Wilaya ya Ngara
Wilaya ya Ngara ni wilaya mojawapo kati ya 8 za Mkoa wa Kagera, kaskazini magharibi mwa Tanzania, yenye postikodi namba 35700 [1].
Wakazi
haririKatika sensa ya mwaka 2012, idadi ya wakazi wa wilaya hiyo ilihesabiwa kuwa 320,056 [2] na katika ile ya mwaka 2022 walihesabiwa 383,092 [3].
Wilaya ya Ngara inakaliwa na makabila makubwa mawili ambayo ni Wahangaza na Washubi. Wilaya hiyo inapakana na nchi za Rwanda na Burundi na lugha ya Wahangaza na Washubi ni Kihangaza na Kishubi ambazo zinaingiliana kwa karibu 92% na lugha za nchi ya Rwanda na Burundi na kuwafanya wenyeji kuelewana kilugha na wakazi wa mataifa hayo jirani.
Barabara
haririNjia kuu za kuingia nchi za Rwanda na Burundi zinapatikana ndani ya wilaya ya Ngara, ambapo kwa Burundi hutumia mpaka wa Kabanga/Kobero kuingia Burundi, mpaka huu unachangia 2.9% ya pato la taifa huku ukitoa 6.2% ya export index ya bidhaa zote za Tanzania zinazotoka nje, kwa upande wa mpaka wa Tanzania na Rwanda mpaka unaotumika ni mpaka wa Rusumo, huu mpaka uchangia 7.1% ya pato la taifa huku export index ikichangia 17.96% ya bidhaa zote za Tanzania zinazotoka nje.
Jina
haririJina la asili la wilaya ya Ngara lilikuwa Kibimba (yaani pori). Chanzo cha jina jipya la Ngara lilitokana na sehemu iliyokuwa maalumu kwa mikutanao ambayo ilifanyika chini ya miti mikubwa inayoitwa iminyinya yingara (ilikuwa miti mikubwa yenye matawi yaliyosambaa) ambapo kwa sasa eneo hilo ndipo ilipo halmashauri ya wilaya ya Ngara pale eneo la junction na mti wa kumbukumbu upo mpaka sasa pale ndani ya majengo ya halmashauri ya wilaya ya Ngara. Mti huo wa Umunyinya uliopandwa halmashauri ya wilaya ya Ngara ambao asili yake imebeba jina la Ngara.
Watawala
haririWilaya ya Ngara ilikuwa na watawala wa kichifu ambapo kulikuwa na machifu wa pande mbili yaani chifu wa Bugufi na Chifu wa Bushubi. Machifu waliotawala Bugufi walikuwa Balamba wa kwanza, Rusengo, Ruvubi, Mpanda, Kanyamazinge na Balamba mtoto wa Kayamazinge. Machifu hao wa Bugufi na Bushubi walikuwa wakikutana eneo la Nyamilama ili kupeana maadili na mbinu za kiutawala mfano lilivyo bunge la Dodoma kwa sasa. Na Bushubi alikuwepo chifu Nsoro.
Eneo la utawala
haririDola la Bugufi lilikuwa likipatikana katika bonde lote la Bugufi linaloanzia kaskazini magharibi mpaka kusini mashariki na wafalme wa Bugufi kuanzia Baramba I mpaka kwa Baramba Imotto wa Kayamazinge walitawala eneo la dola la Bugufi ambayo makao makuu ya dola hilo yalikuwa Kanazi. Mfalme wa kwanza wa Bugufi alikuwa Baramba I aliyeingia Ngara miaka ya 1680 akitokea Rwanda pamoja na wafanyakazi wake (Abagaragu). Kwa asili alikuwa akitokea kwenye ukoo wa kifalme wa Ankole huko Uganda uliokuwa unaitwa Wahinda (royal Bahinda clan of Ankole). HuO ni ukoo ulioibuka baada ya kumeguka kwa ukoo mkubwa wa kifalme wa Wanyiginya kutokana na ndugu wa damu moja kunyang'anyana maeneo ya kutawala ndani ya eneo la maziwa makuu, huo ukoo wa Wanyanginya nao ulifika eneo la Ankole miaka ya 1297 ukitokea Axum huko Ethiopia.
Kama ilivyo kwa wafalme wengine wa ukoo wa Wahinda alikuwa ni Muhima na alioa wake zake kutoka kwenye jamii za Wahima (watutsi). Aliingia Rusumo na kuweka makazi yake katika Mlima Shunga na kuwa mfalme wa kwanza wa Ngara. Mfalme Baramba I alikuwa na watoto wakubwa wawili ambao waliitwa Mpumirizi na Mpanda na Mpumirizi ndiye alikuwa mzaliwa wa kwanza na ndiye alitakiwa awe mfalme lakini haikuwa hivyo, kuna makosa yalifanyika mdogo mtu Mpanda akawa mfalme badala ya kaka yake. Orodha ya wafalme wa Bugufi ni Baramba I, Mpanda, Ruvubi, Rusibana, Rusengo (mdogo wake na Rusibana baada ya Rusibana kufariki vitani kwenye vita kati ya Warundi na Wahangaza), Kinyamazinge mwana wa Rusengo na Baramba II; pia walikuwepo Mpanda II na Ruvubi II ila walikuwa kama machifu wa jina tu kwa sababu uchifu wa madaraka uliishia kwa Baramba II.
Mila
haririMila na desturi za Wahangaza na Washubi zinafanana kwa kila kitu: katika mila zao mtoto alikuwa haruhusiwi kukalia kiti cha baba yake wala kula sahani moja na wazazi wake, hivyo walitengwa pembeni na kula peke yao. Wahangaza walikuwa hawaruhusiwi kula kondoo na mbuzi bali hao waliliwa na kabila duni lijulikanalo kama Watwa ambao ni kabila la asili huko milima ya Urundi (Burundi ya sasa). Hao Watwa walikuwa watumwa na wajakazi wa Wahangaza na Washubi (mbuzi aliitwa impene kwa kilugha kwa sababu waliichukulia kama ipo uchi na ndio sababu ya kutoliwa na kabila hilo enzi hizo).
Imani
haririImani ya Wahangaza na Washubi (dini) ilikuwa ni kuabudu chini ya miti ya Milumba (ikivumu) waliabudu mungu aliyeitwa Kilanga kilumwelu (mungu wa amani) na pia kutambikia kwenye vijumba vidogo vilivyoitwa Indalo (ukifika Bushubi na Kanazi waweza kuviona vijumba hivyo). Aidha wakazi hao waliamini kinga za asili za chale na hirizi.
Utamaduni
haririUtamaduni wa kuoana ilikuwa ni kwamba kijana hakuruhusiwa kutafuta mchumba bali wazazi wake walimchagulia mchumba kwa kuangalia historia ya ukoo au familia anakotoka mchumba husika. Wazazi wa pande zote mbili walikubaliana kwa kupeana mahari (posa) ya jembe la mkia (jembe la asili) au nguo zilizotengenezwa kutokana na magome ya miti (ikibugu). Binti alipelekwa usiku kuolewa.
Msichana akibeba mimba nje ya ndoa ya kimila adhabu yake ilikuwa ni kufungwa jiwe la kusagia na kutupwa mto Ruvubu eneo lililojulikana kama Mmasangano (Nyaburumbi), na adhabu nyingine ilikuwa ni kumfungia sagio (jiwe la kusaga) na kuwekwa njiapanda (amayilabili) ili aliwe na wanyama mpaka kufa. Mabinti wengi waliogopa adhabu hizo, hivyo walitii mila na desturi.
Wahangaza walitumia tiba ya asili yaani mitishamba kwa magonjwa, pia kuondoa mizimu iliyokuwa inawasumbua watu alikuwa anatafutwa mbuzi au kuku mweupe wa kafara na mgonjwa kuruka kafara hiyo kisha kutupwa porini kwenye miti iitwayo imilinzi.
Mahusiano
haririMahusiano ya watu yalidumishwa kwa kutembeleana baada ya kuandaa pombe ya asili yaani "impeke na gwagwa". Kulikuwa na aina mbili za unywaji wa pombe hiyo: aina ya kwanza watu walialikwa na kujumuika sehemu moja walipoitwa na familia iliyoandaa pombe hiyo hasa hasa msimu wa mavuno (kiangazi) kwa kilugha illiitwa "gutumila" na pia njia nyingine ilikuwa ya kwenda na mitungi ya pombe kutembelea familia fulani (kwa kilugha kugemula). Wanawake na watoto walizuiwa kunywa aina za pombe isipokuwa walikunywa pombe ya ndimasi au iliyochakachuliwa (umushalulo).
Burudani ya makabila hayo ni ngoma ya asili ya Wahangaza ilikuwa ikiitwa "miaeleko" yaani ngoma ya asili ambayo ilichezwa kwa madaha huku wakiruka juu.
Uchumi
haririShughuli kuu ya kabila hili ilikuwa kilimo, ufugaji kwa kiasi na uwindaji wa wanyama. Watoto walirithishwa mila na wazazi wao kwa kupewa elimu ya vitendo na hasa kugawa kazi kwa kuzingatia mgawanyiko wa kazi kijinsia.
Chakula kikuu katika wilaya ya Ngara ni ndizi, maharagwe na mihogo; pia hulima zao la kahawa toka mwaka 1950 huku pia miaka ya karibuni wengi wa wakulima wameanza kulima maparachichi (avocado). Pia shughuli za uvuvi hufanyika katika mto Ruvubu (Ruvuvu).
Tanbihi
hariri- ↑ "Nakala iliyohifadhiwa" (PDF). Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2018-08-05. Iliwekwa mnamo 2018-02-01.
- ↑ Sensa ya 2012, Kagera - Ngara-District-Council
- ↑ https://www.nbs.go.tz
Marejeo
hariri- Padre Joseph B. Kalem'imana, Wilaya ya Ngara 1600-1960 - Historia, Utawale, Uchumi na Utamaduni, Mkuki wa Nyota, Dar es Salaam, 2023, ISBN 978-9987-449-32-3
Kata za Wilaya ya Ngara - Mkoa wa Kagera - Tanzania | ||
---|---|---|
Bugarama | Bukiriro | Kabanga | Kanazi | Kasulo | Keza | Kibimba | Kibogora | Kirushya | Mabawe | Mbuba | Muganza | Mugoma | Murukurazo | Murusagamba | Ngara Mjini | Ntobeye | Nyakisasa | Nyamagoma | Nyamiaga | Rulenge | Rusumo |
Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Kagera bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Wilaya ya Ngara kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. Tafadhali usiingize majina ya maafisa au viongozi wa sasa maana wanabadilika mno. |