Jamhuri ya Watu wa Zanzibar
Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ingawa inajitawala katika mambo ya ndani.
Bendera ya Zanzibar | |
Lugha ya Taifa | Kiswahili |
Mji Mkuu | Zanzibar |
Rais | Hussein Ali Mwinyi |
Eneo | km² 2.654 |
Wakazi | 1,303,569 |
Dini | Waislamu takriban 96-99%, Wakristo, Wahindu |
Uhuru | Kutoka Uingereza 19.12.1963, Mapinduzi 12.01.1964 |
Fedha | TSh |
Hadi mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 nchi hiyo ilijulikana kama Usultani wa Zanzibar.
Jina
Jiografia
Eneo lake ni sawa na funguvisiwa la Zanzibar lililopo mbele ya mwambao wa Afrika ya Mashariki karibu na Tanganyika (Tanzania bara).
Linajumuisha visiwa vikubwa vya Unguja na Pemba pamoja na visiwa vidogo vidogo, lakini si kile cha Mafia kilichopo kusini zaidi.
Kiutawala Zanzibar imegawanyika katika mikoa mitano, 3 kisiwani Unguja na 2 kisiwani Pemba.
- Pemba
- Unguja
Historia
Historia inaonyesha kwamba kwa kiasi cha miaka 20,000 kumekuwepo makazi ya binadamu katika visiwa vya Zanzibar.
Visiwa hivyo ni sehemu ya kumbukumbu ya kihistoria ya ulimwengu wakati Waajemi wafanyabiashara walivigundua na kuvifanya makao makuu kwa safari kati ya Mashariki ya Kati, India na Afrika.
Katika kipindi cha karne ya 3 na ya 4, Wabantu walianza biashara na Waarabu waliofika Afrika ya Mashariki.
Katika karne ya 7, Waarabu walifika Zanzibar kibiashara pamoja na kusambaza dini ya Uislamu; Waarabu ndio walioipa jina ZANZIBAR kutokana na maneno ya Kiajemi ZINJI BAR yaani sehemu ya Watu Weusi.
Lugha ya Kiswahili ilianza kutumika kiasi cha karne ya 13 ikitokana na mchanganyiko wa lugha ya Kiarabu na lugha za Kiafrika.
Katika karne ya 16 Wareno walifika Zanzibar lakini utawala wao ulifuatiwa na kutokuwepo utulivu, lakini biashara ya utumwa iliwaweka watu pamoja.
Waarabu kutoka Oman walichukua utawala Zanzibar katika karne ya 17 na Zanzibar ilikuwa makao makuu ya utawala wa Waomani.
Miaka 1820-1870 Zanzibar ilifaidi matunda mazuri ya kiuchumi na maendeleo yaliyosababishwa na utawala wa masultani na hivyo kupelekea kuenea kwa dini ya Kiislamu Zanzibar pamoja na kuwa na mwakilishi nchini Marekani.
Katika karne ya 19 Zanzibar ilikuwa chini ya utawala wa Oman, mwaka 1830 Zanzibar ilikuwa inaongoza kwa kilimo cha karafuu, na hiyo kupelekea haja ya watumwa kuongezeka kutumika katika kilimo. Hatimaye watumwa walikuwa 90% za wakazi wote.
Mwaka 1885 kamisheni kutoka Uingereza na Ujerumani iliamua kuigawa Zanzibar kutoka katika utawala wa Kisultani na ndio ulikuwa mwisho wa utawala wa kujitegemea kwa Zanzibar. Mnamo mwaka 1886 sultani alikubali maridhiano hayo.
Mwaka 1890 Zanzibar ilikuwa chini ya uangalizi wa Waingereza rasmi, lakini uchaguzi wa mwanzo ulifanyika mwaka 1957, na miaka iliyofuata kukawepo fujo na machafuko kutoka kwa Waafrika wanaodai uhuru dhidi ya utawala wa Kiarabu.
Mwezi Desemba mwaka 1963 Waingereza waliipa uhuru Zanzibar chini ya jumuiya ya madola, na tarehe 12 Januari 1964 Zanzibar ilifanya mapinduzi kujikomboa kutoka katika utawala wa sultani.
Muda mchache baadaye iliungana na Tanganyika kuunda Jamhuri ya Muungano wa TANZANIA.
Siasa
Kwa jumla mikoa mitano ya Tanzania imo ndani ya Zanzibar ikiwa mitatu iko Unguja na miwili Pemba.
Zanzibar inatawaliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
Zanzibar ina bunge lake linaloitwa Baraza la Wawakilishi wa Zanzibar lenye wabunge 50 wanaochaguliwa kwa muda wa miaka mitano.
Mji mkuu na makao makuu ya serikali ni Jiji la Zanzibar ambalo liko kisiwa cha Unguja.
Mji mkuu wa kisiwa cha Pemba ni Chake Chake.
Jamhuri ya watu wa Zanzibar ilianzishwa baada ya mapinduzi ya 1964 yaliyomaliza Usultani wa Zanzibar.
Rais wa kwanza alikuwa Abeid Amani Karume hadi mwaka 1972.
Alifuatwa na Aboud Jumbe (1972-1984).
Rais wa tatu aliyemfuata alikuwa Ali Hassan Mwinyi (1984-1995) aliyeendelea kuwa rais wa Tanzania tangu 1985.
Rais Amani Abeid Karume ambaye ni mwana wa rais wa kwanza na alikuwa mgombea wa CCM alichaguliwa mara ya pili na wananchi wote tarehe 30 Oktoba 2005 katika kura iliyopingwa na chama cha upinzani CUF.
Rais aliyefuata ni Ali Mohamed Shein (2010-2020), halafu Hussein Ali Mwinyi.
Watu
Watu wa Zanzibar ni wa asili mbalimbali, hasa watu wa asili ya Afrika Bantu, yakiwemo makabila ya Wahamidu na Watumbatu; halafu Waasia, awali kutoka India na nchi za Kiarabu.
Idadi ya wakazi wa Zanzibar ilikuwa 1,303,569 mwaka 2012, tarehe ya sensa ya mwisho, iliyoonyesha ongezeko la 3.1% kwa mwaka.
Karibu theluthi mbili ya watu wanaishi katika kisiwa cha Zanzibar (Unguja).
Mkoa wa mjini magharibi ndio wenye idadi kubwa ya wakazi, kiasi cha watu 205,870.
Pemba ina jumla ya makazi sawa. Mji mkubwa ni Chake Chake, ukiwa na idadi ya 19,283, mengine ni Wete na Mkoani.
Dini
Dini ya Uislamu ina kiasi cha 97% za wananchi wote.
Waliobaki ni hasa Wakristo. Wa kwanza walikuja wakati wa utawala wa Kireno, halafu wakati wa masultani kuwepo Zanzibar na wa ukoloni wa Uingereza.
Kulikuwa na Wahindu pia lakini wengi wao walikimbia nchi au kuuawa wakati wa mapinduzi ya mwaka 1964.
Kuna misikiti 51, ambayo waadhini wake hugongana wakati wa maombi, pamoja na mahekalu ya Uhindu sita na makanisa kadhaa, yakiwemo Kanisa Kuu Katoliki na Kanisa Kuu la Anglikana katika mji wa Zanzibar Stonetown.
Hasa hilo la mwisho ni maarufu kwa sababu lilijengwa mahali pa soko la watumwa lililofungwa, altari ikiwa imejengwa juu ya nafasi ya mti wa kuwafunga watumwa walioadhibiwa kwa viboko, na batizio kuwa mahali walipotupwa watoto watumwa ambao hawakuuzwa pamoja na mama zao.
Hata hivyo makanisa kadhaa yalichomwa moto katika miaka 2005-2015.
Afya
Upande wa huduma ya afya, vifo vya watoto wachanga bado ni 83 kati ya wazaliwa 1000, na inakadiriwa kuwa utapiamlo huathiri mmoja katika watu watatu wa visiwa.
Matarajio ya maisha wakati wa kuzaliwa ni miaka 48, wakati maambukizi ya VVU / UKIMWI ni madogo sana kwa Zanzibar kuliko Tanzania kwa ujumla (0.6% ya idadi ya watu dhidi ya wastani wa kitaifa wa 8%).
Uchumi
Uchumi wa Zanzibar unategemea kilimo na utalii. Mazao yanayouzwa nje ni hasa karafuu, basibasi, mdalasini na pilipili.
Uchumi wa Zanzibar ni uchumi duni kabisa ambao mwananchi wa kawaida anaishi kwa kiasi cha chini ya dola moja kwa siku au hana uhakika wa kupata chochote.
Wastani wa mapato ya kila mwaka ya US $ 250 na ukweli kwamba karibu nusu ya wakazi wanaishi chini ya mstari wa umaskini. Lakini kuna tofauti kubwa katika kiwango cha maisha kati ya wakazi wa Pemba na Unguja, tena kati ya wakazi wa mijini na vijijini.
Hilo linatokana na viongozi kutoonesha mori katika kutatua matatizo au kuweka mbinu za kuleta maendeleo, badala yake ni kujadili siasa kwa muda mwingi.
Zanzibar ni nchi yenye matumaini katika uchumi lakini, kutokana na migogoro ya kisiasa, imekuwa katika hali duni kabisa, na mabalozi wa Marekani na nchi nyingine walisisitiza mara nyingi umuhimu wa kuwepo ushirikiano katika siasa ili kuiwezesha Zanzibar kuinuka katika hali ya uchumi.
Viungo vya nje
- www.tanzabradford.webs.com/umoja wa watanzania Bradford
- www.tzgr.ewebsite.com/Umoja wa Watanzania Greece
- Tovuti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Archived 13 Desemba 2009 at the Wayback Machine.
- (Kiingereza)Takwimu Archived 19 Juni 2006 at the Wayback Machine.
- (Kifaransa)Picha za Zanzibar
- (Kiingereza)Ramani ya Zanzibar na Tanganyika 1886
- (Kiingereza)Makala ya BBC kuhusu bendera mpya
- Historia na utamaduni wa Zanzibar Archived 7 Februari 2006 at the Wayback Machine.
- (Kiingereza)Zanzibar links Archived 12 Februari 2006 at the Wayback Machine.
- Zanzibar Network kwa Utalii wa Ushirika - NGO Umoja Archived 8 Januari 2008 at the Wayback Machine.
Arusha | Dar es Salaam | Dodoma | Geita | Iringa | Kagera | Katavi | Kigoma | Kilimanjaro | Lindi | Manyara | Mara | Mbeya | Morogoro | Mtwara | Mwanza | Njombe | Pemba Kaskazini | Pemba Kusini | Pwani | Rukwa | Ruvuma | Shinyanga | Simiyu | Singida | Songwe | Tabora | Tanga | Unguja Kaskazini | Unguja Kusini | Unguja Mjini Magharibi |
Makala hii kuhusu maeneo ya Tanzania bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. Usitaje majina ya madiwani na viongozi au maafisa wengine wa sasa maana wanabadilika haraka mno. |