Mabomu ya Hiroshima na Nagasaki

Mabomu ya Hiroshima na Nagasaki yalikuwa silaha za nyuklia za kwanza katika historia ya binadamu. Zilirushwa na jeshi la Marekani kwenye Agosti wa mwaka 1945 juu ya miji ya Hiroshima na Nagasaki nchini Japani na kusababisha mara moja vifo vya watu 100,000 hivi, waliofuatwa na 130,00 za ziada waliokufa kutokana na majeraha na mnururisho katika mwaka 1945. Milipuko, pamoja na mashambulio kutoka Urusi, ilifanya serikali ya Japani kusalimisha amri na hivyo kuleta mwisho wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia[1].

Mawingu ya milipuko ya nyuklia ya Hiroshima na Nagasaki, jinsi yalivyoonekana kutoka kwa ndege
Maeneo chini ya mamlaka ya jeshi la Japani mnamo 1 Agosti 1945: Japani, Korea, sehemu za China, Indonesia, Indochina (Vietnam n.k.), Uthai.

Hali ya vita mnamo Agosti 1945 hariri

Wakati wa kurushwa kwa mabomu Vita Kuu ilikuwa imeshakwisha katika Ulaya baada ya Ujerumani kusalimisha amri kwenye mwezi wa Mei 1945. Maeneo ya Ujerumani yaligawiwa tayari baina ya washindi Marekani, Urusi, Uingereza na Ufaransa. Lakini Japani iliyowahi kuvamia sehemu kubwa za Asia iliendelea kushika nchi nyingi zilizotawaliwa na jeshi lake, kama vile Korea, kaskazini ya China, Indonesia, nchi za Indochina (pamoja na Vietnam, Uthai], Laos). Jeshi la Marekani lilifaulu kupunguza uwezo wa Japani upande wa vita ya bahari na ya angani likaandaa uvamizi wa visiwa vya Japani vyenyewe. Nguvu ya Japani ilionekana kufikia mwisho lakjini viongozi wa Marekani walihofia mapigano makali sana wakati wa kuingia kwenye visiwa vya Japani. Pia Umoja wa Kisovyeti (Urusi), iliyokuwa na mapatano ya kutopigana na Japani tangu 1941, iliandaa kushambulia Wajapani katika China na Manchuria.

Mradi wa Manhattan hariri

Wakati huohuo mabomu ya kwanza ya nyuklia yalikuwa yameandaliwa ambayo kiasili yalitengenezwa kwa kusudi la kuyatumia dhidi ya Ujerumani. Marekani iliwahi kuanza utafiti wa bomu la nyuklia mnamo mwaka 1942 baada ya kupokea taarifa kwamba Ujerumani ilitangulia na uchunguzi wa matumizi ya urani kwa silaha. Utafiti huo uliendeshwa kwa siri kubwa chini ya jina la "Mradi wa Manhattan".

Mwezi wa Julai 1945 kifaa cha kwanza kilikuwa tayari kikafanyiwa jaribio katika jangwa la jimbo la New Mexico kwenye tarehe 16 Julai. Ukali wa mlipuko ulikuwa kupita kiasi, na viongozi wa mradi walielewa kwamba walifaulu kuunda silaha mpya kabisa iliyoshinda kila silaha iliyojulikana katika historia. Wanasayansi wa Mradi wa Manhattan waliendelea kuandaa mabomu mawili mengine.

Maandalizi ya matumizi ya mabomu hariri

Baada ya Mkutano wa Potsdam wa washindi uliofanyika pale Ujerumani, mataifa ya ushirikiano yalitangaza kwamba walitaka kuona Japani kusalimisha amri bila masharti. Ndani ya serikali ya Japani kulikuwa na farakano kati ya hao waliotaka kuendelea kupigana na maadui wakati wanapofika kwenye visiwa vya Japani, na upande mwingine walioona hakuna tumaini la ushindi tena wakapendelea kukubali mashariti ya maadui[2].

Kamati ya kijeshi ya Marekani ilipanga matumizi ya mabomu; waliamua kutolenga mji mkuu na ikulu ya Tenno, badala yake kushambulia mji mkubwa wenye viwanda muhimu katika tasnia ya kijeshi. Hiroshima na Nagasaki ilikuwa kati ya shabaha zilizoteuliwa. Hiroshima ilikuwa na wakazi 255,000, ofisi kuu ya divisheni kadhaa za jeshi na ghala nyingi za silaha. Majengo mengi yalikuwa ya mbao kwa hiyo Wamarekani wapangaji walitegemea moto utaharibu mji wote. Faida nyingine machoni pa wapangaji hao ilikuwa kwamba Hiroshima haikuwa na kambi la wanajeshi wafungwa Wamarekani na Waingereza.

Utekelezaji na chaguo la mwisho ulitegemea hali ya hewa kwenye siku iliyopangwa kwa mlipuko.

Shambulizi la tarehe 6 Agosti hariri

Marubani kadhaa wa ndege kubwa ya B-29-Superfortress waliandaliwa kubeba bomu zito kuliko kawaida. Zoezi muhimu lilikuwa kuondoka haraka baada ya kurusha bomu ili kuwa mbali iwezekanavyo kutoka mlipuko wenyewe, maana mshtuko wa bomu ulikuwa hatari kwa ndege. Marubani hawakuwa na habari kwamba waliandaliwa kubeba aina mpya kabisa ya bomu.

Bomu la kwanza lilikuwa na urefu wa mita 3 na uzito wa tani 4, lenye nguvu ya uharibifu sawa na tani 12,500 za baruti ya TNT. Mafundi waliliita "Little Boy", rubani alitumia jina la mama yake kwa ndege akaandika "Enola Gay". Wahandisi kwenye ndege waliogopa uwezekano wa mlipuko usiopangwa, kwa hiyo walifunga vipuli vya mwisho baada ya kuruka kwa ndege, wakati wako hewani pamoja na ndege mbili zilizobeba wataalamu wa kutazama na kukagulia mlipuko.

Ndege iliruka saa tatu kasorobo usiku ikafika juu ya Hiroshima mnamo saa 2 asubuhi. Wajapani waliona ndege 3 tu, hawakushambulia. Mnamo saa mbili na robo bombu lilitoka kwenye ndege na mlipuko ulitokea mnamo saa mbili na dakika 16 kwenye kimo cha mita 800 juu ya mji. Dhoruba ya moto iliangamiza kilomita za mraba 11 na wingu la moshi na vumbi lilipanda kilomita 13 juu ya uso wa ardhi; nyumba 70,000 katika jumla ya nyumba 76,000 ziliharibika.

Watu 70,000 hadi 80,000 walikufa mara moja. Wale waliokuwa karibu sana na mlipuko walipotea kabisa bila kuacha mabaki, miili yao iligeukia kuwa mvuke. Mnururisho uliendelea kuua watu katika siku, wiki na miezi iliyofuata. Jumla ya wahanga wa Hiroshima imekadiriwa kuwa watu 90.000 hadi 166.000. Hata katika miongo iliyofuata, wakazi wa Hiroshima waliendelea kupata kansa kutokana na mnururisho huo.

Picha hariri

Marejeo hariri

  1. Allen, Louis (1969). "The Nuclear Raids". In Hart, Basil Liddell (ed.). History of the Second World War. 6. London: Purnell. pp. 2566–2576
  2. Richard G. Hewlett and Oscar E. Anderson, Jr.: The New World, 1939/1946, A History of The United States Atomic Energy Commission, Volume I, Pennsylvania State University Press, University Park, Pennsylvania, 1962, uk. 395, Online hapa

Tovuti za Nje hariri

Hali ya sasa hariri

Maazimio hariri

Athira hariri

Maktaba hariri

  • "Nagasaki Archive". Google Earth mapping of Nagasaki bombing archives. Iliwekwa mnamo January 3, 2012.  Check date values in: |accessdate= (help)
  • "Hiroshima Archive". Google Earth mapping of Hiroshima bombing archives. Iliwekwa mnamo January 3, 2012.  Check date values in: |accessdate= (help)

Mkusanyo wa vitabu hariri

Kukumbuka hariri

  Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mabomu ya Hiroshima na Nagasaki kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.