo.

Lakini maendeleo yanategemea watu kuliko pesa, kwa hiyo kazi ya kwanza ni kuandaa raia wa nchi maskini kwa elimu na ufundi.

Inahitajika misaada, mikopo na vitegauchumi tena kwa ukarimu, lakini pia kurekebisha sana sheria za uchumi wa kimataifa.

Upande wao viongozi wa nchi maskini wapokee misaada hiyo kwa uaminifu, na raia wao wajitahidi kutumia vile vyote walivyo navyo.

Maendeleo ya uchumi yasisahaulishe roho ya binadamu, kwa kuwa huyo haishi kwa mkate tu.

Wengi leo wanafadhaishwa na kasi ya ongezeko la watu. Jawabu la kwanza kwa suala hilo ni kuleta usawa mkubwa zaidi kati ya watu na kueneza ujuzi kuhusu kilimo n.k.

Halafu zitungwe sheria zinazosaidia familia, izuiwe kasi ya watu kuhamia mijini, watu waelimishwe kwa ukweli kuhusu hali ya nchi na uzazi wa mpango.

Wote wajiepushe na njia za mkato zinazokwenda kinyume cha maadili na cha haki ya msingi ya wananchi kufunga ndoa na kuzaa wanavyoona vema wenyewe.

Basi, wasaidiwe kuunda dhamiri na kujifunza njia halali za kupanga uzazi.

Wakristo wawe mstari wa mbele katika mshikamano wa kimataifa, wakijua Yesu katika maskini analia na kudai upendo.

Mtaguso uliita kikwazo kuona nchi za Kikristo zikitapanya mali, wakati nyingine zinalemewa na njaa, maradhi n.k.

Wakristo wajitolee kuhamia kwenye shida ili kusaidia kwa hali na mali wakishirikiana na miundo na watu wowote, kwa kuwa tunaye Baba mmoja na tunapaswa kuishi wote kidugu.

Hapo watatambulikana kama wafuasi halisi wa Kristo.

Wakikumbuka kuwa hawataingia mbinguni kwa kusema tu, Bwana, Bwana, bali kwa kutimiza mapenzi ya Baba, wakabili kazi hiyo kubwa ambayo watahukumiwa siku ya mwisho kwa jinsi walivyoifanya.

Viungo vya nje

hariri