Wasubi ni kabila mojawapo kati ya makabila ya Mkoa wa Kagera, nchini Tanzania. Wasubi wamechanganyika na Watanzania wengine na, ukiacha sehemu kubwa ya kabila hili ambao wanaishi katika Wilaya ya Biharamulo, wanapatikana kwenye maeneo mengine nchini Tanzania wakijitafutia riziki na ustawi kwa njia moja au nyingine.

Kabila hili linaongea lugha ya Kisubi ambacho ni Kibantu ingawa Wasubi wote si Wabantu. Wasubi wanaweza kuelewana lugha na majirani zao Wanyambo, Wahaya, Wazinza na Walongo na kwa kiasi fulani makabila mengine ya maziwa makuu, ukiacha baadhi ya makabila, kama vile Wasukuma na Wanyamwezi. Mwaka 1987 idadi ya Washubi ilikadiriwa kuwa 196,000 [1]. Kuna Wasubi wa Biharamuro na Wasubi wa Ngara

Historia

Kabila hili lina historia ndefu kuanzia karne ya 16, wakati Mtawala maarufu kutoka kaskazini mwa Uganda ya sasa, sehemu ya Ankole, aliyejulikana kama Ruhinda, aliposafiri na watoto wake na kuhamishia makazi yake Karagwe.

Baada ya kuanzisha utawala wake Karagwe, watoto wake walielekea maeneo mengine katika eneo la maziwa makuu, maarufu kwa Kiingereza kama Interlucustrine Region.

Mmoja kati ya watoto wa Ruhinda alielekea Lusubi na kuanzisha milki ya kiutawala bila shida yoyote, kama ambavyo ilikuwa kwa maeneo mengine kama Nyarubungo, Katoke, Kitwechembogo, Ruzibha na kwingineko. Hali hiyo ilitokana na maeneo hayo kukaliwa na wakulima wachache ambao hawakuwa na nguvu za kuwazuia wageni ambao walikuwa na uwezo mkubwa wa silaha na utajiri mkubwa wa mifugo, jambo lililoleta matumaini hata kwa wenyeji.

Jamii ya Wasubi iliendelea kuongezeka na kujiimarisha kama milki ya kiutawala ikiwa na mahusiano na milki nyingine jirani, zikiwemo zile za Karagwe (Wanyambo), Buha (Waha), Burundi (Warundi), Rwanda (Wanyarwanda), Buganda (Waganda) na Ankole (Wanyankole).

Mahusiano hayo yalikuwa pamoja na biashara, teknolojia ya chuma, kuoleana, vita vya kupanua au kulinda mipaka, siasa na imani za dini za asili.

Kabila la Wasubi lilikuwa milki kamili wakati Ujerumani ikiitwaa na kuitawala Tanganyika, Rwanda na Burundi. Milki ya Washubi iliendelea kuwepo hata wakati wa utawala wa Mwingereza.

Milki hiyo ilidumu hadi muda mfupi baada ya uhuru, wakati tawala za kichifu zilipoondolewa rasmi na serikali ya Tanganyika ili kuimarisha utaifa miongoni mwa Watanganyika na hatimaye Watanzania.

Eneo

Kutokana na eneo la kijiografia la Wasubi kuwa kubwa kuliko wingi wa watu, eneo hilo lilitawaliwa na uoto wa majani mengi na misitu ya savana. Wilaya iko na mapori ya Burigi, Kimisi amabayo ni sehemu ya hifadhi ya wanyama pori kwa sasa. Wilaya ya Chato ilitengwa kutoka eneo la wilaya hii mama ya Biharamulo

Uchumi

Kwa miaka mingi, jamii ya Wasubi ilitegemea kilimo, ufugaji na uvuvkwa ajili ya uchumi wao. Baadhi ya maeneo wanafuga mifugo mingi ikiwa ndiyo njia kuu ya uchumi. Aina ya ng'ombe wanaofugwa kwa wingi ni aina ya 'ankole' ambao kwa asili ni wakubwa na wana pembe ndefu. Hata hivyo kwa miaka ya karibuni wafugaji wamelazimika kuanza kufuga ng'ombe wenye pembe fupi ambao wanastahimili magonjwa.

Kwa ujumla unaweza kusema Wasubi wanalima kilimo cha mchanganyiko wa mazao ya chakula, biashara na ufugaji. Mazao makuu ni migomba, mahindi, maharagwe, mtama, karanga na mihogo. Mifugo ni pamoja na ng'ombe, mbuzi, kondoo na kuku.

Utamaduni

Chakula kikuu cha Washubi ni ndizi, ingawa, kutokana na kushuka kwa uzalishaji wa zao la migomba, sasa ugali unachukuliwa pia kama moja ya vyakula muhimu.

  Makala hii kuhusu utamaduni wa Tanzania bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Washubi kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.