Perseverance (gari la upelelezi)

(Elekezwa kutoka Perseverance (Mirihi))

Perseverance (tamka: per-se-vi-rens, kwa maana ya "Ustahimilivu") [1] [2] ni jina la gari la upelelezi lililopelekwa kwenye sayari ya Mirihi kwenye Februari 2021. Kusudi lake ni kuzunguka katika kasoko ya Jezero na kukusanya data zake. Ilirushwa na mamlaka ya anga-nje ya Marekani NASA.

Gari la Perseverance likishushwa kutoka roketi ya kulifikisha kwenye uso wa Mirihi.
Picha ya satelaiti ya sehemu ambako Perseverance ilitua; pamoja na parachuti na "decent stage" yaani roketi iliyoishusha
Video ya kutua kwa Perseverance kwenye uso wa Mirihi; Mwanzoni ngao ya kinga cha joto kinatengwa; mwishoni picha ya kuteremsha kwa waya za winchi kutoka chombo cha roketi kilichoipeleka juu ya uso wa sayari

Ilifika kwenye uso wa Mirihi tarehe 18 Februari 2021, baada ya kurushwa kutoka Marekani tarehe 20 Julai 2020[3].

Muundo

hariri

Perseverance ina ukubwa unaolingana na motokaa ya kawaida.

Ina magurudumu sita na kila moja linaendeshwa na mota ya umeme ya pekee. Gari lote linapata nguvu yake kutoka beteri ya kinyuklia inayobadilisha joto kutokana na kuoza kwa dioksidi ya plutoni kuwa umeme[4].

Magurudumu ni ya alumini na kuna tredi kama mabavu usoni ili yasiteleze. Kila gurudumu lina kipenyo cha sentimita 52 likiwa limefungwa kwenye mguu wake wa pekee.[5]

Kuna mkono wenye urefu wa mita 2.1 ulio na vifundo kama mkono wa binadamu.

 
Njia zilizopangwa kwa safari za uchunguzi kwenye Mirihi; angalia mashapo yenye umbo la delta ya mto.

Shabaha

hariri

Perseverance inabeba vifaa mbalimbali vya upimaji pamoja na kamera 19, mikrofoni 2 na helikopta ndogo. Mkono wake unaweza kushika mawe. Kuna pia kekee kwa uchunguzi wa miamba, pamoja na zana nyingine.

Kati ya shabaha zake ni malengo yafuatayo ya kisayansi: [6]

Idadi ya sampuli zitawekwa katika vyombo na kuandaliwa kwa safari ya kipimaanga kingine kitakachokuja kuchukua sampuli hizo kwa utafiti duniani.

Swali moja lililoongoza mpango wa gari hilo ni kama Mirihi iliwahi kuwa na uhai katika nyakati zilizopita. Eneo la uchunguzi wake ni kasoko ya Jezero inayoonekana kama ziwa kubwa lililokauka. Kwenye sehemu mbili kuna mashapo ambayo yanafanana na matope makavu ya mto unaoishia jangwani. Kwa hiyo kazi nyingine ya Perseverance ni kuchungulia udongo na miamba kwa dalili za bakteria au kiumbehai mwingine ambaye aliweza kuishi katika ziwa linalodhaniwa lilikaa hapo.

Inabeba pia kifaa cha kuzalisha oksijeni kwa kupasua dioksidi kabonia inayopatikana katika angahewa la Mirihi. Hili ni jaribio kwa siku zinazokuja ambako binadamu wanaweza kutumwa Mirihi ambao watahitaji oksijeni kwa upumuaji wao[6].

 
Helikopta ndogo ya Mirihi ("Ingenuity")

Jaribio la helikopta ya Mirihi

hariri

Pamoja na Perseverance, helikopta ndogo ilipelekwa Mirihi. Hii ni droni (ndege isiyo na rubani) ndogo yenye uzito wa kg 1.8 pekee iliyopewa jina Ingenuity. Inabeba kamera moja tu [7] [8]. Kusudi lake ni kwanza kuonyesha kama inawezekana kweli kutumia usafiri wa hewani katika angahewa jepesi sana ya sayari hiyo. Pili itatumika kwa kupeleleza njia ya Perseverance kama kuna vizuizi vikubwa. Itaonyesha pia kama chombo chepesi kama hicho kitavumilia ubaridi mkali wa usiku kwenye Mirihi. Ikiweza kutumika tena asubuhi, marubani wake waliopo duniani wataendelea kupeleleza mazingira na kupiga picha.

Mawasiliano yake na Dunia ni kupitia kituo cha redio kilichopo kwenye Perseverance.[9]

Udhibiti

hariri

Gari hilo na kazi zake vinaendeshwa kutoka duniani. Ukumbi wa usimamizi uko kwenye Jet Propulsion Laboratory ya NASA huko Pasadena, Kalifornia. Huko wako wanasayansi, wahandisi na mafundi wanaosimamia kazi zote pamoja na hao wanaoendesha gari hali halisi.

Perseverance ina mwendo wa polepole sana, ikiendelea kwa kasi kubwa inaweza kutembea mita 152 kwa saa. Maana yake kwa kilomita 1 itahitaji angalau saa sita.

Sababu muhimu ya kupanga mwendo wa polepole ni changamoto za udhibiti.

Mawasiliano yanafanyika kupitia mawimbi ya redio ambayo yanaenea kwa kasi ya nuru. Perseverance inarusha na kupokea ujumbe kupitia antena zake; kuna antena inayorusha alama zake moja kwa moja hadi duniani ambako antena kubwa za Mtandao wa Anga za Mbali (Deep Space Network -DSN) zinaipokea na kujibu[10]. Lakini kituo cha kuwasiliana moja kwa moja kwenye gari la Mirihi hakina uwezo kubwa shauri ya haja ya kupunguza uzito wa vifaa; kama data ni nyingi zitarushwa kwanza hadi satelaiti inayozunguka Mirihi na kutoka satelaiti ile hadi duniani.

Ilhali hapa duniani tunapokea mawimbi hayo mara moja, umbali mkubwa katika anga-nje unamaanisha kuna wakati unaopita kati ya kurusha na kupokea. Umbali baina ya Mirihi na Dunia unabadilikabadilika; mara Dunia na Mirihi ziko karibu na hapo mawimbi yanasafiri dakika 5; kama Mirihi na Dunia ziko mbali kati yake mawimbi yanahitaji dakika 20 hivi[11]. Kwa hiyo kama dereva wa gari la Mirihi aliye Kalifornia anaona kizuizi atatuma amri ya "Simama", na amri hiyo itafika kwenye mashine dakika hizo baadaye. Ni vivyo hivyo kwa amri za kupiga kona, kulenga kamera upande mwingine na kadhalika. Hapo mwendo wa polepole umepangwa ambao ni pia mwendo unaotumia umeme kidogo.

Gharama

hariri

NASA imepanga kuwekeza takriban dolar za Marekani bilioni 2.75 katika mradi huo kwa kipindi cha miaka 11. Hii ni pamoja na $ bilioni 2.2 kwa kubuni na kujenga gari, helikopta na roketi, $ milioni 243 kwa huduma za kuvirusha na kufikisha Mirihi, na $ milioni 291 kwa miaka 2.5 ya shughuli zenyewe kwenye Mirihi.[12] [13]

Marejeo

hariri
 1. "NASA EDGE: Mars 2020 Rollout". nasa.gov. NASA. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2020-10-25. Iliwekwa mnamo 19 Februari 2021.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
 2. Landers, Rob. "It's landing day! What you need to know about Perseverance Rover's landing on Mars", 17 February 2021. 
 3. "Launch Windows". mars.nasa.gov. NASA. Iliwekwa mnamo 28 Julai 2020.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
 4. Wheels and Legs, tovuti ya Mars 2020 ya NASA
 5. [https://mars.nasa.gov/mars2020/spacecraft/rover/wheels/ Wheels and Legs], tovuti ya Mars 2020 ya NASA
 6. 6.0 6.1 "Overview". mars.nasa.gov. NASA. Iliwekwa mnamo 6 Oktoba 2020.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
 7. "Mars mission readies tiny chopper for Red Planet flight". BBC News. 29 Agosti 2019.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
 8. Gush, Loren (11 Mei 2018). "NASA is sending a helicopter to Mars to get a bird's-eye view of the planet – The Mars Helicopter is happening, y'all". The Verge. Iliwekwa mnamo 11 Mei 2018.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
 9. Volpe, Richard. "2014 Robotics Activities at JPL" (PDF). Jet Propulsion Laboratory. NASA. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 21 Februari 2021. Iliwekwa mnamo 1 Septemba 2015.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
 10. Communicating with Mars: The Deep Space Network and Perseverance, tovuti ya kampuni ya Peraton.com (inauza silaha)
 11. [https://mars.nasa.gov/mars2020/spacecraft/rover/communications/ Communications], tovuti ya NASA
 12. "Mars Perseverance Landing Press Kit" (PDF). Jet Propulsion Laboratory. NASA. Iliwekwa mnamo 17 Februari 2021.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link) Kigezo:PD-notice
 13. "Cost of Perseverance". The Planetary Society.

Viungo vya nje

hariri