Saba Saba (Tanzania)

Kwa matumizi mengine ya jina hili tazama Sabasaba (maana)

Katika maonyesho ya Kibiashara ya Sabasaba

Saba Saba ni sikukuu katika nchi ya Tanzania inayoadhimishwa tarehe saba, mwezi wa saba (7 Julai) ambayo lengo lake ilibadilishwa kutokana na mabadiliko ya historia na siasa.

Asili ya Saba Saba

hariri

Asili ya Saba Saba ilikuwa kuundwa kwa chama cha Tanganyika African National Union (TANU) kwenye tarehe 7 Julai ya mwaka 1954. Chama hiki kiliongozwa na Julius Nyerere kikawa chama tawala wakati wa uhuru wa Tanganyika kilichoendelea kuongoza siasa ya nchi baada ya kushika viti vyote vya bunge.

Mwaka 1963 Nyerere pamoja na uongozi wa chama waliamua kupeleka nchi kwenye mfumo wa chama kimoja kisheria. Hivyo mwaka 1964 siku ya kuzaliwa kwa chama yaani "Saba Saba Day" iliorodheshwa katika sheria ya sikukuu za umma (Public Holidays Ordinance Act)[1].

Sherehe za Saba Saba wakati wa mfumo wa chama kimoja

hariri

Tangu mwaka 1967 TANU ilitangaza itikadi ya Ujamaa kama siasa rasmi na hapo ilitumia mara nyingi lugha ya kukazia "wakulima na wanfayakazi" jinsi ilivyokuwa kawaida katika vyama vilivyofuata itikadi ya usoshalisti duniani. Hivyo sikukuu ya chama ya Saba Saba iliadhimishwa pia kama "sikukuu ya wakulima na wafanyakazi". Mtindo huu uliendelea kutumiwa pia baada ya mwaka 1977 ambako TANU iliungana na Chama cha Afro-Shirazi (ASP) cha Zanzibar kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Baada ya muungano wa TANU na ASP kuwa CCM sikukuu ikaitwa mara ningi "siku ya wakulima" kwa kufuatana na wito wa kisiasa "Siasa ni Kilimo" uliokazia maendeleo ya taifa kwa njia ya kuboresha kilimo nchini.

Saba Saba ilikuwa sikukuu ya umma maana yake ofisi za serikali na makampuni, maduka makubwa na shule zote zilifungwa. Katika miji yenye makao makuu ya mkoa na mara nyingi pia penye makao makuu ya wilaya kulikuwa na maonyesho, wakati mwingine pamoja na mikutano ya hadhara ambako watu walisikia hotuba za viongozi wa chama na serikali. Kwenye maonyesho kulikuwa na mazao, mifugo na bidhaa za tasnia za eneo pamoja na bidhaa nyingine. Miji mingi nchini Tanzania huwa na maeneo ya Saba Saba (Saba Saba Grounds). Sherehe zilitokea hadi ngazi ya kijiji.

Kati ya maonyesho haya ni hasa Maonyesho ya Saba Saba ya Dar es Salaam (Dar es Salaam International Trade Fair, Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam) ambayo ni maarufu kama tukio la kitaifa na la kimataifa inayoendelea kuvuta wageni wengi hadi leo[2].

Kufutwa kwa Saba Saba wakati wa kuhamia mfumo wa vyama vingi

hariri

Mwaka 1992 Tanzania ilihamia mfumo wa vyama vingi baada ya miaka mingi ya kuwa na chama cha TANU / CCM pekee. Hapo vyama vipya vilipinga sikukuu ya umma iliyoadhimisha kuzaliwa kwa chama kimoja. Hivyo Sikukuu ya Saba Saba ilifutwa mwaka 1993. Badala yake sikukuu mpya ya Nane Nane yaani 8 Agosti ilianzishwa kama "Sikukuu ya Wakulima".

Katika mwaka uliofuata ilitokea hali ya mchanganyo ambako sehemu ya watu waliendelea kuchukua 7 Julai kama sikukuu waliozea na kutofika kazini ilhali wengine walikutana kwa sherehe ya 8 Agosti[3].

Hapo wanasiasa walijadiliana na kufikia mapatano ya kwamba 7 Julai itakuwa tena sikukuu mjini Dar es Salaam ambako maonyesho makubwa hufanyika na 8 Agosti itakuwa sikukuu ya Nane Nane kwa ajili ya wakulima kitaifa.[4]

Saba Saba kama sikukuu ya biashara au ya kiuchumi

hariri

Baadaye Saba Saba ikarudishwa kama sikukuu ya umma kitaifa. Mara nyingi inaelezwa kuwa ni siku ya biashara, sikukuu ya wafanyabiashara au "Dar es Salaam International Trade Fair Day"[5].

Kutokana na mabadiliko katika historia yake kuna mchanganyo kuhusu maana ya siku hii ambako asili yake katika mapambano ya uhuru mara nyingi inasahauliwa[6].

Katika orodha za sikukuu zinazopatikana kwenye intaneti kuna maelezo tofautitofauti zinazoonyesha hali ya kutatanisha kuhusu kusudi na lengo la sikukuu hii.[7] [8]

Siku ya Kiswahili Duniani

hariri

Siku ya Kiswahili Duniani ilianzishwa na UNESCO mnamo mwaka 2021 ili kuadhimishwa kila tarehe 7 Julai kuanzia mwaka 2022.

Marejeo

hariri
  1. www.saflii.org/tz/legis/num_act/phoaa1964317.pdf The Public Holidays Ordinance(Amended) Act 1964, Parliament of Tanzania, tovuti ya Southern African Legal Information Institute, iliangaliwa Julai 2018
  2. Over 2,000 exhibitors for Dar international trade fair as preps gather pace Ilihifadhiwa 30 Juni 2018 kwenye Wayback Machine., tovuti ya gazeti The Citizen, Monday, June 19, 2017, iliangaliwa Julai 2018
  3. Saba Saba – Tanzanian Holiday, tovuti ya allthingskenya.com, iliangaliwa Julai 2018
  4. Tanzania Peasants Day Ilihifadhiwa 18 Januari 2018 kwenye Wayback Machine., tovuti ya aglobalworld.com, iliangaliwa Juai 2018
  5. Public Holidays in Tanzania 2018, tovuti ya ubalozi wa Tanzania huko Washington, Marekani, iliangaliwa Julai 2018
  6. Pius Msekwa: Celebrating annual Saba Saba Day: Fervent appeal for its restoration to its original glory Ilihifadhiwa 4 Agosti 2018 kwenye Wayback Machine., tovuti ya gazeti Daily News, Tanzania, iliangaliwa Julai 2018
  7. „Saba Saba day (July 7) commemorates the founding of the Tanzanian political party“ Ilihifadhiwa 7 Machi 2018 kwenye Wayback Machine., tovuti The Travel World
  8. https://www.officeholidays.com/countries/tanzania/2018.php „Last Day of the annual Dar es Salaam International Trade Fair“, tovuti ya officeholidays.com

Viungo vya nje

hariri