Augustino Ramadhani

Augustino S.L. Ramadhani (28 Desemba 1945 - 28 Aprili 2020) alikuwa mwanasheria, mwanajeshi na mwanatheolojia kutoka Zanzibar, leo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Alijulikana hasa kwa huduma yake akiwa Jaji Mkuu wa Tanzania, baadaye pia katika Tume ya Uchaguzi na Tume ya Katiba.

Augustino S.L. Ramadhani


Mwanajeshi, Jaji, Mwanasiasa, Mchungaji

utaifa Tanzania
ndoa Saada Mbarouk
watoto 4

Maisha binafsi

hariri

Ramadhani alizaliwa mjini Zanzibar, mtaa wa Kisima Majongoo, katika familia ya Kikristo ya Kianglikana akiwa mtoto wa pili kati ya wanne wa mwalimu Mathew Douglas Ramadhani na mkewe Bridget Anna Constance Masoud.

Mwaka 1952 familia ilimfuata baba aliyehamishwa kufundisha Mpwapwa, baadaye Tabora na tena Mpwapwa. Mtoto Augustino alisoma elimu ya msingi hadi 1959 kwenye shule mbalimbali mahali baba yake alipofanya kazi.

Mwaka 1960 alipokewa katika shule ya sekondari "Tabora Boys" alipohitimu mwaka 1965 baada ya kumaliza kidato cha sita. Katika kipindi hiki alipokea taarifa ya kifo cha baba yake alifariki katika ajali nchini Uingereza alipokwenda kusoma. Augustino alikumbukwa Tabora kama mwanariadha wa mpira wa kikapu na pia mpiga kinanda.

Baada ya kumaliza masomo ya Chuo Kikuu na kujiunga na jeshi alimwoa Saada Mbarouk akazaa naye watoto wanne, ambao wawili ni wavulana Francis na Mathew na wawili ni wasichana Marina na Bridget.

Masomo

hariri

Baada ya kuhitimu kidato cha sita alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akasoma fani ya sheria akafikia shahada ya awali mwaka 1970. Katika kipindi hiki alikata kadi ya uanachama wa chama cha TANU. Alikuwa kati ya wanafunzi waliofukuzwa na rais Julius Nyerere mwaka 1966 baada ya kugoma ila aliruhusiwa kurudi 1967.

Maishani mwake alirudi chuoni mara mbili pamoja na kazi mbalimbali, mwala 1978 alipata shahada ya uzamili Dar es Salaam katika Sheria za Kimataifa. Mwaka 2004 alisoma theolojia kwenye Chuo Kikuu cha London nchini Uingereza alipopata shahada ya kwanza ya uchungaji (Bachelor of Divinity).

Mwanasheria jeshini

hariri

Mwaka 1970, baada ya kumaliza Chuo Kikuu, aliingia katika Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) akawa na cheo cha kijeshi hadi mwaka 1997. Baada ya kupata mafunzo katika Chuo cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania alipandishwa cheo kama Luteni wa Pili. Mwaka 1978 alipelekwa Zanzibar kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar. Mwaka 1979 alihitajika tena jeshini akiongoza mahakama ya kijeshi katika Vita vya Kagera akipandishwa cheo hadi Luteni Kanali. Mwaka 1997 alistaafu rasmi jeshini akiwa na cheo cha Brigedia Jenerali.

Jaji Mkuu Zanzibar

hariri

Mwaka 1980 aliitwa tena Zanzibar na kuwa Jaji Mkuu, kazi aliyofanya hadi mwaka 1989. Alibadilisha mfumo wa mahakama visiwani uliofuata bado mitindo ya mapinduzi ambako watu raia, wasio na elimu ya kisheria, waliangalia kesi katika mabaraza ya wananchi. Ramadhani aliunda mfumo wa ngazi za kimahakama hadi Mahakama ya Rufaa.

Mahakama ya Rufaa na Tume ya Uchaguzi

hariri

Mwaka 1989 aliteuliwa na rais Ali Hassan Mwinyi kuwa jaji wa Mahakama ya Rufaa Tanzania. Mwaka 1993 alipewa kazi ya nyongeza akiitwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Alihudumu kwenye cheo hicho hadi mwaka 2003.

Vilevile aliteuliwa kuwa jaji wa Mahakama ya Afrika Mashariki kwenye Novemba 2001 akihudumu hadi mwaka 2007.

Mwaka 2002 alichaguliwa pia kuwa Makamu wa Mwenyekiti Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) hadi 2007.

Jaji Mkuu wa Tanzania

hariri

Mwaka 2007 aliteuliwa na rais Jakaya Kikwete kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania. Aliondoka katika kazi hiyo mwaka 2010 baada ya kufikisha miaka 65, ambao ni umri wa kisheria kwa majaji wa Tanzania.

Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu

hariri

Baada ya kipindi cha Jaji Mkuu alikubali kuwa Jaji wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu alichofanya kuanzia 2010 hadi 2016. Tarehe 14 Septemba 2014 alichaguliwa Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu akipata kura 9 dhidi ya 4 kwa mpinzani wake.

Mchungaji wa Kanisa Anglikana Zanzibar

hariri

Mwaka 2013 alikubali ombi la askofu wa Dayosisi ya Zanzibar akaingia katika utumishi wa Kanisa Anglikana kwenye ngazi ya ushemasi kwa nusu mwaka halafu alitawazwa kuwa kasisi katika ibada iliyofanyika mjini Zanzibar, Unguja tarehe 28 Desemba 2013.

Wakati ule alifundisha pia sheria katika Chuo Kikuu cha Iringa (UoI). Mpaka mauti ilipomkuta, Jaji Ramadhani alikuwa ni Mkuu wa chuo hicho.

Mnamo tarehe 7 Desemba 2019, katika mahafali ya 22 ya Chuo Kikuu cha Iringa (UoI), ambapo mgeni Rasmi alikuwa ni Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Benjamin W. Mkapa, Jaji Ramadhani alitunukiwa Shahada ya Juu ya Heshima ya Sheria (Honoris Causa Juris).

Ramadhani alikuwa mwanachama wa TANU na baadaye CCM tangu siku zake kama mwanafunzi kwenye chuo kikuu. Mwaka 1996 alirudisha kadi yake ya uanachama kufuatana na kanuni za katiba iliyobadilishwa kuwa majaji na wanajeshi wa Tanzania wasiwe wanachama wa chama cha kisiasa. Baada ya kustaafu katika utumishi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alirudi CCM kwenye mwaka 2011.

Mwaka 2015 Ramadhani alijaza fomu ya kuwa mgombea wa urais kwa CCM, lakini hakuteuliwa na chama.

Maandishi

hariri

Amechapisha makala kuhusu Haki za binadamu, kama vile, miongoni mwa nyingine, 'Kukuza Agizo Jipya la Uchumi katika Kuendeleza Nchi: Jukumu la Asasi za Haki za Binadamu', iliyochapishwa katika Kuzungumza juu ya Haki (jarida la msingi la haki za binadamu la Canada), Vol. XI No. 3/1996, na Mchakato wa Uchaguzi katika Demokrasia ya Multiparty, sura katika kitabu cha Haki za Binadamu na Ukombozi nchini Tanzania, (Mkuki na Nyota Publishers, 1978).

Marejeo

hariri
  Makala hii kuhusu mtu huyo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Augustino Ramadhani kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.